Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC) limetoa tafakari yake juu ya matukio yaliyotokea kuanzia Oktoba 29, 2025, ambapo Baraza hilo limeshauri kuwepo na uchunguzi huru utakaoundwa na timu ya wadau kutoka nje na ndani ya nchi, kuchunguza matukio ya mauaji, ambayo Baraza hilo imeyalaani vikali.
Katika taarifa hiyo iliyosomwa leo Novemba 15, 2025, na Rais wa Baraza hilo, Askofu Wolfgang Pisa, TEC imeeleza uchambuzi wake juu ya sababu zilizopelekea maandamano, ambapo imeainisha sababu tatu:
- Matukio ya utekaji, mauaji na kuumizwa kwa raia: “Kumekuwepo na matukio ya waziwazi ya mauaji, utekaji,kupigwa na kuumizwa kwa raia bila kuwepo na nia thabiti ya kukomesha maovu hayo ambayo ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 14,” tamko la TEC linaeleza. “Haki hii [ya kuishi] imethibitishwa kukiukwa na vyombo vya ulinzi na “Wasiojulikana” ambao wanaonekana wana nguvu kuliko vyombo vya dola.”
- Kukosekana demokrasia ya kweli ya namna ya kuwapata viongozi: Tamko hilo limeeleza kuwa hali ya chaguzi kukosa ushindani wa haki, ukweli, uwazi, uhuru na kuaminika limekuwa kilio cha muda mrefu tangu mwaka 2016, jambo ambalo wameliainisha kama kiini cha maandamano katika tafakuri yao.
- Utendaji wa baadhi ya mihimili ya dola: “Kwa kuchambua maandamamo, Baraza la Maaskofu limeng’amua kuwa hasira ya wananchi imechochewa pia na kukosekana mahali pa Raia kupeleka na kufanyiwa kazi malalamiko ya kukiukwa haki zao za msingi. Kwani baadhi ya mihimili inaingiliwa,” tamko hilo linaleza.
TEC imefanya tathmini pia juu ya hali iliyotokea kuanzia Oktoba 29, 2025, ambapo imeeleza kulikuwa na matumizi ya nguvu kupita kiasi, ikiwemo silaha za kivita.
“Hata katika vita huwezi kutumia kila aina ya silaha. Maandamano si vita lakini zimetumika silaha zinazotumika katika vita. Askari waliua ndugu zetu wasio na silaha holela na kwa ukatili mkubwa kama wanyama – kitu kinachotufanya tujiulize binadamu mwenye akili timamu anawezaje kufanya vitendo kama hivyo?” taarifa hiyo ilihoji.
TEC pia imeoneshwa kuguswa na taarifa kuwa baadhi ya majeruhi walikataliwa huduma za kitabibu, jambo ambalo wamelieleza kuwa ni jambo ovu. Katika taarifa hiyo Baraza la Maaskofu limetoa wito miili ya waliopoteza maisha kuachiliwa kwa ndugu na jamaa zao.
“Imethibitika kuwa baadhi ya waliopoteza maisha, miili yao haijapatikana. Inasikitisha ya kuwa baadhi ya watu walipotaka kuwazika wapendwa wao hawakuikuta miili yao. Tunaomba kama wadau wengine walivyokwisha omba kuwa ni hekima na busara kuwapatia wanafamilia miili ya wapendwa wao wakaipumzishe au kuisitiri kwa heshima kadiri ya imani ya dini, mila, desturi na tamaduni zao,” taarifa hiyo imeeleza zaidi.
TEC pia imetoa mapendekezo nane juu ya hatua za kuchukua kuliponya taifa ikiwemo kwanza Mamlaka kulaani mauaji yaliyotokea; wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kuwajibika au kwajibishwa; kuwepo na uchunguzi huru; viongozi kuishi maisha ya uadilifu na uwazi na kuwaachia waliokamatwa.
“Wale wote waliokamatwa kwa hila kabla na baada ya uchaguzi na kuwekwa mahabusu au mahali pasipojulikana waachiwe huru na bila ya masharti yoyote,” taarifa hiyo inaeleza.
Na kuendelea: “Kwa kuwa jambo hili limesababisha maafa tunashauri ufanyike uchunguzi utakaowashirikisha wadau wa ndani na nje. Wadau tunaowapendekeza watoke kwenye tume huru isiyofungamana na upande wowote kama jumuiya na taasisi za Kimataifa, Taasisi za dini, Asasi za kiraia na Wataalamu wa haki na mambo ya Kidemokrasia na Serikali iwe tayari kupokea na kufanyia kazi ripoti watakayoitoa.”
Baraza Maaskofu pia limesisitiza juu ya Katiba mpya na utawala wa sheria kwa kueleza kuwa ni vilio vimekuwepo miaka mingi, na kuhimiza serikali kusikiliza wananchi. Pendekezo la mwisho la baraza hilo ni wito wa kuwataka Watanzania kuendelea kusali kuiombea nchi haki, amani na uponyaji.