Huduma ya mtandao imerudishwa jioni ya Novemba 03, 2025, baada ya huduma ya huduma hiyo kusitishwa na serikali toka Oktoba 29, 2025, baada ya kuibuka kwa maandamano yaliyosambaa katika miji na majiji ya Tanzania.
Huduma ya mtandao imerudishwa ikiwa ni masaa machache toka uapisho wa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na makamu wake, Emmanuel Nchimbi.
Sehemu kubwa ya jumbe ambazo zinaendelea kusambazwa mtandaoni ni zile za watu kuomboleza juu ya wapendwa wao waliofariki kwa kupigwa risasi na watumishi wa vyombo vya ulinzi katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Shughuli za mazishi zimeshafanyika katika baadhi ya maeneo, hasa kwa kuzingatia mila na taratibu za kidini. Huku wengine wakiendelea kupanga misiba, hasa kutokana na ugumu uliotokea wa kusafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine.
Picha na video mbalimbali zinazo onesha majeraha ya watu waliofariki kwa kupigwa risasi pia zimeendelea kuwekwa mitandaoni. Sehemu kubwa ya picha hizo za kuogofya zikionesha vijana wa takribani miaka 17 mpaka 25.
Bado hakuna idadi rasmi ya watu waliofariki, baadhi ya mashirika ya kimataifa tayari wametoa angalizo kuwa idadi ya waliofariki inaweza kuwa kubwa.
Katibu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametoa tamko la kusisitiza juu ya umuhimu wa ustahimilivu.
“Nimesikitishwa na hali inayoendelea Tanzania, ikihusisha ripoti za vifo na watu kuumizwa katika maandamano,” ameeleza Guterres. “Natoa wito kwa wote kuwa na ustahimilivu, kukataa vurugu na kushiriki katika mazungumzo jumuishi na yenye kujenga ili kuzuia kuendelea kwa hali ya mvutano.”
Serikali kupitia Waziri wa Mambo ya Nje, Mahmoud Thabit Kombo imeeleza kuwa nguvu kiasi ilitumika kuwadhibiti waaandamanaji.