Dodoma—Mwaka 2016, Eliza Mathayo ,44, anayeishi Ng’hong’hona mkoani Dodoma alipoteza watoto wake wawili kwa ugonjwa wa selimundu. Alibahatika kupata watoto watano katika maisha yake, huku wanne wakigundulika kuwa na ugonjwa huo.
Katika hao waliosalia, wawili wakiwa na ugonjwa huo, mmoja wapo amegundulika kuwa na tatizo la moyo, hali ambayo imemlazimu kukatisha masomo.
“Wawili walifariki wamebaki watatu, inaniumiza sana,” alisema Eliza wakati akiongea na The Chanzo nyumbani kwake huku akijifuta machozi akiwa ameinamisha kichwa chini, Jumatatu ya Oktoba 13, 2025. Mbali na kupitia misukosuko hiyo, mume wake amemkimbia hali ambayo imemsababishia kupata matatizo ya kisaikolojia.
Kutokana na hali yake, mdogo wake anayeitwa Mariam ndiye anayemsaidia kwa kila kitu. Mariam ambaye alikuwa kavalia kilemba cha maua maua kichwani, shati la rangi ya ugoro, mweusi wa rangi, akiwa amekaa kwenye kiti cha rangi ya chungwa alielezea kiundani changamoto hii inayoikabili familia hii.
“IIivyofika 2016, watoto wanne walienda kulazwa kule hospitali ya rufaa ya mkoa , watoto wawili kweli tuliwapoteza,” alisema Mariam wakati akiongea na The Chanzo akiwa katika hali ya huzuni. Madaktari walivyopima wakasema ule ni ugonjwa wa Selimundu. Ila huyu ambaye ni mtoto wake mkubwa wakasema ana pia tatizo la moyo.”
Aliendelea kusema, mtoto huyo ambaye ameacha shule mwaka jana kutokana na ugonjwa huo, na kubainika kuwa na tatizo la moyo, moyo wake umetanuka, kwa mujibu wa maelezo ya madaktari.
“Tulipohamishwa kliniki ndiyo tumekwenda Hospitali ya Benjamin Mkapa walipompima, wakasema mishipa yake imetanuka sana. kwa hiyo inatakiwa afanyiwe upasuaji. Haikuwezekana, kulingana na hali yetu ya kiuchumi ni hafifu,” alisema huku machozi yakimlenga machoni.
The Chanzo iliweza kuongea na Olivia, ambapo alielezea pia hali yake: “Nasumbuliwa na ugonjwa wa selimundu pamoja na moyo. Nachoka sana,” alisema Olivia Charles ,18, ambaye ni mtoto wa Eliza, wakati akiongea na The Chanzo akiwa katika hali ya kudhofika mwili.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, ugonjwa wa selimundu ni ugonjwa wa kurithi ambapo mtoto hupata ugonjwa huu kwa kurithi vinasaba vyenye ugonjwa kutoka kwa wazazi wake; nusu kutoka kwa baba na nusu kutoka kwa mama. Ugonjwa huu unaaathiri protini aina ya haimoglobini, inayopatikana katika chembe chembe nyekundu za damu, ambapo kazi yake kubwa ni kusafirisha hewa ndani ya mwili.
Dalili kubwa la mgonjwa mmoja wa selimundu ni pamoja na mgonjwa kuwa na upungufu wa damu wa mara kwa mara, kupata maumivu sehemu mbalimbali za mwili kama kichwa, na viungo. Pia kupata shida ya kupumua kwa sababu mzunguko hafifu oksijeni, lakini pia kupata manjano, kifua au tumbo kuuma.
Maumivu ya familia
The Chanzo, iliongozana na Mariam na Eliza hadi kwenye makaburi ambayo watoto waliofariki walizikwa hapo. “Hili hapa kaburi linaloonekana ndiyo la huyo mtoto wetu alikuwa anaitwa Clen Simon Charles,” alisema Mariam akiwa katika hali ya uchungu. “Na hili hapa ndiyo huyo mtoto wetu alikuwa anaitwa Yusuph Simon Charles. Wote walifariki mwaka 2016 walipishana tu siku saba, ambayo ni wiki moja.“Najisikia vibaya,” alisema Eliza akiwa ameinamia makaburi ya watoto wake huku machozi yakimtoka.
The Chanzo ilitoa habari hii kwa njia ya video kupitia mitandao ya kijamii mnamo, Oktoba 13, 2025, ambapo pamoja na mambo mengine, iliweza kutoa namba rasmi za familia kwa wale wenye uwezo kuweza kusaidia familia hiyo.
Ugonjwa wa Selimundu unavyoitesa familia ya mama huyu: Mume amemkimbia, awaangukia Watanzania kwa msaada.
— The Chanzo (@TheChanzo) October 13, 2025
Unaweza kuwasiliana naye kwa namba 0684601059. pic.twitter.com/UzJ7LfzDwW
Baada ya habari hiyo kutoka, familia hiyo iliweza kurudi na kuwashukuru Watanzania kwa namna ambavyo waliweza kuwasaidia, ikiwemo kupatiwa mahitaji pamoja na bima.
“Baada ya stori ile kutoka ya tatizo la mtoto wetu Olivia pamoja na mwenzake Mary. Kuna baadhi ya wadau wemetusaidia kwa mambo mengi, wengine kwa maombi, wengine kwa fedha. Pia kuna msamaria mwingine amejitokeza kutupatia bima [ya afya], bima kubwa. Na bima hiyo itaanza kutumika, ndani ya mwezi ujao,” alieleza Mariam mnamo Oktoba 28, 2025.
“Lakini mpaka sasa kuna dawa ambazo mtoto wetu amemaliza tunahitaji tukazinunue. Ila kutokana na changamoto ya pesa hamna, kwa hiyo naomba wadau wenye mapenzi mema waniunge mkono, ili tukazifate kesho hizo dawa,” aliongeza zaidi.
Somo kubwa ambalo familia hii imejifunza juu ya ugonjwa huu ni umuhimu wa kujiweza kiuchumi, jambo ambalo mpaka sasa limebakia kuwa changamoto.
“Kitu nilicho jifunza kwenye huu ugonjwa wa selimundu, ukiwa unaishi huna hata hela, unaweza ukawakosa watoto. Kwa sababu homa inavyokuja huwa haiangalii mfuko wako una hela au hauna hela. Kwa hiyo unaweza ukawapoteza kabisa. Kwa hiyo kitu nilicho jifunza, inatakiwa tuwe imara [kiuchumi],” aliongeza Mariam.
Familia ya Eliza yenye watoto wenye ugonjwa wa Selimundu ambayo mume aliikimbia, yawashukuru Watanzania kwa msaada.
— The Chanzo (@TheChanzo) October 28, 2025
Unaweza kuwasiliana nao kupitia namba 0684601059. pic.twitter.com/21wmYaJEMi
Suala la Jamii Nzima
Takwimu rasmi kutoka Wiazara ya Afya, zinaonesha watu laki mbili nchini wana ugonjwa wa Selimundu (Sickle Cell) huku watoto Elfu Kumi na Moja (11,000) huzaliwa wakiwa na ugonjwa wa Selimundu kila mwaka.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoshika takwimu za juu duniani ikishika nafasi ya nne kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa selimundu ikitanguliwa na Nigera, India na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha kuwa zaidi ya watoto 300,000 huzaliwa na Sikoseli kila mwaka duniani.
Eliza, Mariam si wazazi pekee waliopoteza watoto wao kwa ugonjwa wa selimundu. Mfano, mwaka 2022 John Jeremiah, mkazi wa Dodoma, naye alipoteza mtoto wake wa umri wa miaka saba [7] aliyekuwa na ugonjwa wa selimundu.
“Alianza kuugua akiwa na miezi tisa, alikuwa akisumbuliwa na miguu na mikono. Tukajaribu kutafuta namna ya kwenda hospitali, tukafanikiwa kumpeleka hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma. Baada ya vipimo ikaonekana ana matatizo ya selimundu.”
Baada ya kuelezwa hali ya mtoto wake, na kupewa dawa za kutumia alisema haikusaidia, hivyo waliamua kwenda kwa mganga wa jadi kupata tiba. Christopher alikuwa ni mtoto wa kwanza kuzaliwa kati ya watoto wawili aliyokuwa nao John. Alisema enzi za uhai wa mtoto wake, walijitahidi kumpambania ili kuokoa uhai wake.
“Kila akiugua alikuwa anajisikia maumivu makali sana. Anasema miguu inauma ama mikono, alikuwa akilia kwa muda mrefu sana anasema nipulizeni tumbo au mikono au miguu. Anatuambia tafuteni kitambaa lowekeni kwenye maji mniwekee maana nasikia maumivu makali sana kwenye miguu au kwenye mikono,” alisema John.
Nikitazama hii picha ya mwanangu najisikia maumivu sana,” alisema Sophia Jeremiah ambaye ni mama wa Chris akiwa analia. “Nahisi hali yetu ngumu ya maisha labda tungekuwa na hela tungemsaidia huyu mtoto.”

Jamii Ifanyaje?
Akiongea na The Chanzo Oktoba 20, 2025 Daktari Bingwa Magonjwa ya Damu kutoka hospitali ya Benjamin Mkapa BMH Dk Stella Malangahe alisema, ugonjwa wa selimundu unapatikana kwa kurithis kutoka kwa baba na mama.
“Vyema kabla hatujaingia katika kitendo cha kupata watoto, ama pale tunapokutana na wenza wetu kupima na kujua hali zetu,” alisisitiza Dk Stella. “Endapo ukijua utaweza kufanya maamuzi sahihi ya eidha kuendelea, halafu mpate mtoto umtibie. Ama kutokuendelea na mahusiano hayo ambayo yanakuweka katika hatari ya kupata mtoto mwenye selimundu.”
Dk Stella alikiri kuwa, ugumu wa maisha wakati mwingine uchangia watoto wenye ugonjwa wa selimundu kuwa na changamoto za kiafya, na wakati mwingine kupoteza maisha.
“Ugumu wa maisha ni moja ya kikwazo ambacho tunapambana nacho kwa watoto wanaoathirika na ugonjwa wa selimundu,” alisema. “Selimundu ni ugonjwa wa kurithi, na ni wa kudumu, bila kupata matibabu ya kupunguza makali, mgonjwa huyu anakuwa ni mtu wa kuugua mara kwa mara.”
Mei 2023, Hospitali ya Benjamin Mkapa ilizindua rasmi huduma za Upandikizaji wa Uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa Selimundu. Takriban watoto 24 wamepandikizwa uloto mpaka sasa. Gharama za upandikizaji wa uloto kwa wagonjwa wa selimundu zinatajwa kuwa kati ya Shilingi milioni 50 kwa mgonjwa mmoja nchini, wakati nje ya nchi matibabu hayo ni Shilingi 120 milioni hadi 150 milioni.
Muanzilishi wa taasisi ya Tanzania Sicklecell Warriors Organization, Prinsila Chassama akiongea na The Chanzo kwa njia ya simu Oktoba 21, 2025 alisema, jamii inapaswa kuwa na muamko wa kutafuta elimu ya magonjwa mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa selimundu.
“Unapokuwa na elimu juu ya ugonjwa fulani inakusaidia kujikinga au kuepuka kutokuupata ule ugonjwa. Au hata kama umeupata kujua namna ya kuishi na ile chagamoto,” alisema “Jamii kwa ujumla ipo kwenye giza, watu hawajui ugonjwa wa selimundu. Unaweza ukawa unatoa elimu hapa au unafanya upimaji wa bure kabisa watu hawasogei wanajiona wao ni wazima.”
Olivia Anafariki
Mnamo Novemba 23, 2025, mwandishi wa makala hii alipokea taarifa za msiba wa Olivia Charles, binti wa miaka 18, ambaye tulimhoji kwenye makala hii mnamo Oktoba 13, 2025.
“Mama yangu wee, yaani Olivia wee. Najua Mungu umempenda zaidi Olivia, nilikuwa nampenda lakini wewe umempenda zaidi. Mungu mpokee Olivia. Umuweke mahala pema peponi, najua mwanangu hana kosa, alikuwa bado mdogo,” hii ni kauli ya Mariam Mathayo mama yake mdogo na Olivia, akilia kwa uchungu baada ya Olivia kufariki Novemba 23, 2025.
Hata hivyo, Novemba 19, 2025, Olivia alizidiwa na kupelekwa katika hospitali ya rufaa ya Benjamin Mkapa iliyopo mkoani Dodoma. “Ninakushukuru kwa wema wako, tazama Olivia tulikuwa tunampambania lakini hayupo tena. Nina kushukuru dada Jackline Mungu akupe wepesi, fanya sehemu na zingine uwii,” aliongeza Mariam huku akiendelea kulia kwa sauti akiwa msibani.

Olivia alikuwa akilia kwa maumivu makali akileza kuwa anasikia kama kuna kitu kinataka kutoka, kama haja ndogo bila chochote kutoka. Walivyomfikisha hospitali madaktari wakampokea na kumpa huduma ya kwanza kupunguza maumivu. Hata hivyo ilivyofika majira ya saa kumi jioni, waliambiwa wafike hospitali, ambapo walijulishwa kuwa Olivia ameshafariki.
Kwa sasa Eliza amebakiwa na watoto wawili, pamoja na simanzi na huzuni, anajitahidi kuifundisha akili yake kukubali ukweli wa mambo yanayoonekana, “Mungu amempenda zaidi.”

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jaquelinevictor88@gmail.com