Godfrey Malisa ni kati ya wanachama watatu wa Chama Cha Mapinduzi, waliojitokeza katika nyakati tofauti tofauti kupinga uteuzi wa Dk.Samia Suluhu Hassan kama mgombea wa chama hicho akieleza kuwa Katiba ya chama hicho ilivunjwa katika uteuzi uliofanyika Januari 19, 2025. Jambo ambalo Chama cha Mapinduzi katika nyakati mbalimbali imelikanusha.
Wengine waliojitokeza ni pamoja na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, aliyejiuzulu kwa kueleza kutorishidhwa na uongozi wa nchi na pia katika chama chake, Polepole ameendelea kusisitiza uteuzi huo wa Januari 19, 2025, ulikuwa ni batili. Mwingine ni Davidlevi Nestory Kindikwa, mwanachama wa chama hicho kutoka Mwanza, aliyesambaza barua aliyoiandika kwa Msajili wa Vyama vya siasa juu ya jambo hilo hilo.
Tofauti na Polepole na Kindikwa, Godfrey Malisa alipeleka malalamiko yake Mahakamani,ambapo Mahakama ilitupilia mbali madai yake, mnamo Agosti 22, 2025. Walalamikiwa katika shauri hilo yaani Bodi ya Wadhamini ya CCM na Katibu Mkuu wa CCM, waliwakilishwa na mawakili wawili Alex Mgongolwa na Fabian Mnada.
Majaji watu akiwemo Jaji Joachim Charles Tiganga, Jaji Evaristo Emmanuel Longopa, na Jaji Griffin Venance Mwakapeje walisikiliza shauri hilo. Majaji walieleza sababu kuu mbili za kutupilia mbali shauri hilo katika hatua za awali, kwanza walieleza kuwa mlalamikaji alishindwa kutumia kikamilifu njia za ndani za kupeleka malalamiko katika chama hicho kabla ya kufika mahakamani, na pili, walionesha makosa katika hati ya kiapo. Masuala yote haya mawili yaliibuliwa na Mawakili wa walalamikiwa katika mapingamizi yao.
Mahakama ikielezea kuhusu hati ya kiapo, ambayo Malisa alitumia kuwasilisha malalamiko yake Mahakamani, Mahakama ilieleza kuwa, jina kuonekana kwanza kama Dr. Godfrey Fataeli Mlamie Malisa, kisha Godfrey Fataeli Mlamie Malisa na Godfrey Fataeli Malisa inafanya kisheria kuwa ni watu watatu tofauti katika nyaraka hiyo inayomtambulisha Malisa, nyaraka ya msingi katika lalamiko hilo.
“Ni wazi kwamba, mtu aliyejitokeza mbele ya Kamishna wa Kiapo na kutambulishwa na Denis Maringo [wakili wa Malisa] siye muapaji, kwani kwa mujibu wa rekodi za Mahakama, ni Godfrey Fataeli Malisa, ilhali mlalamikaji amejitambulisha mwenyewe katika shauri na mwanzoni mwa hati ya kiapo kama Dr. Godfrey Fataeli Mlamie Malisa. Hawa kisheria ni watu watatu tofauti, jambo linalofanya hati ya kiapo kuwa na kasoro zisizoweza kurekebishwa,” ilieleza hukumu ya Mahakama.
Suala lingine ambalo Majaji walilieleza ni kuwa mlalamikaji hakupita katika ngazi stahiki za kulalamika ndani ya CCM. Akifafanua juu ya jambo hili, Wakili wa Malisa, Wakili Denis Maringo, alieleza kwanza muda ulikuwa mfupi sana kuweza kupeleka malalamiko katika njia za ndani za Chama, kwa kuwa mchakato wa kupeleka majina katika Tume ya Uchaguzi ulikuwa unaendelea, hata hivyo Mahakama haikukubaliana na hoja hii.
“Hatukubaliani na hoja hii. Sababu ni kuwa tukio linalolalamikiwa lilitokea Januari 2025. Na malalamikaji alionesha kutoridhika mara tu, baada ya tukio hilo,” Mahakama inaeleza katika uamuzi wake.
“Ushahidi wa hili uko wazi kwa barua ya Februari 11, 2025, aliyoiandika kwa Mwenyekiti wa chama na pia amethibitisha hili katika aya ya nne ya hati ya kiapo, kupitia barua hiyo alimjulisha Mwenyekiti juu ya kusudio lake kukishtaki chama na bodi ya wadhamini.”
“Hata hivyo, alichukua hatua aliyoieleza [kufungua mashtaka] miezi mitano baadae, mnamo Julai 2025. Hii inaonesha kuwa mlalamikaji alikuwa na muda wa kutosha kutumia kikamilifu njia za ndani kabla ya kutafuta msaada wa mahakama,” Mahakama inaendelea kuainisha.
Angalia: CCM Yaeleza Kikao cha Uteuzi wa Wagombea Urais Januari 2025 Kilizingatia Katiba na Kanuni
Kwa mujibu wa Mahakama njia za ndani za kupeleka malalamiko ndani ya CCM zimeainishwa katika Kanuni za Uteuzi wa Wagombea Uongozi Katika Vyombo vya Dola, kanuni ambazo zimeainisha malalamiko yote katika ngazi ya taifa yawasilishwe kwa Katibu Mkuu wa chama.
Majaji walielezea zaidi kuwa barua ya Malisa aliyoiandika Februari 11, 2025, haiwezi kuchukuliwa kama lalamiko rasmi kwa sababu alikijulisha chama juu ya dhumuni lake la kwenda Mahakamani.Majaji wakaeleza hata wakijaribu kuiangalia barua hiyo kama lalamiko rasmi bado inakosa nguvu ya kisheria kwa kuwa iliandikwa kwa Mwenyekiti wa chama badala ya kwenda kwa Katibu wa chama kama kanuni za chama hicho zinavyotaka.
Akiwasilisha hoja za upande wa mlalamikaji, Wakili wa Malisa aliieleza Mahakama kuwa hakukuwa na mantiki kupeleka malalamiko ndani ya chama kwa kuwa wanaolalamikiwa ndio hao hao wangesikiliza malalamiko hayo. Mahakama haikukubaliana pia na hoja hiyo.
“Siyo mtu binafsi anayekaa kusikiliza na kuamua malalamiko; bali ni ‘Kamati ya Siasa’ au ‘Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya NEC’ ndizo hukaa kusikiliza na kuamua kuhusu malalamiko,” Mahakama ilieleza.
“Hivyo basi, hoja kwamba utatuzi huo hauna uhalisia kwa sababu vyombo na maafisa wanaolalamikiwa ndiyo hao hao ambao wangekaa kusikiliza malalamiko hayo, haina msingi. Kwa hiyo tunayatupilia mbali malalamiko haya kwa kuwa hayana mashiko,” Mahakama ilisisitiza.
Katika suala la malalamiko ya Malisa, Kamati Kuu ya Halmashauri kuu ndiyo ilikuwa chombo sahihi cha kusikiliza suala hilo, Mwenyekiti wa Kamati Kuu ni Mwenyekiti wa Chama.
Malisa alifukuzwa kwenye Chama Cha Mapinduzi mnamo Februari 2025 kwa kile ambacho uongozi wa mkoa Kilimanjaro ulieleza kuwa mwanachama huyo alikwenda kinyume na maamuzi ya chama, yaani maamuzi ya chombo kikuu katika chama hicho, Mkutano Mkuu wa Taifa.