The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Wadau Wataka Ufumbuzi wa Mkwamo wa Marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya 1971

Wasema utashi wa kisiasa unakwamisha mchakato huo Jackline Kuwanda

subscribe to our newsletter!

Dodoma – Wadau wa sheria na sera wameitaka Serikali kuharakisha mchakato wa kurekebisha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, wakisema kuchelewa kufanya hivyo kunaendelea kuacha mianya inayowezesha ndoa za utotoni nchini.

Wakizungumza katika mjadala jijini Dodoma Septemba 19, 2026 kuhusu mapungufu ya kisheria na kitaasisi yanayozunguka sheria hiyo, wadau wamesema miongoni mwa vifungu vinavyohitaji marekebisho ni Kifungu cha 13, kinachoruhusu mtoto wa kike mwenye miaka 14 au 15 kuolewa kwa ruhusa ya wazazi au mahakama.

Rogasian Massye, Meneja Miradi wa Jukwaa la Haki za Mtoto Tanzania (TCRF), amesema kuna uhitaji wa kuweka umri wa chini wa ndoa kuwa miaka 18, akisema jamii na wadau wengi tayari wamekubaliana na msimamo huo.

“Sisi tunatamani kuona kiongozi wa nchi, bahati nzuri Rais ni mwanamke, tulitegemea tuone mabadiliko ya haraka kwa sababu yeye ni mwanamke. Lakini bado tunaona kuna kigugumizi,” amesema Massye.

Amesema hoja kwamba dini na mila ni kikwazo cha marekebisho hayo haiwezi tena kutumika, kwa kuwa viongozi wengi wa dini wamekuwa wakishiriki katika majukwaa yanayounga mkono mabadiliko.

“Uongozi wa juu wa nchi umebaki kutoa matamko, na lazima tufike mahali tuwe na matamko ya kijasiri. Tunatamani kuona Mheshimiwa Rais kabla hajatoka madarakani anatuletea ufumbuzi wa hili suala la umri wa mtoto wa kike kuolewa,” amesema.

Mjadala huo unafanyika miaka 10 baada ya Rebeca Gyumi, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Msichana Initiative, kufungua kesi mwaka 2016 kupinga vifungu vya 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa vilivyoruhusu ndoa za watoto walio chini ya miaka 18.

Mahakama iliamuru vifungu hivyo virekebishwe, lakini utekelezaji wa uamuzi huo umechukua muda mrefu, huku wadau wakiendelea kushinikiza Serikali kukamilisha mchakato.

Irene Nambuo, Mratibu wa Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni nchini Tanzania, amesema juhudi za uchechemuzi zinaendelea licha ya mkwamo huo.

SOMA ZAIDI: Kughushi Vyeti vya Ndoa Kunavyokwamisha Jitihada za Kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania

“Tunaendelea na uchechemuzi hizi sheria zilizokuwepo ziwe na uwiano. Kwa sababu muda mwingine katika utekelezaji kuna mkanganyiko na maswali yanajirudia,” amesema Nambuo katika mahojiano na The Chanzo.

Mwezi Mei 2024, Serikali ilisema imekamilisha uandaaji wa muswada wa marekebisho ya Sheria ya Ndoa na kwamba ilikuwa inaandaa taratibu za kuufikisha Bungeni. Serikali ilisema maoni kuhusu mabadiliko hayo yalikusanywa kutoka kwa wazee wa kimila, viongozi wa dini, wanataaluma, wanafunzi, watu mashuhuri na wabunge.

Hata hivyo, zaidi ya miaka miwili baadaye, wadau bado wanataka hatua zaidi zichukuliwe.

Tike Mwambipile, Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TAWLA), amesema mjadala kuhusu marekebisho ya sheria hiyo umefanyika mara kwa mara, lakini bado kuna haja ya kuelewa sababu ya kuchelewa kwake.

“Shida iko wapi? Tumekuwa tukijiuliza mara kwa mara. Labda hatujui shida iko wapi, nini tufanye kwa wakati huu,” amesema.

Amesema sheria hiyo ina vipengele vingi vinavyohitaji kufanyiwa marekebisho kwa sababu ndoa za utotoni zinaendelea kuwaathiri watoto wa kike.

“Kwa maisha tu ya kawaida mtoto wa miaka 14, 15 hawezi kuhimili mikiki ya ndoa. Sisi wa umri wa miaka 40, 50, 60 tunashindwa kukabiliana na hii mikiki, je huyu mtoto inakuwaje?” amehoji.

Josephine Sankey, Mwenyekiti wa Compassionate Empowering Foundation (CEF), amependekeza sheria zote zipitiwe kwa kina kabla ya kupitishwa ili kupunguza uwezekano wa sheria moja kukinzana na nyingine.

Kwa upande wake, Mwelinde Katto, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, amesema kuchelewa kwa marekebisho kunatoa mwanya kwa baadhi ya watu kutumia sheria zilizopo kuendeleza ndoa za utotoni.

Nelson Mutalemwa, Wakili wa Serikali kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria, amesema Serikali inaendelea na mchakato wa maboresho kwa kushirikiana na Ofisi ya TAMISEMI, huku ikiangalia maeneo yanayohitaji marekebisho.

Kauli hiyo iliungwa mkono na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera, Septemba 26, 2026, aliposema Serikali inaendelea na mashauriano ya kurekebisha baadhi ya vifungu vya Sheria ya Ndoa.

“Serikali itaendelea kushughulikia suala la ndoa za utotoni ambalo limekuwa likiwanyima baadhi ya watoto wa Kitanzania fursa ya kuendelea na elimu,” alisema.

Kwa wadau, hatua ya kukamilisha marekebisho hayo ni muhimu katika kuimarisha ulinzi wa watoto wa kike dhidi ya ndoa za utotoni, ambazo zinaweza kukatiza masomo na kuathiri fursa zao za kiafya, kijamii na kiuchumi.

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jaquelinevictor88@gmail.com 

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×