Dar es Salaam. Tume huru ya taifa ya uchaguzi (INEC) imetoa uamuzi wa rufaa zilizowasilishwa na wagombea ubunge na udiwani dhidi ya maamuzi ya wasimamizi wa uchaguzi kufuatia pingamizi za uteuzi kwenye uchaguzi mkuu wa oktoba 2025.
Hadi kufikia tarehe 31 Agosti 2025, Tume ilipokea jumla ya rufaa 33, ambapo rufaa 13 zimefanyiwa maamuzi. Kati ya hizo, rufaa 8 zilihusu nafasi za ubunge na rufaa 5 zilihusu nafasi za udiwani.
Tume imekubali rufaa mbili za wagombea ubunge, ambazo ni; Ezekiel Gabriel Katabi ambaye ni mgombea ubunge jimbo la Muhambwe kupitia Chama Cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) dhidi ya uamuzi wa msimamizi wa uchaguzi jimbo la Muhambwe, hivyo amerudishwa rasmi katika orodha ya wagombea.
Athuman Issah Henku ambaye ni mgombea ubunge jimbo la Ikungi Mashariki kupitia chama cha CUF, rufaa yake dhidi ya uamuzi wa msimamizi wa uchaguzi jimbo la Ikungi imekubaliwa, hivyo anarejea kwenye kinyang’anyiro cha ubunge kuendelea na utaratibu wa kampeni.
Aidha, Rufaa sita (6) za wagombea ubunge zimekataliwa na Tume na hivyo kukubaliana na uamuzi wa wasimamizi wa kutowateua kuwa wagombea ubunge. Rufaa hizo ni za Msowoya Gelard Goodluck wa jimbo la kilombero kupitia ACT-Wazalendo, Innocent Gabriel Siriwa jimbo la Kibamba kupitia ADC na David January Mhanga wa jimbo la Mkuranga kupitia CHAUMMA.
Mwingine ni Christina Gasper Mbise ambaye ni mgombea ubunge jimbo la Ubungo kupitia ADC, Cecil Fransis Akili jimbo la Ndanda kupitia ACT-Wazalendo na Mneke Jafari Saidi mgombea ubunge Jimbo la Newala Vijijini kupitia CUF.
Kwa upande wa udiwani, katika rufaa zilizoamuliwa, mgombea wa udiwani kata ya Mabatini jijini Mbeya kupitia CHAUMMA, Abisai Raston Hankungwe rufaa yake imekataliwa na Tume na hivyo hatashiriki katika uchaguzi.
Mwajuma Hamidu Tito wa CUF ambaye yeye alikua mgombea udiwani kata ya Nanganga, jimbo la Ndanda naye rufaa yake imetupiliwa mbali hivyo hatoshiriki katika uchaguzi. Kwa upande wa mgombea udiwani wa CHAUMMA kata ya Ilolo, jimbo la Vwawa Richard Mwendanjila Kibona yeye amerejeshwa kufuatia kushinda rufaa juu ya pingamizi alilowekewa.
Kwa mujibu wa sheria baada ya uteuzi kufanyika na Tume wagombea wana uhuru wa kukata rufaa iwapo hawakuridhishwa na uamuzi wa msimamizi wa uchaguzi kuhusu uhalali wa pingamizi zilizowekwa dhidi yao. Rufaa hizo ziliwasilishwa kwa Tume ndani ya saa 24 tangu kutolewa kwa uamuzi husika.
Kwa upande mwengine Tume imesisitiza kuwa itaendelea kutoa taarifa kwa umma kuhusu maamuzi ya rufaa zilizobaki mara tu uamuzi unapofanyika.