The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Fahamu Watoto Wanavyoomba Msaada Katika Kila Hatua ya Ukuaji Wao

Tukumbuke kwamba watoto kutuomba msaada si lazima watumie maneno.

subscribe to our newsletter!

Watoto wanapokua, njia zao za kuomba msaada hubadilika. Wakiwa wachanga, wanaomba msaada kwa kulia. Wakiwa vijana, mara nyingi wanaomba msaada kwa ukimya. Na sisi kama wazazi, walezi, ndugu, au watu wazima wanaowazunguka, tunapaswa kujifunza kusoma ishara hizo na kujibu kwa upendo na uelewa.

Tunapoelewa hatua mbalimbali za ukuaji, tunakuwa na nafasi nzuri ya kujenga uhusiano wa karibu na mtoto, uhusiano unaowasaidia kujenga ujasiri na kujua kwamba kuomba msaada si udhaifu, bali ni sehemu ya kukua.

Wakati mtoto bado mchanga, hawezi kuzungumza. Anajieleza kwa kulia, kujikunyata, au kukaa kimya kwa namna inayotuambia kuna kitu hakiko sawa. Wakati mwingine anataka chakula, wakati mwingine kubebwa au kubembelezwa. Katika jamii zetu, mara nyingi mtoto hubebwa mgongoni na mama, bibi au dada mkubwa. Hiyo ndiyo njia yao ya kusema, “nataka kuwa karibu na wewe.”

Wakati huu tunapaswa kuwajibu mapema na kwa upole, mtoto hujenga imani kwamba yupo mahali salama.

Kadri wanavyokua, watoto wanajifunza maneno, na pamoja na manneo hayo — hamu ya kusikilizwa. Umri wa miaka mitatu hadi sita ni kipindi ambacho mtoto anapenda kuonyesha kila kitu anachokifanya: akichora, akiruka, akicheza, au akiimba. 

SOMA ZAIDI: Siku ya Mtoto wa Kike Duniani: Kijiji Kinachomlea Binti ni Kipi Hapa Tanzania? 

Maneno “Mama, angalia!” au “Baba, ona!” yanakuwa sehemu ya maisha ya kila siku. Kwa mtoto, kusikilizwa na kuthibitishwa ni njia ya kuomba msaada na kutaka kuonekana.

Tunapowasikiliza, tujitahidi kuacha shughuli zetu kwa muda mfupi, na kuwajibu kwa upendo, ili kuwasaidia kujenga ujasiri. Wakati mwingine hawahitaji tuwape kitu chochote bali tu tuwaangalie na kuhimiza juhudi zao.

Watoto wa umri wa miaka 6-11 mara nyingi hawasemi waziwazi wanapokwama. Wengine wanasema tu “sijui” kwa hasira au hukataa kufanya mambo wanaoelekezwa kufanya. Wengine wananyamaza wakihofia kuchekwa au kuhukumiwa na wengine hunyamaza huku wakiweka juhudi kutatua changamoto zao wenyewe.

Kama wazazi hapa ndipo busara inapohitajika, na umuhimu wa kujua tabia za watoto wetu unaonekana hapa. Tunapaswa kujitahidi kuwauliza kama wanahitaji msaada pale tunapoona wamekwama kwa upole badala ya ukali. Ndivyo tunavyowajengea mazingira ya kuzungumza changamoto zao na hisia zao.

Umri wa miaka 11-17 ni wakati ambapo watoto wengi wanabadilika. Wengine wanazidi kuwa kimya, wengine wanakuwa wakali, na wengine wanajitenga. Hawatuambii tena “nisaidie” kama walivyokuwa wadogo, lakini hiyo haimaanishi hawahitaji msaada wetu. Kwa kweli, mara nyingi huu ndio wakati wanatuhitaji zaidi — lakini wanahitaji njia salama ya kuzungumza bila kuhisi kuhukumiwa.

SOMA ZAIDI: Vitu Tisa vya Kushangaza Kuhusu Watoto Ambavyo Hukuvijua

Tunapaswa kuwasikiliza kwanza badala ya kuwaambia cha kufanya moja kwa moja. Tunapowaonyesha kwamba tunaweza kuwasikiliza hata kwa yale mambo ambayo ni magumu sisi wazazi na walezi kusikiliza, tunawasaidia kufungua mioyo yao. Na tunapogundua mabadiliko makubwa ya tabia, hisia au mwenendo wao wa maisha, tunapaswa kuchukua hatua mapema si kwa hasira, bali kwa upendo na uwajibikaji.

Watoto wanapofikia umri wa miaka 18 na kuendelea njia yao ya kuomba msaada hubadilika tena. Wengine hupiga simu usiku kuuliza ushauri kuhusu mambo ya maisha na hata kabla ya kufanya maamuzi makubwa. Wakati huu, wanatuhitaji si kama watoa amri, bali kama wasikilizaji, washauri, na watu wanaowaamini.

Tunapaswa kuwajibu kwa heshima, kuwasikiliza kwa makini, na kuwapa uzoefu wetu bila kuwalazimisha kuufuata, ili kuwapa nguvu ya kufanya maamuzi yao wakihisi hawako peke yao. Hapa ndipo uhusiano kati ya mtoto na mzazi unakua kwa kina na kwa heshima.

Tukumbuke kwamba watoto kutuomba msaada si lazima watumie maneno.

Si kila mtoto atasema, “Nisaidie.” Wengine wataomba msaada kupitia macho yao, ukimya wao, au mabadiliko ya tabia madogo. Tukijifunza kusoma ishara hizo mapema, tutaweza kuwasaidia Watoto wetu na kujua kwamba kutuomba msaada si aibu bali ni haki yao.

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×