Msemaji Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Gerson Msigwa ametoa taarifa kuwa watumishi wote wa umma nchini Tanzania kufanyia kazi nyumbani siku ya Oktoba 30, 2025 isipokuwa wale ambao majukumu yao yanawahitaji kuwepo eneo la kazi.
Katika taarifa ya Msigwa ambayo imetoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi na kuchapwa kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram amesema uamuzi huo ni kufuatia angalizo la kiusalama lililotolewa na Jeshi la Polisi kwa wakazi wa Dar es Salaam.
“Aidha, waajiri katika Sekta Binafsi wanashauriwa kuzingatia tahadhari hiyo na kuwaruhusu watumishi wao nao kufanya kazi nyumbani,” imeeleza taarifa hiyo.
Imeeleza pia wananchi wasio na ulazima wa kutoka kwenye makazi yao wanashauriwa kufanyia shughuli zao nyumbani.
Oktoba 29, 2025 jioni mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IJP Camillus Wambura alitoa amri kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam kutotoka nje kuanzia saa 12 jioni, kama angalizo kufuatia vurugu kuripotiwa kwenye baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam siku ya zoezi la kupiga kura.
Ripoti mbalimbali zinaonesha kuwa yamefanyika maandamano maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mbeya, Arusha, Songwe na Shinyanga.