The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Uraibu wa Tramadol: Janga Linalonyemelea Familia za Kitanzania Kimya Kimya

Uholela wa kutumia dawa tiba ya Tramadol yenye asili ya kulevya imewaingiza Watanzania wengi kwenye hali ya uraibu

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Usiku wa saa sita, Magreth Isaya [sio jina lake halisi] mwenye umri wa miaka 40 na mama wa mtoto mmoja, alianza kusumbuliwa na maumivu makali ya vidonda vya tumbo. Usiku huo, huo alikimbizwa hospitali kupatiwa matibabu, na ili kupunguza maumivu hayo Magreth alilazimika kuchomwa sindano ya Tramadol.

Magreth anaeleza kuwa baada ya kuchomwa sindano alipata nafuu, ambapo baada ya siku tat alirudi nyumbani.Hata hivyo baada ya mwezi mmoja kupita, Magreth anasema alianza kusikia tena maumivu makali ya vidonda vya tumbo.

“Nikaenda tena hospitali wakanichoma sindano ya Tramadol, wakanipa na vidonge. Walinipa vya siku tano, wakaniambia nikisikia maumivu niwe nakunywa kimoja mara mbili, kwa hiyo asubuhi na jioni,” anasema. “Kwa hiyo nikachoma hiyo sindano, nikapewa na vidonge nikarudi nyumbani.”

Tramadol ni dawa ya kutuliza maumivu inayotumika kupunguza maumivu ya wastani hadi makali. Mara nyingi hutumika kwa watu wanaoumwa Kansa, Selimundu na magonjwa mengine yanayo sababisha maumivu makali.

Kutokana na ahueni aliyoipata punde tu baada ya kutumia Tramadol, taratibu Magreth akaanza kufanya utumiaji wa Tramadol kuwa mtindo wa maisha. Hakuhangika tena kufuata maelekezo ya daktari.

“Nikawa nikisikia tu maumivu nakunywa vile vidonge. Kwa hiyo nikawa nimejua kumbe nikiumwa vidonda, nina uwezo wa kwenda kununua Tramadol, nikanywa nikapata nafuu,” anaeleza Magreth akiongea na The Chanzo Januari 19, 2026.

“Kwa hiyo baadaye sasa nikawa naenda mwenyewe kununua vile vidonge, nilikuwa nanunua kila siku nilikuwa nanunua vidonge vitano kwa Shilingi 1000. Kwa hiyo mimi nilikuwa nakunywa viwili siyo kimoja sasa.”

“Nilikuwa nakunywa viwili asubuhi, viwili jioni basi nikawa sasa siendi tena hospitali. Kwa hiyo nikinywa hivi vidonge, vidonda haviniumi kabisa . Basi nikawa naenda ‘pharmacy’ nanunua vile vidonge, nakunywa asubuhi na jioni. nilikuwa nikiamka tu kwenye kitanda lazima ninywe vidonge viwili,” anaendelea kueleza akiongea na mwandishi wa The Chanzo.

Anapata Uelewa

Magreth anakumbuka wakati ambao alimpeleka mama yake hospitali, baaada ya kufika hospitali, kwa muonekano wake daktari alimuambia kuwa anaonekana ana shida mwilini mwake.

“Daktari aliniambia una shida, nikamuambia mimi sina shida, akaniambia embu angalia mikono yako mbona kama ina alama alama,” anasimulia Magreth. “Nikamuambia kweli ninachoma sindano, huwa naumwa vidonda vya tumbo. Akaniuliza sindano gani, nikamuambia Tramadol akaniambia unajua madhara ya Tramadol?”

“Akaniambia Tramadol ni nzuri lakini ukizoea inakuwa kama ni uraibu, huwezi kuiacha. Akaniambia inabidi uache mara moja hii sindano, nikamuambia sitaweza kwa sababu mimi inanisaidia kupata ahueni.”

Magreth alijikuta akitegemea Tramadol ili aweze kuishi, haikupita siku bila kutumia dawa hiyo. “Huwezi kuishi bila zile dawa, yaani lazima uchome ndiyo ujisikie vizuri ukafanye kazi. Mimi nilikuwa bila kuchoma Tramadol nilikuwa siwezi kufanya kazi yoyote. Halafu nilikuwa nakuwa na hasira. Dokta akaniambia umejiwahi ungechelewa ndiyo yale yanakuja kuingia mpaka kwenye matumizi ya dawa za kulevya.”

Ili kuondokana na hali hiyo, Magreth aliunganishwa na Mteknolojia Dawa kwa ajili ya kupata matatibu zaidi. “Baada ya kwenda, nikaambiwa Jumatatu niende nikaanze tiba. Nikafika Itega wakanipokea, wakafanya mazungumzo na mimi utaratibu wote nikafata nikamaliza. Wakanipima Tramadol iko kiasi gani mwilini basi nikaanza kunywa dawa. Niliogopa sana, sikujua kama nitaweza kumudu kupita siku bila kunywa Tramadol.”

Magreth alianza kutumia dawa ya Tramadol tangu mwaka 2022, hadi alipo acha mwaka 2025. Alijikuta akitumia kiasi cha Shilingi 10,000 hadi 15,000 kwa ajili ya matumizi ya dawa ya Tramadol kila siku, kutoka kwenye kutumia takribani 2,000 tu mwanzoni.

Tramadol ni moja ya  dawa tiba zenye asili ya kulevya ambapo mtumiaji wa dawa hizi akitumia bila uangalizi wa daktari au kiholela huishia kupata madhara sawa na mtumiaji wa madawa ya kulevya.

Katika taarifa ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa  za Kulevya ya mwaka 2023, Tramadol ilionekana kutumiwa pia na watumiaji wa dawa za kulevya pale wanapokosa dawa hizo.

Janga la kimya kimya

Magreth yeye si mtu pekee, aliyepata athari za matumizi ya dawa za Tramadol. Bahati Simon,28 [sio jina lake halisi] naye ametumia dawa ya Tramadol kwa muda wa miezi 11. kilichopelekea kutumia Tramadol ni baada ya kufanyiwa oparesheni ya kidole tumbo (Appendix).

“Nilivyo fanyiwa oparesheni nikawa na maumivu makali. Nikawa nimepewa ile dawa kama dawa ya maumivu mwanzoni. Basi baada ya hapo, yakawa maumivu yanakuwa makali. Ikawa mara kwa mara natumia Tramadol kwa ajili ya kunisaidia kuondoa maumivu,” aliiambia The Chanzo Januari 26, 2026.

Bahati alianza kutumia vidonge vya Tramadol viwili kwa siku, hadi kufikia kumeza vidonge 10 kwa mara moja.

“Ikapelekea dawa za maumivu nikinywa maumivu hayatulii tena. Kwa hiyo dawa pekee ambayo naweza nikatumia nikiwa naumwa ilikuwa ni hiyo Tramadol. Ugumu unakuja pale unapoamka asubuhi, unapotaka kuanza kufanya kazi yaani huwezi kufanya kazi, huwezi kugusa kitu chochote kama haujanywa ile dawa.”

“Maana yake kinachotokea mwilini kinakutengenezea kama alosto, mwili unakuwa unauma na miguu. Halafu na akili pia inakuwa inachoka, yaani kichwa kinakuwa kama kina kuwa na wenge fulani hivi.”

Bahati anakiri dawa hizo kuuzwa kiholela, hususan kwa baadhi ya maduka ya madawa ambayo ni madogo.

“Maduka ya dawa yanauza tu, ila yanajificha. Ukienda hawakuulizi chochote unapewa tu. Maduka machache sana, hasa hasa maduka makubwa ya madawa ndiyo wanakuuliza cheti cha daktari. Lakini haya maduka mengine madogo madogo hayaulizi cheti cha daktari.”

Bahati anasisitiza watu kutokutumia dawa ya Tramadol bila ya maelekezo kutoka kwa daktari. “Tusitumie dawa kiholela, dawa ya Tramadol inatesa inaumiza. Mimi nilipungua, nilikonda. Kwa sababu unapotumia hii dawa hauli, mimi nilipoteza kabisa hamu ya kula. Na sisi wanawake kwenye kutafuta mtoto unakuwa na ‘hormone imbalance’. Yaani inakuharibia mfumo wa maisha kwa vitu vingi.”

Ripoti ya mwaka 2025 ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na madawa ya kulevya na uhalifu, imebaini kuwa tatizo la matumizi yasiyo ya tiba ya Tramadol limeendelea kuwa tatizo ambapo, nchi za Africa Magharibi na Kati zimeendelea kusumbuliwa zaidi na tatizo hilo. Huku ripoti mbalimbali zikionesha dawa za Tramadol hutumika pia na makundi ya kigaidi, katika uhalifu wao.

Katika mitandao ya kijamii sehemu mbalimbali ikiwemo jukwaa la Jamii Forum, watu mbalimbali wamejitokeza wakilalamika kupata uraibu wa Tramadol, wengi wao wakielezea dalili za uraibu, bila kuelewa kuwa tayari wameshapata tatizo la uraibu. Hii inafanya janga hili kuwa la kimya kimya, hasa kwa kuwa dawa hizi hutumika kwa tiba za kawaida.

Uchunguzi wa The Chanzo

Januari 25, 2026, mwandishi wa The Chanzo, Jackline Kuwanda mkoani Dodoma alifanya uchunguzi kwa baadhi ya maduka ya madawa. Alifanya uchunguzi kwa takriban maduka matano ya madawa yaliyo maeneo yenye makazi mengi ya watu, lengo likiwa kujionea hali halisi ya uuzaji wa dawa ya Tramadol.

Majira ya saa tatu asubuhi, alifika katika moja ya duka la dawa akijifanya mgonjwa anayehitaji dawa hiyo.

“Za asubuhi kaka, salama, nitapata dawa ya Tramadol?

“Ndiyo zipo.”

“Shilingi ngapi?”

“Pakti moja Shilingi 2,000. Ni wewe mwenyewe unatumia?”

“Ndiyo.” 

“Walikuandikia una mezaje kutwa mara mbili? Mara tatu?” 

“Yaani sijaandikiwa, ila tu nimeelekezwa.”

“Basi meza kimoja asubuhi na kimoja jioni.”

Mwandishi huyu, hakudaiwa cheti cha daktari ili kupata dawa hiyo. Muuzaji alienda moja kwa moja eneo la kuchukua dawa, na kumpatia kwa kumpa maelekezo ya kutumia.

Katika duka lililofuata, baada ya mfamasia kuelezwa kuwa anahitaji dawa ya Tramadol, alimtazama usoni na kumuuliza kwa sauti ya chini una cheti? Alijibiwa kuwa hapana.

“Mtumiaji ni wewe mwenyewe?

“Ndiyo.” 

Mfamasia huyo, alitoa dawa na kumpatia, huku mwandishi wa The Chanzo akimuuliza namna ya kutumia dawa hiyo.

“Natumiaje? Kutwa mara mbili. Asubuhi na jioni?

“Ndiyo.”

Hata hivyo sio maduka yote ya dawa hutoa dawa hizi kiholela, wengine wamekuwa wakizingatia maadili ya kazi yao.

“Eti nitapata dawa ya Tramadol?” 

“Tramadol  ipo. 2000 vidonge 10,” alieleza moja ya Mfamasia katika moja ya duka. Hata hivyo baada ya mwandishi kumuambia kuwa hana cheti cha Daktari Mfamasia huyo aligoma kumuuzia dawa hizo.

“Una maumivu makali kiasi kwamba unataka dawa ya Tramadol?  Tramadol kwanza zinauzwa ‘special’, yaani daktari ameandika mtu umpatie Tramadol. Kwa hiyo zile, huwa zinamfanya mtu awe ‘addicted’. Ukizoea Tramadol utajiona akili zako muda mwingine hazifanyi kazi,” alisisitiza Mfamasia huyo.

Katika maduka matano ya madawa, ambayo mwandishi wa The Chanzo alipita, ni maduka mawili pekee ndiyo alidaiwa cheti na daktari na kuelezwa athari za matumizi ya dawa ya Tramadol.

Cocaine ya Watu Masikini

Kutokana na matumizi holela yaliyogeuka kuwa janga kubwa la dawa za kulevya, Afrika Magharibi wameibatiza Tramadol jina la Cocaine ya watu masikini. Hii ni kwa sababu ya gharama nafuu za dawa hizo, upatikanaji rahisi lakini madhara makubwa sawa sawa na Cocaine pale inapotumika kiholela bila kufuata ushauri wa kitalaamu.

Steward Njangaje ni Mteknolojia Dawa, akiongea na The Chanzo Januari 16, 2026 alifafanua kwamba moja ya msukumo wa matumizi holela ya Tramadol yanaweza kuwa ni sababu za kibiashara lakini pia elimu ndogo katika jamii.

“Wako watu wengi ambao wanaenda kwenye maduka ya dawa, wanainunua bila kujali kwamba inatakiwa iwe imeandikwa na daktari ndipo aweza kuipata. Wanapoitumia kwa muda mrefu, katika mazingira hayo ya kuiuza kiholela inapelekea wanapata uraibu. Na inakuja kuleta shida kubwa kwenye mwili wa binadamu hasa kwenye eneo la ubongo,” alifafanua Njangaje.

“Na pengine kwa sababu ya mtu aliyewekeza ‘pharmacy’ anawalazimisha labda wataalam waweze kutoa dawa hizo bila cheti. Na mwisho wa siku zinaleta shida kubwa kiasi hiki.”

Nchini Tanzania kwa mwaka takribani watu milioni 1 hufika katika vituo mbalimbali vya kutibu uraibu wa madawa mbalimbali ya kulevya na yale ya tiba yenye asili ya kulevya. Njangaje ni mmoja wa watendaji katika vituo hivi na hapa anaelezea uzoefu wake.

“Mimi ninayezungumza nafanya kazi kwenye kituo cha kutibu uraibu wa dawa za kulevya nchini. Kimsingi ni kituo kinafanya kazi, kitaifa kinaitwa Itega. Kwa hiyo mpaka sasa Serikali imeanzisha utaratibu wa kutibu watu ambao wameathirika na dawa hizi.”

“Na tuko hapa tunaendelea kutoa hizo huduma, na tunao wagonjwa wengi sana ambao wameathirika na hizo Tramadol. Na tunaendelea kuwapa matibabu. Ili waweze kutoka katika changamoto hizo.”

Wakati ninaongea na Njangaje alikuwa anawahudumia takribani wagonjwa 20 waliofika kupata huduma za tiba ya uraibu wa Tramadol.

“Serikali inahimiza wataalam wa afya tuandike hizi dawa kwa makini. Na inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kwamba hizi dawa zisitumike kiholela. Kama kuna umuhimu wa kuitumia basi, tuhikikishe inakuwa imeandikwa na daktari na imefuata taratibu zote ili mtu aweze kuitumia.”

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jaquelinevictor88@gmail.com

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×