Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza kusitisha leseni ya maudhui, pamoja na kuufungia mtandao wa JamiiForums kupatikana Tanzania, kwa siku tisini kwa kile ambacho mamlaka hiyo imeeleza ni kuchapisha maudhui ya kupotosha umma.
“Mnamo tarehe 04 Septemba 2025, JamiiForums kupitia jukwaa lake na akaunti zake za mitandao ya kijamii ilichapisha maudhui ya kupotosha umma, kukashifu na kudhalilisha Serikali na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinyume na Kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2020 na Marekebisho yake ya mwaka 2022 na 2025,” taarifa ya TCRA inaeleza.
TCRA imeeleza kuwa maudhui hayo yanakiuka Kanuni na kukinzana na utamaduni, mila na desturi za Kitanzania. Kupitia kurasa zake, JamiiForums, imeonesha taarifa waliyopokea kutoka TCRA, ikionesha maudhui yaliyolalamikiwa na TCRA ni yale yaliyomhusisha aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, aliyoyatoa katika mitandao ya kijamii mnamo Septemba 4, 2025, kuhusiana na mfanyabiashara wa Zimbabwe, Wicknell Chivayo.
Taarifa hii kutoka TCRA inakuja siku moja baada ya Mkurugenzi wa JamiiForums, Maxence Melo, kueleza kuwa ofisi hiyo ilivamiwa.
“Kuna uvamizi usio rafiki uliofanyika muda sio mrefu ofisi za JamiiForums, Mikocheni, jijini Dar es Salaam, wakinitafuta mimi,” alieleza Maxence Melo, Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Afrika, kwenye taarifa yake, jana Septemba 05, 2025.
Hata hivyo, Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa, alikanusha taarifa hiyo kwa kueleza kuwa kilichotokea ni utaratibu wa kawaida wa mawasiliano.
“Hakuna uvamizi uliofanyika katika ofisi za JamiiForums. Kilichotokea ni utaratibu wa kawaida wa mawasiliano kati ya Mamlaka za Serikali na wadau wake. Ambapo leo Maafisa wa Serikali walikwenda kuwasilisha barua ya wito kwa Jamii Forums,” alieleza Msigwa.
Katika taarifa yake aliyoitoa jioni kupitia JamiiForums, Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao huo, Maxence Melo alieleza kuwa tukio hilo halijaathiri shughuli za JamiiForums, miundombinu, wafanyakazi wala mali zake.
Melo ametangaza leo, Septemba 06, 2025, kujiuzulu ujumbe wa Bodi katika Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wangu.
“Niliteuliwa Disemba 18, 2023, na nimehudumu kikamilifu majukumu yangu. Natoa shukrani nyingi kwa Wizara, Tume, na wajumbe wenzangu kwa ushirikiano mzuri walionipa katika kipindi chote,” alieleza Melo.
JamiiForums ni moja ya jukwaa kubwa zaidi kuwahi kuanzishwa na kuendeshwa ndani ya Afrika katika zama za mitandao ya kijamii. Ilianzishwa mwaka 2006 na sasa inahudumia moja kwa moja zaidi ya nchi tano katika ukanda wa kusini mwa Afrika.