Chama kikuu cha upinzani Tanzania, CHADEMA kupitia uongozi wake imetangaza Septemba 1 mpaka 7, kuwa wiki ya mashujaa wa kidemokrasia, ambapo kilele chake itakuwa ni Septemba 07, 2025.
Siku hiyo imetengwa ikiwa ni siku ambayo kiongozi wa chama hicho, Tundu Lissu, alinusurika kuuwawa baada ya kushambuliwa kwa risasi mnamo Septemba 07, 2017. Lakini pia ndiyo siku ambayo mwili wa mjumbe wa Sekretarieti ya CHADEMA, Ali Kibao mwili wake ulipatikana baada ya kutekwa na watu wenye silaha mwaka 2024. Katika matukio yote mawili, polisi wameendelea kueleza kuwa wanachunguza.
Katika siku ya kwanza ya maadhimisho hayo, mwanasheria Tito Magoti ameongoza kampeni ya mtandaoni #IamTunduLissu, #MiminiTunduLissu, ambapo pamoja na mjadala uliofanyika mchana, watumiaji wa mitandao wameendelea kusambaza habari kuhusiana na Tundu Lissu, ambaye toka Aprili 10,2025, yupo rumande kwa kushitakiwa makosa ya uhaini.
CHADEMA watafanya Baraza la mtandaoni mnamo Septemba 02, 2025, ambapo mijadala mbalimbali itafanyika.
Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche, mnamo Septemba 07, 2025, bendera za chama hicho zitapepea nusu mlingoti nchi nzima kuwakumbuka wanachama wao na wapigania demokrasia waliofungwa, kutekwa, kupotezwa na hata kuuwawa Tanzania. Shughuli hiyo itaenda sambamba na ibada, na mijadala ya kisiasa, na majadiliano nchi nzima.