Wakati nikiwa mwanafunzi wa shahada ya kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, niliandika utenzi wa Mwanamke Stara. Una beti 19. Ulitokana na mwanaume fulani kuwa aliniona nikiwa mtu wa aibu.
Hivyo, nikandika utenzi wangu kumsihi mwanangu anayeenda kwenye ndoa kuwa mtaratibu maana ndiYo haiba ya mwanamke. Katika jitihada za kusoma waandishi Waswahili nikakutana na Utenzi wa Mwanakupona.
Nikashangaa kwa kiasi gani maudhui ya utenzi wangu yalifanana na wake, lakini uchanga katika uandishi na kwa kipaji haswa bado sijamfikia Mwanakupona. Utenzi wa Mwanakupona umechapishwa pamoja na Inkishafi na Fumo Liyongo kwenye Tenzi Tatu za Kale zilizohaririwa na M.M. Mulokozi (1999).
Utenzi wa Mwanakupona, anatueleza M.M. Mulokozi, ulichukuliwa tangu mwanzo kuwa ni unyango katika mfumo wa ushairi. Hivyo, umeathiri sana kimawaidha na kifani waandishi wa baadaye kama Shaaban Robert anapomuandikia binti yake Utenzi wa Hati baada ya kifo cha mkewe. Kwa miaka ya karibuni, taarab ya Kimasomaso, iliyoimbwa na Issa Matona, ni zao kabisa la aina hii ya tenzi.
Baada ya kuugua maradhi ambayo aliona haponi, inasemeka mwaka 1858 Mwanakupona Binti Mshamu alimuandikia utenzi mwanae wa kike, Mwana Hashima Binti Mataka, ambaye alikuwa hajafika umri wa kuolewa.
SOMA ZAIDI: Utendi wa Fumo Liyongo: Kama Watawala Hawataacha Kutengeneza Hila, Nasi Tuendelee Kubuni Mbinu za Ukombozi
Anafungua utenzi kwa kumuita bintiye ili atulie na asikie anayokusudia kumwambia. Kisha anamuelekeza kipengele kimoja kimoja cha maisha ya utu uzima: kuishika dini, jinsi ya kumtunza mume; na namna gani mwanamke anaujali mwili wake mwenyewe. Anamuelekeza ipi mipaka baina ya mume na mke ili ndoa yao idumu. Kisha anafunga kwa sala.
Kumlea mume
Maudhui yanayotawala ni vipi mwanamke anapaswa kumlea mume kama mtoto ili asipate sababu ya kugombana na kuachana naye. Anasema kwenye ubeti wa 36:
“Mpumbaze apumbae,
Amriye sikatae,
Maovu kieta yeye,
Mungu atakulipia.”
Anayajua mazingira ya wakati wake kwamba ustawi wa mwanamke hutegemea kuishi kwenye ndoa inayodumu. Mafeminia wanaweza kuisoma kwa juu juu na kuona Mwanakupona si mfano bora maana anaona mwanae ni wa kuolewa tu. Lakini kwa katikati ya kare ya 19 Pwani ilitawaliwa na wanaume, mwanamke angekimbilia wapi?
Tukumbuke asingeweza kuuza bidhaa mtandaoni, au kuandika andika tu maoni yake kuhusu wanaume kila mahali na mabwana wa mji huo wasimshukie. Hivyo, kama ustawi wa mwanamke upo kwenye ndoa, ni bora kuiendea ukiwa umedhamiria kuitunza.
SOMA ZAIDI: Inkishafi ya Sayyid Abdallah Bin Ali Bin Nasiri: Kutoka Utajiri Hadi Ufukara
Mwanakupona anaikumbuka miaka jinsi alivyoishi vizuri na mumewe. Bibi yetu huyu anatuasa kuwa wema kwa wenzi wetu. Mwanakupona ameweka wazi misingi ya talaka ni miwili: mke anayemdai mume matunzo kuliko kipato chake atalikiwe. Na mke anayeona kuishi na mumewe kutamtenga na kushika dini adai talaka. Leo tujiulize, kwani haswa mipaka ya mahusiano ya kimapenzi, ama ndoa, ni ipi?
Mwanakupona alikuwa mke mmoja kati ya wake wanne. Kulikuwa na uwezekano wa binti yake kuolewa kwenye ndoa ya mitara. Katika jamii yenye ustawi wa hali ya juu wanaume kuoa wake wengi na warembo kama alivyotuonesha Bin Nasiri kwenye Inkishafi haikuwa kitu cha kushtusha.
Je, kwa nini Mwanakupona haligusii kabisa suala hili? Au anaamini mchawi wa mtu ni mtu mwenyewe? Utaposoma utenzi huu tafadhali niambie nini mawazo yako kuhusu ukimywa wa Mwanakupona juu ya mitara.
Maisha ya Waswahili
Endapo kama umesoma Inkishafi, ni ngumu kujizuia kulinganisha na Mwanakupona katika kujenga taswira ya maisha ya Waswahili kwenye karne ya 19. Kwenye Inkishafi tunaelezewa miji, mabwana, watwana, utajiri na anasa za watu wa Pate.
Kwenye Mwanakupona tunatajiwa kwa majina mambo na vitu muhimu vya kufanya ili mwanamke na mwanaume kuwa nadhifu. Wakati Bin Nasiri anatuonesha kwa ujumla maisha ya watu wa tabaka tawala, Mwanakupona anatuonesha mila na desturi za kuutunza mwili kuanzia kuoga, kufusha na kujipamba.
SOMA ZAIDI: ‘Sanaa ya Ushairi’ Inavyomdhihirisha Shaaban Robert Kama Mshairi Mbobevu
Nimeambiwa nyumba aliyoishi Mwanakupona Lamu bado ipo. Hivyo, ukifika hapo umeshausoma utenzi wa Mwakakupona, na umeshaujua utajiri wa Waswahili uliosimuliwa kwenye Inkshafi, kwa kweli hutakuwa mwenda bure. Kuna chochote utaokota. Tujitahidi kutengeneza desturi za kutembelea miji kale ya Afrika Mashariki kuiona historia yetu.
Majukumu ya uzazi
Nilipogundua nimekaribia beti za mwisho za utenzu huu nilianza kufedheheka. Niliwaza mazingira ya Mwanakupona. Ikumbukwe alikuwa na maradhi yasiyopona. Kwa sababu ya maradhi, haijulikani kama Mwanakupona aliandika kwa mkono wake, au kwa msaada wa karani. Unaona akimlilia Mungu (beti 77-91) kana kwamba akiomba muujiza.
Aliandika utenzi huu wakati pia mume wake, Sheikh Mataka, aliyekuwa mtawala wa Siu, anapambana na watawala wa Omani waliokuwa na makazi Zanzibar. Kukaa katika hatari ya uwezekano wa vita kuanza muda wowote na ugonjwa hakukumzuia Mwanakupona kutimiza majukumu yake ya uzazi.
Na si mzazi kwa binti yake tu kwa sababu kati ya ubeti wa 90 hadi 96 anaelekeza utenzi huu kwa wanawake na watu wote ili waishi kwenye ndoa kadiri walivyoelekezwa na dini ya Kiislamu. Somo liwe kwetu sisi tunaobaki kutamani kuwa waandishi kwa madai ya kuwa na mambo mengi, ikiwemo majukumu ya kifamilia!
Kuna matatizo ya herufi yanayotokana na kuubadilisha muswada wa Mwanakupona kutoka hati ya Ajami (inayotumia msingi wa hati ya Kiarabu: Alif, Baa, Taa) kuingia kwenye hati ya kirumi (A, B, C). Labda kwa chapa zijazo wahariri wafuatilie na waone kama baadhi ya maneno ni ya kubadilisha.
SOMA ZAIDI: Kwaheri Amir Sudi Andanenga, Tanzania Itakukumbuka Daima
Kwenye utenzi huu, herufi ya kiarabu Qaaf imetumika mara nyingi. Kabla sijawaaminisha wasomaji kwamba neno lililoandikwa qaribu ni karibu, labda wahariri wanaweza kusema watu wa Lamu, kwa nyakati hizo, walilitamka kwaribu.
Utafurahia kusoma utenzi huu kwa sababu umeandikwa kwa lugha rahisi yenye kujaa ukarimu. Soma na utafakari ni nini wapaswa kumtendea mwenza, ama mtarajiwa, wako? Na je, wewe binafsi una sifa za kuwa mwenza, au mtarajiwa, mwema?
Diana Kamara hupenda kujitambulisha kama binti wa Adria Kokulengya. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia dianakkamara@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.