The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Hatma ya CCM 2030 Kuamuliwa Juu ya Kaburi la Magufuli?

Yote katika yote ukijumlisha na ‘idiolojia’ ya Magufuli na kama walioshika hatamu wataweza kuihimili au kuizima, inawezekana tukashuhudia 2030 ikawa tofauti sana kwa CCM kuliko mategemo na nadharia zilizozoeleka

subscribe to our newsletter!

Mara nyingi kama sio zote ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kiongozi aliyeko madarakani anapofikia muda wa kustaafu huwa ni vigumu yeye kuamua moja kwa moja nani atakaye kuwa mrithi wake. Hii ilianza na Mwalimu Julius Nyerere, haikuwa siri kuwa chaguo la Nyerere lilikuwa Dkt Salim Ahmed Salim, hata hivyo kwa namna moja au nyingine kundi lililokuwa likimpa nguvu Hayati Ali Hassan Mwinyi lilifanikiwa kumzidi kete Mwalimu.

Lakini pia imekuwa kawaida kwa kiongozi mstaafu wa chama hicho kuwa kiungo muhimu katika kuamua uongozi mpya wa chama hicho, ambao kwa CCM huwa ndiye mgombea wa nafasi ya Urais. Hii tuliona mwaka 1995, katika uchaguzi wa mrithi wa Ali Hassan Mwinyi, ambapo Mstaafu Nyerere, aliweka uzito mkubwa juu ya uchaguzi wa Rais Benjamin Mkapa.

 Lakini pia uchaguzi wa 2015, ambapo Mstaafu Benjamin William Mkapa anatajwa kuwa kiungo muhimu katika kuweka uzito wa kuchaguliwa kwa John Pombe Magufuli. Ni wazi kwa wengi kuwa Magufuli hakuwa karata ya kwanza ya kiongozi aliyepo madarakani wakati huo, Jakaya Mrisho Kikwete. Lakini pia ni ukweli usiopingika, Mstaafu Jakaya Kikwete alikuwa kiungo muhimu katika uchaguzi wa awamu ya pili wa Rais Samia Suluhu.

Kwa hiyo ni kama kuna kanuni fiche inayotokana na mazingira: Aliyeko madarakani hapati anachotamani kupata, Mstaafu huwa kiungo muhimu katika kuamua mrithi au mazingira yajayo. Na tukipiga kurunzi la tafakari toka awamu ya kwanza ya Nyerere tunaweza kuona halikuwa jambo baya, matamanio ya Nyerere kushindwa kufua dafu, ilikuwa ni udhihirisho  kwamba chama hicho sio mradi wa mtu mmoja.

Hatma ya CCM 2030

Siku za hivi karibuni, tumeona mjadala ukiibuka ndani ya CCM juu ya hatma ya chama hicho kuelekea 2030, Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho akaonya wanaozungumzia Urais 2030, huku akihusisha mjadala huo na kukigawa chama hicho. Kwa upande mwingine tunaona Paul Makonda, akieleza kuwa wanaojipanga ndani ya CCM hawawezi kushika Urais, huku akihusisha watu hao wasiofahamika na usaliti dhidi ya Rais Samia.

Binafsi nilihangaika sana kichwani kwangu kutafakari kwani ni nini hasa kimetokea Machi 2026, kilichofanya wana CCM wakaanza kucharuka na hatma ya uongozi wa chama hicho 2030.

Jambo kubwa lililotokea katika mwezi huu ni maadhimisho ya miaka mitano ya kifo cha Rais John Pombe Magufuli, ambapo naweza nikasema kwa mara ya kwanza toka kiongozi huyo kufariki, wafuasi wake wameweza kumuadhimisha bila kukabwa koo na mijadala inayompinga kulinganisha na miaka iliyopita.

Wengi walijumuika ikiwemo viongozi wakuu wa serikali wakiongozwa na Makamu wa Rais, Dkt Emmanuel Nchimbi, na viongozi wengine mashuhuri kama Ridhiwani Kikwete, Dotto Biteko na viongozi mbalimbali waliofanya kazi na Rais Magufuli. Naamini tukio hili lilikuwa kama ‘swichi’ iliyowasha mjadala ndani ya CCM na nitaelezea zaidi.

Kama tukiangalia mirija ya ushawishi ndani ya CCM, jina la Magufuli lina nafasi yake ya kipekee. Kwa Watanzania wengi Magufuli ana sura mbili: wako wanaomuona Magufuli kama kiongozi mwenye uthubutu, aliyejali kwa dhati Watanzania wenye maisha ya chini, ambao tukiwa wakweli ni asilimia 80 ya watu wote. Lakini wako wanaomuona Magufuli kama kiongozi katili, aliyeanzisha matatizo makubwa ya kiuongozi nchini.

Kwa maoni yangu naamini kuna ushahidi wa kutosha kwamba mitazamo yote hii ni sahihi, mazuri ya Magufuli ni mazuri sana, na mabaya ya Magufuli ni mabaya sana.

Hauwezi kuwaambia chochote Watanzania waliyogawiwa mashamba Morogoro baada ya Magufuli kuwakataa walioshikilia maelfu ya hekari za mashamba na kuwafanya watu vijakazi. Hauwezi kuwaambia chochote wafanyabiashara wadogo, mama ntilie, bodaboda, wamachinga juu ya Magufuli, sote tunafahamu alifanya maisha kuwa marahisi kwa makundi haya. Hatuwezi kukataa ukweli Magufuli alikuwa na uthubutu wa kuanzisha SGR, kuimarisha uhuru wa nchi juu ya rasilimali zake kama dhahabu kwa namna ambayo haijawahi kutokea.

Lakini pia huwezi kukataa ukweli kuwa kesi za kubumba zilishamiriki katika kipindi chake, kodi na sheria kutumiwa kukandamiza watu na pia watu wasiojulikana walianza kushika hatamu katika kipindi chake. Hata hivyo matatizo kama watu kutekwa na kupotezwa yameshamiri zaidi baada ya Magufuli kuondoka.

Vitovu vya ushawishi ndani ya CCM

Baada ya Magufuli kufariki watu wengi wasiokubaliana naye walifanya jitihada kubwa kuhakikisha nchi hairudi katika baadhi ya mambo ambayo kimsingi hayakuwa na afya kwa taifa letu.

Lilipotokea wazo la kujenga sanamu ya Magufuli, watu waliwasha moto kweli kweli, kulikuwa na nguvu kubwa ya kuhakikisha rekodi iko sahihi, na wanaharakati wengi, vyama vya siasa na hata baadae CCM walikuja kukubali kwamba mambo hayakuwa mazuri, na lazima yasirudi yalipotoka.

Katika kumpinga Magufuli kulikuwa na ukweli kwamba kwa upande wa pili Magufuli ana ushawishi mkubwa pia kwa watu wengi. Hizi nguvu mbili zilizokinzana ziliwezesha uongozi mpya kuweza kupata nafasi ya kutengeneza njia yake, la sivyo ungejikuta mateka wa uongozi wa Magufuli.

Sasa tuko 2026, kwa kiwango kikubwa wengi wanaofuatilia mambo wamejiridhisha baada ya Oktoba 29, matatizo tuliyonayo ni makubwa kuliko katika historia ya nchi yetu, na ni kupoteza muda na hata ni unafiki kuendelea kumlaumu Magufuli aliyefariki miaka mitano iliyopita. Hii nguvu kinzani kuondoka, ndipo hapo tunaona sasa hatimaye wafuasi na wapenzi wa Magufuli wanapata ari mpya ya kumuenzi Magufuli.

Utofauti uliopo na kumbukumbu zingine za viongozi hivi karibuni, ni kwamba Magufuli anabadilishwa kuwa ‘ideiolojia’, ndio maana unashangaa kuona mtu kama Luhaga Mpina, alivyohamia ACT Wazalendo, alikuwa akizunguka kila kona na wasaidizi wake waliovaa sare zenye picha za Magufuli, ni yeye pekee aliyekuwa akivaa nguo za ACT Wazalendo katika timu yake.

Na kwa kweli kwa CCM, kwa siasa za hivi karibuni jina lenye ushawishi wa ki-itikadi miongoni mwa wananchi wa kawaida ni la Magufuli. Kizuizi kilichokuwa kinazuia Magufuli asishamiri, ni watu waliompinga ambao wengi walikuwa nje ya CCM, kwa sasa watu hao wanaona matatizo waliyonayo ni makubwa—na wafuasi wa Magufuli wanaelewa hakuna nafasi kama sasa. Ndio hapo tulipoona Machi 17 ya mwaka huu ilikuwa kama retreat—reli za siasa za yajayo CCM zilitandazwa.

Tukiangalia vitovu vya ushawishi ndani ya CCM, tutaanza na Rais Samia, ambaye ndiye msimamizi wa vyombo vya dola, lakini tunakuja kwa Rais Jakaya Kikwete, ambaye kwa muda mrefu alikuwa Rais pendwa Tanzania hii ikimanisha ushawishi wake ulikuwa ni ndani na nje ya CCM; hata hivyo ameingia katika mgogoro mpana na watu nje ya CCM kuanzia 2025 na kitovu cha tatu cha ushawishi CCM ni Magufuli.

Kwa tathmini yangu nadhani Magufuli ana nguvu ya ushawishi wa watu na hiyo ni moja ya karata itakayoamua hatma ya CCM. Hata hivyo, kwa muda sasa, CCM kwa kiwango kikubwa nguvu ya vyombo vya dola ndiyo inayoamua muelekeo wa maamuzi ndani ya CCM, na naamini pande zote zitajipanga kuangalia namna zitakavyoitumia nguvu ya vyombo vya dola hata kwa wale wasioshika vyombo hiyo moja kwa moja.

Kwa tathmini yangu, baada ya Oktoba 29, mwenendo wa vyombo vya dola kuamua mazingira ya kisiasa—ninaweza kuulinganisha na puto linalojazwa upepo, nadhani kama umakini usipowekwa kuelekea mbele,  tunaweza kushuhudia upepo ukizidi kiwango katika puto. Itakuwa ni vyema kwa CCM kujaribu kukumbuka kufanya siasa tena.

Sasa, je inawezekana huu ni wakati wa Mstaafu (Hayati) Magufuli kuamua hatma ya CCM 2030? Hakuna kisichowezekana. Hata hivyo kuna sababu nyingi na vishawishi vingi kwa walioshika hatamu sasa kuhakikisha ‘mtu sahihi’, atakayeweza kuhakikisha ulinzi wao baada ya kustaafu ndio anayeshika hatamu. Lakini pia kuna msukumo wa viongozi wengine kuendeleza majina yao baada ya wao kuwa wamestaafu. Lakini pia kuna msukumo kutoka nje ya CCM, ambao unaelekea kuwa nguvu halisi na isiyotabirika kwa CCM.

Yote katika yote ukijumlisha na ‘ideolojia’ ya Magufuli na kama walioshika hatamu wataweza kuihimili au kuizima, inawezekana tukashuhudia 2030 ikawa tofauti sana kwa CCM kuliko mategemo na nadharia zilizozoeleka.

Tony Alfred K ni mchambuzi anayefanya kazi na The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni tony@thechanzo.com  au unaweza kumfuatilia Twitter kupita @tonyalfredk. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×