Dar es Salaam. Wakati mamilioni ya wanawake duniani wakijiandaa kusherehekea siku ya kimataifa ya wanawake duniani, wanawake wa chama cha upinzani Tanzania CHADEMA wamejikuta katika wakati mgumu kusherehekea siku hiyo baada ya misafara yao kuzuiwa katika maeneo mbalimbali usiku wa Machi 06 kuamkia Machi 07, 2026.
Wanawake wa chama hicho wamepanga kusherehekea siku hiyo mkoa wa Mara, huku maandalizi yakiwa yameshafanyika, ikiwemo baadhi yao kuwa tayari wamefika katika mkoa huo.Chama hicho kimeripoti kuwa misafara ya wanawake imezuiwa na Polisi katika maeneo mbalimbali.
Msafara wa wanawake kutoka kinondoni ulizuiwa Mlandizi, lakini pia msafara mwingine wa wanawake kutoka Temeke walizuiwa Dakawa Morogoro. Pia msafara mwingine wa wanawake kutoka Ubungo ulizuiwa Gairo.
Pia msafara mwingine wa wanawake 51 kutoka mkoa wa Kagera ulizuiliwa katika mkoa wa Geita majira ya saa nane usiku katika eneo la Kasamwa. Ambapo wanawake hao walifikishwa katika kituo cha polisi Geita.
Akiongea juu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake CHADEMA, Sharifa Suleiman, alieleza kuwa kauli mbiu ya siku ya wanawake mwaka huu ni Haki na Usawa, Ukitoa Umepata-Chukua Hatua.
Wanawake mkoa wa Mara walitangaza kuwakaribisha kina mama kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake katika mji wa Musoma kwa kueleza kuwa maandalizi tayari yamekamilika.
“Yeyote yule atakayejitokeza kuwazuia wanawake wa Mara kuadhimisha atakuwa amewafanyia ukatili wanawake. Wanawake wa mkoa wa Mara tunawakaribisha wanawake wote katika siku ya mwanamke ambayo ni haki ya kila mwanamke kuadhimisha,” alieleza Veronica Sando mnamo Machi 04, 2026.
Mnamo Machi 01, 2026, Jeshi la Polisi mkoani Mara lilipiga marufuku CHADEMA kupanga maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ikieleza kuwa kuna amri ya kuzuia shughuli za chama hicho.
“Jeshi la Polisi mkoani Mara..limeona picha mjongeo za BAWACHA kwenye mitandao ya kijamii zinazohamasisha kufanya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani tarehe 08-3-2026, mjini Musoma mkoani Mara. Kitendo cha BAWACHA kufanya hivyo ni ukiukwaji wa makusudi wa amri ya Mahakama Kuu ya Tanzania iliyotolewa tarehe 10-06-2025 inayokitaka chama cha siasa CHADEMA kutofanya shughuli za kisiasa hadi kesi yao ya msingi itakapomalizika Mahakamani,” alieleza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo.
Na kuongeza: “Jeshi la Polisi linaendelea kutambua amri hiyo kwani haijatenguliwa. Tunawashauri CHADEMA kurejea mahakamani kumaliza shauri lao badala ya kukaidi amri ya Mahakama, jambo ambalo kimsingi ni dharau kwa mahakama (contempt of court).”
Amri inayotajwa juu ya kuzuia shughuli za CHADEMA ni ile iliyotolewa na Jaji Hamidu Mwanga mnamo Juni 10, 2025. Amri hiyo ilitolewa kufuatia maombi ya wanachama watatu wa CHADEMA kutoka Zanzibar; Bi Maulidah Anna Komu, Said Issa Mohamed na Ahmed Rashid.
Watatu hao walipeleka maombi Mahakamani wakieleza kuwa hakukua na mgawanyo sawa wa mali ndani ya CHADEMA kati ya Zanzibar na Tanganyika. CHADEMA imeendelea kusisitiza kuwa amri hiyo iliyotolewa kisheria inakoma ndani ya miezi sita.
“Kuwashikilia wanachama wa CHADEMA wanaokwenda Musoma kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ni uvunjaji wa wazi kabisa wa Ibara ya 20, 26(2) na 29(1)-(2) & (5) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania,” anaandika Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Rugemeleza Nshala katika ukurasa wake wa X.
“Hakuna amri yoyote au zuio lolote lile la Mahakama juu ya Wanachadema kushiriki katika maadhimisho ya kimataifa ya Siku ya Wanawake au kushiriki katika shughuli za siasa.”
“Sheria i wazi kuwa zuio lolote lile la Mahakama haliwezi kuvuka miezi sita labda kama limehuishwa. Sivyo ilivyofanywa kwenye kesi ya Saidi Issa Mohamed na wenzake wawili haikuhuishwa hivyo zuio hilo lilikoma tarehe 10 Desemba 2025,” Nshala anasisitiza.
Kauli mbiu ya Siku ya Wanawake Duniani ni Haki, Sheria na Utekelezaji kwa Wanawake na Wasichana wote; kwa Tanzania kauli mbiu iliyochaguliwa na serikali ni Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi kufikia Dira 2050.
Wanawake wa vyama mbalimbali vya kisiasa na taasisi mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Mapato, Polisi wameendelea kujitokeza kusherehekea siku hii kwa matukio na matendo ya ukarimu sehemu mbalimbali Tanzania.