Akizungumza katika katika Ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika leo Aprili 03, 2026, katika Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli Bunju, Askofu Stephano Musomba wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo, ametahadharisha juu ya uelekeo wa jamii ya Tanzania akigusia mambo kama uchawa, utengano na dhuluma katika jamii.
“Mila zetu za kiafrika si kawaida mtu anakufa leo unashangilia, si kawaida,” Musomba ameeleza akizungumzia matukio ya hivi karibuni
“Tukae chini tujadili pamoja tumekosea wapi,tuelimishane tueleweshane. Pengine anashangilia kwa sababu hakuna anayeniangalia, pengine haki yangu haijatendeka, ndio maana anashangilia. Kwahiyo tuangalie nini chanzo kinachotufanya tuwe tulivyo kwa nini tumefika katika hali hiyo,” amesesisitiza Musomba.
Askofu Musomba pia amekemea utengano wa kisiasa, ambapo ameonesha kushangazwa na watu wanaotenga binadamu wenzao kwa sababu ya tofauti ya vyama vya siasa.
“Tulitendee haki taifa letu, tulikotoka na tunakoelekea siyo kuzuri.Tulikotoka kuzuri sana lakini tumepotea sehemu,” alionya Askofu Musomba.
Katika mahubiri hayo ambayo amesisitiza suala la ukweli, Askofu Musomba amechambua pia nadharia ya viongozi wa dini kuambiwa wanaingilia siasa, ambapo ameeleza siasa haifuti uumini wa mtu katika dini, na viongozi wa dini wana nafasi ya kuonya. Musomba ametumia muda katika mahubiri yake kukemea kasumba ya uchawa katika jamii
“Sasa ukimweka mwanadamu ni Mungu kosa kubwa sana,na ndio maana tunao wajibu kama viongozi wa dini kufufua dhamiri za waumini wetu,” anaeleza zaidi katika mahubiri yake.
“Zamani tulikuwa tunaogopa sana chawa, tena ukionekana we una chawa unakimbiwa usije Ukaniambukiza. Lakini saa hizi ukiwa na chawa wewe ndiyo wewe.Mijamaa inakunyonya mpaka unakiona cha moto, wanasema we ni mzuri katika dunia hii kumbe huna lolote.”
“Kumbe huna lolote,kwa sababu hii michawa inanyonya tu uchafu wako. Hakuna uzuri wowote hapo ndiyo maana tunasema ukweli, unaleta maendeleo….na ndio maana tunahitaji watu kusikiliza watu wanapokuambia we umekosea.Usiwashambulie, lakini mwanadamu wa leo ni mgumu sana anapenda kusikia yale anayotaka kusikia.”