Waziri wa Madini, Antony Mavunde, amekutana na kufanya mazungumzo na kaimu Balozi wa Marekani, Andrew Lentz, mnamo Januari 21, 2026, huku majadiliano makubwa yakihusu ushirikiano kati ya Marekani na serikali ya Tanzania katika kutafiti madini kinywe, maarufu kama Graphite. Ushirikiano katika mradi huo wa utafiti unatarajiwa kuhusisha Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).
“Kupitia STAMICO na GST tunakwenda kuimarisha uhusiano wetu. Lakini vilevile na kujenga uwezo za kiujuzi kwa watu wetu. Zipo leseni ambazo zinamilikiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), ambazo leseni hizi tunakwenda kufanya utafiti wa pamoja na wenzetu kupitia Wizara ya madini ya Marekani. Kubaini maeneo ambayo yatakuwa na uwekezaji mkubwa,” alieleza Mavunde akiongea Dodoma.
Na kuongeza: “Kwa hiyo tunategemea kupitia utaratibu huo, wa kufanya kazi pamoja na hasa kwenda kwenye utafiti wa kina itasaidia kubaini maeneo ambayo nchi yetu imejaaliwa rasilimali. Na mwisho wa siku kuja kupata mgodi mwingine mkubwa hasa katika maeneo ya mkoa wa Mtwara na Lindi ambapo zoezi hili limefanyika.”
Kikao hicho kinafanyika katika nyakati ambazo Tanzania inafanya jitihada kubwa katika kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia, kufuatia matukio ya Oktoba 29, ambapo, Marekani ilitoa tamko mnamo Disemba 04, kueleza kuwa inafanya mapitio ya mahusiano yake na Tanzania.
Akizungumza katika kikao hicho Lentz, ameeleza makubaliano juu ya utafiti huo ni sehemu ya mifano juu ya nia ya Tanzania kuendeleza mahusiano na Marekani. “Wakati Marekani ikiendelea kufanya mapitio ya mahusiano yake na Tanzania, inaendelea kuangalia fursa mbalimbali za kushirkiano kama tulivyofanya hapa,” alieleza Lentz.
Na kuongeza: “Tutaendelea kuangalia mifano ya wazi itakayoonesha dhamira ya Tanzania kushirikiana kwa dhati na Marekani katika kuongeza vyanzo vya upatikanaji wa madini adimu duniani.”
Madini ya Graphite yanatajwa kuwa sehemu ya madini 12 muhimu kwa ulinzi na NATO, na pia madini muhimu katika mabadiliko ya nishati kuelekea kwenye matumizi ya nishati safi hasa umeme. Baada ya China kutangaza kuzuia kwa kiwango kikubwa uuzwaji nje wa madini muhimu, ikiwemo Graphite, nchi za Magharibi zimekuwa zikitafuta suluhisho, ambapo nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania, zinaonekana kuwa mmoja ya mbadala hasa linapokuja suala la Graphite.
Jitihada za Kidiplomasia
Serikali ya Tanzania imeendelea kufanya jitihada kubwa za kidiplomasia, baada ya Marekani kutangaza kuwa inafanya mapitio ya mahusiano yake na Tanzania kufuatia matukio ya Oktoba 29, ikiwemo mauaji ya raia.
Sehemu ya jitihada hizi ni pamoja na Waziri wa Nje wa Mambo ya Nje kutembelea Marekani manamo Disemba 2025, ambapo alikutana na baadhi ya Wawakilishi wa Bunge la Marekani, hata hivyo hakufanikiwa kukutana na watendaji wa serikali moja kwa moja.
Tanzania pia imeingia mkataba wa miezi 24 na Kampuni ya Ervin Graves Strategy Group ya Marekani, inayoshughulika na masuala ya mikakati hasa ya kidiplomasia na siasa. Jukumu kubwa ililopewa kampuni hii ni kuwezesha serikali ya Tanzania kuwa kwenye ukurasa mzuri na serikali ya Marekani.
Baadhi ya mikakati ambayo kampuni hiyo inategemewa kuitumia ni pamoja na kulandanisha mahitaji ya madini adimu Marekani na fursa za madini hayo ndani ya Tanzania, yaani kutumia fursa hizi kama kichocheo cha mahusiano bora. Kampuni hiyo inatarajiwa kufanya ushawishi kwa wawakilishi wa Bunge la Marekani, lakini pia kwa watendaji wa serikali ya Trump, hasa juu ya kuiwezesha serikali ya Tanzania kuwa na nafasi nzuri zaidi kidiplomasia.
Wachambuzi wengi wanaangalia mkakati wa Tanzania juu ya kukabiliana na shinikizo la kidiplomasia baada ya matukio ya Oktoba 29, kuwa ni pamoja na mategemeo kuwa shinikizo la ndani litapungua lenyewe baada ya watu kusahau na kuendelea na masuala mengine. Hata hivyo jambao hili linaendelea kuwa ligumu kutokana na mpasuko wa kisiasa unao onekana Tanzania hasa baada ya matukio ya Oktoba 29 na siku zilizofuatia.
Mkakati mwingine unaongaliwa ni pamoja na serikali kutumia fursa zilizopo za kibiashara na rasilimali kama nyenzo za kuhakikisha kunakuwa na maelewano katika anga la diplomasia. Pia baadhi ya wachambuzi wanaangalia kuwa hofu ya nchi za magharibi kuiona China ikiongeza ushawishi wake zaidi ndani ya Tanzania, itafanya nchi hizi kupunguza makali ya mashinikizo ya kidiplomasia. Hata hivyo wengine wanaona mvutano unaoendelea duniani kati ya Marekani na Ulaya, pamoja na matukio mengine duniani, yanafanya matukio ya Tanzania kupitwa na mabadiliko ya nyakati katika anga la kimataifa.
Mshauri wa Rais wa masuala ya kidiplomasia, Lazaro Nyalandu, anategemewa kuwa Wahington D.C, Marekani kati ya Januari 20 mpaka Januari 23, 2026. Balozi Nyalandu anategemewa kufanya jitihada za kuwashawishi wawakilishi wa Marekani kutembelea Tanzania, lakini pia kujaribu kupata kundi la wawakilishi wenye ushawishi watakaoweza kuzungumzia masuala ya Tanzania. Sehemu kubwa ya wawakilishi ambao Nyalandu atajaribu kuweza kuwa shawishi ni wale wa chama cha Trump, Republican, ambao pia ni wajumbe wa kamati ya mambo ya nje ya Bunge la Marekani.