Walimu 77 wa shule za sekondari katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza wamelipwa stahiki zao kiasi cha shilingi 85,006,000, ikiwemo posho ya kujikimu baada ya kuajiriwa zilizocheleweshwa kwa takribani miezi sita.
Malipo ya madai hayo yamefanyika kufuata Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) mkoa wa Mwanza kufanya uchambuzi wa mfumo na halmashauri kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza, Abnery Mganga alipokuwa akitoa taarifa utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo katika kipindi cha miezi mitatu ya Oktoba hadi Disemba 2025.
“Kimsingi fedha ilicheleweshwa kwenye akaunti ya Mkurugenzi, yaani baada ya kuwa Serikali imetoa ilitakiwa fedha ile ilipwe moja kwa moja,” amesema Mganga, “Kwa kuwa hakukuwa na vitendo vya rushwa, kwa hiyo hatua tulizochukua sisi ni hizo za kufanya uchambuzi wa mfumo na kudhibiti fedha hizo pengine ucheleweshaji ule ungeweza kuleta kero zaidi au changamoto nyingine ambayo ingesababisha vitendo vya rushwa.”
Katika hatua nyingine Mganga ameeleza kuwa katika kipindi husika TAKUKURU mkoa wa Mwanza pia imefuatilia miradi ya maendeleo 17 yenye thamani ya shilingi bilioni 4.7 ambapo ilitoa mapendekezo yake kwa wakandarasi na taasisi husika zinazotekeleza miradi hiyo.
Ameeleza pia walipokea taarifa 59 ambapo kati ya hizo, 24 zilihusiana na vitendo vya rushwa na 35 zilikuwa ni za vitendo ambavyo sio vya rushwa. Amesema taarifa za vitendo vya rushwa zinafuatiliwa na tayari mashauri 4 yameshafunguliwa mahakamani.