The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Kale ya Washairi wa Pemba: Wasotumia Akili Mnemba

Ukifanikiwa kusoma kitabu hiki, nitafurahi kujua wewe ni #TeamKamange au #TeamSarahani?

subscribe to our newsletter!

Kwa tuliokulia miaka ya 1990, tunakumbuka uhasimu uliokuwepo kati ya Khadija Kopa na Nasma Khamis Kidogo. Mmoja akitoa wimbo, mwingine atafuatia. Ilifika mahali hata wote wawili waliitwa kutengeneza tangazo moja kwa vipande tofauti. 

Na tuliokuwa mashabiki wa Taarab (hata watoto wana ushabiki wa muziki) ilikuwa au unamkubali zaidi Bi. Khadija au Bi. Nasra. Basi zamani hizo za karne ya 19 na ya 20 palikuwa na ushindani usio na mfano kati ya Kamange na Sarahani huko Pemba. 

Ndio mwaka 2011 wakusanyaji wa mashairi haya, Abdurrahman S. Alawy na Abdalla El-Maawy, walitushirikisha nasi ladha hizo kwenye kitabu cha Kale ya Washairi wa Pemba: Kamange na Sarahani. Kitabu hiki kimehaririwa na Abdilatif Abdalla. Makala hii ni mwongozo wangu wa kubuni tu wa jinsi ya kuyasoma mashairi haya kwenye karne hii ya 21. 

Kwanza ni muhimu kutambua tofauti ya muktadha wa ushairi na Kiswahili kwa nyakati za Kamange na Sarahani na sasa. Zamani zile watu hawakuwa na teknolojia ya kuweza kusoma ama kuhifadhi fasihi viganjani. Hivyo, mashairi yalitunzwa kwa nyaraka, kughani na kujua visa na mikasa vilivyofanya mashairi hayo yaandikwe.

Jambo hili linanifikirisha na kunisuta, maana labda kwa majina nawajua washairi kadhaa. Hapa na pale nimeenda kwenye viunga vya washairi. Lakini hakuna haswa juhudi za pamoja kati yetu washairi wa Mshariki mwa Afrika kununua, kusoma na kuandikiana mashairi. Tusingoje Serikali zetu kutuandalia mikutano ama tuzo. 

SOMA ZAIDI: ‘Kale ya Washairi wa Pemba’ na Ufundi wa Mshairi Mahiri Kamange

Mei 2025 lilipopasuka jabali Sauti ya Kiza, tukashindwa hata kuwa na tungo na wasifu thabiti wa Amiri Sudi Andanenga. Alipofariki Kamange mwaka 1910 inajulikana kama yangekusanywa mashairi ya kumlilia yangezidi 100.

Tulipokuwa tunasoma vitabu vya Kiswahili sekondari (miaka ya 2000) ilikuwa lazima kuangalia nafasi ya mwanamke katika jamii. Uzuri wa Kale ya Washairi wa Pemba wametajwa wanawake washairi wengi wa wakati huo, na wale ambao hawakuwa washairi walikuwa wamehifadhi mashairi. 

Hivyo, ni jukumu letu sasa kutafuta nyaraka, maghani na historia zao kuziandika ili tupunguze vilio vya kwamba Waafrika hawaandiki historia zao. Kilio kikubwa zaidi kikiwa ni kwamba wanawake wa Kiafrika hawajaandika wala kuandikwa katika historia.  

Kwenye mashairi yenyewe, Kamange na Sarahani wameandika kuusifu uzuri wa mwanamke. Kwa macho ya kifeminia kuna ugumu wa kuangalia baadhi ya mashairi. Majibizano Mswanifu (mwanafunzi wa Sarahani) na Sarahani kwenye shairi la Mlangilangi na Mkadi kuwa huo Mlangilangi si mzuri kama unavyosifiwa. 

Kwa ustadi, mashairi yote mawili nayapa ithibati ya ubora. Lakini je, ni sawa kwa washairi wawili wote wakiwa wanaume kunoa ujuzi wao kwa kutumia uzuri wa mwanamke? Ama hakuna haja hata ya kufikiria kifeminia kwa sababu washairi hawa hulumbana hata kwa mambo mengine ya maadili na siasa? Naomba kujua maoni ya  wengine.  

SOMA ZAIDI: Funzo Kutoka Riwaya ya ‘Haini’ ya Adam Shafi: Mtu Yeyote, na Muda Wowote, Anaweza Kugeuzwa Mhaini

Washairi hawa wanatufundisha pia kanuni za kuwa watani wa jadi. Kwa umri, Kamange alikuwa mkubwa kwa Sarahani lakini alikubali ufundi wake na hata wakawa wao tu ndio mahasimu maarufu zaidi. Hivyo, wanaweza kutaniana wanaolingana. 

Sio zoezi dogo kujibu shairi la mtu mwingine huku ukijitahidi kubakisha vina vya kati na mwisho bila kurudia maneno. Pia, katika kila  uwanja wa sanaa vinara huwa wawili tu mpaka mwisho wa enzi zao, japo kuwa nyakati walijibizana na washairi wengine, kwa ujumla walijibizana wao kwa wao. 

Ndio maana Kamange alipofariki inasemekana Sarahani hakushabikia ushindani uliendelezwa na wapenzi wao. 

Uhuru wa mashabiki nao uliwekewa mipaka. Mswanifu alipoandika jibu la shairi la Mlangilangi na Mkadi, Sarahani alichukia sana mpaka Mswanifu aliomba radhi. Sarahani alikuwa mwalimu wa ushairi wa Mswanifu. Hivyo aliona amekosewa adabu kwa mwanafunzi wake mwenyewe kumjibiza. 

SOMA ZAIDI: Utenzi wa Mwanakupona na Jitihada za Kumpumbaza Mume Kudumisha Ndoa

La mwisho ni la kutafakari kwa pamoja, je, ni kweli watu wanaweza kubaki mahasimu wa kisanii tu wala wasivuke mpaka na kuweza kudhuriana? Ingelikuwa ni wewe umetoka lupango halafu rafiki yako anakutumia maneno haya, ungejisikiaje? 

“Ukome kwenda usiku, umekupiga mdhana,

Pemba yote yakushuku, baadhi wakunong’ona, 

Yakuswibu kila siku, taazura na laana, 

Nusura angaliona, lizamu na darizeni!”

Sarahani alimuandikia Kamange shairi la Lizamu na Darizeni baada ya kukamatwa kwa kuzurura usiku. 

Unaweza kumsoma mshairi mmoja na usimsome mwingine. Lakini uhondo kamili ni pale utakapowasoma wote wawili, na inapendeza sana pale watu wawili wanaposoma kwa kujibizana ubeti kwa ubeti maana ni kama ngonjera. 

Na ndipo utaelewa kwa nini hata kwa wakati wao watu walijikuta wakimpenda zaidi Kamange au Sarahani. Binafsi Kamange ananifurahisha, haswa akipandwa hasira. Anaandika mashairi yale ambayo tunaita vidonge. 

SOMA ZAIDI: Utendi wa Fumo Liyongo: Kama Watawala Hawataacha Kutengeneza Hila, Nasi Tuendelee Kubuni Mbinu za Ukombozi

Najikuta nikimpenda Sarahani zaidi kwa mtiririko na mawimbi katika ushairi wake. Labda namuona Kamange akiwa na jazba na Sarahani akiwa ni mtulivu. 

Ukifanikiwa kusoma kitabu hiki, nitafurahi kujua wewe ni #TeamKamange au #TeamSarahani? 

Diana Kamara hupenda kujitambulisha kama binti wa Adria Kokulengya. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia dianakkamara@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×