Dodoma. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG ya mwaka 2023/2024 inaonesha Halmashauri 16 zilikusanya mapato ya jumla ya Shilingi bilioni 6.68, kupitia mfumo wa zamani wa ukusanyaji wa mapato LGRCIS, badala kutumia mfumo mpya wa ukusanyaji wa mapato wa TAUSI.
Tatizo hili lilihusishwa na kushindwa kusajili vyanzo fulani vya mapato kama vile ushuru wa hoteli, ada za huduma za machinjio, ada za leseni za uchimbaji wa vifaa vya ujenzi, na vibali vya ujenzi ndani ya mfumo wa TAUSI, hali ambayo ilizuia ukusanyaji wa mapato kwa ufanisi kupitia TAUSI.
Uzoefu wa halmashauri
Ili kupata uzoefu, The Chanzo imetembelea moja ya halamshauri kuelewa nini hasa ni changamoto. Ripoti ya CAG ilionesha, Halmashauri ya Wilaya ya Bahi ilikusanya kiasi cha Shilingi 32,039,329, kwa kutumia mfumo wa zamani.
The Chanzo iliweza kuzungumza na Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA katika Halmashauri hiyo Auson Augustine ambaye alieleza baadhi ya changamoto, ikiwemo za kiufundi.
“Wakati tunaanza kuutumia mfumo kuna baadhi ya vyanzo vilikuwa vinaendelea kufanyiwa maboresho ,” alieleza Augustine akiongea na The Chanzo ofisini kwake Septemba 04, 2025.
“Mpaka sasa hivi vyanzo vyote vimeshafanyiwa maboresho kwenye mfumo wa TAUSI na inakusanywa kwa kutumia TAUSI,”aliongeza zaidi.
Alifafanua zaidi kuwa wakati mfumo unaanza kulikuwa na vifaa vya kukusanya mapato ambavyo havikuendana na mfumo wa TAUSI, hivyo kulazimika kununua vifaa vingine ambavyo viliweza kuendana na mfumo huo.
“Kuhama kutoka mfumo za zamani na kwenda kwenye mfumo mpya yako mambo kadhaa hufanyika, ikiwemo upatanisho wa kifedha, kubadilisha vifaa vilivyokuwa vikitumika kwenye mfumo wa zamani na kuleta kwenye mfumo mpya,” aliongeza.
Mudrika Kassim Mjungu ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Serikali za Mitaa kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI sehemu ya fedha aliiambia The Chanzo suala la baadhi ya halamashauri kutokutekeleza maagizo inaweza kuletwa na mzoea na pia makusudi.
“Ukiona kasema Halmashauri imekusanya nje bila kutumia mfumo wa TAUSI maana yake tayari TAUSI ilikuwa inawezesha kukusanya kwa kutumia TAUSI,” alisema Mudrika wakati akiongea na The Chanzo ofisini kwake Septemba 10, 2025.
“Wakati mwingine Halmashauri wana ile kufuata mazoea, wanatafuta labda urahisi,” aliongeza.
Alifafanua, sababu ya kuacha kutumia mfumo wa zamani ni kutokana na madhaifu yaliyokuwepo, ikiwemo ya baadhi ya watumishi kuutumia mfumo kwa manufaa yao binafsi.
“Na hayo madhaifu kwa wakati mwingine yalikuwa yanatoa mwanya kwa baadhi ya watumishi kwenye Halmashauri,” alieleza Mudrika.
“Ilikuwa ni rahisi kuuchezea, anakusanya, anatumia na mfumo hauna ufuatuliaji wake. Kama Halmashauri ilitumia mfumo wa zamani kukusanya mapato ilikuwa ni ukiukwaji wa miongozo na maelekezo ya viongozi wa Serikali.”
Akiongea kwa njia ya simu na The Chanzo, mnamo Septemba 10, 2025, Mtafiti na Meneja Miradi wa Taasisi ya Wajibu Moses Kimaro alionya juu ya udhaifu unaweza kuwepo katika kutumia mifumo miwili.
“Yaani taarifa wanazo ‘manually’ zinaweza zikawa tofauti na zilizopo kwenye mfumo. Hiyo, inaweza kusababisha athari ya kutokuwa na taarifa sahihi kutokana na kwamba ‘reconciliation’ kati ya mfumo na taarifa zilizopo kwenye makaratasi zinaweza zikawa zinapishana,” alisema Kimaro.
Kimaro alisema, serikali inapaswa kufanyika tathmini, ili kubaini sababu ya Halmashauri kutotumia mfumo wa TAUSI na kutumia mfumo wa zamani wa ukusanyaji wa mapato. Kwa kufahamu changamoto ambazo Halmashauri ilikutana nazo hadi kuendelea kutumia mfumo wa zamani.
Hatari ya upotevu wa fedha za umma
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Serikali za Mitaa kutoka, TAMISEMI, Mudrika Kassim Mjungu anaonya juu ya hatari ya upotevu wa fedha za umma kama mifumo stahiki haitatumika.
“Kumekuwepo na upotevu wa fedha za Serikali za Mitaa pale ambapo wanahama kutumia mfumo ambao umeelekezwa. Wanatumia mifumo ya zamani ambayo siyo sahihi ambayo ni feki, wanatoa risiti ambazo hazitoki kwenye mfumo,” anaeleza Mudrika.
Aliendelea kueleza kuwa hali hiyo ipo kwenye Halmashauri nyingi na hufanyika zaidi kwenye vyanzo vya mazao hasa kwa wanaotumia mashine za POS, ambapo hutumia mifumo mingine ambayo ni feki.
“Lakini hayo yote yanafanywa na watumishi. Wito watumishi waendelee kufuata misingi pamoja na maelekezo ya Serikali. Maana yake wawe na nidhamu ya kazi wanazozifanya za usimamizi wa ukusanyaji wa mapato,” alisema.
Mudrika alisema, mara nyingi fedha zinapokusanywa ziko changamoto nyingine hujitokeza ya kutokupeleka benki, ambayo imekuwa ni changamoto kubwa katika Halmashauri.
“Kuna baadhi ya Halmashauri wamekuwa wakitumia fedha mbichi ambayo nayo ni changamoto. Viongozi wa Serikali wamekuwa wakisisitiza fedha mbichi zisitumike itumike fedha ambayo imeshapelekwa benki. Ili kuongeza udhibiti wa upotevu wa fedha kwenye mamlaka za Serikali za mitaa.”
Hata hivyo, alikiri kuwa mfumo ukiwa mpya na unavyojengwa mahitaji mbalimbali ya wadau yamekuwa yakijitokeza, hivyo kusababisha baadhi ya changamoto kama vile ya mtandao. Changamoto ambayo serikali inaeleza imepata utatuzi na mitandao kwa sasa inafanya vizuri.
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jaquelinevictor88@gmail.com .