Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali Venance Mabeyo amesema kuwa mijadala iliyoibuka juu ya namna ya makabidhiano ya madaraka baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, inawezekana ilitokana na baadhi ya watu kusahau Katiba inasema nini pale Rais anapofariki au kushindwa kuendelea na majukumu yake.
Jenerali Mabeyo ambaye aliyekuwa mkuu wa majeshi wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuanzia Februari 06, 2017 na kustaafu mnamo Juni 30, 2022, ameyasema hayo wakati wa mahojiano yake na Daily News Digital, ikiwa inatimia miaka 3 tangu kifo cha rais wa awamu ya tano, Hayati John Pombe Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021.
“Kwa mujibu wa Katiba, bahati nzuri imeeleza vizuri endapo Rais atafariki au endapo atashindwa kutekeleza majukumu yake kama Rais, atakayeshika madaraka ni Makamu wa Rais,”anaeleza Mabeyo. “Sasa inawezekana watu Katiba walikuwa wameisahau kidogo kukatokea maongezi tofauti.”
SOMA ZAIDI: Mabeyo: Jeshi Lilisimama Kidete Kuilinda Katiba Baada ya Kifo cha Rais Magufuli
Mabeyo anasema anamshukuru Mungu kwa kuwa makabidhiano ya madaraka katika kipindi hiko kigumu ambacho nchi haikuwahi kukipitia yalikwenda vizuri kwa kuwa ilibidi kuhakikisha Katiba inazingatiwa.
“Lakini tukasema tuna taratibu nadhani tukizifuata hazina shida. Tuzizingatie zile ili makabidhiano ya madaraka yaende vizuri,” ameeleza Mabeyo.
Kifo cha Magufuli
Mabeyo anaeleza kuwa madaktari walivyoona hali ya Rais Magufuli inabadilika waliwaita wakuu wa vyombo vya ulinzi yaani Mabeyo, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa Tanzania, Diwani Athumani Msuya na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro.
“Ilipofika jioni saa kumi na mbili na nusu hivi au saa moja kasoro akakata roho, wakuu wa vyombo tuko pale mimi IGP na DGIS(Mkurugenzi wa Usalama),” anaeleza Mabeyo huku akisema kuwa kulikua na kigugumizi nani wa kumtaarifu wa kwanza, Rais Samia wakati huo alikua Tanga, Waziri Mkuu Kasim Majaliwa alikua Dodoma na Katibu Mkuu Kongozi, Bashiru Ally alikua Dodoma.
“Kwa hiyo tuliokuwa Dar es Salaam tulikuwa watatu tu, tukasema kwa kuwa Rais yuko Tanga hebu tumuambie kwanza Waziri Mkuu na Katibu Mkuu Kiongozi waje bila kueleza sababu, bahati nzuri wakaja mapema, sasa mimi kama mwenyekiti wa wakuu wa vyombo ilibidi nieleze Mheshimiwa Rais ameshatutoka.”
“Kwa hiyo tukaanza kushauriana tunafanyaje? Nani anatakiwa atangaze hizi habari kwenye vyombo vya habari wananchi wajue? Ndio tukaanza kutafuta Katiba sasa inasema nini?”
Mabeyo anasema kwa kuwa mtu pekee anayetakiwa kutangaza kwenye vyombo vya habari ni Makamu wa Rais ambaye alikuwa Tanga, ikabidi mawasiliano mengine yafanyike akiwa Tanga, pamoja na kutuma ujumbe kwa familia ya Magufuli.
Suala la kumuapisha Rais kuchukua siku mbili
Mabeyo anakiri kwamba kikawaida ilitakiwa ndani ya saa 24 rais mpya awe ametangazwa na kuapishwa, lakini haikutokea hivyo wakati wa kifo cha Hayati Magufuli kutokana na mjadala ulioibuka kupelekea Rais Samia Suluhu Hassan kuapishwa baada ya siku mbili yaani Machi 19, 2021.
“Kulikuwa na mawazo mawili, aapishwe Rais baada ya kuzika au aapishwe Rais kabla ya kuzika.” amesema Mbeyo. “Lakini logic ikaja kwamba kuna marais wengine watatoka nje ya nchi kuja kumzika mwenzao watapokelewa na makamu wa rais au rais?”
Mabeyo aliendelea kusema kuwa uliibuka mjadala mwingine tena wa namna gani Rais mpya atakavyo apishwa kwa madai kuwa kusiwe na paredi kwa sababu nchi ipo kwenye msiba, kitu ambacho mkuu huyo wa majeshi mstaafu alisema gwaride lazima liwepo na bendera ya Amiri Jeshi Mkuu lazima ipande kwa gwaride.
SOMA ZAIDI: Urais wa Samia Suluhu Unamaanisha Nini kwa Ujenzi wa Tanzania Mpya?
“Nikasema huyu ni Amir Jeshi Mkuu anayeapishwa, asipoapishwa kwa taratibu hizo za kitaifa Jeshi halitamtambua,” anafafanua zaidi Mabeyo.
Sambamba na hilo, ametolea ufafanuzi kwa nini siku ya uapisho wa Rais Samia alisisitiza kuwa atambulike kama ni Amiri Jeshi Mkuu na siyo ‘Amirat Jeshi Mkuu’ kama baadhi ya watu na vyombo vya habari viliyoanza kuibua mjadala.
“Jeshini tuna afisa na askari. Hakuna mwanaume na mwanamke. Kwa hiyo hata amir Jeshi neno lile linabaki kuwa Amir Jeshi ni Commander in Chief, hiyo Amirat ni kidini,” anaendelea kueleza, “tukawauliza na BAKITA wakaeleza vizuri.”
Akizungumzia kuhusu uongozi wa Rais Samia, ambaye ndiye aliyechukua kijiti cha uongozi baada ya kifo cha hayati Magufuli, Mabeyo ameeleza kuwa uongozi wa Rais Samia umekuwa ni wa kushirikisha watu mbalimbali kitu ambacho amesema kuwa ni kizuri katika kufanikisha mambo kwa kitaifa.
4 responses
Nimejifunza kitu kizuri
Ahsante sana CDF msitaafu, umeelezea kwa ufasaha na upendo mkubwa, Mungu akupe afya njema.
Mmefanya jambo la msingi kumuhoji Mkuu wa Majeshi na kafunguka vizuri maana mengi sana yalizungumzwa wakati ule. Kwanza niwapongeze sana mmekua mkiandika habari za uhakia, hiyo haitoshi waandishi na wahariri wenu mpo makini mno nakupelekea makosa madogo madogo ya kiuandishi hayapo na mtu kusoma huku ukipata raha ya kuendelea kusoma habari husika.
Deo Luhamba
Ni kweli yalisemwa mengi mitaani kabla na baada ya kifo cha JPM. Taarifa hii imenisaidia kujua kwamba SIYO kila lisemwalo au kuandikwa ni kweli
Asante Jenerali Mstaafu Mabeyo.