The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Leo Tujadili Maumivu ya Kihisia Wazazi Tunawarithisha Watoto Wetu

Tunaweza kuwathamini wazazi wetu kwa walichojitahidi kufanya, lakini sisi hatuna kisingizio cha kuendeleza mzunguko wa ukatili.

subscribe to our newsletter!

Wengi wetu tumekulia kwenye malezi yaliyotawaliwa na hofu. Tulifundishwa kwamba maneno makali, fimbo, au ukali kupita kiasi ndivyo vigezo vya nidhamu. Kauli kama “Ukikosea, unaadhibiwa” zilikuwa sehemu ya maisha ya kila siku.

Ni kweli, wengi wetu tumekua na maisha yanayoonekana “yamefanikiwa:” tumesoma, tunaheshimu wakubwa, na tunaweza kujitegemea. Lakini ndani yetu, tulibeba pia mbegu za majeraha. Mbegu ambazo sasa hujitokeza kwenye namna tunavyowapenda, tunavyosamehe, au tunavyolea watoto wetu.

Tafiti zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya watoto barani Afrika hupitia adhabu kali majumbani. Kwa wengi wetu, takwimu hizi ni maisha tuliyoishi.

Adhabu za kupiga, au kutishia, mara nyingi hutufundisha kuona ukali kama jambo la kawaida. Hutuacha na hofu, badala ya kuwajibika kwa makosa yetu. Hutufanya tujitenge kihisia na wazazi wetu kwa kuhisi kuwa wao sio sehemu salama. 

Na tunapokua, mara nyingi tunarudia mbinu zilezile. Ndivyo mzunguko wa ukatili unavyoendelea.

SOMA ZAIDI: Namna Wazazi Tunavyoua Ujasiri wa Watoto Wetu Bila Kujua

Watoto wanaokuzwa kwa hofu huishia kuamini kwamba kutumia nguvu, au ukali, ndiyo njia sahihi ya kurekebisha kosa. Shuleni, huwapiga au kuwatisha wenzao wanapokasirika.

Tukiwa watu wazima, tukiingia kwenye migogoro ya kifamilia, au ndoa, tunaishia kuitatua kwa ukali, au hata ukatili, na hivyo kuchochea changamoto kama ukatili wa kijinsia katika jamii zetu. Tukiwa wazazi, mara nyingi tunashika fimbo zilezile tulizopigwa nazo, tukijifariji kwamba “hata sisi tulilelewa hivyo.”

Kwa namna hii, maumivu haya ya kihisia yanageuka kuwa mzunguko unaojirudia kizazi baada ya kizazi.

Ni kweli, wazazi wetu walifanya walichoweza. Wengi wao walikulia katika mazingira magumu na waliamini ukali na fimbo zingetuandaa kustahimili changamoto za maisha. Walikuwa na nia njema. Lakini nia pekee haitoshi bila tafakuri. Malezi hupimwa kwa matokeo yake, si kwa nia tu.

Hivyo basi, tunaweza kuwapa wazazi wetu neema kwa walichokuwa hawakijui, lakini jukumu la kuvunja mzunguko huu liko mikononi mwetu.

SOMA ZAIDI: Tunawaandaje Mabinti Zetu kwa Ajili ya Hedhi Yao ya Kwanza?

Kama kizazi cha sasa, tuna nafasi ya kuchagua kuwapa watoto wetu malezi tofauti. Tunaweza: 

  • kubadilisha hofu kuwa heshima. Nidhamu haihitaji vitisho wala ubabe. Tunapoweka mipaka kwa upendo na utulivu, watoto hujifunza kuwajibika bila hofu.
  • Kuonesha mifano bora wa kusuluhisha migogoro. Mazungumzo, uvumilivu na msamaha vinafunza zaidi kuliko maneno makali au mikono myepesi ya kupiga.
  • Kusikiliza na kuthibitisha hisia. Mtoto anapoongea, tumpe nafasi. Kusikiliza humjengea thamani.
  • Kujifunza mbinu mpya za malezi. Kupitia vitabu, mafunzo, au mijadala ya kijamii, tunaweza kubadili mitazamo tuliyozoea.
  • Kuomba msamaha. Neno dogo la samahani kutoka kwa mzazi linaweza kuponya zaidi ya ukimya wa miaka mingi.

Malezi yetu ni urithi tunaoutengeneza kila siku. Tunaweza kuwathamini wazazi wetu kwa walichojitahidi kufanya, lakini sisi hatuna kisingizio cha kuendeleza mzunguko wa ukatili.  

SOMA ZAIDI: Kwa Nini ni Umuhimu kwa Watoto Kuwatembelea Bibi na Babu Zao?

Swali ni hili: je, vizazi vijavyo vitarithishwa hofu na maumivu ya kihisia, au tutavunja mzunguko huu na kulea watoto wanaokua katika upendo, heshima na amani?

Uamuzi uko mikononi mwetu.

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×