Rangi za njano na kijani zilisambaa Alhamisi ya Agosti 28, 2025, siku ambayo Chama cha Mapinduzi (CCM), kilizindua kampeni zake za uchaguzi katika uwanja wa Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam. Katika mkutano huo uliofunguliwa na marais wastaafu akiwemo Jakaya Mrisho Kikwete, Amani Abeid Karume na Ali Mohamed Shein, CCM ilitumia muda mrefu kupitia viongozi wake waandamizi kuwakumbusha wapiga kura juu ya nyakati ngumu zilizokuwepo wakati Rais Samia akiingia madarakani.
Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete aliweka msingi juu ya hoja hii, ambapo alianza kwa kujibu shutuma kuwa taratibu na kanuni za CCM zilivunjwa katika kumteua Samia kama mgombea wa Urais CCM kwa mwaka 2025.
“Kulikuwepo na maneno au vijineno eti utaratibu umekiukwa na mie nililaumiwa kwa jinsi nilivyosema pale kwenye mkutano mkuu. Lakini nasema waliokuwa wanayasema hayo ama hawafahamu utaratibu wa chama chetu na kama wanafahamu labda wamesahau, au wanajifanya hamnazo,” alieleza Kikwete.
“Tangu tulipoanza mfumo wa vyama vingi, ndani ya CCM tumejiwekea utaratibu kuwa Rais wetu aliopo madarakani anapomaliza kipindi cha kwanza na akataka kipindi cha pili huwa anapewa nafasi pekee yake. Ndivyo ilivyokuwa kwa Rais Mkapa, ndivyo ilivyokuwa kwangu na ndivyo ilivyokuwa kwa Rais Magufuli, kwanini leo kuwe na kelele za kutaka iwe tofauti kwa Rais Samia, sababu yake nini?”aliendelea kuhoji Kikwete.
Rais aliyelivusha Taifa
Kikwete na Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Stephen Wasira walitumia sehemu ya hotuba zao kuwakumbusha Watanzania juu ya nyakati ambazo Rais Samia aliingia mdarakani, yaani kifo cha Rais akiwa madarakani, UVIKO-19 na mashaka na hofu juu ya Rais mwanamke.
“Ikumbukwe kwamba marais sisi tuliopita kwenye huu mchakato tangu vyama vingi tulikuwa na muda wa kujiandaa. Maana kila mmoja alipanga,akatengeneza na timu yake na watu wake na sera zake,” anaeleza Kikwete.
“Lakini Mama samia alijikuta Rais ghafla bila kutarajia, alikuwa ziarani Tanga akaletewa habari kwamba Rais amefariki. Akatoa taarifa usiku wa manane,lakini alichukua muda mfupi sana kujiimarisha katika nafasi hiyo, alikuwa kama Komando aliyetua kwa mamvuli eneo la mapigano huku akiwa anapiga risasi,” aliendelea kufafanua Kikwete.
Kikwete na Wasira kwa pamoja wakagusia pia changamoto iliyomkabili Samia kama Rais wa kwanza mwanamke.
“Alipokea uongozi katika wakati wa mazingira magumu ya kupoteza Rais aliyekuwa madarakani kufuatia kifo cha Rais John Pombe Joseph Magufuli,ni mara ya kwanza nchi kukutwa na tatizo la namna ile. Kulikuwa na mashaka makubwa kwamba mambo yatakuwaje na maswali makubwa yalikuwa hivi huyu mama kweli ataweza kuongoza nchi hii?” Kikwete aliendelea kueleza, suala ambalo hata Wasira aliligusia kwenye hotuba yake.
“Kwa hiyo Rais Samia anachukua uongozi wa nchi katika mazingira hayo ya majanga matatu [UVIKO-19, hali mbaya ya uchumi na kifo cha Rais],nchi ilitikisika na kulikuwa na mawazo mseto na hofu,” anaeleza Wasira, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara,akizungumza kama mtu wa mwisho ili kumkaribisha Samia kuongea.
“Kila mtu alikuwa na hofu ya aina yake. Kwa sababu ya matatizo ya mfumo dume wengine walifikiri uko uhusiano kati ya urais na wanaume,kwa hiyo usipokuwa mwanaume huwi Rais.”
“Wengine walikuwa marafiki wa marehemu na ni haki yao, lakini walikuwa na hofu mabadiliko yale yatawaacha wapi?Walitofautisha matakwa yao na matakwa ya watanzania, na matatizo tunayoyasikia huko nje huko yanatokana na hofu. Hiyo hofu ya kawaida tu, lakini hofu ilikuwa kubwa,” Wasira aliendelea kuelezea.
Wasira na Kikwete wote walitambua kampeni ya 4R, Kikwete akiieleza kama ubunifu, na Wasira akieleza kwamba Samia aliitumia kuyaleta makundi mbalimbali pamoja.
SOMA: 2025: Uchumi Utaimarika, Imani Katika Siasa Itadorora Kabisa Tanzania
Tathmini hii kutoka kwa waandamizi wa CCM inaonekana kuwa moja ya mkakati muhimu wa kampeni katika kuuonesha uongozi wa Samia kwa mchango wake katika kuunganisha Watanzania katikati ya tukio la kifo cha Rais. Wachambuzi wanaangalia hili kama njia ya kumsogeza Samia karibu na mioyo ya watu, kwa kufanya watu kuona changamoto alizokabiliana nazo, hii ni katika kupambana na ukosoaji mkali unaofanywa na vyama vya vikubwa vya upinzani.
CHADEMA na ACT Wazalendo wanaielezea 4R kama kampeni iliyofeli, hii ni baada ya kuibuka kwa matukio mengi ya utekaji na upotezaji wa watu, huku mengi yakihusishwa na siasa.Ukiacha umaliziaji wa miundombinu na huduma za jamii, 4R inatajwa kama moja zao la kipekee la serikali ya awamu ya sita, hii ikimaanisha kampeni hiyo ni alama muhimu ya kuelezea mafanikio au kutofanikiwa kwa serikali ya awamu ya sita.
Mgombea
Katika mkutano kampeni za mwaka huu, Samia na mgombea wake mwenza, Emmanuel Nchimbi wanagombea chini ya kauli mbiu, Kazi na Utu. Akiongea katika ufunguzi wa kampeni zake, Samia alikumbushia na yeye namna alivyoingia madarakani na hatua alizozichukua.
“Nilikabidhiwa nchi ambayo kwa namna yoyote ile ilihitaji muafaka wa kitaifa na kimataifa kuweza kuiongoza. Muafaka kati ya serikali na viongozi wa kisiasa, wana harakati, wafanyabiashara, jumuiya za kimataifa na wananchi kwa ujumla,” anaeleza Samia mwanzoni mwa hotuba yake.
“Leo ikiwa ni miaka minne na miezi mitano baadaye siwezi kusema kwamba tumefanya kila kitu kilichosemwa au kilichoelezwa kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi. Lakini kwa ujasiri mkubwa naweza kusema tumefanya makubwa kuhakikisha nchi yetu inajengwa na taifa linarejea kwenye hali ya utulivu tuliyoizoea,” aliendelea kueleza Rais Samia.

“Kupitia falsafa ya R nne tulihakikisha taifa linaendelea kuwa na heshima ndani ya bara la Afrika na duniani kwa kutunza amani na utulivu,na ripoti ya Global Peace Index ya mwaka huu 2025 inaonesha kuwa Tanzania inaongoza kwa viwango vya amani ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki,” alieleza Rais Samia.
Samia aliendelea kuelezea mafanikio mbalimbali katika huduma za kijamii, miundombinu na uchumi kwa ujumla. Alimalizia hotuba yake kwa kueleza mambo ambayo atayafanya siku mia za kwanza ofisini. Hii ikijumuisha kuanza majaribio ya bima ya afya kwa wote ikihusisha watoto, wazee, kina mama wajawazito na watu wenye ulemavu. Lakini pia ameeleza kuwa serikali itagharimia kwa asilimia mia moja gharama zote za kutibu na kupima magonjwa yasiyoambukiza kwa Watanzania wenye kipato cha chini.
Ahadi nyingine ni pamoja na kuajiri walimu wapya, kuunganisha vyuo na waajiri, na kurasimisha sekta isiyo rasmi. Kwa kuendana na ahadi ya CCM ya kuanzisha mchakato wa Katiba mpya, Samia ameahidi kuunda tume ya maridhiano na upatanishi ndani ya siku 100 za kwanza akichaguliwa kuwa Rais.
“Tukiongozwa na falsafa ya R4 tutaendeleza mashauriano na wadau wa siasa, taasisi za kiraia na sekta binafsi kwa kuunda Tume ya kuanzisha mazungumzo ya maridhiano na upatanishi na kuandaa mazingira ya kuanza kwa mchakato wa Katiba mpya,” alisisitiza Rais Samia.
Na kuongeza: “Kwa ujumla katika miaka mitano ijayo tumejipanga sio kuongeza nguvu tu kwenye miundombinu bali pia kwenye huduma zinazotolewa, kusimamia haki, amani na utulivu wa kisiasa ili kukuza uchumi na kuleta maendeleo.”
CCM pamoja na vyama vingine 18 vinavyoshiriki uchaguzi vinategemea kufanya kampeni katika siku 60 zijazo mpaka Oktoba 28, 2025, siku ya mwisho ya kampeni. Leo, Agosti 29, 2025, CCM inaendelea na kampeni zake katika mkoa wa Morogoro.