The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mfumo wa Haki Jinai Tanzania Unawaangusha Walemavu wa Akili

Namna mifumo ya kimahakama ilivyomfanyia Limi Limbu, mlemavu wa akili anayesota gerezani kwa miaka 11 sasa, ni kielelezo tosha cha namna mifumo yetu ya upatikanaji haki isivyojali utu wa binadamu na upatikanaji wa haki kwa ujumla.

subscribe to our newsletter!

Katika kesi ya Jinai Na. 130 ya mwaka 2012, Mahakama Kuu mkoani Tabora ilisikiliza rufaa kutoka kwa Limi Limbu, mwanamke mwenye ulemavu wa akili ambaye alifikishwa mahakamani kwa kosa la mauaji.

Taarifa iliyowasilishwa mbele ya Mahakama ilidai kwamba mnamo Agosti 25, 2011, katika kijiji cha Mwamabu, wilaya ya Bariadi, mkoani Shinyanga, mlalamikaji alimuua Tabu, ambaye alikuwa na umri wa mwaka mmoja na miezi minane kwa wakati huo, na kupelekea kukamatwa kwake hapo Agosti 26, 2011.

Polisi walidai kuchukua maelezo ya mtuhumiwa siku hiyo ya Agosti 26, lakini Limi hakusaini chochote. Alipofikishwa mahakamani, Limi alisema hafahamu chochote kilichopo kwenye maelezo yaliyochukuliwa na polisi. Uwezo mdogo wa akili wa Limi ulijitokeza wakati wa kesi, huku akiwa hakumbuki chochote, hata taarifa kuhusu yeye binafsi.

Kwa mfano, Limi hakujua jinsi ya kutamka jina lake; hakuwa anajua umri wake; wala hakuweza kukumbuka jina la bibi yake au kijiji ambacho aliishi na hata hakuweza kukumbuka umri wa watoto wake. 

Limi pia alikuwa hajui jina la ukoo la mume wake; jina la mtu aliyezaa naye mtoto wake wa kwanza; au jina la mtu aliyemuua mtoto wake. Licha ya haya yote, Mahakama Kuu ilimtia hatiani Limi kwa mauaji na kumuhukumu kifo mnamo Agosti 28, 2015, miaka minne baada ya kukamatwa kwake.

Muhanga wa ukatili 

Limi, mwenye ulemavu mkubwa wa akili na muathirika wa ukatili wa kijinsia na ukatili wa wa majumbani uliokithiri, alikulia kwenye shamba la wazazi wake, akifanya kazi kwenye shamba hilo huko mkoani Shinyanga.

SOMA ZAIDI: Rais Samia Ataka Kuimarishwa Kwa Mfumo wa Haki Jinai na Madai Nchini

Limi hakupata fursa ya kuendelea na elimu rasmi, kwani aliacha shule alipokuwa Darasa la Tano tu. Limi ana uwezo mdogo wa kufanya kitu chochote kile, akishindwa kujua siku zilizopo kwenye wiki au hata kukisia umri wake. 

Limi amekuwa akishuhudia ukatili mkubwa katika maisha yake yote. Kwa mfano, baba yake alikuwa akimpiga mama yake mara kwa mara, hali iliyomsukuma kuikimbia ndoa hiyo, huku akiwa na watoto wake, akiwemo Limi mwenyewe. Akiwa bado binti mdogo, wanaume katika kjiji chake walikuwa wakimtoa Limi nyumbani kwao kwa nguvu na kumbaka mara kadhaa.

Uwezo wake mdogo wa kiakili ulimzuia Limi kupambana dhidi ya ukatili huu. Mbali na hivyo, baadhi ya wanajamii walimtenga Limi kwa sababu ya ulemavu wake. Marafiki wake wa pekee walikuwa watoto wadogo, ambao aliendelea kucheza nao alipokuwa akikua.

Limi alipata ujauzito kwa kubakwa, na alikuwa na umri wa miaka 15 tu alipojifungua mtoto wake wa kwanza, aliyeitwa Thereza. Wakati huo, Limi hakuelewa kuwa kufanya mapenzi kunaweza kusababisha ujauzito. Zaidi ya hayo, hakujua kwamba alikuwa na mimba hadi mama yake alipomueleza.

Wakati Limi akiwa na umri wa kama miaka 18 aliolewa na mwanaume mwenye umri mkubwa aliyeitwa Maimazi. Limi alizaa watoto wawili, Kuchuma na Tabu, kutoka kwenye ndoa hiyo. Maimazi alimpiga Limi mara kwa mara, na kumbukumbu za ukatili huo wa Maimazi zimebakia katika akili ya Limi. 

SOMA ZAIDI: Rasimu ya Warioba Ina Majibu Yote Samia Anayahitaji Kuhusu Mfumo wa Haki Jinai

Baba yake Limi hatimaye alimsaidia kutoroka kutoka kwa Maimazi. Watoto wake wawili wa kwanza walibaki na Maimazi. Wakati alipotoroka, Limi alimchukua binti yake Tabu aliyekuwa na umri wa takriban mwaka mmoja. 

Baadaye, Limi alihamia kijiji kingine kuishi na mjomba wake Sayi. Akiwa huko, Limi alitakiwa kimapenzi na mtu aliyeitwa Kijiji Nyamagu. Kijiji alijulikana kuwa ni mlevi na aliepukwa na wanakijiji wengi kwa sababu ya sifa zake mbaya. 

Kijiji alimwambia Limi angemuoa, lakini alisema kamwe hatamkubali Tabu kwa sababu alizaa mtoto huyo na mwanaume mwingine. Hatimaye, Kijiji akamuua Tabu na kukimbia na kupelekea Jeshi la Polisi kumkamata Limi na kumpeka mahakamani kwa tuhuma za mauaji hayo na kupelekea kuhukumiwa adhabu ya kifo.

Afungwa bila hatia

Kwa msaada wa wakili, Limi alikata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu. Februari 2018, baada ya kutumikia miaka karibu mitatu akiwa na tuhuma hizo za mauaji, Mahakama ya Rufaa ilifuta hukumu ya Limi kwa sababu Mahakama Kuu haikuweka rekodi ya maandishi kama sheria zinavyotaka.

Uamuzi huo ulipelekea Limi kuondolewa kwenye orodha ya watu wanaosubiri kunyongwa. Hata hivyo, Limi aliendelea kuzuiliwa bila hukumu kwa miaka minne na nusu zaidi wakati akisubiri kufunguliwa kesi nyingine. Septemba 2022 Jamhuri ilifungua kesi mpya ya mauaji katika Mahakamu Kuu.

SOMA ZAIDI: Hivi Ndivyo Serikali Inavyoweza Kuuboresha Mfumo wa Haki Jinai Tanzania

Katika utetezi wa kesi hiyo mpya, wakili wa Limi alifanikiwa kupata kiapo kutoka kwa mwanasaikolojia ambaye alimuaona na kumfanyia tathmini Limi na kuhitimisha kwamba alikuwa na ulemavu mkubwa wa akili ulioendana na ule wa mtoto mwenye umri wa miaka kumi au chini ya hapo.

Hata hivyo, Mahakama haikuruhusu ushahidi wowote wa ulemavu wa akili wa Limi uingizwe na kupokelewa mahakamani na Limi alikutwa na kosa la mauaji na kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa kwa mara ya pili mnamo Septemba 23, 2022. 

Kwa msaada wa wakili, Limi alikata rufaa tena dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu, lakini hakuna tarehe iliyopangwa kwa ajili ya kusikiliza rufaa hiyo. Mpaka wakati wa kuandika makala haya, Limi amekaa gerezani kwa miaka 11, huku mingi akiitumia kusubiri adhabu ya kifo.

Simulizi hii kuhusu maisha ya Limi ni ukumbusho wa wazi wa hatari zinazowakabili watu wenye ulemavu wa akili nchini Tanzania, kubwa miongoni mwao ikiwa ni ukatili wanaoupata mara kwa mara na kushindwa kupata haki zao stahiki. 

Tangu akiwa mdogo, Limi alikumbana na vitendo visivyoelezeka vya ukatili, kutoka kubakwa hadi kuvumilia unyanyasaji wa ndani ya nyumba yao. Maisha yake, yaliyoghubikwa na maafa na unyanyasaji, ni ushahidi wa kushindwa kabisa kwa wale wanaomzunguka kumlinda na kumsaidia.

Kukosa utu

Namna mfumo wa kimahakama ulivyomfanyia Limi ni kielelezo kikubwa cha mifumo yetu ya upatikanaji haki isivyojali utu wa binadamu na upatikanaji wa haki. Licha ya ushahidi wa wazi wa ulemavu wake wa akili, Mahakama zimekataa kuzingatia upande muhimu huu wa utambulisho wake, kumnyima fursa ya kuwasilisha historia kamili ya maisha na hali yake aliyopitia.

SOMA ZAIDI: Changamoto Zinazokabili Utoaji Haki Jinai Kwa Watoto Tanzania Zatajwa

Kushindwa kutambua ulemavu wa Limi siyo tu kunaathiri misingi ya upatikanaji wa haki, lakini pia kunachochea ubaguzi ambao Limi amekuwa akiupata kutoka kwenye jamii yake na mifumo inayopaswa kumlinda na kumtetea. 

Zaidi ya hayo, ukweli kwamba Limi ameishi gerezani kwa zaidi ya muongo mmoja, tena akiwa kwenye orodha ya watu wanaosubiri kunyongwa, kunaufanya mfumo wetu wa taifa wa upatikanaji wa haki kuwa kituko. 

Licha ya kufutwa kwa hukumu yake ya awali kutokana na makosa ya kiufundi, Limi ameingizwa kwenye dimbwi la mateso kwa kusubirishwa kesi yake kusomwa upya kwa miaka sasa.

Kuendelea huku kufungwa kwa Limi, pamoja na tisho la adhabu ya kifo linalomkabili, ni adhabu kali isiyokuwa na faida yoyote ile isipokuwa kumuongezea Limi mateso katika maisha yake. 

Kesi ya Limi inapaswa kutusukuma, kama taifa, kutathmini namna tunavyoliangalia suala la haki na namna mifumo yetu ya kisheria inavyowachukulia watu wasiojiweza katika jamii zetu. 

SOMA ZAIDI: Mahakama Tanzania Isikwepe Wajibu Wake wa Kusimamia Utoaji Haki

Hii kesi inaonesha ni jinsi gani tunahitaji mageuzi kwenye mfumo wetu wa haki jinai ambayo, pamoja na mambo mengine, utaufanya utoe kipaumbele kwa utu, uelewa, na urekebishaji tabia badala ya kuwekeza nguvu zaidi kwenye kuadhibu.

Haki, kwenye muktadha wa kesi ya Limi, haihusiani tu na mama huyu kuadhibiwa kwa uhalifu anaoshukiwa kuufanya bali kuangazia sababu za msingi za hali yake na kumpatia msaada ambao anauhitaji kwa haraka sana.

Mwisho, simulizi ya Limi haihusu kufeli kwa mifumo ya kisheria ya nchi tu bali ni kielelezo cha kushindwa kwetu kama jamii kuwalinda wale wasiojiweza miongoni mwetu. Inatoa wito wa kusimama pamoja na kuikabili mifumo isiyokuwa ya haki na ambayo inachochea ukatili na ukandamizaji ili kujenga jamii yenye upendo na usawa kwa watu wote.


Anna Henga ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC). Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ahenga@humanrights.or.tz au X kama @HengaAnna. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts