Dodoma. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetoa orodha ya majina ya wabunge wanawake wa viti maalum 115 kati ya 116, huku ikibakiza nafasi moja ambayo jina litatangazwa baada ya kufanyika uchaguzi jimbo la Fuoni na jimbo la Siha uliohairishwa.
Katika orodha iliyotolewa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepata viti 113 huku Chama cha Ukombozi wa Umma(CHAUMMA) kikipewa viti viwili.
Waliopata viti hivyo kwa upande wa CHAUMMA ni Devotha Minja ambaye aliyekuwa mgombea mwenza wa Salum Mwalimu katika kiti cha urais kupitia chama hiko. Mwingine ni Sigrada Mligo aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Njombe Mjini.
Kwa upande wa wabunge wateule 113 wa CCM yapo majina ya waliokuwa Wabunge katika kundi la Wabunge 19 wanawake waliofukuzwa uanachama CHADEMA . Wabunge hao ni pamoja na Cecilia Pereso na Salome Makamba.
Kwa upande mwingine pia aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo la Segerea Bonnah Ladislaus Kamoli kupitia CCM kipindi 2015-2025, na kukwaa kisiki katika uchaguzi wa mwaka huu naye anarejea bungeni tena kama mbunge wa viti maalum.
Mwenyekiti wa UWT Taifa Mjumbe wa Kamati Kuu, Marry Pius Chatanda naye ameteuliwa kuwa mbunge wa viti maalum kupitia CCM.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesema uteuzi huu umefanywa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 66(1)(b) na 78(1) pamoja na Sura ya 112 ya Sheria ya Uchaguzi wa Urais, Wabunge na Madiwani namba 1 ya mwaka 2024.
Kikao cha kwanza cha Bunge la 13 kinatarajia kufanyika jijini Dodoma Novemba 11, 2025 ambapo moja ya shughuli zitakazofanyika ni uchaguzi wa Spika, uapisho wa wabunge, kuthibitisha jina la Waziri Mkuu na ufunguzi rasmi wa Bunge.