The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Bila Ukweli na Uwajibikaji kwa Mauaji ya Oktoba 29, Jitihada za ‘Maridhiano’ Zitabaki Kuwa ni Kiini Macho

Sote tukubali ukweli na madhara yake, kisha, labda maridhiano yanaweza kufikiriwa.

subscribe to our newsletter!

Kuna hadithi moja inayojitokeza kwenye mitandao yangu ya jamii mara kwa mara. Ni hadithi ya mtu huko Afrika Kusini ambaye aliokoa kundi la tembo ambao walikuwa wamepangiwa kuuawa kutokana na kuingia vijijini na kuvuruga makazi ya watu. 

Mtu huyu aliyeitwa Lawrence alikaa na tembo hawa ambao walikuwa wajeuri kweli hadi tembo hao walipotulia kwenye mbuga binafsi ya huyu jamaa. Lawrence alielewana sana na kiongozi mama wa kundi. 

Hata hivyo, mbuga ilikuwa kubwa, na mara nyingi tembo walienda mbali katika kutafuta chakula chao. Baada ya miaka mingi, Lawrence alifariki kutokana na shtuko la moyo. Siku mbili baadaye, tembo 21, hao waliookolewa na Lawrence pamoja na watoto wao, wakiongozwa na huyuhuyu tembo mama, walijitokeza nje ya nyumba ya Lawrence.   

Kumbe walikuwa wametembea saa 12 kufikia hapo nyumbani kisha wakakaa pale kwa muda wa siku mbili, wakitoa sauti za huzuni, kabla ya kurudi porini. Halafu ajabu ilikuwa kwamba kwa miaka kadhaa iliyofuata walikuwa wanajitokeza pale nyumbani kwake siku ileile ya kumbukumbu ya kufariki kwake kila mwaka kuendelea kuonesha masikitiko na mshikamano. 

Hapo maswali ni mengi. Lawrence alifariki akiwa safarini, mbali na nyumbani kwake.  Maiti yake kurudishwa nyumbani ili azikwe. Wakati huo, tembo hao walikuwa mbali, muda wa kutembea wa saa 12.  Aidha, walikuwa hawajamtembelea Lawrence mwaka mmoja na nusu. 

SOMA ZAIDI: Barua Kwa Wasanii wa Tanzania: Huwezi Kujiunga na Wawindaji na Kujidai Uko Upande wa Wawindwaji

Sasa walijuaje kwamba alikuwa amefariki? Walihisije? Ujumbe uliwafikiaje? Pili, walipokuwa wanaendelea na maisha yao kama tembo, waliwezaje kumkumbuka Lawrence namna hii baada ya miaka yote hiyo? Kweli alikuwa amewaokoa, lakini miaka mingi ilikuwa imepita.

Tembo hasau kamwe

Labda ndiyo maana kuna msemo wa Kiingereza usemao an elephant never forgets (tembo hasahau kamwe). Lakini, ingawa mfano huu ni wa kipekee, kuna mifano mingi ya wanyama wanaokumbuka waliowatendea mema miaka nenda rudi. 

Kuna mbwa na paka waliotembea zaidi ya maili mia moja baada ya kuachwa na wamiliki wao ili waungane nao tena. Kuna simba yatima ambao walilelewa na binadamu kabla ya kupewa nafasi ya kurudi msituni. Waliowalea walipoingia msituni kuwatafuta baada ya miaka nenda rudi, simba hao wanawakimbilia na kuwarukia kwa furaha. Wanakumbuka!  

Halafu kuna hadithi ya mtu aliyemlea sokwe (gorilla) kwa miaka mitano kabla ya kumrudisha msituni. Sokwe huyu alikuwa mkali kwa binadamu aliyewaona lakini aliyemlea alipokuja baada ya miaka mitano kumtafuta, licha ya kuonywa kwamba sokwe huyo ni mkali kwa binadamu, sokwe alimkaribisha kwa furaha sana, akamtambulisha kwa sokwe wenzie.  

Alilala pembeni mwa kambi ya mtu huyu na hakutaka aondoke.  Na bila kusahau Jane Goodall na sokwe mtu wa Gombe waliomkumbuka hata aondoke kwa muda mrefu namna gani.

SOMA ZAIDI: ‘Askari Wangu Wamefanya Kitu Kibaya Sana’: Ya Nanjing 1937, Tiananmen Square 1989 na Oktoba 29, 2025 Tanzania

Yote haya yanaonesha kwamba hata wanyama hawasahau. Na hawasahau kwa kutendewa mema tu. Hawasahau mabaya pia. Hukohuko Afrika Kusini, tembo wamewahi kuwaua majangili baada ya kuwatambua wakiingia mbugani.

Kwingine, mtu alipoua tembo mtoto, tembo walivamia kijiji cha karibu na kubomoa nyumba kadhaa. Huko India walivamia hata treni baada ya baadhi ya tembo kugongwa na treni. Wanakumbuka na wanaumia.

Sembuse binadamu

Kama wanyama wanakumbuka hivi, binadamu watakosaje kukumbuka? Mwandishi mweusi maarufu wa Marekani, Maya Angelou, aliwahi kusema: Watu watasahau ulichosema. Watu wanasahau ulichotenda. Lakini hawatasahau kamwe ulivyowafanya wajisikie.

Hisia zinaingia mwilini na akilini na kuchimba chini kama mihogo, kama mizizi ya mibuyu na zinakaa. Hazisahauliki kamwe. 

Ndiyo maana ni kupoteza muda kuwasihi watu wasahau maumivu yao. Tena ni kudharau, au kudogosha, maumivu yao. Katika kuwasihi, au hata kuwashurutisha hivyo, unazidi kutonesha vidonda vya mwili na vya moyo. 

SOMA ZAIDI: Tanzania Baada ya Oktoba 29, 2025: Tunarejeshaje Kisiwa cha Amani? 

Ndiyo maana, huko Afrika Kusini baada ya kuondolewa kwa mfumo wa makaburu wa ubaguzi na ukandamizaji, ikaanzishwa Tume ya Ukweli na Maridhiano. Ingawa wengi wanaona kwamba haikukidhi matakwa ya walioonewa na kuteswa, maana, mbele ya tume hiyo, ilitosha mtu aliyefanya maovu sana, hata mauaji, kukiri na kuomba radhi tu, ndipo akasamehewa. Hakushitakiwa. Hakuwajibishwa. 

Maumivu bado yaliendelea, lakini angalau watenda maovu walilazimika kukiri hadharani walichofanya, hata wale waliomwua Steve Biko, ukweli wao ulianikwa hadharani maana viongozi wapya wa Afrika Kusini walitambua kwamba, bila ukweli wote kusemwa, bila watu kuelewa kwa undani yaliyotokea, hakuna maridhiano.

Samora Machel alifanya vilevile huko Msumbiji, na mifano mingine iko Sierra Leone na Canada pia. 

Narudia, wote hawa walielewa kwamba bila ukweli kuainikwa waziwazi hadharani, kudai tugange yajayo tu, turidhiane kama vile kilichotokea ni sawa na mchezo wa mpira tu, ni sawa na kufunika kidonda na kutegemea kwamba kitapona tu. Inabidi kufunua kidonda, kukisafisha vizuri na kutia dawa ndipo kitapona.

Oktoba 29

Kwa nini nasema hivi?  Sote tunajua watu walikufa siku ya uchaguzi Oktoba 29, 2025, na siku zilizofuata. Kila mtu anajua. Wako watu wengi ambao uchungu wao wa kupoteza ndugu na jamaa hautaisha. 

SOMA ZAIDI: Oktoba 29, 2025: Tulichoka Hekima na Busara, Tukajaribu Ujinga, Tumeona Matunda Yake

Mbaya zaidi, wengine wana uchungu zaidi maana hata nafasi ya kutoa heshima ya mwisho na kuwaaga wapendwa wao waliikosa kwa sababu miili ya wapendwa wao haionekani bila sababu yoyote kutolewa. Bila kusahau watu ambao wametoweshwa pasipojulikana na wasiojulikana. 

Na mbaya zaidi tena, hata watu ambao hawakuwepo kwenye maandamano waliuawa, wengine majumbani kwao.  Sasa ndugu na jamaa wa watu hawa, hata wakiamrishwa, au kutishiwa, au kushurutishwa kusahau, hawawezi kusahau. Wanaweza kufungishwa midomo, lakini uchungu na hasira zilizofunikwa zinazidi kutokota. 

Wako wengi pia waliojeruhiwa siku zile na sasa wanafuga jeraha la kudumu. Kila wakiangalia mguu wao, au mkono wao, au sehemu yoyote ya mwili, wanachomwa na hisia kali sana ya kumbukumbu na maumivu yasiyoisha.

Na si hivyo tu. Naamini kwamba Watanzania wasiohesabika bado wanashikwa na kiwewe. Hatukuamini kwamba mauaji kama haya yangeweza kutokea hapa nchini kwetu Tanzania.  Tanzania. Tanzania, kweli?

Tumeona mambo haya yakitokea nchi nyingine, lakini hatukudiriki kufikiria yanaweza kutokea kwetu. Hata kama dalili zilikuwepo, tulizipuuza. Ndiyo maana tumeumia na maumivu haya hayataponeshwa na maagizo, shuruti au ahadi.  

SOMA ZAIDI: Tume Kuchunguza Matukio ya Oktoba 29, 2025: Serikali Iepuke Vishawishi vya Kutaka Kujistiri na Badala Yake Ijikite Kwenye Kuliponya Taifa

Tujifunze kwa wenzetu, ukweli kwanza, tuache kufunika ukweli na badala yake tuuanike  ukweli, tukubali ukweli, sote tukubali ukweli na madhara yake, kisha, labda maridhiano yanaweza kufikiriwa. 

Ndipo tunaweza kuganga yajayo!

Richard Mabala ni mdau wa masuala ya elimu, mshairi na mwandishi wa vitabu. Anapatikana kupitia rmabala@yahoo.com au X kama @MabalaMakengeza. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi. 

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×