Mabeyo: Jeshi Lilisimama Kidete Kuilinda Katiba Baada ya Kifo cha Rais Magufuli

Mkuu wa Majeshi anataja kipindi hicho kama moja ya vipindi vigumu sana wakati wa uongozi wake jeshini.
Lukelo Francis23 June 20223 min

Dar es Salaam. Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) anayemaliza muda wake Jenerali Venance Salvatory Mabeyo ametaja kifo cha Rais wa awamu ya tano John Magufuli, na matukio yaliyofuata baada ya tukio hilo, kama moja kati ya changamoto kubwa alizokabiliana nazo kwani Jeshi lilipaswa kusimama kidete kuilinda Katiba ya nchi.

Mabeyo, aliyeanza kutumikia wadhifa huo mnamo Februari 6, 2017, baada ya kuteuliwa na Rais Magufuli, akichukua nafasi ya Jenerali mstaafu Davis Mwamunyange, alieleza hayo wakati wa mahojiano maalum na kipindi cha Dakika 45 kilichorushwa na kituo cha televisheni cha ITV hapo Juni 22, 2022.

“Nadhani [Watanzania] ni mashuhuda [kwamba] kwa mara ya kwanza, [Tanzania] tukampoteza Rais aliyekuwa madarakani,” Mabeyo, 65, alisema wakati wa mahojiano hayo.

“[Hiki] kilikuwa ni kipindi kigumu kidogo. Lakini tulisimama kidete, kwa utulivu mzuri, kama jeshi, tukitimiza wajibu wetu kwa mujibu wa Katiba, kuilinda nchi yetu [na] kuilinda Katiba.

“Na hilo likapita salama. Tukampokea Rais mpya, ambaye tunaendelea naye mama Samia Suluhu Hassan, na naamini kwamba tunaendelea vizuri. Nchi iko salama mpaka sasa. Wananchi wako watulivu, wanaendelea kufuata miongozo kama inavyotolewa na Serikali,” aliongeza Mabeyo.

Rais Magufuli alifariki mnamo Machi 17, 2021, kutokana na matatizo ya moyo, tukio lilioandika historia mpya kwa taifa la Tanzania ya Rais kufariki akiwa madarakani. Habari za kifo cha Rais huyo aliyekonga nyoyo za watu wengi na kuwakera wengine zilitangazwa usiku wa Machi 18, 2021, na aliyekuwa Makamu wake wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Samia aliapishwa kuwa Rais wa awamu ya sita mnamo Machi 19, 2021, huku Jeshi la Ulinzi (JWTZ), ambalo kazi yake kuu ni kulinda Katiba na mipaka ya nchi, likipongezwa kwa kiasi kikubwa kusimamia uhamisho huo wa madaraka kwa utulivu mkubwa.

Matishio ya ugaidi

Mabeyo, ambaye aliagwa rasmi bungeni hapo Juni 14, 2022, huku Spika wa Bunge Tulia Ackson akimshukuru kwa “utumishi wako uliotukuka” kwa Tanzania, alitaja matishio ya ugaidi ambayo Tanzania imekuwa ikikabiliana nayo kwa miaka ya hivi karibuni kama moja ya “milima” aliyopaswa kuipanda wakati wa uongozi wake.

Matukio haya ni pamoja na yale ya Amboni, mkoani Tanga; Kibiti, mkoa wa Pwani; ugaidi huko mkoani Mwanza; na huko Mtwara kwenye mpaka na Msumbiji ambako magaidi wamekuwa wakifanya maisha ya jamii za karibu na mpaka huo kuwa magumu kwa kutokuwa na uhakika wa usalama wao.

“Kwa kweli, kipindi hicho kilikuwa kigumu sana lakini tunashukuru ushirikiano na wananchi, ushirikiano na vyombo vingine vya usalama, tumeweza kuhimili,” alibainisha Mabeyo kwenye mahojiano hayo.

“Lakini ni bahati mbaya kwamba majirani zetu [Msumbuji] wanakabiliwa sasa na tishio hilo [la ugaidi] kwa kiasi kikubwa. Na sisi kama sehemu ya ukanda wetu huu wa [Nchi za Kusini mwa Afrika] tumekubaliana kwamba tuwasaidie wenzetu,” aliongeza Mabeyo.

Migogoro ya ardhi

Kwenye mahojiano hayo pia, Mabeyo alikiri uwepo wa migogoro ya ardhi baina ya jeshi na wananchi, akisema mingi ya migogoro hiyo inatokana na Serikali kushindwa kulipa fidia kwa wakati lakini pia uvamizi wa maeneo ya jeshi na wananchi.

Migogoro ya ardhi kati ya jeshi na wananchi ni tatizo kubwa ambalo mara kadhaa Serikali imeahidi kutafuta namna bora za kukabiliana nalo.

Hivi karibuni, kwa mfano, Waziri wa Ulinzi Dk Stergomena Tax alikiambia kituo cha habari cha Dar24 kwamba Serikali iliandaa mpango wa miaka mitatu – 2020/2021 mpaka 2022/2023 –kwa ajili ya kutatua migogoro hiyo.

“Kwa sasa wataalam wapo sehemu mbalimbali za nchi ambazo zimeainishwa na kuna baadhi migogogoro imeshatatuliwa na kuna sehemu bado inaendelea kutafutiwa ufumbuzi,” Dk Tax amenukuliwa akisema.

Kwenye mahojiano yake na ITV, Mabeyo alisema jeshi linafanya kila linalowezekana kuhakiksha migogoro iliyopo sasa inatatuliwa na kwamba hakuna migogoro mipya inazalishwa.

Alipoulizwa anatamani kuona jeshi la aina gani muda huu ambao anaenda kustaafu, Mabeyo alisema kwamba anatamani Jeshi la Tanzania liwe la kisasa zaidi, huku likijitegemea na kutoa mchango zaidi katika ujenzi wa uchumi wa nchi.

“Kwa nini wenzetu wanatengeneza zana wanatuletea kutuuzia sisi?” anauliza Mabeyo. “Kwa nini na sisi tusitengeneze zana za kututosheleza sisi wenyewe? [Wenzetu] wana hoteli, wana nyumba nzuri ambazo watu wanakuja wanakaa wanaongeza uchumi wa nchi. Na sisi jeshi letu liwe hivyo.”

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.

Lukelo Francis

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved