The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Sababu Zilizofanya Kampuni Iliyosajiliwa Falme za Kiarabu na Rostam Aziz Kuweza Kununua Kampuni ya Gesi Tanzania Kwa Shilingi 26,000 (Tsh. 26,000)

Kampuni ya Amber Energy Investment kutoka Falme za Kiarabu inategemewa kuwa mmiliki mkubwa katika mradi huo pamoja na mshirika wake Taifa Gas

subscribe to our newsletter!

Mnamo Aprili 13, 2026, kampuni ya Orca Energy iliyoendesha vitalu vya gesi vya Songosongo kwa takribani miaka 25 ilitangaza kuwa imefikia uamuzi wa kuuza biashara yake ya gesi Tanzania kwa takribani dola kumi, ambayo ni sawa na takribani Shilingi 26,000 za kitanzania.

Kampuni hiyo ilitangaza kuwa wanunuzi ni ushirika wa wawili yaani kwanza kampuni ya Amber Energy Investment kutoka Falme za Kiarabu, ambayo ndio itakuwa mmiliki mkubwa kwa asilimia 51 ya hisa; mmiliki hasa wa kampuni hii hajawekwa wazi.

Mshirika wa pili ni Taifa Gas, kampuni inayomilikiwa na mfanyabiashara Rostam Aziz, ambaye atachukua asilimia 49 ya hisa. Kampuni hii kupitia kampuni zake za Pan African Energy Corporation (Mauritius) na  PanAfrican Energy Tanzania (PAET) ndio  mzalishaji mkubwa wa gesi inayotumika kwenye viwanda na umeme Tanzania.

Kati ya mwaka 2021 mpaka mwaka 2025 pekee kampuni hii inayoendesha visima kadhaa vya gesi katika eneo la Songosongo iliweza kupata mapato ya takribani dola milioni 513 ambazo ni sawa na Trilioni 1.3 za Kitanzania.

Sasa imekuwaje ‘mmiliki asiyefahamika’ na Rostam Aziz kuweza kununua kampuni hii kwa shilingi 26,000 pekee?

Maamuzi ya Kuuza Kampuni

Mkataba ambao Tanzania uliingia na kampuni ya Orca-PAET ni mkataba uliokuwa wa miaka 25, yaani kuanzia October 2001 mpaka October 2026.

Ambapo kampuni hii ilipewa mkataba wa kuchimba gesi inayotumika sasa viwandani, na kwenye kuzalisha umeme, kampuni hii ndiyo mzalishaji mkubwa.

Katika mkataba ulioingiwa, kampuni hii ina fursa ya kuongezewa muda wa leseni, yaani leseni ya kuendelea kutafuta gesi mpya, na kuendelea kuzalisha gesi ya sasa iliyopatikana.

Hata hivyo, kusudi kubwa la mkataba kuwa miaka 25, ni kwamba Tanzania itakuwa imejenga uwezo wa kuendesha miradi ya gesi, tofauti na wakati unaanza, kwa hiyo kama kutakuwa na maslahi Tanzania itaweza kuongeza mkataba au kutofanya hivyo.

Kuanzia mwaka 2023, kampuni ya PAET ilituma ujumbe kwa TPDC, ambaye ndiye mshirika wake kwenye gesi, kueleza kuwa serikali iongeze muda wa leseni, hasa kutokana na kazi nzuri iliyofanya kwa kipindi chote.

Hata hivyo, jambo la kuongezewa muda wa leseni halikutokea na muda ukaendelea kuyoyoma, kuelekea ukomo wa leseni yaani Oktoba 2026.

Mazungumzo yaliyofanyika mwanzoni mwa mwaka 2024, yalionesha kampuni hiyo haitapata inachokitaka, yaani kuongezwa kwa muda wa leseni.  Ndipo hapo mnamo Agosti 2024, kampuni hiyo ikaamua kuipeleka Tanzania katika Mahakama za Kimataifa za Usuluhishi wa Biashara, ikidai hasara za takribani Dola Bilioni 1.2, chimbuko kubwa likiwa ni kunyimwa kuongezewa leseni.

Hata hivyo muda wa leseni kuisha yaani Oktoba 2026 umeendelea kukaribia. Kimkataba kampuni hiyo haimiliki gesi, lakini pia haimiliki taarifa muhimu za kijiolojia na wala haimiliki mitambo muhimu ya uchakataji wa gesi, yote haya ni mali ya Tanzania. Kwa hivyo biashara kubwa ya kampuni hii ni leseni na mkataba uliongiwa mwaka 2001 ambao unaisha Oktoba 2026.

Mnamo Aprili 13, 2026, kampuni hii ikitangaza kuuza kampuni yake ya gesi kwa dola 10, hii ikijumuisha kuachana na madai yote, ambapo kampuni hii ilieleza mambo kadhaa yaliyosababisha kufikia hapo.

Bodi ya kampuni hiyo ilieleza kuwa, kuelekea mbele, kampuni hiyo haina thamani yeyote Tanzania. Hii ni kwa sababu; taarifa za kijiolojia zote ni mali ya serikali ya Tanzania. Mali zote zisizohamishika ni mali ya Tanzania. Lakini pia kampuni hiyo inategemea kuwa na mzigo wa madeni ya kodi na tozo zingine za kiutendaji.

Bodi ya kampuni hiyo iliamua kufanya maamuzi ambayo yanayofanana na mkataba unavyosema kuwa leseni itaisha Oktoba 2026. Bodi ya kampuni hiyo ilitanabaisha kuwa ingehitajika kuwa na fedha nyingi  kwa ajili ya kuendelea na kesi ambayo ingechukua muda mrefu, jambo ambalo walionelea ni bora fedha zikatumika kuwalipa wanye hisa.

Hatma ya Kitalu cha Gesi

Kisheria na kimkataba hatma ya gesi, na shughuli zote zilizokuwa zinaendeshwa na PAET zinarudi kwa serikali ya Tanzania.

Kuhusu uzoefu wa kuendesha miradi ya gesi, kwa sasa, uzoefu mkubwa upo serikalini yaani kupitia shirika la TPDC, kupitia kampuni zake ikiwemo GASCO ambayo inaendesha mtambo wa Gesi wa Madimba, lakini pia TPDC inayoendesha vitalu vya gesi pamoja na kampuni ya Maurel & Prom.

Tathmini ya sasa ya PURA inaonesha vitalu vya gesi anavyoachia PAET vinaweza kufanya kazi walau mpaka mwaka 2036 bila utafutaji mwingine.

Hata hivyo katika eneo hilo tayari kuna gesi kati ya Trilioni 1 mpaka Trilioni 2.5 za ujazo, kwa kulinganisha na sasa, gesi iliyotumika toka kuanza kwa uzalishaji mwaka 2004 ni Bilioni za ujazo 544 pekee, hii ikimaanisha kuelekea mbele bado kuna fursa kubwa kwa biashara hiyo.

Kwa Mmiliki Asiyefahamika na Rostam Aziz, ili kurudisha dola 10 waliyotumia kununua biashara hiyo watahitaji kupata mkataba wa kuendesha visima vya gesi vya Songosongo.

Wataalamu wa mambo wanaeleza, itategemea na serikali itakavyoamua, kama kuendelea na lengo la miaka 25 iliyopita kwa TPDC kuendesha nyenzo hizi muhimu za kiuchumi au kupata kampuni nyingine itayoendesha sekta hiyo.

Kwa sasa tayari Tume ya Ushindani imeshatangaza biashara hiyo ya mauziano na kampuni, ambapo kila kitu kikienda sawa kampuni za PAET na PAEM zote zitakuwa chini ya kampuni ya kutoka Falme za Kiarabu, pamoja na Taifa Gas ya Rostam Aziz

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×