The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Wafanyabiashara Wadogo Sio Uchafu, Wala Uholela ni Zao la Muundo wa Uchumi Unaohitaji Ubunifu Kutatua

Uchumi hautengenezi ajira za kutosha, wengi inabidi kukumbilia katika ajira zisizo rasmi katikati ya miji

subscribe to our newsletter!

Kwa wiki mbili sasa Dar es Salaam inaendelea na hamisha hamisha ya wafanyabiashara wadogo katika maeneo yasiyokuwa rasmi. Jambo hili limepokelewa kama maumivu kwa familia nyingi zinazotegemea biashara hizo, hata hivyo utetezi wa serikali na wadau wengine ni kuboresha usafi. Na tukiwa wa kweli kuna wengi wanaofurahia wakiamini kuwa ni tatizo lililokuwa limekithiri.

Binafsi nadhani, kuna uwezekano mkubwa wa kutengeneza tatizo kubwa zaidi, kama umakini usipofanyika; hakuna mtu anayependa kukaa kwenye mabanda pembeni ya barabara, hakuna mtu anayependa kupigwa na jua la Dar es Salaam. Wengi wanafanya hivi kwa sababu hakuna namna nyingine ni lazima kutafuta kipato. Na wanajikuta katika hali hii kwa sababu ya muundo wetu wa kiuchumi.

Tukiangalia hali ya uchumi wetu kwa sasa, ni uchumi unaokuwa lakini usiozalisha ajira za kutosha. Mfano angalia sekta sita zilizokuwa zaidi ni sekta ya Fedha na Bima, Umeme, Madini, Habari na Mawasiliano, Sanaa na Burudani na usafirishaji. Hizi sekta zinaajiri asilimia 7 tu ya Watanzania wote, ukiacha sekta ya usafirishaji iliyoajiri zaidi ya Watanzania Milioni 1.2, sekta tano zilizobaki, zinazoshikilia ukuaji wa uchumi zimeajiri asilimia 2.3 tu ya Watanzania, ambao ni takribani Watanzania 650,000, kwa wale wenye sifa za kufanya kazi. Kwa hiyo mbaya zaidi sehemu kubwa ya Watanzania yaani asilimia 93 wapo katika sekta ambazo ukuaji wake ni chini hata ya ukuaji wa uchumi wa nchi. 

Nataka nikupe mfano wa namna muundo wa kiuchumi unavyosababisha biashara ndogo ndogo kukaa barabarani. Mfano tuchukulie Msasani, eneo ambalo tayari serikali imesafisha, ingawa kina mama waliovunjiwa tayari wamerudi na ndoo zao kila asubuhi. Pale Msasani, kuna eneo linaitwa Bonde la Mpunga, ni maeneo ambayo nyumba zake ni zile nyumba zinalingana kimo na mtu, ni nyumba ambazo zina giza, zimezongana, na nyingi hazijamalizika. Bonde la Mpunga limefichwa na maghorofa na fremu zilizotanda pale Msasani, kama sio mwenyeji, huwezi kudhania kuna sehemu kama Bonde la Mpunga, sababu unakuwa unapita kwenye lami nadhifu, huku kukiwa na maghrofa, pande zote mbili. 

Kwa hiyo watu wa Bonde la Mpunga wakitoka kidogo wanakutana na watu wachache wakifanya kwenye zile sekta murua za uchumi. Vijana, wanawake kwa wazee nadhifu, wengine na magari yao; sasa utafanyaje? Lazima wazifuate na wao hizo hela. Hawawezi kumudu kupangisha fremu, kinachotokea inabidi wakae kwenye eneo la akiba ya barabara, wauze mihogo, chapati, chai; kwa hawa wachache wenye mzunguko; lakini kuna watu wengine pia wanajaribu kuwafuata hawa wachache wenye mzunguko; bodaboda, mafundi na wengine. Kwa hiyo unakuta sasa kuna kina mama walau 50 na vijana wanaotoka Bonde la Mpunga na kuja kuuza maeneo ya hifadhi ya barabara, ambapo sasa kumesafishwa.

Kuna tatizo lingine ambalo miji kama Dar es Salaam inakumbana nalo, wakati hali ya ukosefu wa ajira kwa nchi imeshuka kutoka asilimia 6.2 mpaka asilimia 5.9 kati ya mwaka 2024 na 2025, hali ya mijini ni mbaya, hali ya ukosefu wa ajira hasa kwa vijana kati ya miaka 15 mpaka 24 imeongezeka mara mbili zaidi yaani  kutoka asilimia 6 mpaka asilimia 12.7, kati ya mwaka 2024 na 2025. Dar es Salaam hali ndio mbaya zaidi hasa kwa kundi hili la vijana, ukosefu wa ajira umepanda kutoka asilimia 13.9 mpaka asilimia 19 ndani ya mwaka mmoja na kwa ujumla hali ya ukosefu wa ajira imeongezeka Dar es Salaam kutoka asilimia 7.5 mpaka asilimia 9.3, hata hivyo hali ni mbaya zaidi kwa wanawake. Jambo jingine kubwa zaidi ni kuwa hata kwa vijana wanaohitimu vyuo vikuu hali ya ukosefu wa ajira inakuwa mbaya ambapo imeongezeka karibu mara mbili kati ya mwaka 2024 na 2025, ukosefu wa ajira kwa vijana wahitimu kati ya miaka 15 mpaka 24 imeongezeka kutoka asilimia 12.8 mpaka asilimia 21.9.

Sasa katika hali hii ya ukosefu wa ajira watu wanaenda wapi, wenye elimu na wasio na elimu? Wanaingia katika sekta isiyo rasmi, na kwa mijini ni hasa biashara za chakula ambapo asilimia 83 ni wanawake, lakini pia  wanaingia kwenye biashara za kuuza biadhaa, na labda umakenika wa kutengeneza pikipiki na magari kazi hizi tatu kwa Tanzania ndio zinazoongoza kwa kutoa ajira takribani asilimia 15 ya watu baada ya kilimo ambacho kimeajiri asilimia 54.4 ya Watanzania, na kiukweli ni kazi za mjini. Na Takwimu zinaonesha kati ya mwaka 2024 na 2025, ukiangalia ujumla ongezeko la watu kuingia kazini nilikuwa kwenye sekta isiyo rasmi.

Kwa hiyo hapa ndio unasikia vijana wa Chuo kikuu wanasema wanakuwa mawinga Kariakoo, ndio tunaona ongezeko la vijana, kinamama na kina baba maeneo mbalimbali yasiyorasmi wakijaribu na wao kuvuna uchumi wa miji, unaopita katika mikono michache.

Nitakupa mfano wa pili juu ya hii ondoa ondoa inayoendelea. Kwa sababu bado kwa Dar es Salaam hatujaamua kuangalia mzizi wa tatizo, wafanyabiashara wadogo wadogo wamekuwa wakihamishwa kutoka eneo moja kwenda kwingine, lengo kubwa mara nyingi ni kuwasukumiza pembezoni, ambapo ndio huko hata masoko ambayo hayatumiki ya mamilioni hujengwa na kutelekezwa.

Safisha safisha ya jiji ya miaka kadhaa ilifanya wafanyabiashara wakaenda pembezoni, wengine Mbagala, Tandika, Tegeta, Buza; hata hivyo pembezoni nako kumechangamka, ndipo hapo tunaona sintofahamu kama inayotokea Tandika, wafanyabiashara wamehama wamehama na sasa hawana namna inabidi tu wajipambanie. Na kwa watendaji wa serikali, wanashindwa kuelewa ukaidi wa watu hawa ambao muundo wa uchumi umewakataa, wanatafuta hela za kula na kuishi na watoto wao; kama watendaji wa serikali wakitumia nguvu kupita kiasi, kuna janga linamea, kwa sababu muundo wa uchumi umewatema, kwa sasa wanajipambania.

Sasa nini kifanyike?

Hoja ya Dar es Salaam kuwa safi yenye mpangilio mzuri ni ya muhimu, na hoja ya watu wa Dar es Salaam kupata mkate wao wa kila siku ni ya muhimu zaidi. Usafi na watu kupata mkate ni mambo yanayowezekana kufanyika kwa pamoja.

Jambo la kwanza la kufanya ni lazima watendaji wa serikali, viongozi wa serikali kuamini kwamba miji, na fursa zinazopatikana katika miji, lazima zifurahiwe na wenye nacho na wasionacho, miji si ya matajiri pekee. Serikali inajukumu la kuleta msawazo, kwa wenye nacho na wasionacho kuweza kufaidi matunda ya miji. Kwa hiyo, Halmashauri ya Kindondoni ilivyojenga jengo zuri pale Mwenge, na ikawaondoa wafanyabiashara wadogo, sehemu ya jengo hilo lingetakiwa liwe na nafasi ya wafanyabaishara wadogo, kwa hiyo kuanzia ramani ya ujenzi, muonekano wa jengo lazima uakisi hawa wafanyabiashara wadogo. Kwa hiyo badala ya wao kukaa barabarani, wangekuwa na sehemu ambayo imekaa vyema, lakini ambayo imeendelea.

Pili, sababu kubwa ya watu kutumia maeneo ya hifadhi za barabara ni kwa sababu wanafuata fedha zinazopita katika mikono ya wachache, yaani zile sekta kadhaa za uchumi nilizokuambia mwanzo zinafanya vizuri. Maeneo ya haifadhi yenye nafasi, mfano Msasani walipoondolewa na maeneo mengine, wafanyabiashara warasimishwe, na walipe ushuru kwa halmashauri. Kwa nini ni rahisi kuruhusu vituo vya mafuta, maduka maalum kwenye hizi hifadhi, na tunaona haya kutoa ahueni kwa watu milioni 8 wanaotanga tanga kutafuta namna ya kuweka mkate mezani. Binafsi nimeshuhudia katika nchi zilizoendelea wakiweka nafasi kwa biashara ndogo, nenda New York, utakuta kuna nafasi za wafanyabiashara wadogo, nenda Hague uholanzi, kwenye fukwe zao kuna maduka ila kuna nafasi za wafanyabaishara wadogo, kwingine nimeona hata mitaa ikifungwa kutoa hizi nafasi, sasa hii ni katika nchi ambazo ajira zipo, Tanzania asiliia 95 ya ajira  watu wameajiriwa katika sekta isiyo rasmi, kwa hiyo kuleta utatuzi sio ushamba ni kutatua tatizo la kimsingi. Kwa hiyo hamashauri ziingie makubaliano rasmi na TANROAD juu ya hili, na wafanyabiashara watambulika kama ambavyo wanatambulika katika biashara rasmi.

Tatu, moja ya changamoto ni kuwa uchafu  unakuja kwa sababu ya uholela wa vibanda vinavyojengwa, nadhani mashirika kama Bicco na SIDO kwa kushirikiana na halmashauri, waje na aina ya vibanda vinavyotembea, ambavyo ni nadhifu vya gharama nafuu na vinaweza kusogea.  Hii itawezesha kujenga mfumo unaimarisha usafi, na kuhimiza unadhifu. Vibanda hivyo ndio viwe vinatumika katika maeneo yasiyo ya kudumu, tukumbuke hata sasa wafanyabiashara hao hujenga hivyo vibanda.

Mitandao imeweza kupunguza watu wengi ambao kwa namna moja au nyingine wangeingia na kuwa wamachinga. Niliziona kanuni ambazo zinataka wafanyabiashara mtandaoni kuweka TIN No kwenye profile zao, nadhani kwa sasa lengo lisiwe kukusanya kodi kwa wafanyabiashara hao, bali kuwatengenezea mazingira wezeshi, kwa sababu muundo wa uchumi umewasukuma huko. Kwa hiyo TRA na halmashauri wanaweza kuungana, kutoa utambulisho, ambao kazi kubwa utafanya hawa wafanyabiashara waaminike, kuaminika ndio tatizo kubwa. Vigezo katika halmashauri kuwa mtu lazima awe na eneo maalum la biashara, vinaweza kubadilishwa, badala yake halmashauri na TRA wakahusika kuthibitisha kama page fulani kwa mfano ya instagram, ni ya mtu kweli, na ikatoa namba ambayo mtu anaweza kuthibitisha, hii itakuwa moja ya mchango katika kurahisisha kuaminika kwa biashara za mtandaoni, na kuondoa kasumba ya watu kutafuta lazima maeneo ya biashara.

Kukuza uchumi ni jambo kubwa litakalopunguza changamoto. Lakini kwenye hili mengi yanaelezwa, mimi ningependa kuangalia maeneo mawili, moja miradi mikubwa kama EACOP, mawazo ni kuwa katika fursa kama hizi Watanzania wataweza kujenga mitaji, na hata kutoka na biashara imara. Hata hivyo, kampuni za kigeni zilizopewa mikataba hawatimizi sehemu kubwa ya masharti, na hutumia bado raia wa kigeni kwenye maeneo mengi kama siyo yote, hivyo chachu inakuwa ndogo. Kwa Sekta kama ujenzi, ambayo nayo inaajiri watu wengi, kuna umuhimu wa serikali ambayo ndio moja ya mtoa fursa nyingi kupitia miradi ya ujenzi, kubadilisha baadhi ya mambo yanayofanya kampuni za ndani zisikuwe, hasa kwenye suala la kutokutoa malipo kwa wakati. Kwa sasa sehemu kubwa ya sekta ya ujenzi wa miradi mkiubwa ya serikali inaenda kwa makampuni ya nje, makampuni madogo ya ndani yameshindwa kufurukuta, kwa sababu wengi wanamadeni mengi serikalini yasiyolipwa kwa wakati. Kuna haja ya kuizibua sekta ya ujenzi kwa kulipa malipo kwa mkupuo.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×