The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Serikali Yatahadharisha Kuhusu Mlipuko wa Magonjwa ya Msimu wa Mvua

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya Februari 25, 2026 kupitia kwa Mganda Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe imeonesha kuwa kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wa mafua makali ya Influenza na UVIKO-19 nchini, hali Serikali imesema ni ya kila mwaka kuanzia kipindi cha Novemba hadi Aprili.

subscribe to our newsletter!

Serikali imewatahadharisha wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa mbalimbali ya mlipuko yanayoongezeka wakati huu wa mvua za masika, ikiwemo mafua makali ya Influenza, UVIKO-19, Homa ya Dengue na Kipindupindu.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya Februari 25, 2026 kupitia kwa Mganda Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe imeonesha kuwa kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wa mafua makali ya Influenza na UVIKO-19 nchini,  hali Serikali imesema ni ya kila mwaka kuanzia kipindi cha Novemba hadi Aprili.

“Takwimu za ufuatiliaji zinaonesha kuwa, kila mwaka katika kipindi cha mwezi Novemba hadi Aprili kunakuwa na ongezeko la ugonjwa wa mafua makali ya Influenza na UVIKO-19 hapa nchini na duniani. Hali hii inatutaka kila mmoja wetu kuchukua tahadhari,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Magonjwa haya huenezwa kupitia majimaji kutoka kwenye mfumo wa njia ya hewa ya mgonjwa mwenye maambukizi na husambaa wakati wa kukohoa, kupiga chafya au kuzungumza. Dalili zake ni pamoja na homa kali, kikohozi, maumivu ya kichwa na mwili, mafua, kuwashwa koo na uchovu.

Wizara imewataka wananchi kufunika pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kuepuka misongamano isiyo ya lazima, kuvaa barakoa na kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za afya. “Kuepuka kujitibu au kutumia Antibiotiki bila ushauri wa wataalamu wa afya,” imesisitiza Wizara.

Kuhusu Homa ya Dengue, Wizara imesema maeneo mengi hapa nchini yapo katika kipindi cha mvua za masika zinazopelekea kuongezeka kwa mazalia ya mbu aina ya Aedes wanaosambaza ugonjwa huo.

“Homa ya Dengue huenezwa na mbu aina ya Aedes ambaye ni mweusi mwenye madoa doa meupe na hupendelea kuuma nyakati za asubuhi, mchana na jioni. Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na homa kali, maumivu ya kichwa na viungo, maumivu sehemu za macho na uchovu,” imeeleza taarifa hiyo.

Wizara imewataka wananchi kutokomeza mazalia ya mbu kwa kuzika makopo yaliyotupwa ovyo, matairi ya magari, vifuu na kufukia madimbwi ili kuzuia maji kutuama. Pia kujikinga kwa kuvaa nguo ndefu, kutumia dawa za kufukuza mbu na kuweka nyavu kwenye madirisha.

Kuhusu Kipindupindu, Wizara imesema nchi imekuwa katika mlipuko wa ugonjwa huo ulioathiri mikoa yote isipokuwa Kilimanjaro na Njombe, lakini kwa sasa hali ina mwelekeo mzuri.

“Kwa kipindi cha takriban mwezi mmoja uliopita, nchi yetu haijapata mgonjwa wa Kipindupindu. Hivyo, napenda kuchukua fursa hii kutambua mchango wa Sekta mbalimbali, Taasisi za Dini, Viongozi wa Jamii, Wanahabari, Sekta Binafsi, Wadau chini ya usimamizi wa Shirika la Afya Duniani na Jamii kwa ujumla kwa juhudi kubwa katika kudhibiti ugonjwa huu,” imesema taarifa hiyo.

Hata hivyo, Wizara imeonya kuwa bado kuna hatari kutokana na mvua zinazoendelea na uwepo wa maambukizi nchi jirani. Wananchi wameelekezwa kuendelea kuchukua hatua za kujikinga ikiwemo kuchemsha maji ya kunywa au kutibu kwa dawa maalumu, kunawa mikono kwa sabuni, kuosha matunda kwa maji safi, na kuepuka vyakula vya baridi vilivyoandaliwa katika mazingira machafu.

“Kujenga vyoo bora, kuvitumia na kuviweka katika hali ya usafi nyakati zote ili vijidudu vya ugonjwa visiingie kwenye maji na chakula,” imesema Wizara.

Serikali imewataka pia wananchi kuepuka uchafuzi wa vyanzo vya maji kwa kujisaidia, kutupa taka au kutiririsha maji taka, na kutunza mazingira kwa kuepuka kutupa taka ovyo.

“Serikali imejipanga kufuatilia na kutoa huduma dhidi ya magonjwa yote ya mlipuko na itaendelea kutoa taarifa mara kwa mara iwapo kutakuwa na mabadiliko katika mwenendo wa maambukizi au endapo kutahitajika kuchukua hatua zaidi,” imesema taarifa hiyo.

Ibrahim Mgaza ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Anapatikana kupitia ibrahimmgaza39@gmail.com

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×