Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimezitaka mamlaka za kiuchunguzi visiwani Zanzibar kuharakisha uchunguzi wao ili kumaliza kitendawili cha kupotea kwa kada wake, Juma Juma Makame, maarufu kama Juma wa Juma, ambaye alipotea katika mazingira ya kutatanisha mwaka 2020 na ambaye mpaka sasa hajulikani alipo.
Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na The Chanzo yaliyofanyika Machi 27, 2024, Katibu wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Idara ya Itikadi na Uenezi – Zanzibar, Khamis Mbeto, alisema suala hilo limechukua muda mrefu sana na ni wakati sasa vyombo vya ulinzi na usalama visiwani humo kuharakisha utatuzi wake.
“Masuala yote ya kiuchunguzi, ya kijinai, si ya chama, ni ya polisi,” Mbeto alijibu baada ya kuulizwa na mwandishi kwa nini CCM haionekani kukerwa na kupotea kwa kada wake aliyekitumikia chama kwa miaka mingi.
“Polisi wanaendelea na taratibu zao,” Mbeto alisema kwenye mahojiano hayo. “Mimi ninachosisitiza [ni] kwamba vyombo vya ulinzi na usalama waendelee kufuatilia kwa haraka. Sisi kama chama, lakini pia familia yake, ijue kama huyu mtu amefariki, ama ametekwa, ama kimetokea kitu gani.”
The Chanzo ilimtafuta Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Richard Thadei Mchomvu, kutaka kufahamu uchunguzi wa sakata la kupotea kwa kada huyo umefikia hatua gani.
Jitihada hizo, hata hivyo, hazikuzaa matunda baada ya simu yake ya mkononi kutokupokelewa licha ya kupigiwa mara kwa mara, wala hakujibu ujumbe mfupi wa simu aliotumiwa.
Makame alitoweka Agosti 19, 2020, takribani miezi miwili kabla ya Uchaguzi Mkuu, alipokwenda kwenye mazoezi, kama kawaida yake, akikimbia na kuogelea katika eneo la Mazizini, mjini Unguja. Hakuonekana tena, akiacha familia na marafiki katika simanzi kubwa.
SOMA ZAIDI: Kada wa CCM Zanzibar Apotea Kwa Miaka Miwili. Familia Yataka Majibu
Makame, ambaye amefikisha umri wa miaka 66 mnamo Februari 2, 2023, alipotea katika hali ya kutatanisha punde baada ya kuwa mshindi wa pili katika kinyang’anyiro cha kura za maoni za CCM za kugombea uwakilishi wa jimbo la Chaani.
Kupotea kwa Makame kuliambatana na tetesi za rushwa katika uchaguzi wa ndani uliohusisha wagombea tisa, hali iliyomfanya Makame kuonesha nia ya kukata rufaa juu ya matokeo yaliyompa ushindi Nadir Abdullatif Yussuf Alwardy, ambaye kwa sasa ni mwakilishi wa Chaani kupitia CCM.
Kwenye mazungumzo yake na The Chanzo, Mbeto alisema kwamba Makame “hakuwa na tatizo na CCM,” akidai kwamba chama hicho tawala nchini kimekuwa mstari wa mbele kuifariji familia yake, ikiitembelea mara kwa mara, mara ya mwisho ikiwa ni Disemba 2023.
“Sisi kama chama tukio hili limetusikitisha sana,” Mbeto alisema kwenye mahojiano hayo. “Kumpoteza kada wetu, na siyo kada tu, [Makame] ametumikia Serikalini. Kwa hiyo, si kitu cha kuchukulia kama mchezomchezo. Sisi tumehuzunika.”
Samira Salum, mke mdogo wa Makame, hakuwa tayari kuzungumza na The Chanzo kuhusiana na kupotea kwa mume wake. Kwenye mahojiano yake na The Chanzo yaliyofanyika Februari 2023, Samira alimuelezea mume wake huyo kama mtu mkarimu aliyeipenda familia yake sana.
SOMA ZAIDI: Serikali: Matukio 21 Ya Watu Kutekwa na Kupotea Yamepatiwa Ufumbuzi
“Hakuwa mume pekee, alikua mlinzi na mlezi wetu,” Samira, mama wa miaka sitini mwenye watoto saba, alisema kwenye mahojiano hayo. “Sasa hatujui mume wangu yuko wapi, kama ni mzima au amekufa.”
Familia ililalamikia uchunguzi wa suala hilo kuchukua muda mrefu kuliko ilivyo kawaida, ikizitaka mamlaka za kiuchunguzi kulipa kipaumbele suala la usalama wa Makame. Kwenye mahojiano yake na The Chanzo, Mbeto alisema kwamba hata kama ingekuwa ni yeye angelalamika.
“Kwa sababu muda unakwenda na hatujapata majibu,” alisema Mbeto. “Na kwa sababu Juma wa Juma ni Muislamu, kuna taratibu za kidini [lazima zifuatwe,] kama wake zake wakae vizuka, si ndiyo bwana? Kama kuna mirathi watu warithishwe. Lazima tuhimize hiki kitu.”
Makame, ambaye ni mume kwa wake wawili, Samira Salum na Mwajuma Mkuya, alistaafu utumishi wa umma mwaka 2019, akifanya kazi kama Kamishna Msaidizi wa Kampuni ya Bima ya Zanzibar (ZIC), hii ikiwa ni miaka 43 katika utumishi wa Serikali.
Alipata Shahada ya Uzamili katika fedha mwaka 1993 katika chuo cha Strathclyde, kilichopo katika jiji la Glasgow, nchini Scotland. Aliingia rasmi katika utumishi mwaka 1976, akianza kama mwalimu kabla ya kushika nafasi mbalimbali Serikalini.
Wakati akiwa Serikalini, Makame alishika nyadhifa mbalimbali katika chama, kama vile mjumbe wa kamati za mkoa na wilaya na katika Jumuiya ya Wazazi jimbo la Chaani.
Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.