Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimetoa tamko kufuatia taarifa za kuvamiwa kwa ofisi za jukwaa la Jamii Forum.
“LHRC tunasimama kwa mshikamano na Jamii Africa kufuatia uvamizi usio rafiki katika ofisi zao. Tunalaani vikali tukio hilo na tunaendelea kufuatilia kwa karibu kuhakikisha ukweli unafichuliwa,” imeeleza taarifa ya kituo hicho.
Majira ya mchana wa Septemba 05, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Forum Afrika, Jukwaa la mtandaoni lenye mamilioni ya watumiaji, katika nchi zaidi ya nne Afrika, alieleza kuwa ofisi hizo zimevamiwa.
“Kuna uvamizi usio Rafiki uliofanyika muda sio mrefu ofisi za JamiiForums, Mikocheni jijini Dar wakinitafuta mimi,” alieleza Maxence Melo, Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Afrika, kwenye taarifa yake.
“Nalaani vitendo kama hivi, ila umma utaujua ukweli hivi karibuni,” aliongeza Melo. Inategemewa ofisi hiyo itatoa taarifa zaidi kuhusu tukio hilo.