The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Namna Wazazi Tunavyoua Ujasiri wa Watoto Wetu Bila Kujua

Tukitaka watoto wetu wakue wakiwa na ujasiri, wenye kujiamini na tayari kushinda changamoto za maisha, basi tuwe makini na maneno yetu.

subscribe to our newsletter!

Kila mtoto huzaliwa na mbegu ya kujiamini, na ni jukumu letu kuikuza. Watafiti kama wameonesha kuwa ujasiri wa mtoto unajengwa, ama kuvunjwa, zaidi nyumbani kupitia maneno yetu, vitendo vyetu na hata ukimya wetu.

Tafiti zinaonesha kuwa watoto wanaolelewa kwa upendo usio na masharti na maneno ya kutia moyo hukua wakiwa thabiti zaidi. Kinyume chake, ukosoaji wa mara kwa mara na upendo wa masharti huwafanya wajihisi hawatoshi.

Lakini mara ngapi tumewaambia watoto wetu, “kwa nini huwezi kuwa kama dada yako?” Au tukanyamaza bila kupongeza jitihada zake ndogo? Kwetu ni mambo madogo, lakini kwake ni ujumbe unaoathiri jinsi anavyojiona na taswira yake binafsi.

Mara nyingi bila kujua, tunadhani tunafundisha au kulinda, kumbe tunavunja nguzo muhimu ya utu wao kujiamini.

Watoto wanapokosea, wanahitaji kuelekezwa, si kukandamizwa. Tukiwaambia mara kwa mara, “Wewe huwezi kitu,” au “Siku zote unakosea kosea tu,” tunamjengea mtoto imani kwamba yeye ni wa kushindwa tu. Mwishowe, hata akikosea kidogo, ataona hana maana.

SOMA ZAIDI: Tunawaandaje Mabinti Zetu kwa Ajili ya Hedhi Yao ya Kwanza?

Si jambo zuri kumlinganisha mtoto na jirani, rafiki au ndugu: “Angalia mtoto wa fulani, mbona huwezi kuwa kama yeye?” Maneno haya yanaonekana kama ya kawaida, lakini yanaumiza. Kila mtoto ana safari yake. Kumlazimisha ajione kama mwingine ni sawa na kumwambia: “Wewe hautoshi.”

Kila mzazi anataka kumlinda mtoto wake, lakini tukimzuia mtoto kujaribu mambo mapya, kushindwa na kujifunza, tutatkua tunamlea kuwa mtu anayekosa uthubutu. Wakati mwingine tunapomzuia mtoto kurusha mpira, kupanda baiskeli au hata kwenda dukani peke yake, tunamfunda kimya kimya: “Wewe huwezi.”

Mtoto akichora mchoro mdogo, akaimba kanisani au msikitini, au akasaidia kupika ugali, macho yake hutafuta uthubutu kutoka kwetu. Ukimya wetu huumiza sawa na maneno mabaya. Sifa ndogo tu hujenga moyo wake.

Nidhamu ni muhimu. Lakini adhabu za mara kwa mara bila kueleza sababu ya adhabu hiyo hujenga hofu badala ya maadili. Mtoto atakua na nidhamu ya uoga akitii tu akiwa mbele yako. Nidhamu halisi ni ile inayorekebisha huku ikimfanya mtoto ajue bado anapendwa.

Mtoto anapojaribu kueleza jambo na tunamkatisha au kusema maneno kama, “Nyamaza” tunamfundisha kwa sauti na Mawazo yake hayana thamani. Hatimaye atakua mtu mzima asiye na ujasiri wa kusema mawazo yake, hata pale ambapo yanaweza kusaidia jamii.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini ni Umuhimu kwa Watoto Kuwatembelea Bibi na Babu Zao?

Watoto hawapaswi kupendwa kwa sharti la kufanya vizuri tu. Wengine wanaonyeshwa upendo pale tu wanapopata alama za juu au wanaweza kufanya jambo flani. Lakini pale wanaposhindwa, wanakosa upendo. Huu ni msingi wa kuua ujasiri. Upendo wa kweli ni ule unaodumu   

Kumkemea mtoto mbele ya ndugu, marafiki au darasani humvunja moyo. Mtoto hujifunza aibu, si nidhamu. Rekebisho lina nguvu zaidi likifanywa faraghani, kwa upendo na kwa heshima.

Tunapoweka matarajio makubwa kupita kiasi kwa watoto wetu  tunawajengea watoto presha ya maisha. Pale wanaposhindwa kufikia matarajio hayo, huona wamewaangusha wazazi. Badala ya kuhimiza ukamilifu kwa kila kitu, tuhimize maendeleo ya hatua kwa hatua.

Watoto wanapima thamani yao kwa umakini tunaowapa. Dakika chache za kusikiliza hadithi zao au kucheza nao ni mbolea ya ujasiri wao.

Maneno mabaya kama “mjinga,” “mvivu,” “msumbufu” hubaki kwenye nafsi ya mtoto muda mrefu kuliko tunavyofikiria. Taratibu, mtoto anaweza kuanza kuishi kulingana na majina hayo. Tuwe wazazi tunaosema maneno ya kuwainua, si ya kuwaangusha.

SOMA ZAIDI: Tujifunze Tunavyoweza Kuwasaidia Watoto Wetu Kwenye Safari Yao ya Elimu

Mtoto akihisi kwamba kila mara wazazi wake wanamwambia, “Wewe huwezi kufanya hivyo,” ataamini kweli hawezi. Lakini tukimpa imani, hata akishindwa, atajua bado ana nafasi ya kujaribu tena. Ujasiri huota pale mtoto anapojua wazazi wake wanapomuamini uwezo wake.

Wazazi wenzangu, ujasiri wa mtoto ni kama mmea mdogo. Tunaweza kuuotesha kwa kumpa upendo, kupongezwa na kushikwa mkono, au tunaweza kuuua kwa maneno ya kuumiza, aibu na tabia za kuwapuuzia.

Tukitaka watoto wetu wakue wakiwa na ujasiri, wenye kujiamini na tayari kushinda changamoto za maisha, basi tuwe makini na maneno yetu, tuwafundishe kwa hekima na tuwapende bila masharti.

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×