Jumapili asubuhi, mume wa Ramatulayi, Modu Falli, alimwambia mkewe wasimsubiri kula mchana. Jioni jamaa watatu wa mumewe walifika kumwambia Ramatulayi kwamba mumewe ameoa mke wa pili. Hivyo tu.
Baada ya kuishi na Ramatulayi kwa miaka 25 kwenye ndoa na kupata watoto 12, Modu alimtelekeza mkewe na watoto kwa kulowea kwa mke mdogo, Binetuu, aliyezaa naye watoto watatu ndani ya miaka mitano. Ramatulayi anajikuta sio mjane, sio mtalaka, lakini pia hana mume. Ghafla Modu Falli anafariki.
Ramatulayi akiwa eda anamuandikia barua ndefu shoga yake, Aisatu, aliyeko ughaibuni. Barua Ndefu Kama Hii ni riwaya iliyoandikwa mwaka 1980 na Mariama Bâ. Chapa ya kwanza ya tafsiri ilitoka mwaka 1994. Mimi nimesoma chapa ya 2017.
Unaposoma Barua Ndefu, jambo la muhimu kuliko yote nadhani ni jinsi mwandishi anavyotupa fursa ya kuuona ulimwengu kupitia jicho ya mwanamke. Ramatulayi ni mwalimu, lakini hatusimulii mapambano yake kazini. Mambo anayoandika ni yale yanayotokea majumbani.
Na anaujua ulimwengu huu kwa sababu yeye ndio huwa “mtu wa kwanza kuamka na mtu wa mwisho kulala” (uk 21). Kuna umuhimu wa kuuona ulimwengu kupitia wanawake kwa sababu hatuwezi kuendeleza vita ya ukombozi wa wanawake wakati mitazamo ya wanawake wenyewe hatuijui.
Mfano mzuri wa kuuona ulimwengu kupitia macho ya mwanamke ni jinsi Ramatulayi alivyochukulia mumewe kuoa mke mwingine. Ukiachilia mbali kuwa aliamini mumewe alikuwa na muonekano mzuri, alipenda mtazamo wake juu ya maisha.
SOMA ZAIDI: Kale ya Washairi wa Pemba: Wasotumia Akili Mnemba
Ramatulayi alifurahishwa na jinsi Modu Falli alivyojituma katika kazi na kujiendeleza kwenye elimu na kutokupenda makuu. Ndio maana, kinyume na matarajio ya wengi, Modu Falli alipomuoa Binetuu, Ramatolayi hakudai talaka.
Kulingana na maelezo yake, jambo lililomuumiza baada Binetuu kuolewa ni Modu Falli kuitelekeza familia yake ya kwanza. Je, ni nani angemkomboa Ramatulayi kutoka kwenye ndoa aliyoamini ilikuwa na mwanaume mzuri?
Mila na desturi
Ramatulayi anatwambia tangu mtoto kulingana na mafundisho ya dini, alishajiandaa kisaikolojia kwamba mwanamke hukaa eda mume akifariki. Hivyo, alianza eda akiwa na utulivu.
Lakini anajiuliza kwamba Modu alishafiriki, na mwili wake huko kaburini unaendelea kuharibika, hizi dua mfululizo na karamu zinazoendelea nyumbani kwake ni za nini? Zinamnufaisha nani?
Kwa sababu watu nao kwa msukumo wa jamii huendelea kuweka msiba bila kujiuliza: msiba anawekewa marehemu ama sisi tuliobaki? Mwandishi anatupa changamoto ya kutafakari ni mila zipi zinatupelekesha na hatuzikubali, lakini pia hatuwezi kuzikataa? Na mila zipi tunazikubali na kuzitekeleza kwa moyo mkunjufu kwa sababu tunaziita desturi zetu?
Ramatulayi ni kizazi cha wanawake waliopelekwa shule ili kuikomboa jamii. Waliletwa pamoja na kutoka makoloni ya Ufaransa. Wao walijiona ni jamii ya Waafrika. Walielewa dhulma ya ubeberu kiasi kwamba japo walisoma vyuo vya Wafaransa, walijiweka mstari wa mbele kwenye mapambano ya uhuru kwa kusoma kuhusu mapambano ya Afrika Kaskazini.
SOMA ZAIDI: ‘Kale ya Washairi wa Pemba’ na Ufundi wa Mshairi Mahiri Kamange
Walielewa ugumu wa mila na desturi, huku wakijua hawapaswi kushabikia usasa uliokuwa mbele yao. Na kwa sababu ya wadhifa wao kupanda kwenye jamii kutokana na kusoma, wanawake hawa wasomi walidhani walau wana uhuru wa kuchagua wachumba.
Hivyo, Ramatulayi aliamua kuolewa na Modu Falli badala ya Daudi Dengi. Aisatu, mtoto wa sonara fukara, akaolewa na Maudo Ba mwenye asili ya ukoo wa kifalme. Shoga yao, Jakilini, akaolewa na Samba Diaki, japo walitoka mataifa na imani tofauti.
Lahaula! Wote watatu kikawaramba. Wanaume waliowachagua kuwa waume zao wakachagua wanawake wengine, tena kuwa mabibi zao. Kwa bahati mbaya chaguo la mtu mmoja mmoja haliwezi kubadilisha mfumo unaosukuma mahusiano ya kijamii: mfumo wa ugawaji mali.
Mfumo wa ugawaji mali pia ulibeba mfumo dume. Hivyo, waume zao kwa sababu ya usomi na hadhi ya juu kwenye jamii waliweza kuwaaacha wanawake wasomi wenzao kwenye mataa na kuambaa na wanawake ambao hawakusoma na wadogo kiumri.
Mfumo huu humuadhibu yeyote anayejaribu kuupotezea kama sio kwa mali basi hata kama ilivyomkuta Jakilini akawa sio kichaa lakini pia sio timamu.
Ndoa ni watu wangapi?
Uhuru finyu waliokuwa nao wanawake wasomi katika kuwachagua wachumba wa kuwaoa ulizidi kuwa mdogo kwa sababu wazazi na familia walikuwa na nafasi kubwa sana katika mchakato huo. Mwanaume, pamoja na kumchumbia mhusika, ilibidi kukubalika kwa familia yake.
SOMA ZAIDI: Funzo Kutoka Riwaya ya ‘Haini’ ya Adam Shafi: Mtu Yeyote, na Muda Wowote, Anaweza Kugeuzwa Mhaini
Ramatulayi hakuwahi kumfurahia Daudi Dengi, daktari mkubwa na mtu maarufu. Mama yake Ramatulayi na familia kwa ujumla walimkubali Daudi Dengi zaidi kuliko Modu Falli.
Daudi Dengi alichumbia kwa nguvu ya pesa kwa sababu wakati wa uhaba wa vyakula, alitoa zawadi ya gunia la mchele kwa familia ya Ramatulayi. Na baada ya ndoa, mahusiano na wakwe (kwa wote wawili: mume na mke) yalikuwa sehemu kubwa ya ustawi wa ndoa.
Modu Falli alipomtelekeza mkewe, familia yake iliendeleza mahusiano mazuri na Ramatulayi. Kwa bahati mbaya, mamakwe wa Aisatu alishaamua tangu mwanzo kwamba mwanae hawezi kuwa na mke wa damu hafifu isiyo ya kifalme.
Hivyo, alisuka mkakati wa miaka kadhaa kuhakikisha ndoa ya Aisatu na Maudo Ba inavunjika. Cheti cha ndoa husainiwa na wanandoa, mashahidi wao na anayewafungisha ndoa.
Lakini je, wale walioko kwenye cheti ndio wanandoa peke yao, ama ndoa ni ya kijiji na ukoo? Ningependa kujua mawazo yako kwa sababu mimi nimeshindwa kujibu swali hili.
Uhaini wa mapenzi
Ramatulayi anauita uamuzi wa mwanaume kuoa mke mwingine kuwa uhaini. Kwa nini asiuite usaliti bali uhaini? Nini haswa kinafanya ndoa za mitara kuwa za kihaini wakati ni jambo linalokubalika kwenye jamii zetu?
SOMA ZAIDI: Utenzi wa Mwanakupona na Jitihada za Kumpumbaza Mume Kudumisha Ndoa
Kwa mtizamo wangu, kile anachokiita Ramatulayi uhaini kwenye mapenzi inatokana na mambo mawili. Kwanza, kwa sababu wasomi hupitia mifumo ya kimagharibi, basi kuna namna tu ndoa zao nazo zinategemewa kuwa za kimagharibi: ndoa ya mke mmoja.
Ndio maana kwenye misiba ya baba na wajomba zetu mara kadhaa utaona kuna mke na watoto wa kwenye ndoa. Kulingana na mahusiano baina ya wajane, wakati mwingine wajane-baki hujitokeza na kuvalia kama mjane rasmi, nao wakiwa na makundi yao ya waombolezaji. Hii ni nadharia yangu binafsi.
Pili, uhaini unaweza kutokana na kwamba mke mdogo atabadilisha mustakabli wa ndoa ya mke mkubwa, hivyo mke mkubwa hulazimika kupambana na hali yake. Au uhaini ni jinsi wanaume wanavyochukilia poa wake zao?
Maudo Falli anamuambia Aisatu analazimika kumuoa binamu yake, Nabu mdogo, kwa sababu endapo atakataa mama yake, Bibi Nabu, atakufa kwa mshtuko. Maudo Falli anahakikisha Aisatu hawezi kupinga kauli yake kwa kusema anaongea hivyo kwa uzoefu wake wa kidaktari, wala sio kama mtoto wa kiume asiyeweza kumkatalia mama yake.
Labda uhaini wa mapenzi ni mchanganyiko wa mambo zaidi ya moja?
Mtindo wa uandishi
Mwandishi anatumia mtindo wa kujenga taswira kisha akakuuliza swali. Hivyo, Barua Ndefu imeandikwa kwa barua fupifupi 25, kila moja ikibeba dhumuni kuu la barua hiyo na mada ndogondogo zitokanazo na maongezi.
SOMA ZAIDI: Utendi wa Fumo Liyongo: Kama Watawala Hawataacha Kutengeneza Hila, Nasi Tuendelee Kubuni Mbinu za Ukombozi
Mada hizo ni kama vile kupiga ramli na ushirikina, usafiri wa umma na matabaka, ushiriki wa wanawake katika bunge na vyama vya siasa, ukombozi wa jamii, mipango miji na mimba shuleni. Madhumuni ya barua, mada ndogondogo na dhamira ya mwandishi vimefungamana pamoja.
Ramatulayi anaamini msingi wa ukombozi wetu ni familia. Hivyo, hakuna ukombozi kama ndoa na malezi ya watoto havijatengamaa. Safari ya ukombozi ni endelevu kwani japo kitabu kimeandika maisha ya Senegali baada ya uhuru, barani Afrika kote, hata sasa, wake kwa waume tunatawaliwa na migogoro ileile kwenye familia.
Mtafsiri, Prof. C. Maganga, alifanya kazi kubwa na nzuri. Kitabu kinasomeka bila kumpoteza msomaji kwenye msamiati au mtiririko. Labda kwenye chapa za mbeleni watafsiri wakumbuke kuandika maneno djini na Ramatulayi kama tunavyoyatumia Waswahili badala ya kuonekana kama tafsiri ya Kifaransa.
Djini ni sawa kwa Kifaransa kwa sababu silabi /ja/ inatamkwa tofauti na yetu. Ramatulayi inaweza kuandikwa Rahmatulayi kwani Wafaransa hawana matamshi ya silabi /ha/ kwenye lugha yao.
Maisha mapya, barua mpya
“Ninakutanabaisha tena, kwamba sikatai kuyaanza maisha upya tena. Pamoja na yote yaliyonisibu kudanganywa na kunyanyaswa matumaini bado ninayo. Ni katika udongo mweusi na mchafu unaosababisha kichefuchefu ndimo mmea wa kijani huota, nami najihisi kwamba tamaa mpya ya uzazi inanikereketa.
“Neno bahati linaficha kituo fulani, ama sivyo? Nitakwenda kukitafuta hicho kitu. Potelea mbali kwa upande wangu ikiwa nitawajibika tena kukuandikia barua ndefu kama hii. Ramatulayi” (94).
READ MORE: Utenzi wa Mwanakupona na Jitihada za Kumpumbaza Mume Kudumisha Ndoa
Hii ndio jinsi Ramatulayi anamaliza Barua Ndefu. Ramatulayi anaamini pindi atakapomaliza eda ataanza maisha mapya. Ana matumaini kwamba baada ya kuishi miaka mitano kwenye ndoa na mume mtoro, sasa ana matumaini ya kuendelea kuishi akiwa mjane.
Mimi nilidhani wasichana wadogo ndio huwa na ndoto za kufanikiwa kimaisha kwa kuwa na kazi nzuri na kuzitambua haki zao. Kumbe hata mwanamke mjane, anayeanza kujukuu na anayekaribia kustaafu anaweza kuwa na ndoto na matarajio kwenye maisha? Ni nini huwa ndoto za wanawake watu wazima na wazee?
Diana Kamara hupenda kujitambulisha kama binti wa Adria Kokulengya. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia dianakkamara@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.