Kwa mujibu wa ibara ya 50(1) ya Mkataba unaoanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki kila nchi mwanachama wa Jumuiya zinapaswa kuchagua wawakilishi tisa kwenda kuwa wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa upande wa Tanzania utaratibu wa kuwapata wawakilishi hawa kwa kiasi kikubwa unafanana na ule wa kuwapata wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo vyama vya siasa kupitia michakato yake ya ndani huteua wagombea wa nafasi hizo. Tofauti ni kwamba wawakilishi wa mwisho hupigiwa kura na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa kanuni ya 15, 16 na 17 za Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la mwaka 2025.
Kwa upande wa Tanzania wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki walichaguliwa mwaka 2022 kwa kipindi cha miaka mitano, ambapo watamaliza muda wao mwaka 2027.
Wabunge hao ni pamoja na Selema Ladislaus Gladness, James Kinyasi Millya, Ngole Khalifan Mashaka, Abdulla Hasnuu Makame, Ng’waru Jumanne Magembe, Machano Ali Machano, Angela Charles Kizigha, Ansar Kachwamba na Mohamed Juma Nadra.
Kati ya wabunge hawa tisa, watatu yaani Angela Charles Kizigha, James Kinyasi , na Dkt Ng’waru Jumanne Magembe ni wabunge wa Bunge la Tanzania. Kizigha akiwa ameteuliwa mnamo Aprili 02, 2026, huku James Kinyasi akiwa ni Mbunge wa Simanjiro na Dkt Ngwaru Jumanne Maghembe akiwa ni Mbunge wa Mwanga walioapishwa toka Novemba 2025.
Swali kubwa linalojitokeza kwa sasa ambalo ndio litakuwa kiini cha andiko langu ni: Je Tanzania inakiuka mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa wabunge wake watatu: James Millya, Ng’waru Maghembe na Anjela Kizigha kuendelea kuwa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki wakati huohuo wakiwa wabunge wa Bunge la Tanzania?
Mkataba wa Uanzishwaji wa EAC
Ibara ya 50(1) ya Mkataba unaoanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki imeainisha kwamba kila nchi mwanachama itachagua wabunge tisa(9) wasiotokana na Bunge la nchi mwanachama kuwa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki.
Pia ibara ya 51(2)(c) ya Mkataba huo inaeleza kuwa Mbunge atapoteza sifa za kuwa Mbunge wa Jumuiya endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa bunge la nchi mwanachama.
Kwa lugha nyingine moja ya sifa kuu na ya msingi ya Mtanzania kuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki ni asiwe Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hii ni sifa isiyobadilika wala kuepukika.
Kutokana na vipengele hivi vya Mkataba, utata unaibuka juu ya uhalali wa Ng’waru Jumanne Maghembe, James Kinyasi Millya na Angela Charles Kizigha kama Wabunge halali wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ukiondoa mbali nafasi za ubunge, katika hali ya kipekee baada ya James Millya na Ng’waru Maghembe kuapishwa kuwa wabunge waliteuliwa pia kuwa Manaibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje.
Kwa mujibu wa ibara ya 5 ya Mkataba unaoanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki kuna chombo kinachoitwa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki. Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama ndio wanaounda baraza hili. Ambapo kwa Tanzania ni Mohamed Thabiti Kombo ambaye kiitifaki akiwa na dharura anawakilishwa na moja ya manaibu waziri wake ambao ni James Millya au Ng’waru Maghembe.
Yaani kwa lugha nyingine ni kwamba kuna wakati James Millya na Ng’waru Maghembe wanaweza kuwa wajumbe wa vyombo viwili tofauti kwa wakati mmoja licha ya ibara ya 51(2)(c) ya Mkataba kuzuia mtu anayeshika wadhifa wa uwaziri katika nchi wanachama kuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki.
Kurekebisha Makosa
Wabunge hawa watatu walikosa sifa za kuendelea kuwa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki mara tu walipochaguliwa kuwa wabunge au baadhi yao manaibu mawaziri kwa mujibu wa ibara ya 51(2)(c) ya Mkataba, hivyo kuendelea kwao kuwa wabunge kunakiuka moja kwa moja, Mkataba unaoanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ingawa kwa Angela Kizigha naweza kusema bado ni mapema mno kuhitimisha kwa sababu ndio kwanza ana siku tano pekee tangu ateuliwe, lakini kwa Millya na Maghembe ni uvunjifu wa wazi wa Mkabata. Kwa sababu mpaka nachapisha andiko hili, bado Millya na Maghembe ni wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki kwa mujibu wa tovuti ya Bunge la Afrika Mashariki.
Naweza kusema hii si mara ya kwanza kwa Tanzania kukutana na sintofahamu au usahaulifu wa aina hii. Mnamo mwaka 2005 baada ya Dkt Harson Mwakyembe na Beatrice Shelukindo kuchaguliwa kuwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa wakati huohuo wakiwa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki walilazimika kujiuzulu mara moja kama hitaji la ibara ya 51 (3)(c ) inavyoainisha. Jambo hili lililotambuliwa pia na Mahakama ya Afrika Mashariki katika kesi iliyofunguliwa na Christopher Mtikila.
Baada ya Mwakyembe na Beatrice Shelukindo kujiuzulu nafasi zao Bunge la Jumuiya, mnamo Machi 2006, Bunge la Tanzania lilifanya uchaguzi mdogo kujaza nafasi za Mwakyembe na Shelukindo ambapo walichaguliwa Dr. Norman Sigalla na Hulda Stanley Kibacha.
Sakata la usahaulifu wa Mkataba, liliwahi kuikumba Kenya katika mchakato wake wa kuchagua wawakilishi kutoka Kenya katika Bunge la Afrika Mashariki. Sakata lililopelekea kufunguliwa kwa shauri katika Mahakama ya Afrika Mashariki, shauri maarufu la Prof. Peter Anyang Nyong’o na wenzake ambapo Mahakama iliamua kwamba utaratibu uliotumiwa na Kenya kuchagua wawakilishi wake katika Bunge la Afrika Mashariki ulikiuka ibara ya 50 ya Mkataba.
Kwa mfano wa Mwakyembe na Beatrice Shelukindo ni ushauri wangu kwamba James Millya, Ng’waru Maghembe na Angela Charles Kizigha wajiuzulu nafasi zao za Ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki mara moja na bila kuchelewa, kama ilivyo takwa katika ibara ya 51(3)(c) ya Mkataba ili kuendelea kulinda misingi muhimu inayohakikisha uhai wa Jumuiya sasa na baadae.
Maduhu William ni Wakili wa Mahakama Kuu na mtetezi wa Haki za Binadamu, pia ni Meneja wa Haki za Binadamu kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu , anapatikana kupitia mkulwa@humanrights.or.tz .Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.comkwa ufafanuzi zaidi.