Nimeona barua ya Msajili wa vyama vya siasa Kwenda kwa CHADEMA iliyowapa CHADEMA siku kumi na nne(14) za kujieleza ni kwanini wasichukuliwe hatua za kisheria ikiwemo ama kusimamishwa kwa usajili wa chama husika au kupigwa faini.
Pamoja na mambo mengine ofisi ya Msajili imeainisha tuhuma mbalimbali ikiwemo kuhamasisha maandamano kwa lengo la kushinikiza mwenyekiti wao ndugu Tundu Lissu kuachiwa huru, tuhuma nyingine ni matumizi ya lugha za uchochezi na matusi, katika kuhalalisha tuhuma hizo ofisi ya Msajili imenukuu kauli za viongozi kadhaa wa CHADEMA akiwemo makamu mwenyekiti wa chama ndugu John Heche, mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Korogwe na mwisho msimamo wa kamati kuu ya chama hicho uliotolewa kwa umma na katibu mkuu wa chama hicho ndugu John Mnyika tarehe 05 Mei 2026.
Vifungu alivyonukuu Msajili
Katika barua iliyowasilishwa CHADEMA Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imenukuu vifungu kadhaa vya sheria kama sehemu ya kuhalalisha tuhuma ilizotoa kwa CHADEMA. Nitaanza na kifungu kimoja baada ya kingine, uhalali wake kisheria na kama kina uhusiano wa moja kwa moja na tuhuma zilizotolewa dhidi ya CHADEMA na mwisho kama Msajili wa vyama vya siasa ana mamlaka kisheria kuchukua hatua alizoainisha kuzichukua katika barua yake.
Kabla ya kuanza kujadili vifungu tajwa, naomba nikiri kwamba ni kweli Msajili wa vyama vya siasa ndiye mamlaka kuu iliyopewa mamlaka kisheria ya kushughulika na masuala yote yanayohusu uendeshaji wa shughuli za vyama vya siasa ikiwemo kusajili na kufuta vyama kama ilivyoanisha katika vifungu vya 4, 7, 12, 13, 19, 20, 24(3)(4), 29(2),30, 32,33,35, 36, 37, 39, 43, 44, 46.
Sasa naomba nianze na vifungu vya Sheria vilivyonukuliwa katika barua ya Msajili.
Kifungu cha 7, kwa mujibu wa barua ya Msajili wa Vyama pamoja na mambo mengine imenukuu kifungu cha 7 ikikitumia kama kifungu wezeshi(Enabling provision) kinachompa Mamlaka Msajili wa Vyama vya Siasa kutoa fursa kwa chama cha siasa kinachoonekana kukiuka masharti ya sheria ya usajili sanjali na Sheria ya Vyama vya siasa. Kwa ujumla kifungu hicho kinazungumzia zaidi mamlaka ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuomba nyaraka yoyote ama kwa kiongozi moja kwa moja au chama cha siasa.

Kwa mujibu wa kifungu hiki Bunge halikudhamiria kumpa Msajili mamlaka ya kutoa wasaa kwa chama cha siasa kuwasilisha maelezo ni kwanini kisichukuliwe hatua za kisheria bali dhamira ya Bunge ilikuwa kumpa mamlaka Msajili mamlaka ya wakati wowote anaoona inafaa kuomba nyaraka au mpango wa utekelezaji wa shughuli za kila siku za chama husika.
Hivyo kwa maoni yangu Msajili amejielekeza vibaya kutumia kifungu cha 7 kama kifungu wezeshi kinachompa mamlaka ya kukipa chama fursa ya kuwasilisha maelezo kwani hakina uhusiano na kanuni hiyo.
Kifungu cha 19(2), kwa ujumla kifungu cha 19 kinahusu masharti ya jumla kuhusu usajili wa muda yaani( Provisional registration) kwa chama cha siasa ambapo pamoja na mambo mengine kifungu cha 19(2) kinaweka masharti ya chama cha siasa kutokidhi vigezo vya kupata usajili wa muda ikiwa (a) chama husika kinaonekana kuwa na dalili za kuhamasisha kauli za kidini (b)chama husika kinaonekana kuwa na viashiria vya kuhamasisha ukabila na ukanda, (c) chama husika kinaonekana kuhamasisha kuvunjwa kwa muungano (d) chama husika kinaonekana kutumia njia zisizo za kikatiba kupata madalaka (e) chama husika kinaonekana kufanya shughuli zake za kisiasa katika upande mmoja wa muungano (f) chama husika kutoruhusu kufanyika kwa uchaguzi wa viongozi na (g) chama husika kuruhusu viongozi wake kutumia lugha za matusi, kashifa, uchochezi ambayo yanaweza kupelekea uvunjifu wa amani.
Kwa ujumla kifungu cha 19(2) kinahusu masharti ya jumla kwa chama cha siasa kupata usajili wa muda(provisional registration) masharti ambayo hayatumiki kwa CHADEMA. Kwa maoni yangu Ofisi ya Msajili kutumia kifungu cha 19(2) kama kifungu wezeshi(enabling provision) kama sehemu ya kuhalalisha tuhuma dhidi ya CHADEMA ni kujielekeza vibaya kwani dhamira ya Bunge ilikuwa kumpa mamlaka Msajili kujiridhisha kabla hajatoa usajili wa muda kwa chama cha siasa.

Kwa kuzingatia ukweli kwamba CHADEMA ni chama chenye usajili wa kudumu tayari na hivyo kutumia kifungu cha 19(2) kuhalalisha tuhuma dhidi yake ni kujielekeza vibaya kwani kifungu hicho kinavihusu zaidi vyama vyenye usajili wa muda.
Kusitisha au kufuta usajili
Kifungu cha 39(2), kwa ujumla kifungu cha 39 kinampa mamlaka Msajili wa Vyama vya Siasa ama kusitisha au kufuta usajili wa chama cha siasa baada ya kuonekana kukiuka masharti ya Sheria ya Vyama vya Siasa au Katiba ya chama husika. Kifungu cha 39(2) kinaweka masharti ambayo yanapashwa kufuatwa na Msajili kabla hajatekeleza mamlaka aliyopewa katika kifungu cha 39(1). Nitaelezea hapo baadaye masharti ambayo yanapashwa kufuatwa kabla hatua za kusitisha au kufuta chama cha siasa.
Kifungu cha 45, kwa ujumla kifungu cha 45(1) kinahusu masharti ya jumla ya adhabu ikiwemo faini, kusitishwa kwa shughuli za chama, kufutwa kwa chama na kifungo kwa chama kitachokiuka utaratibu wa usajili wake ambapo kitapigwa faini isiyopungua millioni tatu(3) na isiyozidi millioni kumi(10) au kifungo kisichopungua miezi sita na kichozidi mwaka mmoja au vyote kwa pamoja.
Kifungu cha 45(2) kinahusu masharti ya jumla katika makosa ambayo yanafanywa na vyama vya siasa huku yakiwa hayajaanishwa moja kwa moja katika katika Sheria ya Vyama vya Siasa sura ya 258 rekebu ya 2023 ambapo kitapigwa faini isiyopungua million kumi na isiyozidi million Hamsini, kusitishwa au kufutwa kwa usajili.
Katika kifungu hiki mamlaka pekee aliyonayo Msajili ni ama kusitisha shughuli za chama husika au kukifuta, lakini katika eneo la faini au kifungo nafikiri haya ni mamlaka ya mahakama na si Msajili.
Mamlaka ya kutoa faini yapo katika baadhi ya taasisi za umma zenye hadhi ya mamlaka au mabaraza yaani( regulatory authorities au tribunals) na kwa kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa hana hadhi ya udhibiti kwa mujibu wa sheria ni maoni yangu kuwa hana mamlaka kisheria ya kutoza faini kwa vyama vya siasa. Ni mahakama pekee ndio itakayoweza kukitumia kifungu hiki katika eneo la faini na kifungo.
Kwa chama cha siasa chenye usajili wa kudumu kama CHADEMA mazingira pekee yanayoweza kupelekea chama cha siasa kufutwa ni haya yafuatayo:
i. Chama kushindwa kuitisha mkutano mkuu wa mwaka kwa ajili ya kufanya uchaguzi wa viongozi wakuu wa kitaifa kwa mujibu wa masharti ya Katiba ya chama husika kama ilivyoanishwa katika kifungu cha 29(1)(2) cha Sheria ya Vyama vya Siasa
ii. Chama cha siasa kushindwa kuwasilisha tamko la mali, matumizi, michango ya wahisani mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa chama husika kwa mujibu wa kifungu cha 30(1)(4)(a)
iii. Chama kuwasilisha tamko la uongo kwa mujibu wa kifungu cha 30(4))b) cha Sheria ya Vyama vya Siasa.
Utaratibu wa kufuta chama
Kabla Msajili wa Vyama vya Siasa hajatekeleza mamlaka ya kusitisha shughuli za chama cha siasa au kukifuta atapashwa kufuata taratibu zifuatazo kwa mujibu wa kifungu cha 39(2):
- Kutoa fursa ya kukisikiliza chama husika, fursa hiyo ni sharti itolewe kwa maandishi huku taarifa hiyo ikiainisha tuhuma na sababu.
- Chama husika kushindwa kuwasilisha utetezi wake ndani ya muda ulioanishwa ndani ya taarifa ya mashitaka
- Msajili awe amewasilisha taarifa ya kusudio la kusitisha shughuli za chama au kukifuata chama husika kwa Waziri mwenye dhamana na masuala ya vyama vya siasa pamoja na kiambatanisho cha utetezi kama kipo.
- Msajili hatofuta au kusitisha shughuli za chama cha siasa miezi 12 kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu.
Uamuzi wa Msajili wa Vyama vya siasa katika kutekeleza mamlaka yake kusitisha au kufuta chama cha siasa kama ilivyoanishwa katika vifungu vya 19(1)(2), 29 na 30 vya Sheria ya Vyama vya Siasa utakuwa wa mwisho na hautahojiwa katika mahakama yoyote ingawa haitatafsiriwa kuzuia uamuzi huo kupingwa mahakama kuu kwa njia ya mapitio(Judicial Review).
Kwa maoni yangu kwa barua ambayo Msajili amewaandikia CHADEMA sanjali na tuhuma alizoainisha katika barua hiyo, sababu zilizoanishwa katika barua hiyo si miongoni mwa sababu ambazo zimeanishwa katika vifungu vya 29 na 30 ambazo ndio sababu pekee zinazoweza kupelekea CHADEMA ama kusitishiwa kufanya shughuli zake au kufutiwa usajili. Ni maoni yangu kwamba Msajili amejielekeza vibaya kutumia kifungu cha 19(2) cha Sheria ya Vyama vya Siasa kwani kifungu hicho kinahusu vyama vyenye usajili wa muda(Provisional registration).
Naomba nihitimishe kwa kuzishauri mamlaka za Serikali akiwemo Msajili wa Vyama vya Siasa kama ifuatavyo
- Kutumia vyombo vilivyoanishwa katika Sheria ya Vyama vya siasa ikiwemo Baraza la Vyama vya Siasa kama linavyoanzishwa katika kifungu cha 43 cha Sheria ya Vyama vya Siasa kutatua migogoro ya kisiasa baina ya Msajili na vyama vya siasa badala ya kutumia mabavu ikiwemo kutishia kufuta vyama
- Mamlaka za Tanzania ikiwemo Jeshi la Polisi ziwe na ustahimilivu katika masuala yanayohusu kauli za majukwaani ikiwemo za kisiasa badala ya kutumia mkono wa Mahakama kushitakiana.
Maduhu William ni Wakili wa Mahakama Kuu na mtetezi wa Haki za Binadamu, pia ni Meneja wa Haki za Binadamu kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu , anapatikana kupitia mkulwa@humanrights.or.tz .Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.comkwa ufafanuzi zaidi.