Oktoba 11 ya kila mwaka, dunia huadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike, siku muhimu ya kutambua nguvu, uwezo, na changamoto wanazokabiliana wasichana kote ulimwenguni. Siku hii hutukumbusha kuwa, kama wazazi, walezi na jamii, tunayo nafasi ya kipekee ya kuwasaidia mabinti zetu kujiamini, kuota ndoto kubwa, na kuzitimiza bila hofu.
Hapa nchini kwetu, kulea mtoto wa kike haijawahi kuwa jukumu la mzazi peke yake. Kwa asili yetu, tumejifunza kulea kwa umoja. Msichana hukua akiwa amezungukwa na bibi anayemsimulia hadithi zenye mafunzo ya hekima, shangazi anayemshauri, dada mkubwa ambaye ni mfano wa kuigwa, walimu wanaomtia moyo, na majirani wanaomtazama kwa upendo. Utamaduni huu wa kijiji ni zawadi inayomjengea mtoto wa kike msingi wa kujitambua, kuthamini utu wake, na wa kutambua nafasi yake duniani.
Tunapomzunguka msichana kwa imani na upendo, tunamjengea uwezo wa kujiona kwa macho mapya. Anaanza kuamini kuwa ndoto zake zina thamani, kuwa sauti yake ni muhimu, na kuwa ana nafasi ya kuleta mabadiliko katika jamii yake. Lakini imani hii haiji kwa maneno, inahitaji vitendo, mifano hai, na mazingira salama yanayompa nafasi binti huyo kukua bila hofu.
Akina mama, walezi na wanawake tunaowazunguka mabinti zetu tunayo nafasi ya kipekee. Wanapotuona tukisimama imara katika maisha yetu, iwe ni katika kazi zetu, kwenye elimu, katika biashara, na hata mahusiano yetu na watu wanaotuzunguka wanajifunza kwamba wao pia wanaweza kuwa zaidi ya walivyowahi kufikiri hapo mwanzo. Hivyo basi, tuwe mifano mizuri ya kuigwa kwao.
Lakini, kijiji cha mtoto wa kike hakiko nyumbani tu. Kila msichana anakua ndani ya jamii yenye sura nyingi. Atakwenda shule, ataenda kanisani au msikitini, atakutana na vikundi vya watoto au vijana wenzake pamoja na vikundi vya wanawake.
SOMA ZAIDI: Vitu Tisa vya Kushangaza Kuhusu Watoto Ambavyo Hukuvijua
Huko atakutana na walimu wanaomtia moyo kuuliza maswali, majirani wanaomsikiliza kwa upendo, na viongozi wanaompa nafasi ya kushiriki na kutoa mawazo yake. Kila mmoja wao anachangia katika safari yake ya kujitambua.
Pia, kuna nguvu ya makundi rika, haswa wale akina dada waliowazidi umri. Wale wanaosimama na kusema, “Nilipitia hapa, na wewe utaweza,” pamoja na akina kaka wanaowashika mkono wadogo zao wa kike pale dunia inapowavunja moyo. Makundi haya huwaonesha mabinti hao kwamba ndoto zao haziko mbali na viganja vya mikono yao; ni matokeo ya ujasiri, bidii na imani isiyotetereka.
Kwa tafakuri hii, sisi kama jamii tunapaswa kuwajengea mabinti zetu vijiji hivi kwa makusudi. Tuwazunguke mabinti wetu na watu watakaowainua, tuwape nafasi ya kuzungumza, tuwasikilize na tuwatie moyo kuamini uwezo wao.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.