Dodoma. Serikali inatarajia kuwasilisha Bungeni bajeti kuu kwa mwaka wa fedha 2026/27 siku ya Juni 10, 2026 majira ya 10 jioni ambayo ni Alhamisi ya mbili ya mwezi Juni kama ilivyo desturi kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri wa Fedha Balozi Khamis Mussa Omar amesema bajeti hiyo ni ya kipekee kwani ndiyo bajeti ya kwanza katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025-2030.
Katika mwaka mwaka wa fedha wa 2026/27 Serikali inatarajia kukusanya na kutumia kiasi cha shilingi trilioni 62.3, sawa na ongezeko la takribani asilimia 10 ukilinganisha na bajeti ya shilingi trilioni 56.49 katika mwaka wa fedha wa 2025/26.
Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 46.8 zinatarajiwa kukusanywa kupitia mapato ya ndani ili kugharamia sehemu kubwa ya matumizi yaliyopangwa. Ambapo Balozi Omar ameeleza kuwa kumekuwa na mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa mapato ya ndani.
“Mwaka huu 2025/26 tumekuwa na mwenendo mzuri wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ambapo kwa kiasi kikubwa yamefikia lengo,” amesema Balozi Omar.
Amesema kuwa kwa ujumla bajeti hii ina lengo la kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kuongeza ajira, kuvutia uwekezaji na kuimarisha ustawi wa wananchi na
“Fedha hizi zitaelekezwa katika kuendelea na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), kuboresha mtandao wa barabara, kuimarisha huduma za maji, kuendeleza miradi ya nishati pamoja na uwekezaji katika rasilimali watu na maendeleo ya ujuzi,” amesema Balozi Omar.
Usomaji wa bajeti kuu ya Serikali utatanguliwa na taarifa ya hali ya uchumi kwa mwaka 2025 na mwelekeo wa uchumi kwa mwaka 2026. Taarifa hiyo itasomwa Bungeni asubuhi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo.
Ameeleza pia uandaaji wa bajeti umeshilikisha wadau mbalimbali kupitia Kamati ya Wataalam wa Maboresho ya Kodi (Task Force on Tax Reforms) pamoja na Kamati ya Ushauri ya Ngazi ya Juu ya ‘Think Tank’ ambapo mapendekezo 727 yalitolewa.
“Kati ya mapendekezo hayo, 125 yalikubaliwa kama yalivyowasilishwa, 121 yalifanyiwa maboresho na kukubaliwa, huku 295 yakikataliwa baada ya kufanyiwa uchambuzi wa kina,”