The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Mwanzo-Mwisho Simulizi ya Kutekwa kwa Msaidizi Binafsi wa Tundu Lissu: Watekaji ‘Walifyatua Riasasi Nyingi Sana’

David Djumbe alinusurika baada ya kuruka kutoka kwenye gari ya watekaji na kukimbilia msituni.

subscribe to our newsletter!

Maelezo haya yalitolewa mnamo asubuhi ya Mei 21, 2026, Allan Macha alizungumza akiwa makao makuu ya CHADEMA. David Djumbe alizungumza nyumbani kwake asubuhi hiyo hiyo baada ya kufika na kupokelewa na familia yake.

Allan macha

Mimi ninaitwa Alan Macha ni jirani na rafiki wa Bwana David Djumbe. Ninachokisimulia hapa ni tukio lililotutokea jana [Mei 20, 2026] baada ya mimi kutoka katika shughuli zangu ninazozifanya za kila siku nikirejea nyumbani.

Kwanza Bwana David Djumbe ambaye ni jirani yangu na Rafiki yangu nilikuwa nina muda mrefu hatujaonana kutokana na hali ya sintofahamu ya usalama wake ndani ya nchi yetu. Lakini kwa bahati nzuri jana wakati nakaribia kutoka ofisini kwangu kurudi nyumbani akanitafuta kwenye simu na kunieleza ya kwamba yupo katika garage moja ambapo gari yake inarekebishwa, kwa hiyo ninaweza kum-pick kwa sababu mimi nilikuwa na gari,  na kuweza kurejea naye nyumbani kwa sababu tunaishi mtaa mmoja.

Baada ya kumpick tulirejea nyumbani pamoja kwenye majira ya saa nne na kama dakika tano hivi usiku wakati tumekaribia karibu na nyumbani kwake kwenye umbali wa takribani mita 20 au 25 kutoka kwenye nyumba yake na eneo la tukio lilipotokea. Tukaona gari inatufuata nyuma ikiwa speed sana na pikipiki mbili zikiwa ina iescort. Ile gari ilivyokuwa speed nikamuuliza; kwa sababu mimi nilimuomba yeye aendeshe gari baada ya kukutana naye garage. Kwa sababu ninaumwa mgongo nikamuomba anisaidie kuendesha.

Nikamuliza unaona hiyo gari inavyokuja kwa spidi hiyo? Akasema na mimi simuelewi na barabara ilivyo mbovu mbona spidi siyo ya kawaida. Nikamuambia basi mpishe apite, kile kitendo cha yeye kusogea kushoto ili ile gari ipite, ikaja ikablock mara ya kwanza, akaendelea kusogea mbele na kubana kushoto zaidi, ikablock tena mara ya pili. Ikabidi na yeye atoke resi akimbie mahali pana uwazi panafanyika shughuli za ufyatuaji wa matofali na uuzwaji wa vifaa vya ujenzi pana space.

Ile gari ikaja ikablock kabisa na kwenye ile gari iliyokuwa inatublock ambayo ni Toyota Probox namba sikuweza kuisoma kwa haraka lakini inamalizikia na ‘EBE’. Wakashuka watu takribani sita au zaidi na kile kitendo cha wao kushuka kwa sababu sisi kwenye gari tulikuwa hatujalock milango, haraka sana tukakuta wameshafungua milango ya gari letu na kujitambulisha wao ni Askari Polisi, tuko chini ya ulinzi.

Kile kitendo walivyokuwa wanakifanya kilikuwa kama vile jambo la kimafia kama vile mtu anavyoangalia movie za utekaji zilivyo. Sasa wakati ule wanasema mko chini ya ulinzi, Bwana David Djumbe akawahi kuhoji tupo chini ya ulinzi kwa kosa gani? Na mimi pia nikauliza kosa letu ni nini?

Kutekwa

Kile kitendo cha kuuliza yeye wakawa wameshagawanyika watu zaidi ya wanne wanapambana naye ili wamtoe pale kwenye usukani wampakie kwenye Pro Box. Na mimi wengine wakawa tayari wameshanikamata na mimi wanataka wanipakie kwenye Pro Box, nikajishika kwa nguvu huku nikipiga mayowe na kelele nyingi kwa sababu pale ni karibu na nyumbani, nikisema watekaji, watekaji-wezi, wezi. Nikijua tutapata msaada.

Kwa bahati nzuri wakati napiga zile kelele, wakatokeza Bodaboda ambao walikuwa wanarejesha watu nyumbani na wengine wanarudi baada ya kupeleka abiria. Wakawa na wao wameshuhudia lile tukio na kile kitendo cha wale watekaji au waliojitambulisha kuwa ni Askari kuona watu wanakuja, wakaingia naye kwenye Pro Box na wengine wakagawanyika wakaingia kwenye ile gari yangu na gari yangu ndiyo ikawa ya kwanza mbele kuongoza msafara wa kukimbia.

Kwa vile Bodaboda walishafika na sisi tulipiga makelele mengi, ikabidi wazifukuze. Mimi wakati napiga kelele nilibahatika kutoka na simu yangu, kuna Rafiki yangu yupo maeneo ya karibu na Mingoi ana ka-pub, ka-grocery fulani hivi pale na huwa mara nyingi nikitoka ofisini naweza nikapita pale nikaspend muda kidogo na kwenda nyumbani.

Nikampigia simu nikamueleza scenario ya tukio lililotokea na gari yangu anaijua. Nikamuambia gari yangu tumetekwa na wameondoka na gari yangu na wameondoka na jirani yangu Djumbe nilikuwa naye kwenye gari. Naomba kama mnaweza muweke barrier ili wakifika hapo tujue kweli ni watu gani.

Kwa hiyo ile taarifa nilivyoitoa haraka kwa sababu mimi vijana wengi wanaoendesha Bodaboda pale wananifahamu na yule alivyokuwa ninaongea naye pale walikuwepo Bodaboda kwenye grocery yake. Watu wengi wakawa tayari wameshaji-organize wakiwa na Bodaboda na kuweka barrier ambayo ilikuwa ni viroba vyenye vifusi na mabenchi.

Na mimi nikawa nimepakiwa na Bodaboda ambaye alishuhudia lile tukio wakati linafanyika-zile rapsha. Kwa hiyo tukawa tunaifukuza ile gari yangu ambayo iko mbele na ile Pro Box  yao ambayo ipo nyuma ya ile gari yangu.

Sasa mimi nikawa tayari nina taharuki, mimi ninachokitamani ni kublock ile gari yangu ingawaje tupo na pikipiki. Kwa hiyo tukaipita ile Pro Box ambayo alikuwa amebebwa yeye, spidi zile gari zilivyokuwa zinatembea ni spidi ya ajabu sana. Mimi mwenyewe hiyo gari ninayo zaidi ya miaka sita lakini sikuwahi kuamini kama ile gari ina mwendo huo.

Kwa hiyo watu waliokuwa barabarani wanarudi majumbani walivyoona zile gari zinavyopita kwa spidi ile wengi walipisha wakijua ni kitu kisicho cha kawaida. Kwa hiyo lile tukio tumelifukuza zile gari mpaka kufika pale kwenye barrier ndio na wao wakapunguza mwendo. Nikaendelea kupaza sauti na kupiga kelele watekaji, watekaji; wamemchukua Djumbe na gari yangu wako nayo. Na kwa vile watu wanananiona mimi ninapiga kelele na gari yangu wanalifahamu kweli wakajua ni tukio la kweli, nikazidi kuwavuta watu wengi pamoja na bodaboda wa kijiwe cha Mingoi.

Wale walivyoona bado watu wanazidi kuongezeka wakaangalia pale palipokuwa na barrier wakagonga wakapita. Hiyo process ya kukimbizana na bodaboda wanafukuzia nyuma ikaendelea mpaka tukapita Bunju. Wakati tunafika Bunju ikawa barabarani kulikuwa na trekta linarudi majira ya sa nne na dakika kumi na kitu. Wale bodaboda wakawa hawawezi kuendelea kwa spidi waliyokuwa nayo, lakini wale wakatoa kushoto na wakaenda kwa spidi ile ile.

Bahati nzuri yule ndugu yangu au rafiki yangu niliyempigia simu nikimuambia tumetekwa na gari yangu imeondoka ambaye alikuwa ndio mmiliki wa ile grocery ni mwanajeshi. Akaniambia kwenye simu: mimi nimechukua pikipiki niko nao, kwa hiyo ninyi endeleeni kuja. Kwa hiyo na mimi nikawaomba wale bodaboda wasiache kuendelea kutupa support tuweze kukimbiza tujue kama wataingia kituo cha polisi tujue basi ni polisi wenyewe, tujue jambo likoje ili nikaweze kuripoti.

Chakushangaza walivyofika maeneo ya karibu na Boko Magengeni wakaingia hii njia ya kuingilia kwenda Mbweni, kwa spidi za ajabu sana na watu wameshuhudia hilo tukio. Baadaye walivyoona bodaboda wanaongezeka wakaenda wakazunguka wakarudia hii barabara kama wanarudi ile njia waliyoingilia, walivyofika maeneo ya ile baa moja inaitwa Mashati, wakafyatua risasi kama mbili juu ili watu wapungue. Lakini bado Bodaboda wakaendelea.

Wakafika barabara ya mbele yake, wakaingia sasa moja kwa moja hii barabara ya kunyoosha kwenda Mbweni kule kuliko na ule msitu wa eneo la usalama. Walivyoenda wakafika pale kwenye ile barrier, kwa sababu ile barabara ina barrier. Walivyofika kwenye barrier hawakwenda tena kwa spidi ile wakapunguza spidi na baadae wakazima magari wakapaki.

Wakashuka wote ndani, wakafyatua risasi nyingi sana kuelekea kule ambapo bodaboda walikuwa wanazifukuzia. Kwahiyo bodaboda wengi na watu waliokuwa wanasogea wakaona ile taharuki tukaanza kurudi nyuma kwa kukimbia pia. Walioweza kugeuka na bodaboda , walioweza kukimbia kwa miguu.

Taarifa kupelekwa Polisi

Lakini baadae Bodaboda wakasema tusikimbie, maana walivyofyatua zile risasi walifika mahali wakatulia. Lakini lile eneo, ni eneo la usalama na pana barrier, Bodaboda hawakuthubutu kuingia. Na kwa ile situation ya wao kufyatua risasi ikapelekea watu pia kuwa na hofu ya kwenda. Kilichotokea baada ya lile tukio la ufyatuaji wa risasi kutulia, wakawa kuna baadhi ya bodaboda walitoa mawazo pale akawepo Bodaboda mmoja aliyekuwa na namba ya OCD, akampigia simu akamueleza scenario ya tukio ambalo ameliona, akamuambia na mhusika wa gari ambayo imechukuliwa yuko hapa msikilize. Sikuweza kujua alikuwa amempigia OCD wa Wilaya ipi, lakini mimi nikamueleza scenario ya jambo lilivyo, akanisikiliza baadaye akaniambia sawa.

Tulivyoendelea kukaa pale baadhi ya ndugu wakawa wameshapata taarifa ya kitu kilichotokea. Nikawa ninapokea simu za kuniambia nirudi nyumbani kama mimi nimeweza kutoka, nirudi nyumbani. Lakini mzee wangu mmoja aliyenipigia nikamuuliza nitarudi nyumbani bila kwenda kuripoti polisi, akaniambia kuripoti polisi ndio jambo la muhimu zaidi.

Nikatoka pale, kwa sababu tukio lilipo na kwenda kituo cha polisi Mbweni ni karibu. Tukaenda kituo cha polisi Mbweni tukakuta Askari wanne, wawili wakiwa wamekaa nje wana silaha, mmoja yupo kaunta na mmoja aliyekuwa anatusikiliza alikuwa amevaa rubega juu ya kimasai. Akatusikiliza lakini akasema ngoja kwanza niwasiliane na wakubwa zangu, wakapiga simu nyingi sana.

Nakumbuka wakati mimi niko kwenye jambo kama hilo ninajaribu kufikiria ni wapi ninaweza kupata masaada wa haraka wa kuweza mimi kunifikisha pale ambapo ninaweza nikasaidika. Kwa hiyo rafiki yangu yeyote ambaye nilihisi labda yupo kwenye chombo chochote cha usalama wa nchi hii niliwajulisha, siwezi nikataja majina lakini nilijulisha zaidi ya watu wanne, watano. Mmojawapo akaniambia kama umetoka nakuomba usiendelee kufuatilia, wewe hakikisha unarudi nyumbani.

Lakini nilivyoenda pale polisi baada ya kutoa maelezo wakatuambia tusubiri, ameambiwa asubiri kabla ya kufugua RB au kunichukua maelezo. Tukakaa pale pamoja na yule Mwanajeshi aliyenisaidia kuweka barrier na kuifukuza ile gari kwa pikipiki. Baada ya kama dakika 20 hivi tukawa hatuitwi kwenda kutoa maelezo au kuchukuliwa maelezo. Akaenda akawauliza kama tunashindwa kupata msaada je, mnaniruhusu niombe msaada pengine ninapotoka mimi. Kwa sababu yeye ni mwanajeshi, wakamuuliza wewe tunadhani ni Afande mwenzetu, unazifahamu protocol za kiaskari.

Kama hili tukio limetokea ukanda wa Mapinga au upande wa Kibaha linatakiwa liripotiwe Kibaha. Lakini wakati ninyi mmetueleza hii situation na sisi tumewasiliana na wakubwa zetu, kwa hiyo tayari tumeshalink taarifa, sisi tunawashauri ili liweze kuwa na ufuatiliaji mzuri, mrudi Mapinga Polisi mkaripoti. Wakati huo wanatuambia hivyo,  tumeshatumia zaidi ya masaa mawili toka hilo tukio limetokea.

Kwa hiyo kile kitendo cha kutoka Mbweni Polisi mpaka kufika Mapinga ni almost karibu saa saba [usiku]. Tulivyofika Mapinga Polisi nikatoa briefing ya tukio lilivyokuwa, nilimkuta Askari wa kike pale nakumbuka ni WP5808, akanisikiliza akaniambia kaka huwezi ukasema wewe wamekudhibiti watu watatu wakashindwa kuondoka na wewe. Wakaondoka na gari na huyo jirani yako, aidha unadaiwa…. Nikamuambia sina deni na mtu wala hakuna biashara useme pengine kuna kitu ambacho mtu anaweza kufuata cha dizaini hiyo.

Akaniuliza je huyo mwenzako anafanya kazi gani, mimi nikamweleza, huyu mtu anafanya biashara zake za kawaida na pia ni mwanasiasa, akaniambia ngoja na mimi niwasiliane na wakubwa zangu. Akapiga simu kadhaa, nikaongea na mmoja niliona jina lake kwenye hiyo simu yake anaitwa Afande Amina. Nikazungumza naye baadaye akasema sawa nipe huyo Askari niongee naye, wakazungumza baadaye akampigia RCO wa mkoa wa Pwani.

Akazungumza na RCO wa mkoa wa Pwani almost ilikuwa inakaribia saa saba naa kuelekea saa nane. RCO wa mkoa wa Pwani akaniambia nisikilize nikupe taarifa sahihi niliyonayo. Hii ni baada ya kunihoji particulars zangu: majina, ninafanya kazi gani, labda ninamiliki kampuni gani, ni kipi amabcho ninakifahamu kwa huyo jirani yangu, huyo jirani yangu anafanya nini, ni mwanachama wa chama gani. Nilivyomueleza akaniambia hao ndio hao wanaharakati.

Sasa baada ya kuniambia vile, nikamuambia sasa Afande naomba unishauri mimi nifanye nini. Akaniambia nisikilize maelekezo ninayokuambia, taarifa nilizonazo rasmi, gari yako imetelekezwa Mbweni na nimetoa maelekezo ipelekwe kituo cha polisi Mbweni. Wewe kesho asubuhi unatakiwa uende ukaifuatilie gari yako, nikamuambia samahani Afande kwenye gari nilikuwa nina laptop ambayo ndio kila kitu kwenye kampuni yangu, ndio imebeba kila kitu, particulars zote kwenye kampuni yangu. Na pia nilikuwa nina fedha taslimu kwenye begi, akaniuliza shilingi ngapi nikamuambia kiasi cha shilingi laki nane na elfu sabini.

Baada ya hapo akaniambia mimi siwezi nikaguarantee hivyo vitu unavyovitaja kwa sababu sijaenda kwenye ukaguzi wa gari. Baada ya hapo nikamuomba ya kwamba je Mbweni Polisi nitaenda kwa maelezo kama haya nitakayoeleza kwa mdomo au kuna kitu ninachoandikiwa, aidha kama kuna RB au kuna maelezo au pengine ninaenda kumuona nani. Akaniambia wakati wa kwenda utanijulisha, utanipigia simu na chukua namba yangu ya simu kwa huyo Askari, then wakati wa kwenda hiyo asubuhi unipigie simu.

Baada ya kupata taarifa hizo ikanilazimu niombe walionipa support ya kwenda pale wanipeleke nyumbani nilivyofika nyumbani ndio nikakuta taharuki tayari. Familia ya Djumbe wako kwenye sintofahamu, familia yangu iko kwenye sintofahamu, lakini tukakubaliana kwa vile Djumbe ni mwanachama wa CHADEMA lazima pia hizi taarifa tuzipeleke kwenye ofisi ya makao makuu ya chama ili waweze kufanya ufuatiliaji zaidi.

Ndipo asubuhi nilivyokuja, ikabidi tuje kwanza ofisi za chama. Tukiwa hapa ndipo Naibu Katibu Mkuu akaniambia amepata taarifa kutoka kwa familia niliyowaacha nyumbani kwamba bwana Djumbe amepatikana, lakini hali yake ni mbaya na yupo na pingu. Wakati niko kwenye hayo maelezo ananieleza, ndio tukauona ugeni wa maafisa wa polisi

Djumbe

Mjira ya saa nne kasoro nilikuwa nimetoka kwenye shughuli zangu narejea nyumbani, nikiwa na jirani yangu, rafiki yangu na nilikuwa natumia gari yake. Mimi nilikuwa naendesha, yeye amekaa upande wa pili. Wakati tumekaribia kabisa nyumbani kwangu, plot moja kabla ya nyumbani kwangu, gari imekuja ikanipita upande wa kulia ikaniovertake haraka, gari aina ya Pro Box ikaniblock kwa mbele, halafu gari nyingine ikaniblock kwa nyuma wakashuka watu wengi nafikiri kama watano au sita.

Wakafungua mlango wangu wakamshusha yule bwana ambaye nilikuwa naye upande wa pili, wakanibeba kwa nguvu, sasa na mimi nikajua ni utekaji, nikaanza kupambana nao napiga kelele watekaji, watekaji, watekaji.

Nikaanza kupambana nao, napiga ngumi na nini lakini wakanizidi wakaja wengi, wakanirusha nyuma ya hiyo gari halafu wakanifunga pingu kama mnavyoziona hizi. Wakanifunga hizi pingu ndio wakaendelea kunishambulia sasa. Hizi damu mnazoziona walikuwa wananishambulia na kitako cha bunduki wanapiga kichwani na wanasema leo ndiyo siku yako ya mwisho.

Na mimi sasa nikawa najaribu kupambana nao, lakini sasa kwa sababu nilikuwa nimeshapigwa pingu, ikawa ngumu kuwakabili. Lakini wakati tunakwenda, barabara ni mbaya sana kutokea pale nyumbani kwangu mpaka kwenye barabara ya lami. Ile gari ilikuwa inakimbia inaruka sana, kwa hiyo pingu hizi zikakaza kwenye mikono sana kidogo nikawa nahisi mikono inataka kukatika. Kama unavyoona zimekaza sana.

Kwa hiyo sasa nikawa nakosa nguvu ya kukabiliana nao. Lakini nikapata nguvu baada ya kugundua kwamba wanajadili kuna bodaboda wanafuatilia, wanafuatilia hiyo gari. Na wakawa wanajadili wanasema bodaboda wanafuatilia na wanaongezeka. Sasa wakati wanakimbia na mimi nikawa najaribu kutumia fursa ya attention waliyoihamishia kwa bodaboda. Walikuwa wameNiweka kwenye buti ya ile gari ya probox, nimejaribu kushika lock ya kwanza, ya pili zote zikawa haziwezi kufunguka na nimefungwa pingu. Hata hivyo walikuwa wamenikanyaga pia.

Walivyoona bodaboda wanafuatilia sana, wakawa wanaelekezana twende kituo cha Polisi Mbweni, yule mwingine akasema hapana bosi amesema hii ishu siyo ya kupelekwa polisi. Huyu hatakiwi kufikishwa polisi, tunatakiwa tumfikishe kwa bosi amalizwe leo hii hii. Hatakiwi kwenda polisi.

Lakini sasa kwa sababu ya kukimbia hao bodaboda wakajikuta  wamefika ule msitu wa pale Mbweni, ule wa usalama. Sasa mimi nilikuwa sijui, lakini nikahisi walivyofika pale wakaona wana fursa ya kukabiliana na hao bodaboda. Wakashuka wote kuanza kupiga risasi, nimesikia wakisema wapige risasi hao bodaboda, piga risasi, wapige risasi wasiendelee kutufuata. Sasa wakashuka wote kwenye gari wakiwa wanaamini mimi niko kwenye buti siwezi kunyanyuka na nilikuwa nimefungwa hizi pingu.

Niliopoona tu wameshuka na wako upande mmoja wa gari, nikajirusha kwenye siti ya katikati haraka haraka, nikapeleka mikono yangu kwenye lock nikaitoa nikashukia upande wa pili, upande huo kuna msitu nikaingia msituni. Kwa hiyo wanakuja kushituka wanarudi kwenye gari mimi nimeshaingia msituni, wakaanza kunifuatilia wanapiga risasi, msitu umefunga sana hawawezi kupita.

Mimi nikawa natambaa, kiasi kwamba suruali yangu imenaswa kwenye miba nikaiacha humo, siwezi kujitoa kwa sababu nimefungwa pingu, nimetambaa kwenye miba kwa muda wa saa nzima na nusu ndio nikaweza kutoka upande wa pili.

Kwa hiyo namshukuru Mungu angalau niko salama sasa nimeweza kutoroka kwenye mikono ya hao wauaji.

Sikuwa na wallet ila nilikuwa na hela kama laki saba, wallet yangu nilikuwa sijaibeba. Hizo hela wameninyang’anya kabisa wakati naona amenikanyaga ameshanifunga pingu, ananipiga na kitako cha bastola kichwani, akaingiza mkono akachukua.

Nilikuwa nimebaba hizo hela kwa sababu gari yangu ilikuwa iko garage, nilikuwa najua wakimaliza kutengeneza niwalipe mafundi. Huyo amechukua kabisa huyo alikuwa ananipiga na hicho kitako cha bunduki, ni askari mweusi mweusi lakini anaonekana ana lafudhi ya kizanzibari.

Ndio anaonekana alikuwa kiongozi wa huo msafara, kwa sababu wenzake wakati wanasema hao bodaboda wanatufuatilia inabidi tukimbilie polisi Mbweni, yeye akawaambia bosi amesema huyo hatakiwi kufikishwa kituo cha polisi, tunatakiwa tutoroke tuwakimbie hao bodaboda, huyu anatakiwa afikishwa kwa bosi akamalizane naye.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×