Baraza Kuu la Waisalamu Tanzania (BAKWATA) kwa kushirikiana na taasisi washirika limetoa tamko juu ya matukio yaliyotokea toka Oktoba 29.
“Siku ile ya kupiga kura kulizuka genge lililokuwa likiwatisha watu kwa kupora mali na kuharibu mali pamoja na miundo mbinu mbalimbali. Kutokana na vitendo hivi vya kihalifu ambao vililazimu vyombo vyetu vya usalama kudhibiti hali hiyo ndani yake kukatokea vifo vya watu wasio na hatia na wengine kupata ulemavu wa kudumu,” ilieleza taarifa hiyo ikijaribu kujenga hoja juu ya mauaji yaliyotokea nchini.
Taarifa hiyo iliyosomwa na Sheikh Issa Othman ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Ulamaa imeitaka serikali kuchukua hatua dhidi wa vinara wa matukio yaliyotokea toka Oktoba 29.
“Lakini pia sisi kwa umoja wetu, tunaitaka serikali ifanye uchunguzi wa kina juu ya kina nani ndio walikuwa vinara wa kuchochea vijana wetu katika kufanya uharibifu huu mkubwa kuwahi kutokea katika nchi yetu, mpaka kufikia maisha ya watu kupotea,” imeeleza taarifa hiyo.
Katika taarifa hiyo BAKWATA imeendelea kusisitiza juu ya falsafa yake kuwa amani inaanza na haki ndiyo inafuatia, ambapo BAKWATA imeonya juu ya kuitwa wajinga.
“Siku zote tumekuwa mstari wa mbele katika kusimamia na kuhimiza amani katika nchi yetu. Hata pale ambapo kufanya hivyo kunapokuwa kunatulazimu kukubali maumivu makubwa lakini tulikuwa tayari kufanya hivyo,” taarifa hiyo inasisitiza. “Tunataka tueleweke na viongozi wa dini wenzetu kuwa sisi siyo wajinga na hatuwezi kuwa wajinga kwa sababu ya kuzungumzia na kuhimiza amani na mwisho kabisa tunatoa pongezi.”
Taarifa hiyo imehitimishwa kwa pongezi kwa Rais Samia, makamu wake na viongozi wengine wa serikali.