The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Je, Matakwa ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar Yanakinzana na Yale ya Demokrasia ya Vyama Vingi?

Ismail Jussa, mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo, anatolea ufafanuzi wa suala hili na mengineyo mengi kwenye sehemu hii ya kwanza ya mahojiano maalum kati yake na The Chanzo.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi ameonya kwamba Serikali ya Umoja wa Kitaaifa visiwani humo inaweza ikawepo hatarini endapo kama viongozi wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo, ambao ni washirika katika Serikali hiyo, wataendelea na utaratibu wao wa kumkosoa hadharani, hususan kwa shutuma ambazo ameziita hazina ushahidi.

Mnamo Machi 30, 2022, wakati wa mkutano wake wa mwisho wa mwezi na waandishi wa habari, Rais Mwinyi alivunja ukimya juu ya ukosoaji unaoendelea kuelekezwa kwake na viongozi wa ACT-Wazalendo, akisema hatua hiyo inahatarisha “umoja na mshikamano wa Wazanzibari.”

Ingawaje hakusema, Mwinyi alionekana kujibu shutuma zilizoelekezwa kwake na mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo Ismail Jussa, ambaye akiwa kwenye moja ya mikutano ya hadhara iliyofanyika kisiwani Unguja amewashutuma viongozi wa Serikali kugawa zabuni za Serikali kwa ndugu na marafiki zao.

“Neema zimekuja lakini siyo kwa Wazanzibari,” Jussa alisema. “Zimekuja kwao, familia yao na marafiki zao. Mkiona nchi imezungushwa mabati kila mahali tafuteni aliyepewa kazi hiyo [ni] nani? Mnanisikia? Mkiona mabati yamezungushwa, maana wanahamaki, wanakwambia ‘mabati [ni] maendeleo.’ Mbona hamtutangazii utaratibu uliopita kuwapatia zabuni hao mliowapa kazi zenu?”

Rais Mwinyi hakufurahishwa na kauli hii na anadhani kwamba kama Jussa alikuwa na dukuduku lolote kuhusu namna Serikali inavyoendesha mambo yake basi angetafuta majibu kwa njia nyengine badala ya kukosoa hadharani.

“Hakuna aliyekamilika,” Rais Mwinyi aliwaambia waandishi wa habari kwenye mkutano wake huo wa mwisho wa mwezi. “Panapotokea tatizo ni wajibu wetu kama viongozi kukaa chini kujadili [na] kuona tunapata ufumbuzi wa yale ambayo tunaona ni changamoto. Badala ya kukaa na kuzungumza maneno hadharani, mengine makali kabisa, mengine ni shutuma na tuhuma ambazo hazijawekewa ushahidi. Jambo hilo naliona halifai.”

Kuweza kufahamu kwa undani sakata hili, pamoja na athari ambazo jambo husika linaweza kuleta kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na hatma nzima ya demokrasia ya vyama vingi visiwani humo, The Chanzo imefanya mahojiano maalum na Ismail Jussa. Endelea …

The Chanzo: Hii ni mara ya pili, kusema ukweli, kufanya mahojiano na The Chanzo, hususan mimi [Khalifa Said, mwandishi The Chanzo] na wewe. Mara ya kwanza ilikuwa kwa njia ya simu ambapo ilikuwa ni punde tu ukiwa unaendelea kurejea kutokana na kile ambacho kilikutokea wakati wa uchaguzi. Unaendeleaje kwa sasa?

Ismail Jussa: Mimi ninashukuru Khalifa. Ninashukuru kila siku zikienda napata nafuu zaidi. Bado, bila shaka, kwenye mguu nachechemea. Lakini nashukuru kwamba mradi naweza kusimama, nikatembea. Kwa hiyo, nafika ninapotaka kufika. Hata kama kasi ya mwendo imepungua lakini angalau naweza kufanya shughuli zangu. Kwa hiyo, nashukuru.

The Chanzo: Nashukuru sana. Nadhani tuanzie pale tunapohitaji kuanzia. Kwa siku za hivi karibuni, kwenye mikutano ya hadhara ambayo mnaendelea kuifanya huko Zanzibar, chama cha ACT-Wazalendo, wewe umekuwa ukizungumza kwenye mikutano hii ya hadhara, na sana sana umekuwa ukizungumza mambo mengi, lakini moja ya jambo ambalo umekuwa ukizungumza ni kuhusiana na namna Rais Hussein Mwinyi anavyoendesha Serikali yake na anavyoendesha nchi kwa ujumla. Na moja kati ya kitu ambacho umekuwa ukikizungumza, hasa siku za hivi karibuni, ni zile shutma kwamba anatoa kazi au zabuni za kazi mbalimbali za Serikali kwa ndugu, marafiki na familia yake. Rais yeye mwenyewe Hussein Mwinyi hajakanusha kusema ukweli ameonesha tu kusikitika na akisema kwamba tuhuma kama hizo hazijawasilishwa, hazijaambatanishwa na ushahidi wowote. Na swali langu lilikuwa ni kwamba, unadhani ni haki kwa kiongozi kama wewe wa dhifa yako kumshtumu Rais wa nchi na vitu ambavyo hauna ushahidi navyo?

Ismail Jussa: Vizuri sana. Swali zuri sana Khalifa. Nadhani kwanza niweke wazi kwamba katika hotuba zangu zote hakuna pahala ambapo nimemtaja mtu. Na nikifanya hivyo sio kwa bahati mbaya. Nilifanya hivyo kwa makusudi kwa sababu nashukuru kwamba tumepata bahati ya kulelewa na kiongozi wa kisiasa wa kariba ya Maalim Seif [Sharif Hamad] ambaye alikuwa anafanya ujue unazungumza nini, vipi, wapi na kwa namna gani.

Kwa hiyo, kwanza sikutaja mtu jina. Na kwangu mimi mwitikio wake au namna ilivyopokelewa na hasa na mwenyewe Rais Hussein Mwinyi ni kama vile ametafsiri kwamba nimemuelekezea yeye moja kwa moja. Lakini kusema hivyo niseme kwamba bila shaka nilichokisema kilikuwa kimeelekezwa kwenye Serikali ambayo yeye ndio anaiongoza na kinapoelekezwa katika Serikali ambayo wewe ukiwa Rais basi huwezi kukwepa lawama hata kama pengine hakikuhusu moja kwa moja.

Katika mfumo wa Urais, au mfumo unaoongozwa na Rais mwenye madaraka, kuna usemi maarufu ambao ulirithiwa kutoka Marekani unaosema, [kwa Kiingereza], “The buck stop at the president.” Kwa hiyo, ni kwamba utakaposukuma jambo lolote hatimae mwisho litaishia kwa kiongozi mkuu wa Serikali ambaye katika mfumo wa Jamuhuri unaongozwa na Rais.

Sasa tukizungumza haya ambayo nimeyazungumza, tumeyazungumza kwa nini? Kwa sababu nchi zetu hizi zimetoka mbali sana katika masuala mazima ya uendeshaji wa Serikali na vile vile masuala ya huduma mbalimbali ambazo Serikali inakuwa inazitoa na vile vile huduma ambazo Serikali inazihitaji iwe kwa kuhitaji bidhaa au kwa kuhitaji huduma kwa maana ya bidhaa au huduma.

Na baada ya misukosuko mingi kuna mabadiliko yamefanyika ili kuongeza uwazi katika uendeshaji wa masuala ya nchi na vile vile kuondosha matumizi mabaya ya madaraka. Moja katika eneo hili lililofanyika ni kupitisha sheria ya manunuzi ya umma. Na sheria ile imeweka taratibu zake kwa hakika, kwa mfano, kwa Zanzibar kumeundwa vitu vinavyoitwa Kitengo cha Usimamizi wa Manunuzi ambazo zipo katika kila wizara ya Serikali na katika kila shirika au taasisi mbalimbali za Serikali.

Kwa hiyo, kiuhalisia moja kati ya matatizo sugu ambayo yamekuwepo katika Serikali zetu imekuwa ni jinsi gani zabuni zinatolewa Serikali inapokuwa inataka huduma au inapotaka bidhaa mbalimbali, iwe katika ujenzi, iwe katika masuala ya pengine utoaji wa huduma mahususi katika maeneo mahususi na mara nyingi utakuta katika yale maeneo ambapo yanajumuisha matumizi makubwa kwa upande wa Serikali basi bado tuna tatizo kubwa sana la uwazi.

Kwa hiyo, nilipotoa tuhuma zile ni suala la kwamba masuala haya hayafanywi kwa uwazi. Na kwa hakika na bado hata hapa leo sitaki kutoa mifano mahususi lakini ukiangalia tumesema hapa kwa lugha ya jumla jumla tutasema kwamba tumeona kuna ujenzi unafanyika Zanzibar, ujenzi wa masoko lakini swali ninalojiuliza ni kwamba lini palitangazwa kwamba zabuni, palitangazwa zabuni kwamba Serikali inakusudia kujenga masoko pahala fulani yenye mahitaji ya namna fulani na kwa hiyo yoyote ambaye anajiona kwamba ana uwezo aombe zabuni katika masuala hayo?

The Chanzo: Hilo umelizungumzia lakini ninachotaka kukifahamu ni kwamba kwa sababu yeye mwenyewe Mwinyi anadhani hayo madai hayana ushahidi na ni kitu kimoja kusema kwamba utaratibu wa kutoa zabuni haufati sheria au haupo wazi na ni kitu kingine kabisa kusema kwamba kazi zinatolewa kwa ndugu na familia za viongozi.

Ismail Jussa: Ndio maana nasema nilikuwa nakuja huko huko. Kwa hiyo, ninachosema ni kwamba kunapokuwa hakuna uwazi katika masuala haya kwanza kunakaribisha watu kuibua wasiwasi juu ya masuala haya. Lakini Zanzibar ni pahala padogo, tunajuana, na haya mambo yanaonekana.

Kwa hiyo, sisi kwa sasa tunamkumbusha hilo, hata mimi juzi katika hotuba ambayo nimeitoa ikiwa ni mwitikio baada ya maelezo ambayo yametolewa na upande wa Serikali nimelisisitiza hilo. Kwamba vitu hivyo viwekwe wazi kwa sababu vitakapowekwa wazi tutajua nani ni mnufaika wa zabuni hizo.

The Chanzo: Unataka kusema kwamba kauli yako ya kusema kwamba ndugu na marafiki wa Rais Mwinyi, viongozi labda, kwa sababu hukumtaja Rais Mwinyi kama ulivyozungumza ni sahihi kabisa, kwamba viongozi wa Serikali wananufaika na tenda na zabuni zinatolewa serikalini, ni hisia tu, unahisi kwa sababu unaona mchakato haukuwa wazi kwa hiyo unahisi kwamba hizi zabuni zitakuwa zinapelekwa kwa ndugu zao kwa familia zao na si kwamba ni kitu ambacho unaushahidi nacho. Kwa mfano ukiitwa mahakamani tuseme lete ushahidi wa hiki unachokizungumza, unao uwezo wa kupeleka ushahidi mahakamani?

Ismail Jussa: Ninachosema kwamba suala la ushahidi litarudi kwa Serikali. Kwa sababu kama nilivyosema kwamba ni jukumu la Serikali kueleza uwazi na watakapotoa huo ushahidi ndio utakapotusaidia sisi kuonesha nani anahusika na kufaidika na zabuni hizi.

Lakini nitakuhakikishia tu kwamba kwa yeyote ambaye ananifahamu huwa sina kawaida ya kuzungumza kitu kwa hisia tu. Kwa hiyo, nasema kwa sasa hivi nimeamua kuliachia pale lakini nataka nikuhakikishie kwamba nilipozungumza hayo masuala yanafahamika Zanzibar na kuna masuala mengi ambayo yanahitaji majibu juu ya waliofaidika na zabuni hizi ambazo zimetolewa.

The Chanzo: Unanithibitisha kwamba ushahidi unao?

Ismail Jussa: Ndio.

The Chanzo: Sawa. Kitu kingine ambacho Rais Mwinyi amekilalamikia na ambacho mimi nadhani napaswa kukuuliza, kwa sababu hata mimi pia nimejiuliza, ni kwa namna gani wewe labda na chama chako cha ACT-Wazalendo kina halalisha ukosoaji wa Serikali ya Rais Mwinyi wakati nyinyi ni sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa na endapo kwa mfano mngekuwa mna malalamiko, mna madukuduku ingekuwa ni rahisi kwenu kuweza kupata ufafanuzi wa haya mambo kutoka kwa wahusika, kutoka kwa viongozi wahusika badala ya kuyatumia kisiasa kuja kuyaongea kwenye mikutano ya hadhara. Unahalalisha vipi ukosoaji wenu kama chama cha upinzani wakati mkiwa ni sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, na mnaweza mkawa na uwezo wa moja kwa moja kumpata Rais kwa mfano ili awapatie ufafanuzi wa madukuduku yenu au masuala yenu ambayo mnayo?

Ismail Jussa: Kwanza nadhani kila chama kinakuwa na utamaduni wake wala sidhani kwamba kuwemo ndani ya Serikali kunazuia, hata ingekuwa Serikali yenyewe inaongozwa na chama chetu kama labda ndio chama kikuu kinachoongoza Serikali, hiyo ingetuzuia kuikosoa utendaji wa Serikali ambayo inaongozwa na ACT Wazalendo, hivyo ni kwamba ni washirika wadogo tena wadogo sana.

Na kulithibitisha hilo sio kwetu sisi tu hata ukitizama kwa mfano Chama cha Mapinduzi (CCM) chenyewe ambacho kinaiongoza hiyo Serikali, karibuni tu hapa kulifanyika kikao cha Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi tulimuona Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi akitoka hadharani akiitaka Serikali ichukue hatua kwa sababu ya kutoridhika na mwenendo wa Jeshi la Polisi.

Sasa ikiwa CCM inafanya ambayo ndio inayoongoza Serikali hiyo, sembuse kwa chama ambacho kinaongozwa na watu wachache tu? Kwa hiyo, nadhani katika demokrasia hasa ni kawaida itakuwa ni jambo la ajabu kwa mfano kwamba uone ukienda Uingereza ukute Serikali inayoongozwa kihafidhina kwa hiyo ukiwa wewe ni kiongozi au mbunge wa kihafidhina kwamba utakuwa hupaswi kuisema Serikali kwa sababu inaongozwa na chama chako isipokuwa ukazungumzie ndani, si kweli.

Lakini tuchukulie mfano mwingine. Tuna vyombo hapa, Bunge na Baraza la Wawakilishi, kazi zake ni kuisimamia Serikali na pale watu wanalipwa mishahara, wanalipwa posho kwenda kuisema Serikali, uwe ni wa chama kile kinachoongoza Serikali au uwe ni wa chama cha upinzani.

Kwa hiyo, nadhani haya masuala wengine tunakuwa tunazidisha kuyachukulia kama masuala nyeti, kutokuwa na ngozi ngumu ya kuweza kuhimili upinzani na ukosoaji. Lakini katika hali ya kawaida ni jambo la kawaida kabisa kuisema Serikali, uwe wewe ni sehemu ya Serikali hiyo au sio sehemu ya Serikali.

The Chanzo: Lakini wito ni tofauti na ukosoaji. Kwa mfano, mfano ulioutoa wa Katibu Mwenezi wa CCM ni tofauti na ambacho ACT-Wazalendo inakifanya Zanzibar. Ni kitu kimoja kusema kwamba mnaitaka Serikali kuwa wazi kwenye utoaji wa zabuni na ni kitu kingine kabisa kusema kwamba wanaonufaika na zabuni zinazotolewa ni familia, marafiki na ndugu wa viongozi wa Serikali, si ndio? Namaanisha ni mifano miwili tofauti.

Ismail Jussa: Hapana, nadhani labda ni mtindo. Bila shaka Katibu Mwenezi wa CCM atabakia kuwa Katibu Mwenezi wa CCM. Ni mtu tofauti na Jussa. Ana mtindo wake wa kufikisha na mimi nina mtindo wangu wa kufikisha. Lakini mantiki ni ile ile kwamba unakosoa.

Namna ya ukosoaji unaweza ukawa ni tofauti na yenyewe inategemea kila mmoja ana mtindo wake wa kufikisha ujumbe. Lakini kama nilivyosema huu ni mfano mmoja tu nimekupa. Mifano ya nchi nyingine ambapo ni kawaida na hapa hapa nimekupa mfano mwingine kwamba kwa mfano tuna Bunge na Baraza la Wawakilishi watu wanalipwa mishahara, wanalipwa posho kwa kazi ya kwenda kuikosoa Serikali.

Wanaofanya kazi ile ni watu wanaotoka chama kile kile au wanatoka katika chama kingine kinachoongoza Serikali. Kwa hiyo, si jambo la ajabu, wala si jambo la kituko kuisema Serikali kwa mambo ambayo unahisi hayaendi sawa na ninadhani ndio msingi wa demokrasia.

The Chanzo: Kuisema Serikali, mimi najiuliza tu kumsema mtu pia hadharani ambaye unauwezo wa kumpata moja kwa moja kwenda ili akupatie ufumbuzi wa madukuduku yako. Kwa mfano, utajisikia amani, au unadhani ni haki kwa kiongozi wenu wa chama kwa mfano, Zitto Kabwe, kwenda kukukosoa Twitter wakati anauwezo wa kukufikia, akaja kukuuliza na kupata ufumbuzi kuhusiana na jambo fulani? Kitu ambacho Makamu wa Kwanza wa Rais Othman Massoud anaweza kukifanya kwa Rais Mwinyi kutaka ufumbuzi wa madukuduku yoyote ambayo kama chama cha siasa mnayo. Ndio hoja yangu, unadhani ni haki?

Ismail Jussa: Mimi ninaweza kusema ni haki na ninadhani tutofautishe baina ya masuala yanayohusu mtu na mtu katika mahusiano yao binafsi na masuala ya uendeshaji wa nchi na misingi ya kidemokrasia hasa mnapokuwa na mfumo wa vyama vingi.

Na mimi sitopenda kuzungumzia kwa sababu ndio desturi yangu napenda, sitopenda kumsemea kwa mfano Makamu wa Kwanza wa Rais lakini pengine na yeye pengine hata kama anamtindo wake ya kwamba amefikia kuzungumza hadharani atakuwa na sababu zake kwamba huko ndani kuna nini mpaka amefikia pahala pa kuzungumza hadharani.

Hilo nadhani yeye ndio atakuwa anaweza kulijibu zaidi. Kwangu mimi narudia pale pale kwamba msingi wa demokrasia katika nchi ambayo ina mfumo wa vyama vingi ni jambo la kawaida kabisa, uwe unatoka chama kile kile au uwe unatoka chama kingine.

Na ninadhani ni haki na ninadhani ni haki vilevile kwa sababu msingi wa yote haya ni kuuhisha mijadala kwa sababu haya masuala yanahusu watu, na sisi tupo pale tunaitwa viongozi uwe wa Serikali au wa chama cha siasa kwa sababu kuna watu ambao wamekuamini na wanakutegemea uwasemee.

Kwa hiyo, ninapoyasema hadharani ni kwa sababu jawabu halipaswi kuja kwangu tu mimi. Sisi tunakuwa ni kama vile kioo lakini vilevile sisi ni masikio na macho ya jamii. Kwa hiyo, kuna masuala ambayo huwa tunayapokea kutoka katika jamii, ni jukumu letu kuyapazia sauti kwa sababu jamii kama mtu mmoja mmoja hawana nafasi ambayo sisi tunazipata za kuzungumza, tunawasemea wao na ndio maana na jawabu zinapotoka au majibu yanapotoka yatoke katika uwazi ili jamii yote isikie.

Hicho ndio kiini cha demokrasia. Kwa sababu mkishafikia hapo kama kuna wasiwasi utakuwa unaondoka na wananchi wote watakuwa wamepata majibu ya maswali ambayo wanayauliza. Kwa hiyo, mara nyingine inaweza kuwa mimi ninauliza lakini ninaweza kuwa ninahoji, ninauliza au nasema kile ambacho jamii huko chini inakihoji. Wao hawana fursa ambayo mimi ninayo ya jukwaa ambalo ninalipata la kuweza kuliuliza.

The Chanzo. Vizuri, ukizingatia kile ambacho amekizungumza kwenye mkutano wake wa kila mwisho wa mwezi na wahariri na waandishi wa vyombo vya habari, Rais Mwinyi alionesha wasiwasi kwamba endapo ACT-Wazalendo mtaendelea na mnachoendelea kukifanya ambacho ni kuisema Serikali yake hadharani yeye anadhani hiyo inahatarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa au mshikamano au umoja wa Wazanzibar. Unadhani hoja yake ina msingi kiasi gani kwa mfano?

Ismail Jussa: Mimi nadhani ni uoga tu wa kisiasa. Narudia palepale kwamba kila chama kina utamaduni wake. Labda Chama cha Mapinduzi au labda yeye binafsi hakuzoea masuala haya na kwa hiyo ndio maana anayachukulia kwa hofu na hiyo pengine hata kama lugha iliyotumika ni lugha nyepesi lakini pengine kutishia, kuashiria kwamba inaweza kuhatarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa mimi ukiniuliza sioni hivyo Khalifa.

Kwa nini? Kwa sababu kwanza kama tungezungumzia kuhatarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa basi matendo ya Serikali na yeye binafsi akiwa kiongozi wa Serikali pengine yanatishia zaidi kuliko haya ambayo sisi kama tunayohisi kama hatutendewi haki tunavyolalamika.

Kwa mfano, tumesema kwamba tumeunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuna mambo ambayo walikubaliana baina yake na marehemu Maalim Seif wakati ACT-Wazalendo inakubali kujiunga au kuingia katika ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Na ni suala la kikatiba lakini halikuwa jepesi kutokana na mazingira yaliyotokea katika kile kinachoitwa uchaguzi.

Sisi hatuuiti uchaguzi kwa sababu ni uchaguzi ambao hata wagombea hawaruhusiwi kushiriki kusimamia kuhesabu kura na kutangaza matokeo na kufanya majumuisho. Huwezi ukauita kama ni uchaguzi. Lakini pamoja na yale yaliyotokea tukaamua kuingia ndani ya Serikali, yalikuwepo mambo ambayo walikubaliana baina yao.

Sasa yanapokuwa yale hayatekelezwi pengine hayo ndio yangepeswa kumtia zaidi wasiwasi yeye kwamba yanaweza kupelekea hali ya hati hati katika utulivu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Lakini teuzi ambazo kama nilivyosema hata hilo pia nimelizungumzia, teuzi ambazo zinafanyika, kuna mambo unaweza kusema kwamba, unatuambia kwamba tukupe muda na sisi kwa uungwana kabisa tukaridhia kukupa muda lakini wakati tunakupa huo muda kuna vitu unavyovifanya ambavyo vinazua maswali.

Kwa mfano, moja katika misingi iliyopelekea watu kufanya maridhiano na mimi nashukuru nilikuwa sehemu ya mchakato unaitwa maridhiano ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni kutokuwepo kwa mifumo ya haki katika nchi. Sasa leo baada ya yote yaliyotokea unapoona kwamba unafanya teuzi katika taasisi ambazo zinagusa misingi mikuu ya utoaji wa haki na ukachagua watu au ukateua watu ambao wenyewe jamii inawajua, sio inawatilia mashaka labda kuwa na wasiwasi, inawajua nafasi yao katika kutufikisha katika mkorogo ambao ulipatikana au uchafuzi ambao ulifanyika.

Kwa mfano, unamchagua Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP), DPP ni nafasi kubwa sana katika katika suala la utoaji wa haki, kwa sababu yeye ndio anayesimamia upelekaji wa mashtaka mbalimbali katika mahakama, alitakiwa mtu ambaye hawezi kutiliwa mashaka nafasi yake ya kusimama katika bila kujiegemeza katika milengo ya kisiasa. Sasa unampomchagua mtu.

Hata kama ni mwanasheria ambaye anajulikana kwa kutoa maneno ya kejeli na dhihaka na vijembe dhidi ya upinzani na viongozi wa upinzani halafu ukampa nafasi kama hiyo hioneshi ishara njema kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Unampomchagua mtu ambaye alikuwa ni mjumbe wa Tume ya Uchaguzi, Kamishna wa Tume ya Uchaguzi ambayo ndio iliyoshiriki kufanya uchafuzi wa mwaka 2020 ambaye akiwa Jaji ndiye ambaye alikuwa amewasimamia kuwaengua wagombea wa upinzani wasiopungua kumi na nne katika nafasi za Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi mbali ya wagombea wa Udiwani. Leo huyo ndio ukamfanye Kaimu Jaji Mkuu.

Unapopendekeza mtu awe Kamishna wa Polisi ambaye kabla ya hapo alikuwa ni Kamanda wa Polisi wa mkoa na wakati wake ndio alisimamia vipigo kwa pamoja ambavyo binafsi mimi vimenikuta, lakini sisemi kwa shida yangu binafsi, nazungumza kwa ujumla wake unapofanya teuzi kama hizi haya hayawezi kujenga imani kwa upande wa pili.

Lakini kama hilo halitoshi, nimalizie kwa sababu mifano ni mingi, unapofanya mabadiliko kwenye Baraza la Mawaziri ukawachukua tena watu ambao walisimama hadharani kusema kwamba wanataka kupeleka hoja binafsi ya kuvunja Serikali ya Umoja wa Kitaifa leo wanaingia kuisimamia Serikali ya Umoja wa Kitaifa halafu wewe utuambie kwamba haya tunayoyafanya sisi ndio yanayotikisa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Nadhani haya matendo kwa upande wake ndio yanayotikisa misingi kabisa ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

The Chanzo: Unadhani kwa kiasi fulani kama hivyo ulivyozungumza matakwa ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa yanaweza yakawa kwa kiasi fulani yanakinzana na matakwa ya mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi, kwamba mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa unaweza ukawa mzuri kwa kudumisha umoja na mshikamano wa wananchi lakini madhara yake madogo yanaweza yakawa ni kwamba demokrasia ya vyama vingi isitekelezwe kama inavyopaswa kwa sababu hicho ndicho tunachokiona kwa sasa. Tunaona kwamba nyinyi mnafanya kile ambacho mnapaswa kufanya kama chama cha upinzani lakini hapo hapo nyinyi ni sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa na Rais aliopo anaona kwamba nyinyi mnachokifanya kinakinzana na matakwa ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Labda hiyo unaizungumziaje?

Ismail Jussa: Nadhani ili kulijibu swali lako hilo Khalifa tuangalie mambo kadhaa.  Kwanza ni ukweli kwamba unapokuwa na mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kiasi fulani unakwaza ile hali ya siasa za ushindani katika uhalisia wake.

Kwa sababu pengine sio nyie ambao hammo ndani ya Serikali kwa wale ambao wanaingia ndani ya Serikali sasa wanafungika na taratibu za uendeshaji wa nchi, kwa mfano, kwa sababu watakuwa ni Wajumbe wa Baraza la Mawaziri wanatakiwa wanapokuwa na mawazo kuyafikisha huko.

Sasa ikiwa hayakubaliwi, hayatekelezwi kiasi gani watafanya ni jukumu la wao. Lakini kwa kiasi fulani inakwaza ule ushindani na niseme kwamba hata tuliposukuma mfumo huu, haukukusudiwa kwamba utakuwa ni mfumo wa kudumu wa Zanzibar.

Uliletwa au tulisukumwa na tukashawishi jamii kukubali kupitia njia ya kura ya maoni Zanzibar kwa sababu ya kutaka kutibu tatizo ambalo limekuwepo kwa muda mrefu la siasa za kufa na kupona ambazo zimepelekea hatari na hujuma nyingi katika Zanzibar.

Zimepelekea athari kubwa sana, watu wamekuwa wakipoteza maisha kila chaguzi, watu wanaumizwa, wanajeruhiwa, wanaachwa na ulemevu, watu wameathirika sana kisaikolojia, kuna watu wamebakwa, mpaka leo kuna watu wataendelea kuishi nayo katika umri wako wote.

Kuna masuala ya wizi wa kura katika chaguzi, kuna masuala ya watu kunyimwa haki katika chaguzi. Lakini hayaishii katika chaguzi tu baadae unakuta kwamba yanaingia katika mpaka huduma za kijamii.

Tunajua sote, kwa mfano, kwamba imekuwa ni kawaida katika uendeshaji wa Serikali Zanzibar kwamba Chama cha Mapinduzi kikishafanya hayo kinayoyafanya ili kuchukua madaraka kwa nguvu basi bado kinawabagua watu katika utoaji wa haki.

Masheha, Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa, Wizara za Serikali zimekuwa hazitoi haki ki sawasawa. Kwa hiyo, ilipokuja hoja ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ilikusudiwa kwanza kujaribu kutibu suala hili kwa kuwa na kipindi ambacho kilidhaniwa kitajenga umoja baina yetu mpaka mfumo huu uzoeleke. Kwamba hakuna mtu ambaye kwa kuwa na Serikali anapaswa kuhodhi haki nyingine zote za sheria na kuamua nani ampe nani asimpe.

Hilo moja. Lakini la pili kuna suala zima sasa la kwamba ili tegemewa kwamba labda hofu ya vurugu katika chaguzi na CCM kulazimishwa kubakia madarakani inakuja kwa sababu ya hofu ya kwamba ikipoteza uchaguzi itakuwa imepoteza kila kitu.

Kwa hiyo, tuwe na mfumo ambapo unahakikishia sote ni washindi, kwamba hakuna mshindi kuchukua kila kitu kwamba kutakuwa na mfumo wa ushirikiano kiasi ambacho ukishindwa uchaguzi hupotezi kila kitu kama ambavyo ukishinda uchaguzi huchukui kila kitu.

Kwa hiyo, ilifanya hili lije kwa muda fulani lijenge mazingira ya kuaminiana ifanye kwamba suala la watu kupokezana madaraka, leo anaongoza huyu kesho anaongoza yule, lizoeleke huku mnafanya kazi pamoja mpaka mkifika pahala pa kuaminiana mrudi katika mfumo ule wa kawaida ambapo kunakuwa na Serikali na upinzani.

Lakini kwa upande wa pili tunasema hata hilo si kama peke yake linakwaza demokrasia. Nitakupa mfano. Tulipokuwa katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya mwaka 2010 hadi 2015 chombo ambacho ungetegemea kingeisimamia Serikali ni Baraza la Wawakilishi, tulifika pahala ikawa Baraza la Wawakilishi limekuwa limehuika zaidi kwa mijadala moto moto na kuiweka Serikali katika jamvi kuibana ijieleze zaidi wakati wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuliko hata ilipokuwa na huo upinzani.

Kwa nini? Kwa sababu ilifika pahala palikuwa na Serikali ambayo inaundwa na mawaziri wanaotoka pande zote mbili, vyama ambavyo vilikuwa na uwakilishi katika Serikali.

Kwa hiyo, hawa mawaziri wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wakawa ni wajibu wao kuitetea Serikali lakini huku wawakilishi ambao si sehemu ya Serikali kwa maana si sehemu ya Baraza la Mawaziri hawa iwe wanatoka upande wowote, tukawa tumeshikana kwa pamoja kuhakikisha kwamba tunibana Serikali.

Kwa hiyo, si kweli kwamba inaua demokrasia katika kutegemea tunautekeleza vipi huo mfumo. Lakini bila shaka katika ile hali ya ushindani ya kupima kwa mfano utekelezaji wa sera ni kweli kwamba hilo linakwaza katika ushindani.

Lakini kama nilivyosema ilikusudiwa kwamba hili liwe ni njia ya mpito ili baadae tukishazoeana tukajengeana imani turudi katika chaguzi za ushindani ambapo kutakuwa na Serikali na kutakuwa na upinzani ambayo ni msingi wa demokrasia ya vyama vingi.

The Chanzo: Na unadhani labda tangu kuanzishwa kwake na kutekelezwa kwake mpaka hivi sasa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa kiasi fulani imetimiza hilo lengo ambalo umeligusia hapo la kuwafanya watu wazoee kwamba chama kingine kinaweza kikaingia madarakani kikaendesha Serikali? Kwa sababu hicho kitu ambacho umekizungumza kwamba huo mfumo ulikuzuia kufanikisha hilo, unadhani ni kwa kiasi gani labda hilo lengo limefanikishwa?

Ismail Jussa: Vizuri. Halijafanikiwa bado. Ndio jibu la moja kwa moka kwa sababu ukichukua kwa mfano kwamba uchaguzi wa mwaka 2015 baada ya kipindi kimoja cha miaka mitano cha Serikali ya Umoja wa Kitaifa na uchaguzi ule dunia nzima waangalizi wa ndani na nje chama cha CUF kwa wakati ule na mgombea wake wa Urais ambaye alikuwa ni Maalim Seif Sharif Hamad alikuwa ameshinda.

Kwa hiyo, ungetegemea baada ya kufanya kazi kwa miaka mitano basi CCM iridhie matokeo na Serikali aiongoze Maalim Seif CCM ikiwa ni mshirika kama ambavyo CUF ilikuwa kutokea 2010 hadi 2015. Lakini hilo halikufanyika.

Lakini pamoja na kusema hayo niseme pengine kwa hali ya siasa za migawanyiko na kutiliana shaka na chuki na hasama ambazo zimekuwepo Zanzibar pengine usingetegemea kwa kipindi cha miaka mitano kwa maana ya mhula mmoja tu peke yake ikatosha kutibu au kuponyesha ile misuguano na majeraha na kutokuaminiana ambako kumekuwa kwa miaka.

Lakini kama tutazungumzia kwa kipindi kile bila shaka haikufanya kazi hiyo na pengine hata sasa na ukimsikiliza Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar wa hivi sasa Mheshimiwa Othman Masoud hotuba zake amekuwa akilisisitiza hilo kila wakati.

Kwamba hatuwezi kuzungumzia uwajibikaji wa watendaji wadogo wadogo, kwamba ikiwa msingi mkuu wa uwajibishaji ambao ni wananchi kuiwajibisha Serikali yao kupitia uchaguzi kwa sababu pale ndipo unapopima kwamba umetekeleza ahadi zako ama hujatekeleza, ikiwa hilo haliheshimiwi kwamba wananchi hawana kauli baina yake tunafanya chaguzi za ajabu ajabu kwa kwa kauli zake mwenyewe anazozitumia Mheshimiwa Othman Masoud anasema tumekuwa na chaguzi za chorichori, ukifika hapo kwa hiyo ule msingi wenyewe wa uwajibikaji unakuwa umeondoka.

Na kwa hiyo mtu ambaye mwenyewe hakuingia katika mfumo wa haki hawezi akataka haki ya kuingia katika mfumo wa uwajibikaji, hawezi akataka uwajibikaji kwa maafisa waliokuwepo chini yake.

Kwa hiyo, nasema bado tuna kazi ndefu pamoja na hayo nasema sisi jukumu letu ni kuendelea kusukuma kwa sababu bado halijafika pahala pa kusema kwamba hali ile ya misuguano iliyokuwepo ni ya afadhali zaidi kuliko hii ya kuwa na mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Mazungumzo haya yamebadilishwa kutoka kwenye sauti kwenda kwenye maneno na mwandishi wa The Chanzo Lukelo Francis. Joseph Kiraty amesimamia na kuzalisha mahojiano haya. Kwa maoni yoyote kuhusiana na mahojiano haya, wasiliana na wahiri wetu kupitia editor@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *