The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Wasilisho Kamili la Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman la Ripoti Kuhusu Matukio ya Oktoba 29, 2025, Alilolitoa Mbele ya Rais Samia Aprili 23, 2026

Rais ameishukuru Tume kwa kukamilisha kazi hiyo muhimu, akibainisha hatua kadhaa Serikali yake inapanga kuchukua kutekeleza mapendekezo yake.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam – Baada ya uchunguzi wake uliodumu kwa siku 153, Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Ghasia na Uvunjifu wa Amani Yaliyotokea Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 iliwasilisha ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa hafla iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, hapo Aprili 23, 2026.

Hili hapa chini ni wasilisho kamili alilolitoa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman. Baada ya kuanza kwa kutambua uwepo wa wageni waalikwa mbalimbali, Jaji Chande alianza wasilisho lake kwa kutoa utangulizi kama ifuatavyo: 

Angalizo la Mhariri: Maudhui yafuatayo yamehaririwa kuboresha usomaji mzuri:

Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia uzima, afya na nguvu ya kukamilisha kazi tuliyopewa nawe Mheshimiwa Rais na kutuwezesha kuifikia siku ya leo ambapo tunaiwasilisha rasmi kwako na kwa umma wa Watanzania matokeo ya kazi hiyo.

Kwa niaba ya Makamishna wenzangu pamoja na Sekretarieti ya Tume, nitoe shukrani za dhati kwako Mheshimiwa Rais kwa imani kubwa uliyonayo kwetu kutukabidhi jukumu hili kubwa na muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu. Nikushukuru pia kwa ushirikiano ambao tumeupata kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi iliyotuwezesha kukamilisha kazi hii.

Mheshimiwa Rais, mimi na wenzangu kwenye Tume tuna deni kubwa la shukrani kwa Watanzania wenzetu ambao walituamini sana, na wakatupa ushirikiano mkubwa sana hadi ukaridhia kutupa muda zaidi wa kuhakikisha hakuna aliyekuwa na ushahidi au maoni na ambaye kwa hiari yake alikuwa tayari kuwa sehemu ya safari ya kuliponya Taifa anakosa nafasi ya kuwasiliana nasi. Tunakushukuru sana.

Kote tulikoenda, wananchi waliofika mbele ya Tume wameeleza kuhusu yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 na kukiri kwamba sivyo tulivyo Watanzania kwa asili yetu, kwa hulka zetu na kwa malezi ya Waasisi wa Taifa la Tanzania. Wengi wa waliojeruhiwa, waliopata misiba ya kufiwa na wapendwa wao, na waliopata hasara kwa mali zao kuharibiwa au kuibiwa, wamekiri, na kwa kweli wana haki ya kuwa na machungu makubwa sana. Lakini, wote waliowasiliana na Tume kwa njia mbalimbali wametuamini na kutupa ushirikiano mkubwa na tunaamini kuwa Ripoti tunayoiwasilisha kwako leo, na mapendekezo yaliyomo, yanabeba dhamira ya pamoja ya Taifa ya kutibu majeraha, kuwajibika kila panapostahili, lakini muhimu zaidi kujifunza na kusonga mbele.

Aidha, niwashukuru Makamishna wenzangu pamoja na Sekretarieti ya Tume kwa kufanya kazi bila kuchoka kwa siku zote 153. Mwisho, japo si kwa umuhimu, tunatambua kuwa kazi ya Tume isingetekelezwa kwa mafanikio bila ushirikiano tulioupata kutoka kwa viongozi na watendaji wa Serikali katika ngazi mbalimbali, wadau wa sekta ya umma na binafsi pamoja na umma wa Watanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Rais, uwekezaji mkubwa ambao Serikali imefanya katika kuboresha sekta ya afya umekuwa msaada mkubwa wakati wa dharura zilizotokea. Wafanyakazi kwenye vituo vya afya na hospitali, za umma, taasisi za dini na binafsi, vilivyohusika walifanya kazi kubwa sana, katika mazingira magumu mno, wengine wakibaki kazini kwa zaidi ya saa 72 mfululizo kuwahudumia majeruhi. Tunawashukuru pia viongozi wa vituo hivyo kwa kuipatia Tume taarifa zote tulizozihitaji.

Vilevile, shukrani zetu ziwaendelee wataalamu katika nyanja mbalimbali walioisaidia Tume kuyaelewa masuala mahsusi, kama vile uchunguzi wa kisayansi kwa baadhi ya vielelezo (forensic and GIS Analysis), uchunguzi wa sauti na video (forensic audio and video analyst), uchunguzi wa maiti (Pathologist), uchunguzi wa vilipuzi (ballistic expert), wachambuzi wa picha (Photographic analyst), taarifa za wataalamu wa masuala ya saikolojia na sosholojia pamoja na masuala ya uchumi na fedha.

Hadidu Rejea na Mawanda ya Kazi

Mheshimiwa Rais, jukumu kuu la Tume lilikuwa kubaini ukweli (fact finding) kuhusu matukio ya ghasia za wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 kwa kuongozwa na Hadidu Rejea sita zifuatazo:

  1. Kuchunguza na kubaini chanzo halisi cha ghasia zilizotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025 na siku chache zilizofuata;
  2. Kuchunguza lengo kuu lililokusudiwa na waliohusika katika kupanga na kutekeleza vitendo hivyo vya ghasia na uvunjifu wa amani;
  3. Kuchunguza na kubaini madhara yaliyojitokeza kutokana na ghasia hizo, ikiwemo vifo, majeruhi, uharibifu wa mali na miundombinu pamoja na madhara ya kiuchumi na kijamii;
  4. Kuchunguza mazingira na hatua zilizochukuliwa katika kubaini na kukabiliana na ghasia zilizojitokeza;
  5. Kupendekeza maeneo yanayohitaji kuimarishwa zaidi ili kuongeza uwajibikaji wa viongozi na raia kwenye kulinda amani, utawala wa sheria, haki za binadamu, utawala bora na mfumo madhubuti wa majadiliano ya kisiasa, kijamii na kiuchumi hadi kufikia maridhiano ya kitaifa na kuhakikisha vurugu kama hizo hazitokei tena; na
  6. Kuchunguza jambo lolote ambalo Tume itaona kuwa ni muhimu na linaendana na majukumu yake.

Mheshimiwa Rais, mawanda ya kazi, yalihusu kufanya uchunguzi wa matukio ya wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 na masuala yote yanayohusiana na matukio hayo kama yalivyobainishwa kwenye Hadidu Rejea. Aidha, kazi ya uchunguzi ilihusisha maeneo 202 yaliyoathirika zaidi katika wilaya 21 na mikoa 11 ambayo ni Dar es Salaam (Wilaya za Ilala, Kinondoni, Temeke, Ubungo); Mbeya (Wilaya za Mbeya, Mbeya Vijijini na Kyela); Songwe (Wilaya za Mbozi na Momba); Mwanza (Wilaya za Nyamagana na Ilemela); Geita (Wilaya ya Geita); Arusha (Wilaya za Arumeru na Arusha); Iringa (Wilaya ya Iringa); Dodoma (Wilaya ya Dodoma); Shinyanga (Wilaya ya Kahama); Mara (Wilaya za Musoma, Tarime na Bunda); na Ruvuma (Wilaya ya Songea). Vilevile, Tume ilitembelea Zanzibar na Mkoa wa Kilimanjaro kama sampuli ya maeneo ambayo hayakuwa na ghasia ili kujifunza mazingira yaliyosababisha hali hiyo.

Methodolojia ya Uchunguzi

Mheshimiwa Rais, hatua ya kwanza ya kazi ya Tume ilikuwa kujiwekea Kanuni za Utendaji (Rules of Procedure), kwa mujibu wa Kifungu cha 11 cha Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32, Toleo la Mwaka 2023, ili kuongoza utendaji kazi wa Tume. Kadhalika Tume iliandaa methodolojia iliyoongoza namna ya kufanya kazi yake kwa mujibu wa Hadidu Rejea.

Katika kukusanya ushahidi, taarifa na maoni, Tume ilitumia vyanzo vya moja kwa moja (primary sources) na vyanzo rejea (secondary sources) kwa kutumia mbinu za kimaelezo (qualitative techniques) na mbinu za kitakwimu (quantitative techniques). Vyanzo vya moja kwa moja vilihusisha mashahidi, mashuhuda wa matukio na wadau mbalimbali, kupitia mahojiano ya ana kwa ana na vikao vya majadiliano. Mahojiano yaliwahusisha pia viongozi wa vyama vya siasa na dini, viongozi wa Serikali waliopo madarakani na wastaafu. Vyanzo rejea vilitumika kukusanya, kufanya mapitio na kuchambua nyaraka mbalimbali ili kupata ukweli na uthibitisho wa kilichotokea ikiwa ni pamoja na Taarifa za Tume za Uchunguzi mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

Soma Pia: Hotuba Kamili ya Rais Samia Akipokea Ripoti ya Tume Kuhusu Matukio ya Oktoba 29, 2025, Wakati wa Hafla Iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Aprili 23, 2026

Aidha, Tume ilizingatia viwango vya kimataifa vinavyotakiwa katika kufanya uchunguzi wa aina hii, hususan, katika kuhakikisha usalama, usiri na ulinzi wa mashahidi na watoa taarifa. Mashahidi, mashuhuda na watoa taarifa wote ambao hawakutaka kutoa ushahidi au taarifa kwa njia ya wazi au mbele ya hadhara, walifanya hivyo kwa faragha.

Moja ya mbinu muhimu zilizotumika ni mahojiano ya ana kwa ana, ambapo kundi kubwa lililohusika ni la waathirika (wafiwa, majeruhi, waliopotelewa ndugu, walioharibiwa au kuibiwa mali) kupitia usikilizwaji wa wazi na wa faragha (public and closed hearing) pamoja na kuchukuliwa maelezo kwa viapo vya maandishi (Affidavits). Jumla ya waathirika 1,323 walisikilizwa na maelezo ya kiapo kuchukuliwa kutoka kwa waathirika 953.

Aidha, Tume ilipokea jumla ya mawasilisho ya maandishi 149 kupitia njia ya posta, 283 kufikishwa kwa mkono Ofisi ya Tume na 457 kupitia barua pepe (email). Vilevile, jumla ya madodoso 4,891 yalipokelewa, ujumbe mfupi kupitia sms 33,250, WhatsApp 23,195 na kupata maoni kupitia simu za Tume. Katika ziara za mikoani, Tume ilifanya mijadala ya vikundi 170 vyenye jumla ya washiriki 2,099, na kwa upande wa Dar es Salaam jumla ya mijadala ya vikundi 31 vilivyokuwa na washiriki 1,466.

Mheshimiwa Rais, katika mikoa na wilaya zilizotajwa, Tume ilikutana na waathirika (wafiwa, majeruhi, waliopotelewa na ndugu, na walioharibiwa/kuibiwa mali); makundi maalumu ya wananchi (mama lishe/baba lishe, bodaboda, machinga, watoto wasio na makazi maalumu, na wajasiriamali wadogo); mahabusu waliotuhumiwa kuhusika na ghasia za wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu; viongozi wa dini; wawakilishi wa taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs); maafisa ustawi wa jamii; viongozi wa umma na wa kisiasa wastaafu na walioko madarakani; viongozi na watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama; waganga kutoka hospitali na vituo vya afya binafsi (private health facilities); Waganga Wakuu wa Mikoa (RMOs) pamoja na timu zao; Wakuu wa Mashtaka wa Mikoa; Kamati za Usalama za Mikoa na Wilaya; pamoja na wadau wengine waliokuwa tayari kutoa taarifa, ushahidi na maoni yaliyohitajika kwa ajili ya kazi za Tume.

Hata hivyo, vipo vyama vya siasa vichache, wanasiasa, wanaharakati na viongozi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali walioalikwa kwa maandishi kufika mbele ya Tume lakini hawakufanya hivyo. Tume inaridhika kuwa ambaye hakuja mbele ya Tume ni kwa utashi wake, tunaouheshimu, lakini si kwa kunyimwa, au kukosa fursa ya kuwa sehemu ya safari hii.

Mheshimiwa Rais, ushahidi wa kidijitali ulikuwa sehemu muhimu katika uchunguzi wa Tume, hususan, katika kuelewa madhara ya kibinadamu. Jumla ya picha mnato 450 na picha mjongeo 860 zilikusanywa kwa njia mbalimbali na baadhi zilikuwa zimesambazwa mtandaoni kwa zaidi ya mara moja. Picha hizo zilipatikana au ziliwasilishwa na mashuhuda wa matukio, watoa taarifa au vyombo vya ulinzi na usalama na vyanzo vya wazi (Open sources), ikiwemo vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Katika kubaini uhalisia wake, baadhi ya picha zilichambuliwa na kufanyiwa uchunguzi wa kisayansi (yaani Forensic and Geographic Information System Analysis) kwa kutumia wataalamu walioidhinishwa. Uchunguzi huo, hususan, kwa picha zilizokuwa zikizungunguka zaidi mitandaoni na kwenye vyombo vya habari, baadhi yake zilikuwa halisi na za kweli, nyingine hazikuwa halisi, na zimechezewa kwa kutumia akili unde au nusu ukweli. Methodolojia hii iliiwezesha Tume kutofautisha picha halisi na zisizo halisi. Mfano, mmojawapo ni picha ambayo imetumika sana kuonesha maiti zikiwa kwenye mifuko ya bluu zikizikwa kwenye kaburi la halaiki. Picha hiyo, kwa mujibu wa uchunguzi imekuwa ikitumika sehemu nyingine duniani.

Matumizi ya ushahidi na taarifa mseto kutoka vyanzo anuwai yalilenga kuzingatia na kukidhi viwango vya uthibitisho vinavyotumiwa na Tume za Uchunguzi za Kimataifa, yaani ushahidi ambao mtu yeyote mwenye busara ya kutosha atauamini (reasonable grounds to believe) ili kubaini hoja (factual findings). Tume ilitegemea zaidi ushahidi na taarifa mseto zilizokusanywa kutoka vyanzo anuwai vya moja kwa moja (Primary Sources) na vya rejea (Secondary Sources). Vilevile, vielelezo vya kidijitali, ikiwemo picha za satelaiti, vilifanyiwa uchunguzi wa kisayansi kwa kutumia wataalamu wenye sifa na viwango vya kimataifa, ili kuvithibitisha na kuvihakiki. Tume pia ilizingatia umuhimu wa kuwa na ushahidi unaojitosheleza na ushahidi mwingine unaohitaji kuungwa mkono (corroboration).

Matokeo ya Uchunguzi

Mheshimiwa Rais, baada ya kueleza methodolojia ya uchunguzi, naomba sasa nijielekeze kwenye matokeo ya uchunguzi.

Nitaanza na chanzo cha ghasia ambapo, katika muktadha wa Ripoti hii, tumetofautisha kati ya chanzo na kichocheo cha ghasia. Chanzo ni sababu, asili, chimbuko au mzizi wa suala ambalo limedumu kwa muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi na kuwa na athari hasi katika jamii. Kichocheo ni kitu kinachotia shauku, ari, hamasa, msukumo au motisha ya kufanya jambo fulani. Kwa maneno mengine, chanzo ni kama mafuta na kichocheo ni kama kiberiti.

Tume ilipokea na kuorodhesha jumla ya maeneo 31 yaliyotajwa na mashahidi kuwa ni chanzo cha ghasia za wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025. Baada ya kuchakata orodha hiyo, Tume iliainisha na kubainisha vyanzo vitano (5) na vichocheo nane (8). Nitaanza kuelezea vyanzo na baadaye vichocheo.

Kwa mujibu wa uchunguzi, ghasia za wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 zilitokana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwepo katika jamii kwa muda mrefu bila kutatuliwa. Vyanzo hivyo ni pamoja na vifuatavyo:

Mosi, yapo masuala ya kisiasa yanayojumuisha madai ya Katiba Mpya, demokrasia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, malalamiko ndani ya vyama vya siasa, madai ya maboresho ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na mfumo mzima wa uchaguzi;

Pili, ni masuala ya kiuchumi yanayojumuisha ugumu wa maisha; ukosefu wa ajira na kukosekana kwa usawa katika fursa za ajira na za kiuchumi; mazingira ya biashara na uwekezaji yasiyo rafiki; utitiri wa kodi na tozo na mfumo usio rafiki wa utozaji na ukusanyaji;

Tatu, masuala ya kijamii yanayojumuisha mmomonyoko wa maadili na kushuka kwa uzalendo, kutopatiwa ufumbuzi na majibu stahiki kwa kero katika jamii kama vile; rushwa, ubadhirifu wa mali za umma na madai ya utekaji na kupotea kwa watu.

Kwa mujibu wa takwimu za Jeshi la Polisi, kati ya mwaka 2023 hadi 2025 watu 758 walipotea, kutekwa au kujiteka, kati ya hao, watu 513 walipatikana na mashauri 8 yalifunguliwa ambapo upelelezi unaendelea. Hivyo, katika jumla ya watu 758 waliopotea, kutekwa au kujiteka kwa sababu mbalimbali watu 245 hawajapatikana. Takwimu hizo zinaakisi malalamiko ya wananchi kuhusu masuala ya utekaji na kupotea kwa watu.

Katika matukio hayo, Jeshi la Polisi lilieleza kuwa sababu za kupotea au kutekwa ni pamoja na: masuala ya kimapenzi (113); imani za kishirikina (87); waliotekwa na wahalifu kwa lengo la kujipatia kipato au mali (97); waliojihusisha na vitendo vya kihalifu kwa chuki na kulipiza visasi (47); waliojiteka wao wenyewe kutokana na sababu mbalimbali za kudaiwa (madeni) na kukwepa mkono wa sheria (56); walioondoka bila taarifa (74); na usafirishaji haramu wa binadamu (39).

Nne, utendaji usioridhisha wa baadhi ya watendaji na watumishi wa umma, hususan, ngazi za chini (Mamlaka za Serikali za Mitaa) ikiwa ni pamoja na kutosikiliza au kutatua kero za wananchi kwa wakati, na utekelezaji hafifu wa mapendekezo ya Tume zinazoundwa; na

Tano, ni masuala yanayohusu uhusiano wa kimataifa katika dunia ya leo na ijayo ambapo mataifa mengi yanatanguliza mbele maslahi yao kama msingi wa mahusiano na kujaribu mbinu na mikakati mbalimbali ya kujiweka katika nafasi nzuri kuendeleza maslahi yao katika nchi nyingine, hasa zinazoendelea na zenye raslimali nyingi.

Mheshimiwa Rais, ushahidi na taarifa vimeonesha kuwa baadhi ya wanasiasa na wanaharakati walitumia changamoto za wananchi zinazotokana na vyanzo mbalimbali vilivyobainishwa kama fursa ya kuwashawishi na kuwachochea wananchi kushiriki katika ghasia za wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu kwa kutumia kaulimbiu na matamko mbalimbali.

Ushahidi na taarifa vimeonesha kuwa baadhi ya wanasiasa na wanaharakati walitumia changamoto za wananchi zinazotokana na vyanzo mbalimbali vilivyobainishwa kama fursa ya kuwashawishi wananchi kushiriki katika ghasia za wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu kwa kutumia kaulimbiu na matamko mbalimbali. Tathmini ya Tume imebaini kuwa, vilikuwepo vichocheo mahsusi vilivyoamsha ari ya kufanya ghasia wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu. Vichocheo hivyo vinaweza kuwekwa katika makundi matatu.

Kundi la kwanza linahusu mitandao ya kijamii ambayo, kwa mujibu wa mashahidi waliokuja mbele ya Tume, mitandao hiyo ilitumika kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa kiwango kikubwa kuliko ambavyo imewahi kutokea nchini Tanzania. Aidha, waliibuka wabuni mada kwenye mitandao (content creators), ikiwemo mada za kuhamasisha wananchi kutoshiriki Uchaguzi Mkuu na/au kuhakikisha haufanyiki. Mitandao hiyo ilitumika pia kuandaa majukwaa ya majadiliano na kupanga mbinu na kuwaelekeza waliokubali kushiriki vurugu za kuzuia Uchaguzi Mkuu namna ya kufanikisha lengo hilo. Wapo pia mashahidi walioshiriki kufanya ghasia waliokuja mbele ya Tume na kukiri kuwa baadhi yao walipewa simu maalumu za mkononi na kupewa kazi ya kupiga picha na video za matukio kama vile majeruhi na vifo au kupiga picha jirani na magari ya JWTZ, sambamba na picha za maeneo ambayo wafanya ghasia walikuwa wamefanikiwa kufanya uharibifu na kisha picha na video zote hizo kurushwa moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii ili kuibua hasira za wananchi na kuwahamasisha nao wajitokeze kufanya ghasia kwa vile waliaminishwa kuwa JWTZ iko pamoja nao.

Kundi la pili la vichocheo ni kauli za baadhi ya wanasiasa ambazo zilikuja kugeuka na kuwa kaulimbiu za waliokuwa wanafanya ghasia. Mifano ya kauli mbiu hizo, ambazo baadhi ya washiriki katika ghasia walikiri kuzitumia ni zifuatazo:

  1. “No Reforms No Election”;
  2. (b) “Oktoba Tunatiki”;
  3. (c) “Oktoba Tunatoka”;
  4. (d) “Tumedhamiria uchaguzi hautafanyika”;
  5. (e) “Samia Must Go”;
  6. (f) “Tunataka kuikomboa nchi yetu”;
  7. (g) “Hakuna uchaguzi chini ya Serikali hii”;
  8. (h) “Tutahakikisha nchi haisimami mpaka Serikali iondoke”;
  9. (i) “Hakutakuwa na Uchaguzi bila mabadiliko ya mfumo”;
  10. (j) “Serikali hii imepoteza uhalali wa kuongoza nchi”;
  11. (k) “Ni lazima shinikizo la wananchi liongezeke hadi Serikali iondoke”; na
  12. (l) “Mchakato wa kuwapata wagonbea umekiuka taratibu, wagonbea si halali, mchakato urudiwe”.

Kundi la tatu la vichocheo linahusu baadhi ya maeneo ya nchi ambapo waliokusudia kugombea viti vya udiwani na ubunge majina yao yalikatwa kwenye ngazi za juu za vyama hivyo, na hivyo wakaona kuwa ghasia zilizokuwa zinafanywa zinawasaidia kudai mabadiliko ya mfumo wa kupata wagombea ndani ya vyama vyao, na wakashiriki chini-chini kuwahamasisha wafuasi wao kushiriki ghasia.

Lengo la Wahusika

Mheshimiwa Rais, kabla ya kuzungumzia lengo la walioshiriki matukio yaliyokuwa yanachunguza ghasia ni muhimu kupata jibu la swali iwapo yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 yalikuwa maandamano ya amani, na hivyo kustahili kinga na utetezi kwa mujibu wa mikataba au sheria za kimataifa, kikanda na kitaifa, au la. Majibu ya swali hilo ni muhimu kwa vile baadhi ya wadau, ikiwemo watetezi wa haki za binadamu ndani na nje ya nchi, walidai kuwa wahusika walikuwa na haki ya kikatiba kufanya maandamano katika siku hiyo hata kama ilitangazwa kuwa siku ya Uchaguzi.

Hivyo, Tume ilifanya uchambuzi wa mikataba, sheria na kanuni mbalimbali za kimataifa, kikanda na kitaifa kuhusu dhana na haki ya maandamano ya amani na mipaka yake.

Mheshimiwa Rais, maandamano ni miongoni mwa haki za msingi zinazotambuliwa na Ibara ya 21 ya Mkataba wa Kimataifa Kuhusu Haki za Kiraia na za Kisiasa, 1966 (International Covenant on Civil and Political Rights (ICCPR)) uliopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 16 Desemba, 1966. Pamoja na mambo mengine, Ibara hii inatambua haki ya kukusanyika kwa amani. Aidha, mkataba huu unaruhusu Serikali kuweka mipaka kwa ajili ya: usalama wa taifa; usalama wa umma; afya au maadili ya jamii; na kulinda haki za watu wengine. Vilevile, uwekaji wa mipaka ni lazima uzingatie haki ya msingi ya kuishi kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 6 inayotaja kuwa kila binadamu ana haki ya asili ya kuishi pamoja na Ibara ya 21 inayotambua wigo na ukomo wa maandamano kama yapo kisheria, halali, ulazima, uzingatiwaji wa uwiano na ni lazima kwa ulinzi na usalama wa umma.

Haki ya kukusanyika na kuandamana kwa amani imeelezwa katika Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu, 1981 na Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, 1999 kuwa ni haki ya msingi inayotakiwa kulindwa na kuheshimiwa. Katika Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu (African Charter on Human and Peoples’ Rights) (Mkataba wa Banjul), 1981, haki ya kukusanyika kwa uhuru na amani imetambuliwa na Ibara ya 11. Ibara hiyo imeweka wazi kuwa kila mtu ana haki ya kukusanyika kwa uhuru pamoja na wengine. Aidha, Serikali zinaweza kuweka masharti kuhusu haki hiyo kwa ajili ya maslahi ya usalama wa taifa, usalama wa umma, afya, maadili, pamoja na haki na uhuru wa watu wengine.

Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu imeweka Mwongozo Kuhusu Uhuru wa Kujumuika na Kukusanyika Barani Afrika (The Guidelines on Freedom of Association and Assembly in Africa) uliopitishwa mwaka 2017 ili kulinda haki ya maandamano barani Afrika. Mwongozo huo unazitaka nchi wanachama kuhakikisha maandamano ya amani yanaruhusiwa kwa mujibu wa sheria za nchi, wajibu wa Serikali kuruhusu mijumuiko unabainishwa katika Katiba za nchi; Polisi wanapaswa kulinda waandamanaji, na matumizi ya nguvu kupita kiasi hayaruhusiwi.

Mheshimiwa Rais, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, imeweka haki za msingi za binadamu ikiwemo haki ya kuishi na uhuru wa kukusanyika na kuandamana kama sehemu ya kutumia haki ya uhuru wa kutoa maoni na kujieleza pamoja na uhuru wa kukutana wa watu wengine kwa hiari na kwa amani. Aidha, Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi (Sura ya 322), Kanuni za Jeshi la Polisi na miongozo mingine ya kitaifa inaelezea mipaka ya maandamano na matumizi ya nguvu na silaha.

Kwa mujibu wa sheria na kanuni hizo, Tume ilichambua kama yaliyotokea tarehe 29 Oktoba, 2025 yalikuwa maandamano ya amani na ikabaini yafuatayo:

  1. Maandamano ya amani hayafanywi siku ya Uchaguzi Mkuu kwa kuwa haki ya kufanya maandamano wakati huo inaweza kuingilia haki za wananchi wengine, hususan haki ya kupiga kura na haki ya kugombea. Kufanya maandamano siku ya uchaguzi sio jambo la kawaida katika nchi zenye demokrasia na utawala wa sheria;
  2. Haki ya kila mtu kushiriki uchaguzi kama mpiga kura au mgombea ni haki ya kikatiba kwa mujibu wa Ibara ya 5 ambayo haipaswi kupokwa. Ghasia zilipangwa na kutekelezwa siku iliyotangazwa kisheria kuwa ni siku ya Uchaguzi Mkuu. Hivyo, kufanya ghasia siku hiyo ilikuwa ni kupoka haki ya Kikatiba na Kisheria za wananchi wengine ikiwemo haki ya kupiga na kupigiwa kura;
  3. Washiriki wa ghasia za wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wali-beba silaha za aina mbalimbali zikiwemo mawe, nondo, mkuki, sururu, fimbo, marungu, visu, viberiti, vilipuzi, bunduki, manati, kombeo, rato na mapanga jambo ambalo haliruhusiwi kisheria katika maandamano ya amani. Hii ni kinyume na sheria na taratibu za Kimataifa (Ibara ya 21 ya Mkataba wa Haki za Kiraia na Kisiasa, 1966), Kikanda (Ibara ya 11 ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Watu na Binadamu, 1981 na Ibara ya 10 na 11 ya Mkataba wa Ulaya wa Haki za Binadamu, 1950) na Kitaifa (Ibara ya 18 na 20 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977) haziruhusu maandamano ya watu waliobeba silaha; na
  4. Sheria na taratibu za Kimataifa, Kikanda na Kitaifa haziruhusu maandamano yanayosababisha taharuki katika jamii, kuhatarisha usalama wa Taifa, kusababisha uharibifu wa mali za umma na binafsi pamoja na kuhatarisha maisha ya watu wengine. Mambo hayo yakifanyika, yanakuwa kinyume cha tafsiri ya maandamano ya amani.

Kwa kuzingatia sheria na kanuni zinazotawala maandamano ya amani kimataifa, kikanda na kitaifa na ushahidi uliowasilishwa mbele ya Tume, ni maoni ya Tume kuwa kilichotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba, 2025 hakikuwa maandamano ya amani na hivyo kuwa nje ya kinga za sheria na kanuni hizo.

Isitoshe, Tume imepata ushahidi usio na shaka kuwa matukio ya ghasia za Oktoba 2025 yalipangwa, yaliratibiwa, yalifadhiliwa na kutekelezwa na watu waliopata mafunzo. Waratibu walitumia mbinu mbalimbali, ikiwemo kuwatumia watu wasio na ufahamu wa kina na vijana waliokata tamaa, huku wakihakikisha kuwa vitendo vya ghasia vinafanyika kwa wakati mmoja katika maeneo tofauti ili kuwachanganya na kuwatawanya Polisi.

Mheshimiwa Rais, taarifa na ushahidi unathibitisha kuwa, kuna watu waliokuwa wakizunguka katika maeneo mbalimbali kama vile mitaani, vyuoni, kwenye masoko na stendi za mabasi wakishawishi na kuwaandikisha (recruit) watu mbalimbali kushiriki katika ghasia za wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu. Mfano; watoto wanaoishi katika mazingira magumu, waendesha pikipiki (bodaboda) na wajasiriamali wadogo walieleza kuwa walipewa fedha kati ya sh. 10,000 hadi sh. 50,000 na waliahidiwa ajira na maisha bora. Ilielezwa zaidi kuwa kuanzia tarehe 12 Oktoba, 2025 hadi 28 Oktoba, 2025 waliwekwa pamoja, kupewa mafunzo, kuandaliwa na kuhamasishwa kuwa sehemu ya kuanzisha na kushiriki ghasia siku ya Uchaguzi.

Aidha ilibainika kuwa, makundi yaliyoshawishiwa ndio walihusika zaidi kutekeleza ghasia, wakati wahusika wakuu wa ghasia na waratibu hawakuwepo kwenye maeneo ya matukio, hali iliyochangia kwa kiasi kikubwa kutokukamatwa kwao, huku wengi wa waliokamatwa wakiwa ni wananchi wa kawaida wakiwemo, wafuata mkumbo, au kushawishiwa kwa malipo kidogo au ahadi za kunufaika na mabadiliko waliyoyapanga, bila kuwa na uelewa wa malengo halisi ya wahusika wakuu na waandaji.

Kutokana na ushahidi, taarifa na maoni yaliyopatikana, Tume imebainisha na kuainisha mbinu 16 zilizotumiwa na wahusika wakuu na waratibu kufanikisha ghasia za wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu. Baadhi ya mbinu hizo ni: kuweka vizuizi barabarani, kuchoma moto mali mbalimbali, matumizi ya ishara mbalimbali kutambuana, matumizi ya pikipiki kuanzisha ghasia, na uanzishaji wa ghasia sehemu nyingi kwa wakati mmoja.

Mheshimiwa Rais, kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa kwenye Tume, na maelezo niliyoyatoa hapo juu, matukio yale yalikuwa na malengo makuu yafuatayo:

Kutokana na ushahidi uliotolewa mbele ya Tume, lengo kuu la ghasia za Oktoba, 2025 ilikuwa kuzuia au kuvuruga Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba, 2025. Lengo hili linajidhihirisha kupitia vitendo mbalimbali vya wafanya ghasia ikiwemo kuharibu vituo na vifaa vya kupigia kura; kushambulia askari, mawakala na wasimamizi wa uchaguzi; kuharibu mali za wasimamizi wa uchaguzi; vitisho, madhara na mashambulizi dhidi ya wananchi waliojitokeza kupiga kura; na kupora mali za wasimamizi wa uchaguzi.

Kupitia ushahidi, taarifa na maoni ikiwemo majadiliano na wataalamu wa uchumi, ilionekana kuwa, kupitia ghasia za Uchaguzi Mkuu, vijana walioshiriki walipata mwanya wa kufikisha ujumbe kwa Serikali kuwa wanataka kusikilizwa na kutatuliwa changamoto zinazowakabili. Ilibainika kuwa waratibu wa ghasia walitumia malalamiko ya wananchi dhidi ya Serikali wakati wanawashawishi kushiriki kwenye ghasia.

Kwa mujibu wa ushahidi, taarifa na maoni, miongoni mwa wafanya ghasia, yalijitokeza makundi makubwa yaliyokuwa na lengo la kuiba na kupora mali. Ushahidi wa moja kwa moja wa waathirika walioporwa mali au kuibiwa pamoja na picha za kidigitali (CCTV) na za kupitia picha mnato na picha mjongeo, unaonesha namna vitendo vya wizi na uporaji vilivyofanywa na makundi hayo. Mfano wizi na uporaji uliotokea katika maduka na maeneo mengine ya biashara kwenye Mikoa iliyotembelewa na Tume. Vitendo hivi vilithibitishwa pia na baadhi ya wamiliki wa mali na biashara waliofika mbele ya Tume kutoa ushahidi.

Madhara ya Ghasia

Mheshimiwa Rais, uliiagiza Tume ichunguze na kubaini madhara makuu yaliyotokea wakati wa ghasia za tarehe 29 Oktoba, 2025 hususan, yale ya kibinadamu, kiuchumi na kijamii. Tume ilipokea na kuchambua ushahidi, taarifa na maoni kutoka kwa waathirika, wataalam, na washauri mbalimbali ili kubaini ukubwa na uhalisia wa madhara yaliyotokea.

Sheria za kimataifa, kikanda na Ibara 14 ya Katiba yetu inampa kila binadamu haki ya uhai na ulinzi wa haki hiyo na jamii. Haki hiyo inaweza kunyimwa tu kwa utaratibu uliyowekwa na sheria. Tume haikuchukulia uchambuzi wa idadi ya vifo kama upekuzi au msako wa namba, bali inaupa uzito sana uhai wa binadamu na heshima kubwa anayostahili kila maiti baada ya kifo ambao pia ndio utamaduni wetu.

Kwenye tathmini yake Tume imetegemea vyanzo vingi ya ushahidi, ushauri wa kitaalam na taarifa, zikiwemo kutoka kwa wafiwa, waathirika na wahudumu wa afya mahospitalini. Imechambua taarifa kutoka Wizara ya Afya, Vituo vya Afya vya sekta ya umma ngazi ya Taifa, Mkoa na Wilaya na maeneo yao na zile za Hospitali binafsi. Tume ilipokea pia vibali vya mazishi kutoka kwa familia. Vyanzo vingine ni Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) yenye mamlaka ya usajili wa vifo; Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) yenye jukumu la uchunguzi wa sayansi jinai na inayosimamia uchunguzi wa vinasaba; Halmashauri za Miji na maoni ya Wataalam wa Pathologia na fani nyingine. Tume ilipata fursa ya kuhojiana moja kwa moja na waganga na madaktari bingwa themanini (80) wa sekta ya umma na binafsi kutoka mikoa 11 iliyotembelewa na Tume, sambamba na picha mnato na mjongeo zilizothibitika kuwa na ukweli.

Tathmini ya Tume ni kuwa jumla ya vifo vilivyotokana na ghasia za Uchaguzi Mkuu ni 518, ambapo, wanaume ni 490, sawa na asilimia 94.6 na wanawake ni 28, sawa na asilimia 5.4. Vingi kati vya vifo hivyo vilikuwa sio vya kawaida (unnatural). Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa na vifo vingi zaidi, ukiwa na vifo 182, ikifuatiwa na Mkoa wa Mwanza vifo 90; Mbeya vifo 80; na Mkoa wa Arusha vifo 53.

Kati ya vifo hivyo 518, ishirini na moja (21) vilikua vya watoto. Katika kundi hilo, 15 walikuwa watoto wenye umri kati ya miaka 15 – 17, wanne (4) walikuwa na umri kati ya miaka 7 – 10, na wawili (2) umri chini ya miaka mitano.

Vifo 502 sawa na asilimia 96.9 vilikuwa vya raia (civilians), na 16 sawa na asilimia 3.1 vilikuwa vya maafisa na askari wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Kati ya watu 518 waliofariki, 373 walifikishwa hospitali wakiwa wamefariki, majeruhi 121 walifariki wakati wakiwa wanapatiwa matibabu, na maiti 24 hakuna taarifa kutoka vituo vya kutolea huduma za afya.

Kati ya maiti 518, maiti 480 sawa na asilimia 92.7 zilitambuliwa na kuchukuliwa na ndugu na familia.

Mheshimiwa Rais, uchunguzi wa maiti (post-mortem) chini ya Sheria ya Uchunguzi wa Vifo Vyenye Mashaka ulifanyika katika hospitali mbalimbali za Rufaa Jijini Dar es Salaam na mikoani kwa maiti 260. Maiti nyingine hazikufanyiwa uchunguzi kwa kukosekana kwa ridhaa za ndugu na familia, ambao walitaka kuchukua maiti za ndugu zao kwa haraka ili wazike. Kati ya maiti 260 zilizofanyiwa uchunguzi nyingi zilibainika kuwa na majeraha ya kutobolewa na vitu vyenye ncha kali au kuvunjika katika sehemu mbalimbali za miili. Majeraha hayo yalisababisha kupoteza damu nyingi hivyo kusababisha vifo. Aidha, maiti 21 hazikuonesha aina yoyote ya majeraha na maiti 6 zilikuwa na majeraha ya moto.

Maiti 485 kati ya maiti 518 zilitambuliwa na kuchukuliwa na ndugu kutoka vituo vya afya kwa ajili ya mazishi na maiti 9 hazikutambuliwa na hazikuchukuliwa. Kati ya hizo, maiti sita (6) zilizikwa kwa mujibu wa Kanuni za Utupaji wa Taka na Mabaki ya Miili ya Binadamu, na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Maiti 3 zote kutoka Mkoa wa Dar es Salaam hadi tarehe 31 Machi, 2026 zilikuwa bado katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Uchunguzi wa vinasaba (DNA) ulifanyika kwa maiti 274 kwa lengo la kuchukua taarifa za kutambua maiti kwa usahihi. Taarifa hizi za uchunguzi zitasaidia kutambua ndugu wa marehemu kwa usahihi pale itakapohitajika.

Tume ilimuagiza Mtaalam na Daktari Bingwa wa Pathologia kufanya uchambuzi wa taarifa za uchunguzi wa maiti (post mortem reports) ili kubaini sababu halisi na namna vifo hivyo vilivyotokea na maeneo ya mwili yaliyoathiriwa. Katika kutekeleza agizo hilo, taarifa za uchunguzi wa maiti 219 zilifanyiwa uchambuzi.

Uchambuzi huo ulibainisha kuwa maiti zote 219 zilitokana na vifo visivyo vya kawaida. Sababu ya kifo ya moja kwa moja (immediate cause) ya vifo 147 ilikuwa ni kuvuja damu nyingi, 41 kujeruhiwa ubongo (brain injury), 12 kukosa hewa; 9 kujeruhiwa uti wa mgongo; 5 majeraha mbalimbali, 4 mshtuko wa moyo na kifo kimoja (1) sababu halisi haikujulikana. Vilevile, sababu halisi ya vifo (underlying/antecedent cause) vingi ilikuwa kupigwa risasi vifo 197 sawa na asilimia 90.0 na vifo 22 sawa na asilimia 10 havikuhusiana na risasi.

Taarifa ya uchambuzi wa Mtaalam ilibainisha kuwa maiti 166 zilikuwa na majeraha sehemu za mikono na miguu, maiti 36 zilikuwa na majeraha sehemu za kifua na tumbo na maiti 12 zilikuwa na majeraha sehemu za kichwa na shingo. Maiti moja ilikuwa haina baadhi ya viungo.

Hata hivyo, kutokana na mazingira ya ghasia pamoja na madai ya baadhi ya mashahidi, idadi ya vifo inaweza kubadilika kutokana na uwezekano wa kuwepo kwa baadhi ya ndugu ambao walizika miili ya wapendwa wao bila kuifikisha kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na hawakupata fursa ya kufika mbele ya Tume. Vilevile, inawezekana kulikuwa na majeruhi ambao waliamua kutibiwa nje ya mfumo rasmi wakafariki bila taarifa zao kufikishwa panapostahili. Tume pia ilipokea ushahidi wa madai kuhusu watu kupotea au kutopatikana tangu wakati wa Uchaguzi Mkuu. Kwa kuzingatia ufafanuzi uliotolewa, idadi ya vifo iliyotolewa kwenye Ripoti hii inaweza isiwe ya mwisho (not final and conclusive).

Tathmini ya Tume Kuhusu Vifo

Mheshimiwa Rais, Tume inatambua kuwa vifo vimeacha pengo kubwa katika familia na jamii na kuathiri kwa kiasi kikubwa nguvu kazi ya taifa. Madhara yaliyotokea yamesababisha baadhi ya familia kupoteza tegemeo lao kuu na hivyo kuziweka katika hali ya utegemezi wa kiuchumi na kijamii.

Tume ilipokea ushahidi kuhusu watu 39 ambao inadaiwa kuwa walifariki au kupotea, ikiwemo baadhi ambao awali inasemekana miili yao ilionekana kwenye hospitali/vituo vya afya na kutambuliwa na ndugu lakini baadaye miili hiyo haikuonekana tena walivyoifuata huko. Wengine walisema kuwa walizika nguo za marehemu ili tu kuhitimisha msiba. Hili ni moja ya jambo muhimu ambalo Tume imetoa mapendekezo ili lifanyiwe kazi mapema iwezekanavyo.

Tume pia ilipokea madai kutoka kwa waathirika na mashahidi wengine kuhusu watu kupigwa risasi, kujeruhiwa au kuuawa katika maeneo ambayo hayakuwa na ghasia au vurugu. Kuna madai ya watu kupigwa risasi kwenye makazi yao ikiwa ni pamoja na ndani ya nyumba au sebuleni na ndani ya maduka. Hizo ni tuhuma nzito zinazoashiria uwezekano wa matumizi ya silaha za moto kinyume na miongozo na kanuni za kimataifa, kikanda na kitaifa kuhusu matumizi ya silaha hizo. Hili ni jambo jingine linalohitaji kufanyiwa upelelezi wa kina na wa kijinai.

Tathmini ya Tume inaonyesha kuwa hadi tarehe 31 Machi 2026, majeruhi waliokuwa wamehudumiwa katika vituo vya umma na binafsi vya kutolea huduma za afya kutokana na ghasia za wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu, walikuwa 2,390. Kati yao, raia (civilian) walikuwa 2,270 sawa na asilimia 95.0, na maafisa na askari wa vyombo vya ulinzi na usalama walikuwa 120 sawa na asilimia 5.0. Kuna uwezekano kuwa baadhi ya majeruhi hawamo katika idadi hiyo kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na: uwezekano wa baadhi ya majeruhi kuendelea kupata matibabu nje ya vituo rasmi vya kutolea huduma za afya na wengine kukimbilia nchi jirani, hususan, kwa mikoa ya mipakani ya Mbeya, Songwe, Arusha na Mara kwa hofu ya kukamatwa.

Majeruhi waliopata majeraha makubwa walikuwa 219 sawa na asilimia 9.2 ya majeruhi wote. Kati yao, majeruhi 197 walikuwa na majeraha yaliyotokana na risasi na 22 hayakutokana na risasi. Wengi wa majeruhi katika kundi hili walilazimika kulazwa ili kupata huduma za matibabu.

Aidha, majeruhi 2,171 walipata majeraha madogo ambapo walipata huduma na kuruhusiwa. Kati yao, majeruhi 833 walikuwa na majeraha yaliyotokana na risasi katika sehemu za chini ya mwili, wakati majeruhi 126 walikuwa na majeraha sehemu za juu ya mwili. Uchunguzi wa kitabibu kwa majeruhi wote waliofika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ulibainisha kuwa hapakuwepo na majeruhi yeyote aliyeteswa (torture).

Mheshimiwa Rais, kulikuwepo na madai kupitia vyombo vya habari vya kimataifa na mitandao ya kijamii kuhusu kuwepo kwa makaburi ya halaiki katika eneo la makaburi ya Kondo, Kunduchi, Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam. Tume ilifanya uchunguzi ikiwa ni pamoja na kutembelea na kukagua eneo lote la makaburi, kufanya mahojiano na kupata taarifa ya Afisa Msimamizi wa makaburi katika Manispaa ya Kinondoni na kuchukua ushahidi wa msimamizi wa makaburi ya Kondo.

Vilevile, Tume iliwashirikisha wataalamu mbalimbali ili kufanya uchunguzi wa kisayansi kuhusu madai hayo ikiwa ni pamoja na picha ya satelaiti iliyotumika. Maoni ya wataalam hao, wakiwemo wa uchambuzi wa mbali na mifumo ya Taarifa za Kijiografia (Remote Sensing and Geographic Information Systems) ni kuwa madai haya hayakuweza kuthibitishwa.

Tume pia ilifanya ukaguzi na kubaini kuwa eneo la makaburi ya Kondo linazungukwa na makazi ya watu, na ambalo bado linatumika kwa shughuli za kilimo cha msimu na lina ulinzi muda wote. Kutokana na ushahidi na uchunguzi wa Tume wa uwandani, na kwa kuzingatia hali iliyoonekana katika eneo la Makaburi ya Kondo pamoja na taarifa za Wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi, Tume imebaini kuwa, madai ya kuwepo kwa makaburi ya halaiki eneo la Kondo hayakuweza kuthibitishwa.

Mheshimiwa Rais, madhara makubwa ya kiuchumi ni yale yanayohusu mali za watu binafsi na mali za Serikali kuharibiwa.

Tume imebaini kutoka vyanzo mbalimbali kuwa mali iliyoharibiwa ina thamani ya sh. bilioni 125. Kati ya mali hizo, mali za sekta binafsi (watu binafsi, vituo vya mafuta, CCM na benki) zina thamani ya sh. bilioni 89.0 sawa na asilimia 71.2 na mali za umma (Mali za Serikali na taasisi kama vile Shule, TRA, Mahakama, Polisi, DART, TANROADS, TANESCO na TTCL) zina thamani ya sh. bilioni 36 sawa na asilimia 28.8. na Sekta binafsi ndio imepata athari kubwa kuliko sekta ya umma.

Ushahidi wa Waathirika wengi waliopoteza mali binafsi unaonyesha machungu waliopata na wanayoendelea kuwa nayo. Mfano mstaafu mmoja aliieleza Tume kuwa: “Baada ya kustaafu nilienda Equity Bank Tanzania Limited (EFTA) kwa ajili ya Mkopo wa gari la kufanyia biashara kiasi cha sh. 180,000,000/- kabla ya riba, nikanunua Tipper la mchanga lenye namba za usajili T 476 EMW ambapo kila mwezi nilikuwa narejesha sh. 6,942,401/-. Gari hiyo baada ya kuinunua ilikuwa inaegeshwa kwenye eneo la TANROAD Kimara Temboni baada ya kazi. Tangu gari inunuliwe ilifanya kazi kwa miezi miwili tu na tarehe 29.10.2025 wakati wa ghasia za Uchaguzi Mkuu eneo la kuegesha magari la TANROAD liliwamiwa na gari yangu ikawa imechomwa moto na kuteketekea kabisa. Nimejaribu kutafuta msaada kwenye bima ila imeshindikana kwa kuwa ilikuwa na bima kubwa (comprehensive) na sio ya majanga ya kisiasa (political risk).”

Wajasiriamali wadogo na wa kati waliporwa au kuibwa mali zenye thamani ya sh. bilioni 1.6. Shahidi kutoka Tegeta, Dar es Salaam aliyeeleza kuwa: “Mimi ni mfanya biashara wa simu, siku ya Uchaguzi Mkuu duka langu lilivamiwa na wafanya vurugu wakaiba simu zote ndani ya duka, simu zenyewe ni za mkopo, nina hali mbaya sana hata sijui nitafanyaje, uwezo wangu haupo tena, hapa nilipo nimejaa msongo wa mawazo.”

Kuna uwezekano wa thamani ya mali zilizoharibiwa au kuibiwa kutoka kundi hili kuwa kubwa zaidi kutokana na changamoto ya utunzaji wa kumbukumbu na taarifa za biashara za wajasiriamali hao.

Zipo pia hasara kwa upande wa Sekta ya Fedha, kwa mfano, jumla ya sh. milioni 621.7 ziliiporwa na kuibiwa kutoka kwenye viotomotela (ATM) vya Mabenki makubwa matatu, CRDB, NMB na NBC.

Sekta nyingine zilizoathirika kiuchumi ni kushuka kwa Masoko ya Fedha, mabadiliko ya mzunguko wa fedha, usafiri na usafirishaji, na utalii.

Kwa mujibu wa taarifa ya Februari 2026 ya Kampuni ya Kimataifa ya Kutathmini Kiwango cha Nchi Kuaminiwa katika Kukopa ya Moody’s, kiwango cha Tanzania cha kuaminiwa katika kukopa (credit rating) kimebakia katika kiwango cha B1. Hali hiyo inaifanya Tanzania iendelee kuaminika na wakopeshaji kama ilivyokuwa kabla ya Uchaguzi Mkuu. Aidha, wachumi waliokutana na Tume walisisitiza kuwa iwapo vihatarishi vya kisiasa (political risks) havitashughulikiwa ipasavyo, kiwango hicho kinaweza kushuka.

Kwa mujibu wa Benki Kuu, uamuzi wa Mheshimiwa Rais, kuunda Tume ya Uchunguzi ulikuwa ni uamuzi mzuri sana, na ni kianzio muhimu cha kujenga imani (confidence) kwa Uchumi wa Tanzania.

Mheshimiwa Rais, Tume ilibaini kuwepo kwa watu waliopata madhara ya kijamii (social), kihisia (emotional), kiroho (spiritual), kiakili (mental) na kimwili (physical) ambao wanahitaji kupatiwa huduma ya afya ya akili, kisaikolojia na kijamii (Mental Health and Psychosocial Support – MHPSS).

Matukio kama vile vifo, ulemavu wa kudumu, majeraha ya mwili, kupoteza ndugu na kuporwa au kuharibiwa mali zilizowekezwa kwa muda mrefu yamesababisha athari za kisaikolojia na changamoto za kijamii miongoni mwa wananchi. Athari hizo zimejitokeza kwa namna tofauti, ikiwemo watu kupata msongo wa mawazo, huzuni, hofu, kupoteza imani ya mifumo ya kijamii na kisiasa.

Aidha, katika mazingira hayo kumeibuka migawanyiko ambapo jamii imepoteza mshikamano na kuaminiana. Kundi lingine ambalo liliathirika ni waganga, wauguzi na wahudumu kwenye Vituo vya afya, wengi wao walifanya kazi saa 72 mfululizo bila kwenda makwao, ambako waliacha familia na kutokuwa na mawasiliano nao kipindi hicho. Kuna ambao wakikumbuka yaliyotokea na huduma walizotoa, hawataki tena kuendelea na fani zao.

Shahidi mwingine kutoka Mkoa wa Shinyanga alisema kuwa: “Baada ya kupigwa risasi ya mguu nilipoteza uwezo wa kutembea kama zamani, maisha yangu yamebadilika sana. Ukosefu wa baiskeli ya kunisaidia kusafiri kutoka eneo moja kwenda lingine, hususan, kwenda shuleni, umeninyima uhuru wa kushiriki maisha ya kawaida kama vijana wenzangu. Nimejikuta nikiwa na huzuni na msongo wa mawazo kwa sababu siwezi kufika shuleni, kushirikiana na marafiki, wala kuendelea na ndoto zangu. Mara nyingi najihisi sina thamani na nimeachwa peke yangu, hali ambayo imenifanya niishi katika upweke.”

Wakati wa kusikiliza mashahidi, Tume ilibaini uwepo wa watu 710 wenye uhitaji wa msaada wa kisaikolojia na ilichukua hatua. Iliwaunganisha moja kwa moja na Wizara yenye dhamana ya masuala ya Maendeleo ya jamii ili waweze kuchunguzwa na kupatiwa msaada wa kisaikolojia. Tunashukuru hilo lilifanyika na waathirika wote 710 walifikiwa na walipatiwa huduma za kisaikolojia Mikoani na Wilayani.

Hatua za Kubaini, Kuzuia na Kudhibiti

Mheshimiwa Rais, kuhusu hatua zilizochukuliwa katika kubaini, kuzuia na kudhibiti ghasia, uchunguzi umebaini masuala kadhaa kama ifuatavyo:

Viashiria vya kutokea kwa ghasia siku ya Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba 2025, vyenye lengo la kuzuia au kuvuruga Uchaguzi, vilianza kujitokeza kupitia mitandao ya kijamii miezi takriban sita kabla ya Siku ya Uchaguzi. Kwa nyakati tofauti kuanzia mwezi Aprili hadi Oktoba 2025, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilikuwa ikiwasilisha taarifa zinazoonesha viashiria vya ghasia kwa vyombo vya ulinzi na usalama na taasisi nyingine ili zichukue hatua stahiki. Tarehe 17 Oktoba, 2025, TCRA ilibaini bango mitandaoni lililokuwa na maudhui yanayohamasisha ghasia na kuzuia uchaguzi. Bango hilo lilionesha malengo ya maandamano yaliyodaiwa kuwa ya Kitaifa, kuwa ni kuzuia na kuvuruga Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 29 Oktoba, 2025. Katika taarifa yake ya tarehe 26 Oktoba, 2025, TCRA ilibaini kuwepo kwa mijadala katika moja ya mitandao ya kijamii kuhusu namna watakavyotekeleza ghasia siku ya Uchaguzi. Majadiliano hayo yalionesha kuwa, siku ya uchaguzi wangeharibu mifumo ya umeme ili kuiingiza nchi gizani, kuchoma moto vituo vya mafuta, na kuchoma moto vituo vya kupigia kura kwa lengo la kuzuia au kuvuruga Uchaguzi.

Mheshimiwa Rais, licha ya viashiria vya mitandaoni vilivyokuwa wazi zaidi, kulikuwa na viashiria ambavyo Tume ilivigundua kupitia mashahidi waliofika mbele yake. Mifano, ni kuwepo kwa vijana wasiopungua 500 katika majengo, misitu na makambi katika maeneo mbalimbali nchini kwa takriban zaidi ya siku 28 ambapo walihifadhiwa na kupatiwa mafunzo kwa ajili ya kufanya ghasia siku ya Uchaguzi Mkuu. Tume katika uchunguzi wake ilibaini kuwa, moja ya nyumba hizo iliyopo Dar es Salaam, ilikuwa umbali wa takribani mita kumi kutoka Kituo cha Polisi.

Pamoja na Tume kupokea ushahidi ulioonyesha kuwepo kwa baadhi ya viashiria vya mipango ya vurugu siku ya Uchaguzi, hakuna ushahidi unaoonesha kubaini na kuchukuliwa kwa hatua stahiki mapema kabla ya matukio ya uvunjifu wa amani.

Kama nilivyoeleza awali, uvunjifu wa amani uliotokea ulithibitisha kiwango kikubwa cha matayarisho ya vurugu hizo. Wafanya ghasia walitumia mbinu ambazo hazikutarajiwa. Mbinu hizo ni pamoja na kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani kwa wakati mmoja katika sehemu mbalimbali za miji na sehemu nyingine, kwa kutumia mbinu ya mtawanyo (dispersal violence points) ili kuwazuia polisi wasiweze kukabiliana nao na kuwadhibiti kwa urahisi.

Mheshimiwa Rais, mashahidi wengi waliofika mbele ya Tume, walieleza kuwa waliona ishara za vurugu kupitia mitandao ya kijamii, na wengine kutoa taarifa mbele ya Tume kuhusu hofu waliyokuwa nayo, kwa mfano:

Kiongozi mmoja wa dini aliiambia Tume kuwa, kabla ya siku ya uchaguzi, mtoto wake alikuwa na taarifa kuhusu vurugu zilizokuwa zinapangwa kuzuia uchaguzi usifanyike. Aliposhindwa kuwasihi baba na mama yake wasijitokeze kupiga kura, aliwashauri kuwa angalau wasafishe vidole vyao mara baada ya kupiga kura kwa kuwa wapo watu waliojipanga kukata vidole vya watakaopiga kura.

Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika ngazi ya Taifa, Mikoa na Wilaya, kama walivyokuwa Watanzania wengine, “walishtukizwa” na hawakuwa wamejiandaa vya kutosha kwa aina ya ghasia zilizotokea tarehe 29 Oktoba 2025, zilizozuka karibu wakati mmoja nchi nzima katika Mikoa 14, Wilaya 43 na maeneo 202 Nchini.

Kupitia mabaraza ya Polisi, maafisa, wakaguzi na askari walipata fursa ya kuielezea Tume namna ghasia zilivyokuwa kubwa na hatarishi kwa maisha yao kutokana na wafanya ghasia kutumia mbinu na silaha mbalimbali kukabiliana na askari. Askari mmoja alithibitisha kuwa Jeshi la Polisi halikutegemea aina, ukubwa na usambazaji wa vurugu zilizotokea siku na baada ya uchaguzi kwa kueleza kuwa: ‘‘Tulijipanga kwa maandamano, yaliyotokea na mtawanyiko”. Afisa mwingine kutoka Vyombo vya Ulinzi na Usalama alieleza kwamba ”tulijipanga kwa maandamano, yaliyotokea ilikuwa ni uyoga nchi nzima”

Mheshimiwa Rais, baadhi ya kamati za mikoa ziliijulisha Tume kupitia Taarifa zao kuhusu hatua mbalimbali walizochukua kudhibiti matishio ya uvunjifu wa amani. Mfano, Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Katavi katika taarifa yake ilieleza kuwa baada ya kuanza kuona viashiria vya kuwepo kwa ghasia wakati wa uchaguzi, iliimarisha mikakati ya utafutaji wa taarifa za kiintelijensia na kuzifanyia kazi kwa haraka. Aidha, Kamati ya Mkoa na kamati za wilaya za usalama zilianza kufanya vikao vya pamoja ambapo katika kipindi hicho zilikutana mara kumi na moja.

Hali kadhalika, Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Kilimanjaro iliieleza Tume kuwa baada ya kuanza kuona viashiria vya uwezekano wa kuwepo ghasia wakati wa Uchaguzi ilichukua hatua mbalimbali ikiwemo kufanya vikao vya Kamati mara kwa mara kwa lengo la kupeana taarifa, kukutana na viongozi wa vyama vya siasa mara kwa mara, kukutana na vikundi vya vijana na kuwasisitizia umuhimu wa amani, pamoja na kuimarisha misamiati ya ulinzi na usalama.

Mheshimiwa Rais, Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi (Sura ya 322) inabainisha majukumu ya Jeshi la Polisi kuwa ni pamoja na kulinda raia na mali zao (Kif. 5(1). Aidha, ili kutekeleza jukumu hilo askari wa Jeshi la Polisi wameruhusiwa kubeba silaha wakati wa utekelezaji wa majukumu yao rasmi (Kif. 5(2). Hata hivyo, Ruhusa ya kubeba silaha inayotolewa chini ya Sheria hii siyo ruhusa ya moja kwa moja ya matumizi ya silaha hizo. Matumizi ya silaha yanapaswa kuzingatia misingi ya sheria na miongozo mbalimbali kuhusu matumizi ya silaha za moto. Kifungu cha 29(1) kinaainisha masharti na mazingira ambayo silaha za moto dhidi ya binadamu zinaweza kutumika:

29 (1) (b) mtu yeyote ambaye kwa kutumia nguvu-

(i) anaokoa au anajaribu kumuokoa mtu mwingine yeyote kutoka katika ulinzi halali; au

(ii) anazuia au kujaribu kuzuia kukamatwa kihalali kwa mtu mwingine yeyote;

Masharti ya Kifungu cha 29(1)(b) cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi yanaendana na Kanuni ya 9 ya Kanuni za Msingi za Umoja wa Mataifa Kuhusu Matumizi ya Nguvu na Silaha za Moto kwa Maafisa wa Vyombo vya Utekelezaji wa Sheria zilizopitishwa mwaka 1990 [The UN Basic Principles on the Use of Force and Firearms 1990- BPUFF]

Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai Kifungu cha 12(1) na (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai kinatoa mwongozo wa kisheria kuhusu ukamataji wa mtuhumiwa na matumizi ya nguvu wakati wa kukamata.

Mheshimiwa Rais, kanuni za Jumla za Jeshi la Polisi (The Police General Orders) (PGOs) Kwa mujibu wa Kanuni ya 274 (PGO) ya Kanuni za Jumla za Jeshi la Polisi, matumizi ya nguvu yanasimamiwa na kanuni kuu nne zinazojulikana kwa kifupi kama PLAN –

  • Uwiano (Proportionality): Matumizi ya nguvu lazima yawiane na tishio husika. Kadri upinzani unavyoongezeka kuanzia static (ilani), active (udhibiti mkali) na ominous (hatarishi) hadi lethal (inayoweza kusababisha kifo) ndivyo kiwango cha nguvu kinavyoruhusiwa kuongezeka kwa uwiano.
  • Uhalali (Legality): Uhalali wa matumizi ya nguvu unatokana na kufuata mamlaka na taratibu zilizowekwa kisheria. Kwa mujibu wa Kanuni za Jumla za Polisi (PGO 274 (3), ikisomwa pamoja na Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (Kif. 22), Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi (kif. 44) na Kanuni za Adhabu (Kif. 78) zinaelekeza uhalali wa Jeshi la Polisi kutumia nguvu panapohitajika kufanya hivyo.
  • Uwajibikaji (Accountability): Askari asipozingatia misingi ya matumizi ya silaha atawajibika binafsi. Kila Ofisa au Polisi anawajibika binafsi kwa matumizi yoyote yasiyofaa ya silaha zilizoko chini ya uangalizi na udhibiti wake. Msimamo huu wa kisheria ulithibitishwa katika shauri la Republic Vs G 2573/Pc Pacificus S/O Cleophace Simon [2018] TZCA 423
  • Ulazima (Necessity): Polisi wanaweza kutumia nguvu pale ambapo ni lazima sana (strictly necessary) kufanya hivyo ili kudhibiti hali kulingana na tishio (PGO 274 (3) & (4). Aidha, masharti hayo yanaendana na masharti ya aya ya 11 ya Sura ya Kwanza ya Mwongozo wa Kudhibiti Ghasia unaosisitiza kuwa nguvu itumike pale inapohitajika kurejesha sheria na utulivu haraka.

Mheshimiwa Rais, kwa kuzingatia misingi ya Mwongozo wa Matumizi ya Nguvu (Use of Force Continuum) Tume ilichambua ushahidi kuhusu matumizi ya nguvu katika maeneo mbalimbali na kubaini kuwa hatua za matumizi ya nguvu zilitofautiana kati ya eneo moja na jingine.

Yapo maeneo ambayo hatua ya kwanza ya uwepo wa askari iliwezesha kuzuia ghasia kuendelea. Yapo pia maeneo mengine ambayo, kutokana na kiwango cha tishio kwa uhai wa askari na raia wengine, ililazimu kutumika kwa hatua za juu.

Katika kituo cha Polisi cha Salasala, Dar es Salaam mmoja wa askari aliyekuwa katika kituo hicho alieleza kuwa, wakiwa kituoni hapo walivamiwa na kundi la watu zaidi ya 150 wakiwa na silaha za jadi ikiwemo mapanga, mishale, mikuki na madumu ya mafuta ya petroli. Kutokana na hali hiyo walilazimika kutumia mabomu ya machozi na baadaye kuamua kukimbia baada ya kuzidiwa nguvu.

Shahidi mwingine kutoka Kituo cha Nyamagana Mwanza alieleza hali ilivyokuwa eneo la Stendi Kuu ya mabasi ya kwenda Nyegezi ambapo kundi la watu kati ya 300 – 400 wakiwa na silaha za jadi zikiwemo mapanga, sime, nondo na marungu wakiwa wanafanya ghasia ikiwa ni pamoja na kuchoma moto mali za watu. Kutokana na hali ilivyokuwa walilazimika kutumia mabomu ya machozi na hali ilipozidi kuwa mbaya na ya hatari, walilazimika kutumia silaha za moto. Kwa mujibu wa shahidi huyu, katika tukio hilo askari walikuwa tisa dhidi ya kundi la wafanya ghasia zaidi ya 400.

Askari mwingine kutoka Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mwanza alieleza kuwa, tarehe 30 Oktoba, 2025 saa saba mchana wakiwa katika eneo la karibu na benki za CRDB na NMB Buswelu, askari Polisi walikuwa wakiwaokoa askari wenzao walilazimika kutumia mabomu ya machozi ili kuwatawanya wafanya ghasia na kuwaokoa askari wenzao waliokuwa katika hali mbaya.

Shahidi anaeleza zaidi kuwa katika eneo la Buhongwa ambako wafanya vurugu walikuwa zaidi ya 2000 wakiwashambulia askari, walilazimika kutumia mabomu ya kishindo na mabomu ya machozi. Gari waliyokuwa wanaitumia iliharibiwa vibaya na baadhi ya askari walumbwa na kuwa katika hali mbaya na hatari kubwa. Anaeleza kuwa: “Mazingira yalikuwa ya hatari ya kupoteza maisha. Wahalifu walikuwa na mapanga, mawe, matofali, marungu. Hatukutumia silaha ya moto. Mimi nilipigwa jiwe la joint na kiwiko na kuumia sana.”

Mkuu wa Polisi wa Wilaya Kinondoni ameeleza hatua mbalimbali alizochukua kutawanya kundi kubwa la wafanya ghasia waliokuwa na silaha za jadi. Kwa kuanzia anasema, walikaa kama watazamaji lakini baadaye wafanyaghasia waliongezeka na kufikia kati ya 200 hadi 300 na wakaanza kuwarushia Polisi mawe, na baadaye Polisi walitumia mabomu ya machozi, lakini wafanyaghasia hawakutawanyika. Walianza kuwashambulia Polisi kwa nondo na madumu ya mafuta. Katika hali hiyo, walilazimika kutumia silaha za moto ili kujilinda na kudhibiti ghasia.

Katika tukio la kuchomwa moto Kituo cha Polisi cha Makuyuni, Arusha kundi la wafanya ghasia wasiopungua 300 lilivamia kituo hicho wakiwa na silaha mbalimbali kama vile nondo na madumu ya mafuta. Askari walitoa ilani ya kuwataka watawanyike lakini waliendelea kuwashambulia. Baada ya hapo, walilazimika kutumia mabomu ya machozi lakini wakaendelea kuwashambulia Polisi ikiwa ni pamoja na kumjeruhi askari mmoja gotini kwa kipisi cha nondo na ndipo walilazimika kutumia risasi za moto.

Hali kama hiyo ilijitokeza katika maeneo mengine kama vile: eneo la kituo cha Polisi Nyamagana na Mabatini Mwanza ambapo, kundi la wafanya ghasia kati ya 500 – 1,000 wakiwa na silaha za jadi waliivamiwa sehemu hiyo. Ilisomwa ilani ya kuwatawanya na baada ya hapo yalitumika mabomu ya machozi baada ya wafanya ghasia kuanza kuwashambulia Polisi kwa vilipuzi.

Mheshimiwa Rais, aidha, Tume ilipokea ushahidi kutoka kwa baadhi ya mashahidi waliodai Polisi kutumia nguvu katika kudhibiti ghasia kama ifuatavyo:

Tarehe 30 Oktoba, 2025 Mkazi wa Momba, Songwe majira ya mchana alikuwa kisimani kuchota maji na mtoto wake. Walisikia milio ya mabomu akawa anakimbia akiwa amembeha mtoto, mtoto alidondoka chini baada ya kupigwa risasi kichwani.

Mkazi mmoja wa Maruango Wilaya ya Arumeru, aliitarifu Tume kuhusu tukio la mwanae mwenye umri wa miaka 35 aliyepigwa risasi nne na Askari Polisi katika eneo la Kimandolu siku ya tarehe 29 Oktoba, 2025 akiwa karibu na dukani kwake. Kwa mujibu wa maelezo ya shahidi, mwanae alipigwa risasi ya mkononi akaanguka chini kisha askari walimfuata na kumpiga risasi tatu mgongoni na kuvunjika mifupa miwili ya uti wa mgongo, na nyingine chini ya moyo, na hivyo imeshindikana kuitoa. Kwa sasa mwanae anaendelea na matibabu hospitali moja ya rufaa. Tukio hili pia ni moja ya matukio yanayohitaji upelelezi wa kina.

Tarehe 29 Oktoba, 2025, majira ya saa kumi na moja jioni wakazi wawili wa Kinyerezi, Dar es Salaam, waliona gari ya Polisi ikipita lakini ilirudi nyuma na Polisi watatu walishuka na wawili kati yao walipiga magoti na kuwafyatua risasi, ambapo risasi moja ilimpata mmoja wao ambaye alidondoka na wenzake waliokuwepo walikimbia.

Katika mji wa Mwanza, Tume ilipata taarifa ya tukio la mauaji ya watu wapatao 13 lililodaiwa kutokea tarehe 31 Oktoba, 2025 katika kibanda cha TV kilichopo eneo la Mji Mwema Jijini Mwanza. Shahidi mmoja ambaye alijitambulisha kama manusura wa tukio hilo, aliieleza Tume kupitia maelezo yake ya kiapo kuwa tarehe 31 Oktoba, 2025 watu wanaodhaniwa kuwa ni askari polisi walivamia kibanda hicho na kuwapiga risasi watu takribani 13 akiwemo shahidi huyu ambaye alinusurika. Kwa mujibu wa maelezo yake, pamoja nae wapo wengine wawili walionusurika ambapo mmoja alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospital ya Bugando na mwingine kijijini kwake. Hili ni moja ya matukio yanayohitaji uchunguzi wa kina.

Mheshimiwa Rais, Serikali ina wajibu kupitia Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha usalama wa raia na mali zao, na inapotokea hali yoyote inayoweza kuathiri usalama, Serikali kupitia vyombo hivyo inapaswa kuchukua hatua stahiki za kurejesha utulivu kwa mujibu wa sheria na miongozo.

Pale ambapo hatua zilizochukuliwa zimesababisha madhara kwa raia kutokana na matumizi ya nguvu ya afisa au maafisa wa vyombo vya ulinzi na usalama, upelelezi wa haraka, huru na kamilifu unapaswa kufanyika ili kubaini chanzo na kuchukua hatua stahiki. Lengo ni kulinda imani ya wananchi kwa Serikali na vyombo vyake ili kuhakikisha dosari zilizojitokeza hazijirudii.

Utawala wa Sheria na Uwajibikaji

Mheshimiwa Rais, kuhusu masuala ya utawala wa sheria na uwajibikaji, uchunguzi ulibaini yafuatayo:

Mosi, katika kudhibiti ghasia, Jeshi la Polisi lilisaidiwa na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama chini ya uratibu wake. Kupitia operesheni ya pamoja ghasia hizo ziliweza kudhibitiwa kulingana na mwelekeo na ukubwa wa ghasia. Aidha, katika kutekeleza majukumu hayo, silaha baridi na moto zilitumika kwa kutegemea mazingira yaliyokuwepo;

Pili, taarifa zilikuwepo lakini hazikutafsiriwa kwa usahihi na vihatarishi (risks) havikuchambuliwa kwa uzito stahiki. Miongoni mwa sababu za hali hii ni kuamini kuwa kwa utamaduni na amani iliyozoeleka nchini Tanzania ghasia zisingetokea (cognitive bias), sambamba na ukosefu wa mifumo ya uchanganuzi iliyopangwa vizuri (lack of structured analytical frameworks), na udhaifu wa kuweka mipango thabiti kulingana na mazingira na vihatarishi vilivyojitokeza (weak scenario planning);

Tatu, wanaharakati na wanasiasa walitumia changamoto za kijamii kuwashawishi wananchi kufanya ghasia zilizosababisha madhara makubwa ya kibinadamu pamoja na uhalifu mwingine.

Mheshimiwa Rais, kuhusu maridhiano na Katiba Mpya, Tume imebaini yafuatayo:

Mosi, matukio ya Oktoba 2025 pamoja na changamoto ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu vimesababisha nyufa na majeraha kwa Taifa. Hivyo, maridhiano na muafaka wa Kitaifa ni hatua muhimu katika kuponya majeraha na kurejesha amani, kuaminiana, mshikamano na utengamano ndani ya jamii na taifa kwa ujumla. Maridhiano yanapaswa kuwa mtambuka yakijumuisha nyanja za kisiasa, kijamii na kiuchumi ili kutathmini zaidi ukweli, kuponya majeraha, kutafuta suluhisho na kufikia muafaka wa kisiasa, kukubaliana juu ya msingi na mambo yanayohusu Katiba Mpya na kurejesha umoja na mshikamano wa kitaifa;

Pili, kwa kuzingatia nafasi ya taasisi za dini katika kulinda tunu ya amani na kujenga utengamano katika jamii, upo umuhimu wa kufanyika majadiliano baina ya dini kama sehemu ya maridhiano ya kijamii. Hivyo, majadiliano, maridhiano na muafaka miongoni mwa viongozi wa dini yataimarisha uelewano miongoni mwao na kukubaliana kuhusu mipaka kati ya dini na siasa katika utekelezaji wa majukumu yao, kisha mapendekezo yao yawasilishwe Serikalini kwa hatua stahiki kwa ajili ya utulivu wa kisiasa na kijamii na kuepuka mikanganyiko katika siku zijazo;

Tatu, maridhiano yatakayofanywa katika ngazi ya kitaifa yanapaswa kushuka hadi ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kutumia mifumo ya utawala iliyopo kwenye Wilaya, Tarafa, Kata na Vijiji; na

Nne, ili kuhakikisha mchakato wa maridhiano na muafaka wa kitaifa unafanikiwa na kusaidia kukwamua mikwamo itakayojitokeza ni muhimu kuwe na Baraza la Ushauri la Wazee lisilo rasmi ili wazee watoe ushauri katika kutatua changamoto au mvutano katika jamii na mambo mengine ya kitaifa.

Mapendekezo 

Mheshimiwa Rais:

Tume inawasilisha mapendekezo mbalimbali yakiwemo ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu. Kwa minajili ya wasilisho hili, naomba nieleze baadhi tu ya mapendekezo hayo.

Mheshimiwa Rais, baadhi ya mapendekezo makubwa ya muda mfupi ni pamoja na yafuatayo:

Mosi, Serikali kuweka utaratibu wa kuhakikisha majeruhi waliopata ulemavu kutokana na ghasia za Oktoba 2025 wanapata huduma za matibabu bure, ikiwa ni pamoja na watakaohitaji vifaa saidizi na viungo bandia (prostheses);

Pili, Serikali kutenga siku ya Maombolezo ya Kitaifa kuwakumbuka Watanzania zaidi ya 500 waliofariki kwenye ghasia za wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025;

Tatu, Serikali iweke mkakati na kutenga rasilimali kwa ajili ya utoaji wa huduma za msaada wa kisaikolojia na kijamii pamoja na kufanyika kwa tathmini ya haraka (Rapid Assessment) ya athari za kisaikolojia na kijamii katika maeneo yaliyoathirika na ghasia za Oktoba 2025;

Nne, ni maoni ya Tume kwamba, ni muhimu Katiba Mpya ipatikane ifikapo mwaka 2028 ili itumike katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa wa 2029 na uchaguzi mkuu wa 2030. Ili kufikia lengo la kupata Katiba kabla ya 2029, Serikali iunde Kamati ya Wataalamu wa Katiba ambayo itakuwa na: jukumu la kupitia Katiba iliyopo; rasimu ya Katiba ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba; Katiba Pendekezwa ya Mwaka 2014; ripoti za Tume, Kamati na Vikosi Kazi mbalimbali. Baada ya kufanya mapitio ya nyaraka hizo, Kamati ya Wataalam itapata maoni na michango ya wananchi na kisha kuandaa rasimu ya Katiba Mpya itakayopigiwa kura na wananchi (referendum);

Tano, Serikali iunde Tume ya Maridhiano na Muafaka wa Kitaifa, kupitia mamlaka ya Rais chini ya Ibara ya 36 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo itakua shirikishi na itakayosimamia na kuongoza maridhiano katika nyanja za kisiasa, kijamii na kiuchumi ili kutathmini zaidi ukweli, kuponya majeraha, kutafuta suluhisho na muafaka wa kisiasa, na kurejesha umoja na mshikamano wa kitaifa;

Sita, sambamba na Tume ya Maridhiano na Muafaka wa Kitaifa, liundwe Baraza la Wazee la Ushauri litakalojumuisha baadhi ya viongozi wakuu wastaafu pamoja na wazee wengine wenye kukubalika katika jamii na wenye uzalendo ili kuisaidia Tume ya Maridhiano kunapotokea mkwamo;

Saba, Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi itekelezwe kikamilifu, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa uteuzi wa Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume unafanyika kwa kuzingatia sheria iliyorekebishwa mwaka 2024. Aidha, Tume iruhusiwe kuajiri watumishi wake ili wawe na wajibu wa kusimamia shughuli za uchaguzi angalau hadi ngazi ya Jimbo. Katika ngazi ya wasimamizi wasaidizi na wasimamizi wa vituo, INEC iendelee kutumia watumishi wanaoajiriwa kwa muda. Hatua hii, itaondoa malalamiko ya vyama vya siasa na wananchi kuhusu uhuru wa INEC;

Nane, Tume imebaini kuwa yapo maeneo yenye viashiria vya jinai na yanayohitaji uwajibikaji. Hivyo, inapendekezwa kuundwa Tume ya Uchunguzi wa Kijinai Kufuatia Matukio ya Ghasia ya Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 kwa mujibu wa Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura 32 Toleo la 2023. Tume hiyo itakuwa na jukumu la kupeleleza na kufuatilia masuala mahsusi yanayohitaji upelelezi zaidi ili kushughulikia tuhuma zilizobainishwa katika taarifa ya Tume. Masuala hayo ni pamoja na kubaini wahusika wakuu wa ghasia, matukio tatanishi ya vifo na majeruhi, maiti ambazo hazijapatikana, na kupendekeza hatua za uwajibikaji;

Tisa, Jeshi la Polisi libuni na kutekeleza mkakati madhubuti wa kurejesha na kuimarisha uhusiano wake na jamii kwa manufaa ya ulinzi na usalama wa raia na Nchi kwa ujumla, kama ilivyopendekezwa na Tume ya Haki Jinai;

Kumi, Serikali na vyombo vya dola vitekeleze majukumu yake kwa namna inayoonesha wazi kuzingatia mazingira ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa. Hatua hiyo italeta usawa katika uwanja wa ushindani na kuondoa malalamiko ya wadau wa siasa na wananchi kwa ujumla kuhusu kukosekana kwa demokrasia katika siasa za vyama vingi nchini;

Kumi na moja, maadili ya viongozi yasimamiwe kwa karibu, ikiwa ni pamoja na mtindo wa maisha usioendana na taratibu na miiko ya utumishi wa umma, ili kubaini na kudhibiti vitendo visivyokubalika, kama vile rushwa na ufisadi; na

Kumi na mbili, Sheria ya Baraza la Taifa la Vijana, Sura ya 441, itekelezwe na baraza liundwe na lianze kutumika kama jukwaa la majadiliano kuhusu masuala yanayowahusu vijana.

Mheshimiwa Rais, yafuatayo ni baadhi ya mapendekezo ya muda wa kati:

Mosi, Serikali iimarishe mifumo ya uwajibikaji kwa kuhakikisha watendaji wote, hususan, wa ngazi za kati na chini, wanasikiliza na kushughulikia kero za wananchi kwa wakati, na kuwajibika pale wanaposhindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo na wanapokiuka sheria. Ili kutekeleza jukumu hili kwa ufanisi, ni muhimu kuviwezesha vitengo vya ufuatiliaji na tathmini katika taasisi ambavyo kwa muundo wa sasa vinawajibika moja kwa moja kwa mkuu wa taasisi;

Pili, Serikali iendelee na iweke kipaumbele katika kutekeleza mapendekezo yanayotolewa na tume au vikosi kazi mbalimbali inavyoviunda kwa mfano Tume ya Haki Jinai. Hatua hiyo itapunguza au kuondoa malalamiko ya wananchi na mivutano isiyo ya lazima na wadau wa siasa;

Tatu, Serikali iimarishe mifumo ya ajira na uteuzi wa viongozi na watendaji wakuu kwa kuzingatia sifa na ushindani wa haki (merit-based system) na kutenganisha utumishi wa umma na ushawishi wa kisiasa. Aidha, utaratibu wa kuwaendeleza watumishi mara kwa mara uimarishwe;

Nne, Serikali iimarishe usalama, ulinzi, na ufuatiliaji katika maeneo ya mipakani, hasa yenye vipenyo vingi, ili kuzuia uharifu na uingiaji nchini kiholela;

Tano, Serikali iimarishe ulinzi shirikishi kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuwashirikisha wananchi ikiwa ni pamoja na kurejesha mfumo wa nyumba kumi kisheria. Hatua hii itasaidia kubaini viashiria vya uhalifu na kuchukua hatua stahiki kwa wakati. Mathalani, ushahidi ulibaini kuwepo nyumba mbalimbali kwenye makazi ya watu zilizotumika kama makambi ya kuwahifadhi vijana waliokuwa wanaandaliwa na kupatiwa mafunzo kwa ajili ya kufanya ghasia. Hata hivyo, mifumo ya ulinzi haikuweza kubaini kuhusu makambi hayo;

Sita, kuwepo na mfumo madhubuti wa usimamizi wa fursa zinazotolewa kwa vijana kama vile mikopo, ajira, ununuzi na ushiriki katika miradi ya Serikali ili kuhakikisha kuwa zinatumiwa kwa kuzingatia sheria na taratibu na hakuna upendeleo wala mashinikizo ya kisiasa;

Saba, Serikali ifanye mapitio ya vipaumbele vya bajeti na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ili rasilimali zaidi zielekezwe kwenye eneo la uwezeshaji wananchi kiuchumi; na

Nane, Serikali ichukue hatua ya kuboresha mfumo wa kisheria wa usimamizi wa majanga kwa kupanua wigo wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa, Sura ya 242 ili kujumuisha majanga yanayotokana na matukio ya uvunjifu wa amani. Maboresho hayo yawezeshe kuwepo kwa mfumo wa mawasiliano wakati wa majanga (close loop communication) unaohusisha wadau wote (first responders) wanaokuwa kwenye majanga kama Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, watoa huduma za afya, na wananchi. Aidha, yafanyike mazoezi ya utayari kwa wadau wote (emergency response mechanism), hatua hii itapunguza athari za majanga ya aina hiyo yanapotokea.

Mheshimiwa Rais, mapendekezo ya muda mrefu ni pamoja na yafuatayo:

Mosi, Serikali irejeshe utaratibu wa vijana wote wanaomaliza kidato cha sita kushiriki mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kama sharti la lazima ili kuwajengea uzalendo na uwezo wa kujitegemea. Aidha, kuwe na utaratibu wa kuwezesha wahitimu wa JKT kujiajiri kwa kuishirikisha Sekta Binafsi; na

Pili, Serikali ibuni na kutekeleza mkakati wa makazi maalumu (barracks) kwa maafisa na askari wa vyombo vya ulinzi na usalama ili kuepuka mgongano wa maslahi na kulinda usalama wao kama ilivyopendekezwa na Tume ya Haki Jinai.

Hitimisho

Mheshimiwa Rais, nimetaja baadhi tu ya mapendekezo yaliyomo kwenye Ripoti; bila shaka wadau mbalimbali watapata fursa ya kuyasoma kwa kina ndani ya Ripoti. Hali kadhalika, tunategemea, kwa siku kama tatu zijazo, kukutana na wanahabari pamoja na wadau wengine kwa ajili ya majadiliano mapana na ufafanuzi.

Pamoja na ugumu wa yaliyotokea Oktoba 29, tunampongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuunda Tume hii, na kutuamini kufanya kazi yenye maslahi mapana kwa Taifa letu.

Tulisikiliza vilio vya waliopoteza wapendwa wao, waliojeruhiwa, na waliopoteza mali. Tuliona macho ya vijana waliokamatwa wakiuliza kwa wasiwasi mustakbali wao. Tulikutana na familia ambazo hadi leo hazijaielewa ni nani aliyemuua mpendwa wao na kwa nini.

Lakini pia kwa upande mwingine, tunaiona Tanzania yenye upande wa ujasiri, uzalendo na hekima. Tulisikiliza viongozi wa dini wakiomba amani kwa nguvu ya kweli. Tuliona Wazee wenye heshima wakitoa maneno ya busara. Tulipata ushirikiano wa wananchi ambao walikuja kutoa ushahidi kwa sababu wanalipenda Taifa lao. Siyo jambo la kawaida kwa Tume kama hii kuwasiliana kwa karibu sana na kwa namna moja au nyingine na watu wapatao 63,603. Tunawashukuru wote.

Nihitimishe kwa kurejea shukrani zangu kwako Mheshimiwa Rais kwa imani kubwa kwa Tume na niwashukuru washiriki wote kwa kunisikiliza.

Ahsanteni sana!

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×