Dar es salaam.Serikali imeyafuta mashirika na taasisi za umma nne, na kuunganisha mashirika na taasisi 16. Uamuzi huu umekuja kufuatia maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan juu ya kuboresha ufanisi wa taasisi na mashirika ya umma.
Akipokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa serikali mnamo Machi 29, 2023, Rais Samia aligusia juu ya kuyafuta mashirika yasiyo na tija.
“Kuna haja ya kufanya tathimini kama baadhi ya mashirika ya umma yanafaa kuendelea kuwa nayo, yale yanayofaa yaendelee na yasiyo na tija yafutwe,” alieleza Rais Samia.
Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa, Disemba 15, 2023, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo inaeleza kuwa Serikali imeunda timu ya wataalamu kufanya tathmini ya mashirika ya umma.
Taarifa hiyo inaonesha mabadiliko haya yaliyotangazwa yanatokana na mapendekezo ya awamu ya kwanza ya timu hiyo ya wataalamu.
Mashirika na taasisi za umma zilizofutwa ni pamoja na Shirika la Uzalishaji wa Jeshi la Polisi (TPFCS), Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC).
Mashirika mengine ni Shirika la Elimu Kibaha (KEC) lililovunjwa na kuwa Shule ya Sekondari Kibaha na Bodi ya Pareto ambayo imefutwa na shughuli zake kuhamishiwa katika Mamlaka ya Usimamizi wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko.
Yaunganishwa
Kwa upande wa mashirika na taasisi zilizounganishwa na kuwa taasisi moja ni pamoja na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Wakala wa Ufilisi na Udhamini (RITA) na Kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA).
Nyingine ni Benki ya Kilimo ya Maendeleo (TADB) na Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) zinaunganishwa na kuwa taasisi moja itakayohusika na mikopo na ugharamiaji wa maendeleo ya kilimo nchini.
Bodi ya Chai inaunganishwa na Wakala wa Maendeleo ya Wakulima wa Chai Tanzania.
Bodi ya Nyama inaunganishwa na Bodi ya Maziwa kuunda taasisi moja ya kuendeleza na kusimamia mazao ya mifugo yakiwemo nyama na maziwa.
Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CARMATREC), Taasisi ya Uandishi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO) na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) nazo zinaunganishwa na kuwa taasisi moja.
Taasisi ya Utafiti wa Chai Tanzania (TRIT), Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku Tanzania (TORITA) na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TACRI) zinaunganishwa na kuwa sehemu ya muundo wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).
Watumishi watolewa hofu
Serikali imewatoa hofu watumishi kutoka katika mashirika yaliyoathirika na kueleza kuwa watapangiwa kazi zingine katika utumishi wa umma na maslahi yao yatazingatiwa ipasavyo.
Akizungumzia juu ya mabadiliko yanayokuja katika kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi za umma mnamo Agosti 19, 2023, Rais Samia alisisitiza pia kuwa hakuna nguvu kazi au ajira itakayopotea.
“Takwimu zinatuonesha kwamba asilimia 17 ya ajira ndani ya nchi inatolewa na shirika na taasisi na wakala hizi,” alielezea Rais Samia.
“Hakuna nguvu kazi au ajira itakayopotea, wote ambao wako kwenye mashirika aidha watamezwa kwingine au kutakuja mashirika mengine ambayo yana maana zaidi,” alifafanua zaidi Rais Samia.
Taarifa ya Serikali inaeleza kuwa marekebisho ya kisheria yatafanyika kwa mashirika yaliyoanzishwa kisheria ili kuruhusu mabadiliko haya yaliyotangazwa
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com
One Response
Tatizo la mashirika ya umma litasalia kwenye ownership.
Ufumbuzi wa Tatizo ni kuwapa ownership kwa kufanya yawe Plc public listed company.