Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala Ndogo ya Dar es Salaam, imeahirisha kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, baada ya Magereza kushindwa kumfikisha mahakamani kwa sababu za kiusalama.
Kesi hiyo awali ilipangwa kuendelea leo Novemba 10, 2025, baada ya kuahirishwa tarehe 3 Novemba 2025 kutokana na changamoto za kiusalama.
Kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa mahakamani, hali ya utulivu katika maeneo ya Dar es Salaam, Ruvuma na Mbeya imechangia kushindwa kwa mashahidi kusafiri na kufanya maandalizi ya shauri hilo.
Upande wa mashtaka uliomba mahakama kuahirisha kesi hiyo kwa mujibu wa Kifungu cha 302(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20, kama ilivyorekebishwa mwaka 2023, na kuomba muda wa siku 14 zaidi kwa maandalizi.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, mahakama ilikataa ombi la upande wa mashtaka kuhairisha kwa siku 14 na kuamuru kuahirisha kesi hiyo hadi Jumatano, Novemba 12, 2025.
Aidha, mahakama imeagiza hati ya wito itolewe ili kuhakikisha Tundu Lissu anafikishwa mahakamani siku hiyo kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wa ushahidi.