Mwandishi wa Habari, Kelvin Justine Raphael maarufu kama Zungu, amepewa onyo na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), kwa madai ya kukiuka maadili ya taaluma ya uandishi wa habari. Hii inakuja baada ya Zungu kuchapisha malalamiko yake juu ya ndege za ATCL kuchelewesha safari bila kutoa taarifa za kutosha.
Katika taarifa yake iliyotolewa leo Februari 23, 2026, Bodi ya Ithibati inaeleza kuwa ilimuita Zungu juu ya maudhui yake kabla ya kufikia uamuzi wa kutoa onyo.
“Baada ya kumwita na kumpa fursa ya kusikilizwa kwa mujibu wa taratibu, Bodi imejiridhisha pasipo shaka kuwa mwandishi huyo alitoa kauli zenye matusi, kejeli na lugha isiyo ya staha na isiyozingatia mizania kinyume na misingi na maadili ya taaluma ya habari,” taarifa ya Bodi ya Ithibati inaeleza.
“Mwandishi husika amekiri na ameomba radhi kwa makosa hayo. Hata hivyo, Bodi imemtaka kuondoa mara moja maudhui hayo katika majukwaa yote aliyoyachapisha, kuacha mara moja tabia hiyo, na kurejea katika misingi ya maadili, weledi na uwajibikaji wa taaluma yake,” taarifa hiyo iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Ithibati, Patrick Kipangula inasisitiza zaidi.
Katika machapisho aliyoyaweka mnamo Februari 22, 2026, katika kurasa zake binafsi za mitandao ya kijamii, Zungu ali-ilalamikia ATCL kuchelewesha safari, jambo ambalo lilimuathiri binafsi ikiwemo kumkosesha fursa kubwa ya kiuchumi.
Baada ya taarifa hiyo ya Bodi ya Ithibati, Zungu ameandika katika ukurasa wake wa Instagram kuwa wamekuwa na kikao kizuri sana cha kujenga na kupata elimu. Wakili William Maduhu, wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ametoa maoni yake juu ya hatua hiyo ya Bodi ambapo ameeleza kuwa ina ukakasi wa kisheria.
“Zungu kulalamikia ndege kuchelewa, nafikiri alikuwa anatoa maoni kama raia, kama mteja wa ATCL. Kwa hiyo alikuwa na haki na wajibu wa kutoa malalamiko yake. Ndiyo maana taarifa hii kaichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram ambao kisheria hauhitaji Ithibati yeyote,” anaeleza Wakili Maduhu.
“Bodi haina Mamlaka ya kujielekeza yenyewe kutoa onyo, yaani Mamlaka ya kisheria haina,” anaeleza zaidi Wakili maduhu.
“Mtu ambaye anahisi kutendewa jambo baya ndiye anapaswa kuwasilisha malalamiko kwenye vyombo husika. Bodi ikishakaa , ikasikiliza hayo malalamiko au Baraza likaka, halafu likamkuta mwandishi ana hatia na ikampa adhabu ya kufuta labda leseni au onyo; kazi ya Bodi itakuwa kutekeleza maagizo ya Baraza au maagizo ya Bodi,” anafafanua zaidi Wakili Maduhu.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 12(1) cha Sheria ya Huduma za Habari (2023), Bodi ya Ithibati ina wajumbe saba ambapo kwa sasa Mwenyekiti wao ni Tido Mhando. Wajumbe wengine ni pamoja na Msemaji Mkuu wa Serikali, mjumbe kutoka taasisi za elimu ya juu, Katibu wa Baraza la Habari, mjumbe kutoka vyombo vya habari binafsi na mjumbe mwingine kutoka vyombo vya habari vya serikali pamoja na mjumbe kutoka Azaki.
Wakili Maduhu anaeleza kuwa jukumu la kutoa onyo au hatua zozote zingefanyika baada ya Bodi hii kukaa, na sio kwa taarifa ya moja kwa moja ya Kaimu Mkurugenzi wa Bodi.
“Mimi ningemshauri kwamba naweza kuwa Wakili wake, tuyalalamikie haya maamuzi ya Bodi ya Ithibati kwa mfumo wa mapitio Mahakama Kuu, kwamba Bodi imejielekeza isivyo, kwa kutumia Mamlaka ambayo kisheria haina. Hata kama wametoa tu onyo, akinyamaza, akisema aiache hivi hivi kuna siku watamfutia leseni kabisa,” anafafanua zaidi Wakili Maduhu.
Shirika la Ndege la ATCL lilitoa taarifa mnamo Februari 22, 2026, na kueleza kuwa ndege yake aina ya Boeing 737-9 MAX yenye nambari TC 102, ilishindwa kutua uwanja wa ndege wa Mwanza mnamo Februari 21, 2026, kutokana na hali mbaya ya hewa, ambapo kwa mujibu wa ATCL ndege hiyo ilielekezwa kwenda uwanja wa KIA. Shirika hilo liliomba radhi kwa abiria waliokumbwa na kadhia hiyo.
Katika taarifa yake Bodi ya Ithibati imeonya kuwa mwandishi husika akirudia, Bodi hiyo haitasita kuchukua hatua kali zaidi za kinidhamu, ikiwa ni pamoja na kusimamisha au kufuta ithibati yake.