The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

ACT Wazalendo: Tunavizia Hisani ya CCM? Tunapaswa Kuwajibika

Ikiwa siasa ni tasnia inayohusisha hisia kali na za watu wengi, uamuzi wa kushiriki kwenye shughuli za Rais katika kipindi hiki kunajenga hisia kali za uasi na chuki kwa umma dhidi ya wanachama na chama chetu.

subscribe to our newsletter!

Nchi inafukuta! Ni vilio mtaani, vilio mtandaoni. Nchi ni kama imepigwa ganzi. Si wenye vyama, si wasio na vyama, si wanaojidanganya kwamba wao hawataki kujihusisha na siasa, si hata baadhi ya watu wa CCM, kote ni simanzi. Hatimaye wamebaini, ufedhuli hauna chama. Hata hivyo, walioketi kwenye viti vya enzi, wanajitoa ufahamu. Hawaoni machungu ya wananchi. Hawana soni. Wamejaa viburi.

Wakati yote haya yakiendelea, wakati tukiendelea kuomboleza, tukiendelea kuuguza vidonda na tukiendelea kufarijiana na machungu; wakati nimekaa zangu, nikitafakari zangu hatma na mustakabali wa nchi yangu, ninasikia chama changu cha ACT Wazalendo kipo Dodoma kwenye shughuli ya uapishaji wa Rais, siku ya tarehe 03 Novemba 2025.

Hakika suala na uamuzi huu wa kuhudhuria uapisho huo ulinifadhaisha sana. Sijawahi kuhisi kusalitiwa kisiasa kwa kiwango nilichohisi siku hii. Sijawahi kuhisi dharau ya kisiasa, kama kuona namna gani chama chetu kimewadharau wananchi siku hiyo. Sijawahi kujiona mjinga, kama kuona wakati wanachama tunahimizana “Mapambano Yaendelee”, kumbe pembeni kuna watu wengine, wana mapambano mengine yanayoendelea.

Wakati sote tukiwa waombolezaji kutokana na msiba wa kitaifa uliotokana na mauaji yaliyotokea kuanzia tarehe 29 Novemba 2025; wakati chama chetu kilichosimama imara na kufanya maamuzi sahihi kabisa na ya kishujaa, kuikabili CCM, licha ya ukweli kwamba tulitarajia uchaguzi utakuwa kituko na utanajisiwa kwa viwango visivyo mithilika, kikiendelea kuuguza vidonda vya uchaguzi; wakati ambao wanachama wanakabiliwa na kila aina ya hujuma, manyanyaso, mateso na purukushani za kiusalama, wakiwindwa kutokana na misimamo yao; wakati ambao viongozi wa chama katika ngazi mbali mbali na wagombea wetu nchini kote wakizongwa na kila aina ya changamoto za kiuchumi, kisiasa, kijamii na hata kisaikolojia, baada ya uchaguzi; wakati haya na mengine mengi yakiendelea hadharani na nyuma ya pazia, chama kinatuma wawakilishi kwenda kushuhudia uapisho wa Rais, ambaye kwa msingi huu Serikali na chama chake ndio msingi wa mateso yetu, kweli?

Inastaajabisha sana, kuona chama kinachukua uamuzi huu wa kushiriki kuapishwa kwa Rais, wakati ambapo hakijatoa tamko lolote kuhusu uchaguzi na mauaji yaliyotokea. Ni kweli kwamba, mpaka siku ya tarehe 03 Novemba, kinaweza kuwepo kisingizio kwamba nchi ilikuwa imefungwa na hivyo viongozi walishindwa kuwasilisha tamko la chama kwa wakati, lakini, kama kweli nchi ilikuwa imefungwa kiasi hicho, ilikuwaje wawakilishi hawa wakafanikiwa kufika kwenye shughuli ya uapisho, tena ndani ya Ikulu?

Kwa kuwa mpaka saa hii chama hakijajitenga na uwakilishi huu, wala viongozi hawajatamka kwamba wawakilishi hao wameenda katika uapisho huo pasipo ridhaa yao, inatafakarisha zaidi kuhoji kwamba viongozi walioshindwa kukaa kujadiliana kuhusu mustakabali wa kitaifa na kutoa tamko, wameweza kujadiliana na kukubaliana na wawakilishi hawa kwenda kushuhudia shughuli hizo za uapisho?

SOMA ZAIDI: ACT Wazalendo: Miaka 11 na Dira ya Mapambano ya Ukombozi wa Umma

Bila shaka maswali na hoja ni nyingi. Ni kwa nini tumeenda kwenye shughuli za kuapishwa kwa Rais mpaka sasa ni fumbo. Kwa fumbo hili viongozi wa chama wanapaswa kutusaidia kulifumbua. Hata hivyo, fikra kuu inayotawala fumbo hilo ni kwamba mahudhurio yetu yanakusudia kupata “hisani” ya ruzuku na viti maalum. Swali kuu hata hivyo, je hisani hii ina tija? [Is it worth it?] Hakika viongozi wetu watakuwa na majibu katika hilo.

Pamoja na majibu yao, haituondolei haki, wajibu na uhalali kwa wanachama kuwa na mtazamo katika hilo, hususani ukizingatia suala hili bado halina taarifa rasmi ya kupata baraka zote za chama. Katika tathmini yangu, uamuzi huu hauna tija kwa chama kisiasa hata kidogo. Uamuzi huu wa kushiriki katika kuapishwa kwa Rais ni kuianza miaka mitano mipya ya kiutawala kwa mguu mbaya. Uamuzi huu unaendelea kutubagaza na unaendeleza mtazamo hasi unaofungamanishwa na chama chetu, wa kujihusisha na “siasa za sahani” na si siasa za matumaini na siasa za umma na ukombozi.

Ikiwa siasa ni tasnia inayohusisha hisia kali na za watu wengi, uamuzi wa kushiriki kwenye shughuli za Rais katika kipindi hiki kunajenga hisia kali za uasi na chuki kwa umma dhidi ya wanachama na chama chetu. Ni tathmini na imani yangu kwamba hisia za mapenzi na matumaini yeyote yaliyopo kwa chama chetu, hata kama ni madogo kiasi gani, yamenajisiwa kwa viwango vikubwa zaidi na uamuzi huu wa kushiriki uapisho wa Rais, ambaye ametangazwa kwa kila aina ya mizengwe, hususani ukizingatia mgombea wetu wa Urais, Ndugu Luhaga Joelson Mpina amezuiliwa kugombea kinyemela na kesi yake ikiwa Mahakama ya Rufaa.

Kutokana na hili tunapaswa kuwajibika haraka sana, ili kurejesha na kujenga hisia na mahusiano yeyote chanya na umma wa Tanzania. Katika kuwajibika, iwapo tuna dhamira ya kweli na dhamira yeyote ile ya kujenga mahusiano yetu na umma wa Tanzania na kufikia ukombozi wowote ule wa kuondoka na udhalimu unatokana na Serikali ya Chama cha Mapinduzi, hatua zifuatazo zinapaswa na ninapendekeza zichukuliwe:

1.      Viongozi wawili waliokiwakilisha chama katika shughuli za kumuapisha Rais wajiuzuru au wavuliwe nyadhfa zao zote walizokuwa nazo haraka sana. Pamoja na hayo, viongozi hao wanapaswa kupewa likizo ya kushika wadhfa wowote wa kiongozi ndani ya chama katika kipindi chote cha miaka mitano, ikiwemo nafasi za uwakilishi wowote wa chama katika Serikali, bungeni au popote pale;

2.      Viongozi wakuu wa chama watoe kauli kulaani kitendo cha viongozi hao kushiriki shughuli ya kuapishwa kwa Rais na watueleze bayana wamehusika vipi na viongozi hao kwenda kuhudhuria na kushiriki shughuli ya uapishaji wakati nchini kote wanachama wanasubiri tamko la chama kuhusu yaliyofanywa na inayoitwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Vyombo vya Ulinzi na CCM katika uchaguzi huu;

3.      Katibu Mkuu, Ndugu Ado Shaibu, awajibike na ajiuzuru mara moja wadhfa wake, kwa kuwa, viongozi waliohudhuria wote wawili hutokana na mapendekezo na uchaguzi wake. Kushindwa kuwajibika kutokana na makosa ya watendaji wake, iwe wametumwa na chama au la, kunapelekea chama chetu kuendeleza uongozi butu, dhaifu na unaolea ujinga, kama inavyofanywa na ulivyoasisiwa na CCM;

4.      Vile vile, Kiongozi wa Chama ajiuzuru mara moja, kwa kuwa yeye kama kiongozi mkuu wa siasa, mshauri na mwelekezaji mkuu kwa viongozi wote na maafisa wa chama; anapaswa kuwajibika kwa hatua hii. Ni imani na uelewa wetu kwamba jambo hilo haliwezi kufanyika bila ridhaa yake; kwa maana hiyo, Kiongozi wa Chama ameridhia kitendo hicho wakati wanachama wetu wengi wakiwa katika vituo mbali mbali vya polisi, na wengine wengi wakiwa wamekimbia nyumba zao kwa ajili ya kunusuru maisha yao;

5.      Inapaswa viongozi wote wa Ngome ya Vijana kujitafakari na kuwajibika na kuwajibishana, kutokana na ukimya wao katika kipindi hiki ambapo vijana wengi kuuliwa na kudhurika, kwa kuchukua uamuzi wa kishujaa kusimamia haki na wajibu wao kwa taifa, kudai ukombozi wa nchi yetu, ama kwa kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi au kueleza hisia zao kwa namna yoyote ile;

6.      Sisi wanachama pia tunawajibu wa kusimama na kuwajibika kukilinda chama chetu na taifa letu. Tunapaswa kuushinikiza uongozi na kukishinikiza chama chetu kujiepusha kujihusisha na uongozi huu wa CCM usiokuwa na haya, usiojali maumivu wananchi wanaopitia na kuishia kutoa kauli za dharau, kebehi, vitisho na zisizo za faraja, busara wala matumaini ya kuijenga nchi yetu. Tunapaswa kuhakikisha Chama chetu hakijengi uswahiba na serikali na watu wote wasiofadhaishwa wala kuumizwa na damu za Watanzania zilizomwagwa, kwani kufanya hivyo ni kuwadharau na kuwasiliti wananchi, ambao ni wahanga wa udhalimu wa serikali hii;

7.      Chama kinapaswa, bila kupepesa macho na kwa ukali wote, kulaani yaliyotokea na kueleza pasipo kificho kwamba serikali hii ndio inawajibika na madhila yote yaliyotokea. Pamoja na kufanya hivyo, inapaswa chama chetu kusimama upande wa umma na sio upande wa watawala; na inapaswa kufanya haya kwa kujiepusha na kujihusisha na “siasa za mezani, sahani na kinywani”.

SOMA ZAIDI: Hatimaye ACT-Wazalendo Wanatoka Mafichoni?

Rai yangu kwa wanachama wenzangu, hususani ambao kama mimi wanakereka na kuchoshwa kuitwa CCM B ili hali tunaichukia CCM kwa akili, nguvu, nafsi na kila kitu chetu; tuna jukumu la kukataa na kukemea mienendo yote inayotuhusianisha na “U-CCM”. Tunajukumu la kijamii na kisiasa la kuungana na kuunganisha nguvu na vijana wa Tanzania, pasipo kujali ufuasi wa vyama vyetu, ili kuhakikisha tunaijenga Tanzania mpya – Tanzania ya haki, uhuru, maendeleo kwa wote na uchumi imara wa kitaifa na kwa wananchi; kujenga Taifa la Wote kwa Maslahi ya Wote!

Rai yangu kwa vijana wenzangu wa ACT Wazalendo na Tanzania kwa ujumla, tunapaswa kukumbuka na kuyaishi maneno na rai ya Mwalimu Nyerere alipokuwa akiaga Umoja wa Mataifa mwaka 1985:

“To be silent when we see danger, to refrain from attacking policies which we see contrary to the interests of peace and justice; to do these things would be to surrender our freedom and dignity. That, we shall never do!”

“Kunyamaza tunapoona hatari, kujizuia kushambulia sera ambazo tunaona zinapingana na maslahi ya amani na haki; kufanya hivyo itakuwa ni kujisalimisha uhuru wetu na heshima yetu. Hayo, hatutafanya kamwe!”

Jasper “Kido” Sabuni ni mwandishi wa kitabu cha “Love Chronicles”, wakili na pia ni mwanachama wa Chama cha ACT Wazalendo. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia kidojasper@gmail.com au X kama @JasperKido. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×