Bajeti ya Shilingi Trilioni 2.44 imepitishwa na Bunge mnamo Mei 25, 2026, kwa ajili ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mwaka wa fedha 2026/27. Bajeti hii ni ongezeko kutoka Trilioni 2.06 kwa bajeti iliyokuwa mwaka wa fedha 2025/26.
Bajeti hii mpya inapitishwa wakati Wizara ikiripoti kuwa katika bajeti ya sasa mpaka kufikia Aprili 2025 imeweza kupokea takribani asilimia 106 ya fedha zote zilizotengwa. Matumizi haya juu ya bajeti yanatokana na kiasi cha shilingi Bilioni 414 kilichotolewa kutoka serikali kuu kwenda kwenye Wizara kwa ajili ya Operesheni Maalum mwaka 2025.
Ingawa Wizara haijaeleza kiundani operesheni hiyo maalum iliyofanyika mwaka wa fedha 2025/26 ilikuwa ni ipi, ukubwa wa matumizi unaonesha operesheni hi, ni ile iliyofanyika kufuatia maandamano ya Oktoba 29, 2025. Mnamo Oktoba 29, 2025, Mkuu wa Jeshi la Polisi alitangaza operesheni maalumu, ikihusisha zuio la kutoka nje. Operesheni hiyo ambayo serikali imesisitiza ilihitajika, imeendelea kukosolewa vikali kufuatia mauaji ya Watanzania katika mikoa mbalimbali Tanzania.
Wizara imeeleza mpaka kufikia Aprili 2026 ilipokea Trilioni 2.19 kulinganisha na bajeti iliyopitishwa ya Trilioni 2.06. Katika bajeti iliyopitishwa, Bilioni 950.3 zilitengwa kwa ajili ya mishahara, ambapo mpaka Aprili 2026, Bilioni 887.36 zimeshatumika, hii ikimaanisha bado kuna kiwango kitakachohitajika mpaka kufikia mwisho wa bajeti Juni 2026.
Katika eneo la matumizi mengineyo, Wizara imepokea Bilioni 632.09 kati ya bajeti ya shilingi Bilioni 701 na pia kwenye bajeti ya maendeleo, Wizara imepokea Bilioni 670 mpaka kufikia Aprili 2026, ikiwa fedha zilizopitishwa ni Bilioni 415, ikimaanisha kulikuwa na nyongeza ya Bilioni 255 kwenye eneo hilo.
Vipaumbele vya Wizara 2026/27
Katika bajeti iliyopitishwa kwa mwaka 2026/27, Trilioni 1.95 imetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida inayojumuisha Trilioni 1.18 kwa ajili ya mishahara na Bilioni 769.5 kwa matumizi mengineyo.
Maeneo ya kipaumbele ya bajeti mpya ni pamoja na maboresho ya mindombinu ya kidigitali na kawaida. Wizara inakusudia kujenga vituo vipya vya polisi pamoja na maboresho ya vituo vilivyoharibiwa kufuatia maandamano ya Oktoba 29, 2025. Wizara imeweka pia nguvu kubwa kwenye kujiimarisha kidigitali, hasa katika kupambana na uhalifu mtandaoni.
“Katika mwaka wa fedha 2026/27 Wizara kupitia Jeshi la Polisi itandelea kudhibiti uhalifu nchini ikiwemo matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, udukuzi wa taarifa kimtandao na kukamilisha uanzishaji wa ofisi za kanda za upelelezi wa makosa ya jinai na uhalifu wa kimtandao katika jiji la Dodoma na Zanzibar,” Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobasi Katambi alilieleza Bunge.
“Na kuimarisha vikosi maalum kudhibiti taarifa potofu na uchochezi mtandaoni. Pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu athari za kusambaza taarifa za uongo,” taarifa hiyo inaongeza.
Wizara pia imepanga kuongeza uwezo katika kupambana na uhamiaji haramu pamoja na usafirishaji haramu wa binadamu, na kuboresha magereza na huduma za uhamiaji.
Katika kuhitimisha hotuba ya bajeti, Waziri wa Mambo ya Ndani alieleza mambo kadhaa ambayo ni matishio ya moja kwa moja ya usalama wa nchi. Baadhi ya mambo hayo ni uhamiaji haramu, wananchi kushindwa kutoa taarifa wanapoona dalili za uhalifu. Pia taasisi kama NGO zinapochepuka kutoka kwenye majukumu yake pamoja na vyama vya siasa.
“Vyama vya siasa visipotumika vizuri ni tishio kubwa la usalama. Ni tishio kubwa la usalama pale viongozi wa vyama vya siasa watakapotumia ndimi na kauli zao, maandiko na machapisho, kuhamasisha vurugu na sio mapatano,” Waziri wa Mmabo ya Ndani alilieleza Bunge.
“Pale itakapotumika ndimi na kauli zao kuhamasisha wananchi kwenda kufanya mambo ambayo yanapelekea kuvunja amani ya nchi. Tutazidi kukumbushana na kusimamia taratibu, kwa sababu Wizara ya Mambo ya Ndani ni msimamizi wa masuala yote ya amani na usalama na nidhamu ya taifa kwenye utekelezaji wa sheria,” ameendelea kusisitiza.
Katambi ameeleza kuwa malalamiko yamekuwa yakielekezwa kwa Polisi na vyama vya siasa kwa sababu vyama hivyo havitimizi wajibu wake. Hata hivyo vyama vikuu vya upinzani ikiwemo CHADEMA na ACT Wazalendo wamekuwa wakisisitiza juu ya Polisi kuacha kushiriki moja kwa moja katika siasa wakieleza jambo hilo linahatarisha Umoja wa kitaifa.