Hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kuunda Tume ya Uchunguzi ni mwelekeo mzuri, na inaweza kusaidia kuliponya taifa kwa maumivu yaliyotokea kuanzia Oktoba 29, 2025 mpaka sasa. Hata hivyo, muundo wa tume hiyo una shida, kwanza, kwa kukosa uwiano sahihi wa uwakilishi kulingana na asili ya mgogoro wenyewe.
Hadidu za rejea ni mada nyingine inayojitegemea, ni vyema kusubiri, na kuna swali endapo ripoti itafanywa siri au itatangazwa kwa umma kila mmoja aweze kuisoma na kufanya uchambuzi wake.
Kitendo cha kuunda tume kinaashiria hatua zimeanza kuchukuliwa kama Rais alivyoahidi siku alipohutubia Bunge jijini Dodoma Novemba 15, 2025. Lakini muhimu zaidi majina ya wajumbe, taaluma zao, na nafasi walizowahi kushika Serikalini, ni jambo linalojenga taswira kinzani na dhana ya kuunda Tume ya Uchunguzi.
Inapotokea taifa lipo katika mgogoro mkubwa kama huu, wananchi wanategemea chombo cha kutafuta ukweli, chombo kinachoakisi hisia na maslahi ya pande zote husika katika mgogoro, hasa walioathirika moja kwa moja na mgogoro, au hata wasioegemea upande wowote wanaoweza kuhoji bila kujali ni upande upi umetenda makosa, au upi umetendewa, na hata kukosoa msimamo rasmi wa Serikali.
Kwa mshangao wa wadadisi wa mambo, badala yake wameteuliwa wastaafu watupu wa nafasi nyeti Serikalini, wakiwemo majaji, mabalozi na wanajeshi, akiwemo aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, Stergomena Tax, wakati mgogoro ukitokea.
SOMA ZAIDI: Tanzania Baada ya Oktoba 29, 2025: Tunarejeshaje Kisiwa cha Amani?
Kwamba kwenye taarifa ya uteuzi hakutajwa kwa nafasi hiyo, akielezwa kuwa aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), inaashiria kwamba hata mwandishi wa taarifa kwa umma ameona haya kusema kuwa mteule huyo wiki iliyopita alikuwa bado Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!
Imani ya wananchi
Kwa sehemu kubwa ya maisha yao wajumbe hawa wamefanya kazi Serikalini na hata kuteuliwa na Rais katika nyadhifa tofauti, tena kwa nyakati tofauti. Utawatenganisha vipi na mfumo wa uongozi wa nchi unaolaumiwa kwa ukandamizaji?
Unawajengea vipi wananchi imani kwamba watatendewa haki wakati upo upande unaituhumu Serikali kuhusika na mauaji yaliyotokea? Huenda wastaafu hao ni waaminifu na hawana matatizo machoni mwa wananchi, lakini utaondoa vipi lawama kwamba ni tume ya funika kombe mwanaharamu apite?
Kwa kawaida, ghasia zitokanazo na uchaguzi huathiri zaidi wananchi wa kawaida – vijana, wanaharakati, wafuasi wa vyama vya upinzani, na makundi ya kiraia. Kitendo cha kuwaacha nje ya tume hiyo tayari kinaashiria kutengwa kwao, licha ya kuumia kwao katika mgogoro huo.
Haitakuwa kazi nyepesi kwa tume kuuaminisha umma kuwa imebeba maslahi ya kila aliyeumizwa na ghasia za kuanzia Oktoba 29, 2025 na kwamba itatenda haki katika kuhakikisha ukweli unapatikana.
SOMA ZAIDI: Oktoba 29, 2025: Tulichoka Hekima na Busara, Tukajaribu Ujinga, Tumeona Matunda Yake
Uwakilishi ungeweza kutanuliwa wigo kwa kuwaongeweza watetezi wa haki za binadamu, viongozi wa dini, wafanyabiashara, waandishi wa habari huru, madaktari, wasomi wa vyuo vikuu, wanasheria, na vijana.
Mitizamo ya kizamani
Ukisoma orodha ya wateuliwa unaweza kudhani ni kamati ya kufuatilia maslahi ya wastaafu. Ni kweli kwamba wastaafu wana utajiri mkubwa wa uzoefu na busara, lakini wana uwezekano wa kubeba mitizamo ya kizamani, au fikra zilizopitwa na wakati kulinganisha na changamoto za 2025-2030 na mbele zaidi ya hapo.
Migogoro ya kisiasa hulazimu kusikiliza watu wanaoweza kutoa changamoto kwa dhana, fikra na maoni ya kusogeza taifa mbele. Si watu watakaoshindwa kujiuliza na kuuliza maswali magumu na kupata mwangaza mpya mbele ya changamoto inayowakabili.
Ukiangalia safu ya wajumbe wa Tume ya Uchunguzi unaona kama vile unatafutwa uaminifu wa kisiasa, political loyalty kwa kimombo, kuliko kutaka kuibua ukweli, au kupata majibu ya kimageuzi.
Ukitathmini kwa makini, na kulinganisha na nchi nyingine zilizounda tume za maridhiano, utaona kwamba kinachofanyika ni Serikali kujisitiri zaidi kuliko kuponya taifa lililopitia maumivu yatokanayo na mvutano wa kisiasa.
SOMA ZAIDI: Wananchi Dar Waeleza Matamanio Yao Binafsi Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025
Ili kufikia malengo ya kweli ya maridhiano, lazima watu waongee kwa uwazi, ukweli, wajumuishwe kupitia makundi yao ya kijamii, pasipo hofu, kificho wala hila.
Mwaka 1995, wakati Afrika Kusini ilipounda Tume ya Ukweli na Maridhiano, aliyeteuliwa kuwa Mwenyekiti alikuwa hayati Askofu Desmond Tutu, ambaye alikubalika na kuheshimika ndani na nje ya Afrika Kusini.
Tume ile ilidumu mpaka 2002, na kufanikiwa kurejesha utulivu katika nchi hiyo tajiri zaidi Afrika, na baadaye zikafuata hatua nyingine. Hatusemi tumefikia ugumu waliopitia Afrika Kusini, lakini siku zote ni vyema kuazima mbinu za utatuzi wa migogoro ya ndani zilizofanikiwa katika nchi nyingine.
Kwa mfano, Rwanda, kupitia Mahakama za Gacaca (2001-2012). Vilevile, tume za usuluhishi Sierra Leone (1999-2004), Kenya (2008-2013) na Burundi, ambapo tume iliyoundwa 2014 bado inaendelea na kazi mpaka sasa.
Hiyo ni mifano michache tu barani Afrika, ukitathmini muundo wake utaona ulikuwa na uwakilishi mpana zaidi.
Uhalali dhaifu
Hatua ya kuundwa kwa tume iliyotangazwa na Mheshimiwa Rais Samia ni muhimu, lakini kuijaza wajumbe ambao wanaweza kuelezewa kuwa “wandani wa Serikali” kunadhoofisha uhalali wake. Hili lingeweza kuepukika.
SOMA ZAIDI: Wananchi Dar Waeleza Sifa za Mwakilishi Wanayemtaka Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025
Uponyaji unahitaji uaminifu, na uaminifu unatokana na ushiriki wa matabaka tofauti katika jamii, na usiokuwa na upendeleo. Hii ingeweza kuitwa Tume ya Wabobezi Waliostaafu baada ya kuitumikia Serikali kwa miaka mingi, lakini si tume inayoweza kutenda haki kwa uhuru. Na ripoti yao itabainisha yote ambayo umma unayajua na itachapishwa bila kificho?
Isitoshe, Tanzania haina historia nzuri ya tume zinazoundwa na Rais. Tume ya Haki Jinai iliyoteuliwa mwaka 2023 kutathmini mfumo wa utoaji haki nchini ilikamilisha kazi yake, lakini ripoti kamili haijawahi kuwekwa hadharani, kando na muhtasari uliochapishwa kwa madhumuni ya kuikabidhi kwa Mheshimiwa Rais.
Kimsingi, mmiliki wa ripoti ni aliyeunda Tume, siyo mwananchi anayelalamika; isipompendeza mmiliki anaweza kuiweka kabatini. Ni wazi kuwa mapendekezo ya Tume ile kama yangefanyiwa kazi hata kwa asilimia 25, baadhi ya matatizo yanayozungumza sasa, ikiwemo yale ya kuhusisha vyombo vya kuwalinda raia na mali zao, yasingetokea.
Na hili ndiyo tatizo letu la msingi, kwamba inapotokea changamoto tunafanya tathmini na tujifunze tulipokosea. Lakini baada ya kujifunza, hatutekelezi mapendekezo ili kuepusha changamoto isijirudie tena hata kama ni kwa namna nyingine.
Mwandishi wa makala haya ameomba utambulisho wake usiwekwe hadharani. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.