The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kwenye Hili la SUK, ACT-Wazalendo Wamekalia Kuti Kavu

Namna pekee ambayo haitakuwa na madhara kwa ACT-Wazalendo ni endapo kama chama hicho hakimaanishi kile inachosema, yaani inatishia nyau tu lakini inajua haiwezi kutoka kwenye SUK.

subscribe to our newsletter!

Wiki hii kuna mambo mengi na muhimu yametokea hapa Tanzania ambayo kwa kweli ningependa nichangie maoni na tafakuri yangu kuchagiza mijadala na soga zilizoambatana na masuala hayo. Hata hivyo, nimeamua nibaki na mvutano kati ya ACT-Wazalendo na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhusiana na hatma ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) huko Zanzibar.

Huu ni uamuzi wa makusudi unaotokana na imani yangu kwamba kushajihisha jambo fulani, watu wanapaswa walijadili suala hilo kwa mapana na marefu yake ili kupanua wigo wa maoni na mawazo ambayo wahusika, yaani wale wanaopaswa kufanya maamuzi, wanaweza kufaidika nayo. 

Ni bahati mbaya sana kwamba mambo mengi yanatokea kwa wakati mmoja na kwa kasi ya ajabu sana kiasi ya kwamba hayatoi nafasi kwa wananchi kuyadili kwa kina. Ndiyo maana haishangazi kukuta watu wanajadili hili leo, na kesho wamerukia suala lingine, huku hata tukiwa hatujuwi tuliishia wapi kwenye lile la jana!

Hali hii inawanufaisha watawala, siwezi kuwaita viongozi, wanaotegemea watu wasahau haraka, wakijua hicho ni kibali cha wao kujifanyia mambo kadiri wanavyoona inafaa, wakiwa na uhakika wa kutowajibishwa kwani watawaliwa wana muda mchache na kumbukumbu fupi sana vinavyowafanya washindwe kuisimamia Serikali yao ipasavyo.

Kutokana na ukweli huu, je, tunaweza kuishangaa hali ya kimaendeleo isiyoridhisha tuliyopiga kama taifa? Unasongaje mbele bila mawazo? Unakuwaje na uhakika wa kupatia kwenye uamuzi fulani bila mjadala mpana wa suala husika ambao ungeweza kupunguza nafasi za kukosea? Kushindwa kujadili yanayotuhusu kwa kina ni kujiangamiza.

Lakini nirudi kwenye kusudio langu la kuandika safu hii, ambalo kimsingi ni kuitahadharisha ACT-Wazalendo kwamba msimamo waliouchukua wa kutishia kujitoa kwenye SUK baada ya makubaliano yao na CCM kutokufanyiwa kazi, ni msimamo unaowaweka kwenye mtego mithili ya yule aliyekalia kuti kavu juu ya mnazi.

Ushindi ni nini?

Swali la msingi ambalo ningependa wana-ACT-Wazalendo wajiulize ni hili, kwenye huu mvutano wao na CCM, ushindi unaonekana vipi, au kwa maneno mengine, ushindi haswa ni nini? Bila shaka, jibu la haraka ni kutekelezwa kwa kile ACT-Wazalendo wanakiita makubaliano kati yao na CCM yaliyowafanya wabadilishe msimamo na kujiunga na SUK hapo Disemba 6, 2020.

SOMA ZAIDI: ACT-Wazalendo Isiipatie CCM Inachotaka kwa Kujitoa Serikali ya Umoja wa Kitaifa

Hii itajumuisha kuundwa kwa tume huru ya kijaji kuchunguza madhila ya uchaguzi wa 2020; mageuzi ya msingi kwenye mfumo wa uchaguzi Zanzibar; na kuanzishwa kwa tume ya kudumu ya maridhiano na umoja wa kitaifa. Lakini tunajua kwamba ushindi huu uko mbali sana maana CCM hawajaonesha nia ya hata kulifikiria jambo hilo.

Kimsingi, CCM wameukataa wito wa kutekeleza makubaliano hayo yaliyoingiwa kati ya hayati Maalim Seif Sharif Hamad, akiwa mwenyekiti taifa wa ACT-Wazalendo na Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi, ikisema makubaliano hayo hayapo kisheria na hivyo hakuna ulazima wa kuyatekeleza.

Pia, ukweli kwamba CCM wameamua Katibu wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Idara ya Itikadi na Uenezi – Zanzibar, Khamis Mbeto, kuwa ndiye atakayekuwa anaijibu ACT-Wazalendo kwenye suala hilo, badala ya Mwinyi au Naibu Katibu Mkuu wa chama, inaonesha ni kiasi gani CCM wanawekeza umuhimu mdogo sana kwenye suala husika.

Isingekuwa shida kama CCM wasingefanyia kazi madai haya ya ACT-Wazalendo kama isingekuwa kwa tishio ambalo chama hicho kimetoa endapo kama kilio chake hakitasikilizwa, tishio la kujitoa kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), tishio ambalo linaiweka ACT-Wazalendo kwenye wakati mgumu na hatari kuliko inavyofikiria.

Hatari

Hatari ya kwanza ni ACT Wazalendo kuwekwa kwenye nafasi ya kujitetea kwa CCM wakati inapaswa kuwa kinyume chake. Kwa mfano, CCM imekuwa ikiikumbusha ACT-Wazalendo kwamba SUK ni takwa la kikatiba lililotokana na utashi wa Wazanzibari wenyewe na hivyo haiwezi kuweka masharti ya utekelezaji wa takwa hilo. Hili nakubaliana nalo.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar Imefeli?

ACT-Wazalendo wenyewe wanaonekana kutokufanya vizuri kwenye kutetea msimamo wao huu. Kwenye mkutano wake na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho zilizopo Vuga, mjini Unguja, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo (Zanzibar), Ismail Jussa, alishindwa kuijibu hoja hii na badala yake akataja namna CCM inavyokiuka Katiba.

CCM hawajawahi kujali Katiba wala sheria, hilo linajulikana, na ndicho kinachoifanya hatua yake ya kuiweka ACT-Wazalendo kwenye nafasi ya kujitetea kuwa yenye kuvutia kwani ungetegemea ACT-Wazalendo kuikaba koo CCM kwa kukiuka, au kutaka kukiuka, matakwa ya kikatiba.

Hatari ya pili ya msimamo waliouchukua ACT-Wazalendo inahusiana na nini watafanya baada ya kutoka kwenye SUK na vipi hatua hiyo itawasaidia wao kama chama kuchukua dola la Kizanzibari, lengo la muda mrefu, na kutetea maslahi ya Wanzanzibari, kama lengo la muda mfupi la chama.

Mtu anaweza kuuliza, vipi kuhusu siasa ndani ya Baraza la Wawakilishi? Na mimi nitauliza, unapataje wawakilishi kama utaisusia CCM ifanye kama inavyojisikia, ikiwemo kuratibu uchaguzi? Ni jambo ambalo haliingii akilini na uzuri ni kwamba tumeshawahi kulishuhudia hili huko nyuma, husuan kwenye uchaguzi mkuu wa 2020 uliofanyika kukiwa hakuna SUK Zanzibar.

SOMA ZAIDI: Je, Matakwa ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar Yanakinzana na Yale ya Demokrasia ya Vyama Vingi?

Namna pekee ambayo haitakuwa na madhara kwa ACT-Wazalendo ni endapo kama chama hicho hakimaanishi kile inachosema, yaani inatishia nyau tu lakini inajua haiwezi kutoka kwenye SUK. Hakuna faida yoyote ambayo ACT Wazalendo kama taasisi, itapata kutoka kwenye uamuzi huo na wala uamuzi huo haukidhi maslahi yoyote yale ya kitaifa.

Bado nina matumaini kwamba viongozi waandamizi wa chama hicho hawajachoka hivyo kiakili kiasi ya kuipa CCM pilau kwenye sahani ya udongo, au kaure kama tunavyosema Pemba, kwa kuamua kujitoa kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kuelekea uchaguzi mkuu. 

Chama cha Wananchi (CUF) kiliwahi kufanya makosa hayo huko nyuma na hakuna ushahidi wowote, labda ACT-Wazalendo watuletee, unaonesha kwamba uamuzi ulikuwa na faida kwake au kwa Wazanzibari.

Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Aisee sijaona ukiwashauri ACT Wazalendo wafanyeje, je, CCM kumwachia mketo azungumzie SUK si sawa na dharau kwa kumuepusha mwinyi asiingie kwenye kadhia ya kutotekeleza makubaliano yake na Maalim Seif? Hii SUK kama ni takwa la wazanzibar basi wapewe nafasi ya kuchakata maoni iwe wanavyoitaka wao, badala ya kuiacha iwe mithili ya mchezo wa karata tatu, kekundu umeliwa. Naogopa tusija rudia ya mwaka 2007! Usiku mwema Khalifa, sikujua kama waweza andika Kiswahili kizuri hivi!!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts