Dar es Salaam. Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDASA) imetoa tamko la kutaka matukio ya kuteka na kupoteza Watanzania kukomeshwa ili kunusuru taifa na madhara zaidi.
Tamko hilo lililotolewa mnamo Oktoba 24, 2025, limeangazia mazingira ya kisiasa na kiusalama likipiga kurunzi kwenye matukio ya utekaji yanayoonekana kushika mizizi Tanzania.
“Katiba ya Tanzania inaeleza kuwa Serikali na vyombo vyake vitakuwa na wajibu wa kutoa nafasi sawa kwa raia wote na kuhakikisha vitendo kama vile dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, na uonevu kwa raia wake vinadhibitiwa,” imeeleza taarifa hiyo.
“Kwa bahati mbaya, masuala ya utekaji, mauaji, na kupiga watu kinyama yamekuwa ya kawaida kwa miaka ya hivi karibuni. Je serikali na vyombo vyake vya dola wameshindwa kuyadhibiti kikamilifu matukio haya na hivyo kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kikatiba?”
Taarifa hiyo imenukuu ripoti ya Kituo cha Haki za Binadamu( LHRC) ambapo LHRC ilibainisha matukio takribani ya watu 87 kutekwa na kupotezwa.Taarifa hiyo pia inatoa angalizo kuwa ukosefu wa uweledi kwa upande wa yombo vya usalama wa raia hasa Jeshi la Polisi kunaweza kupelekea wananchi kukosa Imani na kuanza kujihami kwa kujichukulia sheria mkononi.
“Utekwaji na kupotezwa kwa watanzania wenzetu kumeonekana kubeba taswira ya chuki za kisiasa,” imeeleza taarifa hiyo. “Jambo hili halileti taswira nzuri kwa nchi yetu kwani linaharibu maana na mantiki nzima ya kuwa na demokrasia ya vyama vingi na utawala bora.”
Katika tamko hilo wasomi hao wametahadharisha hatari wanazoziona katika jamii: kwanza, uwezekano wa jamii kuwa ya watu wao wasioweza kutoa mchango na ubunifu wa kujenga taifa. Pili uwezekano wa Watanzania kuichukia serikali, jambo ambalo wanatahadharisha linaweza kuwa mwanya kutoa nafasi ya ushawishi wa maadui kutoka nje.
Pia wametahadharisha kuwa, matokeo ya vikosi vya watekaji kutumika kudhibiti wakosoaji inaweza kusababisha, watekaji hao kujikita mizizi kwenye mifumo yote ya kiutawala.
Wasomi hao pia wametahadharisha juu ya hatari ya nchi kupoteza uwezo wa kutambua viashiria vya kuibuka kwa makundi ya kigaidi na hata kufanya ugaidi kushamiri nchini. Wasomi hao wamependekeza kuundwa kwa tume ya kijaji au kamati ya kibunge