Dodoma. Tume ya Rais iliyoundwa kuangalia masuala ya ardhi katika eneo la Ngorongoro imependekeza uwepo wa sheria rasmi itakayohakikisha uhamaji endelevu kutoka Ngorongoro.
Tume hiyo iliyozinduliwa rasmi Februari 20, 2025, ikiongozwa na Jaji Gerald Ndika, iliundwa kufuatia mgogoro wa ardhi unaoendelea kutoka katika jamii ya wamasai ambao ni wakazi wa Ngorongoro.
Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa wakazi hao wa eneo la Ngorongoro kuhama ikieleza dhima kubwa ni kulinda uhifadhi; jamii hiyo imeendelea kuonesha kuwa maeneo hayo ni makazi yao ya asili, na uwepo wao hauna athari hasi katika mazingira hayo.
Akisoma mapendekezo ya Tume hiyo leo Machi 12, 2025, huko jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Tume hiyo ameeleza kuwa mfumo wa matumizi mseto ya ardhi ndani ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro siyo endelevu.
“Inapendekezwa Sheria ya Hifadhi ya Ngorongoro sura 284 ifanyiwe mapitio na marekebisho kwa kuwashirikisha wadau wote muhimu ili iendane na wakati na mahitaji ya sasa,” ameeleza Mwenyekiti wa Tume hiyo.
Na kuongeza: “Ili kuimarisha ustawi wa jamii na uhifadhi endelevu shughuli zisizo za kiuhifadhi zitekelezwe nje ya eneo la hifadhi.”
Tume hiyo imependekeza pia serikali kutoa vibali maalum vya wakazi wa eneo hilo na pia kufanya suala la kuhama kuwa endelevu na la kisheria.
“Uhamaji katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro uwe endelevu na uwekewe msingi wa kisheria,” Mwenyekiti wa Tume hiyo Gerald Ndika anaeleza.